Moyo Ulioonja Maumivu

Moyo Ulioonja Maumivu

SEHEMU YA 29

Mara baada ya kujua kwamba Violeth alikuwa na mimba, makampuni mbalimbali yakaanza kujisogeza na kuomba kufanya nao biashara, yaani mtoto atakapozaliwa basi wao wawe wa kwanza kumpiga picha na kumtupia kwenye mitandao ya kijamii.

Lilikuwa dili kubwa sana. Benki kubwa ya Africa Union ikapanga kuingiza kiasi cha shilingi milioni mia nne kwa umiliki wa picha ya kwanza kwa mtoto atakayezaliwa.

“Ila watakuwa mapacha,” alisema Theo huku akimwangalia meneja wa benki hiyo.
“Mapacha?”

“Ndiyo!”
“Basi tutaweka mara mbili zaidi. Naomba asichukue mtu nafasi hiyo,” alisema meneja huyo.
“Haina shida.”

Mimba yake ilikuwa ni ya mwezi mmoja lakini kila alipopita watu walikuwa bize kuangalia tumbo lake. Alionekana kuwa mwanamke mwenye furaha mno, alitabasamu kila wakati, mapenzi yao yalikuwa wazi na hawakutaka kujificha hata kidogo.

Theo alisimamisha mambo yake mengine kwa ajili ya mke wake, aliamini huyo ndiye alikuwa furaha yake, bila yeye maisha yake hayakuwa na kitu hivyo ilikuwa ni lazima amuheshimu kwa kila kitu.

Siku zilikwenda mbele, miezi ikakatika mpaka ulipofika mwezi wa mwisho, mwezi wa uchungu ambao alitakiwa kwenda kujifungua. Mwezi huo waandishi wa habari walikuwa makini, masikio yao yalikuwa ni kusikilizia ni hospitali gani Violeth angekwenda kujifungulia.

Hakukuwa na aliyejua, Theo hakumwambia mtu yeyote yule, alifanya kila kitu kuwa siri. Kazi ilikuwa kwa Watanzania, wazee wa kubashiri, wengine walisema Violeth angejifungulia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wengine walisema Agha Khan, wengine Hindu Mandal, kila mtu muda huo alisema lake.

Theo alitafutwa ili alizungumzie jambo hilo, hakutaka kusema lolote lile, aliwaambia waandishi kwamba walitakiwa kusubiri kwani huo haukuwa muda sahihi wa kuwaambia kitu chochote kuhusu mke wake.

Siku zilikatika mpaka siku ambayo Violeth alijisikia uchungu na kupelekwa katika Hospitali ya kisasa ya St. Joseph Medical Centre iliyokuwa Upanga kwa ajili ya kujifungua.
 
SEHEMU YA 30

Ilikuwa ni usiku mwingi, mke wake alipokelewa na kuingizwa ndani ya chumba kimoja kilichoandikwa ‘Labour’ mlangoni. Aliambiwa asubiri nje, hakuwa na jinsi, alisubiri huku akiwa na marafiki zake wawili.

Hakukaa kwenye benchi, kila alipoyaangalia aliona kama yana misumali, alisimama huku akitembea huku na kule, alikuwa akimuomba Mungu, amuongoze mke wake na ajifungue salama kabisa.

Alikaa hapo kwa zaidi ya saa mbili, mlango haukufunguliwa, alishikwa na hofu, alionekana kuwa na woga kupita kawaida. Alihitaji kujua kilichokuwa kikiendelea, alionekana kuhisi jambo, akawaangalia wenzake na kuwauliza kuhusu kilichokuwa kikiendelea.

“Usiwe na hofu! Violeth atajifungua salama,” alisema rafiki yake mmoja.

Kwa kumwangalia tu waligundua kwamba mwanaume huyo alikuwa akiogopa mno, kitu kilichokuja kichwani mwake ni kwamba mke wake alipata tatizo na ndiyo maana mlango ulichukua muda mrefu mpaka kufunguliwa.
 
SEHEMU YA 31

Alipoona amechoka, akausogelea mlango na kuanza kuugonga, alihitaji ufunguliwe ili aone kile kilichokuwa kimeendelea humo..

“Dokta! Fungua mlango...fungua mlango...” alisema Theo huku machozi yakianza kumtoka, aliisikia sauti moyoni mwake ikimwambia kuna moja limetokea, inawezekana mke wake akawa amefariki ama watoto wake.

Alijitahidi kuipinga sauti hiyo kwa nguvu kubwa, haikupingika, iliendelea kumwambia hivyohivyo kitu kilichomfanya kuwa na hofu zaidi na zaidi.

Baada ya dakika kadhaa za kugonga mlango ule, mara ukafunguliwa na kukutanisha macho yake na daktari.

Kwa muonekano wa mtu huyo tu ulimwambia kulikuwa na jambo kubwa lililokuwa limetokea huko, alionekana tofauti, kama kweli mke wake alijifungua salama, inamaanisha daktari huyo angeonekana kuwa na furaha na si kama alivyokuwa.

“Nini kinaendelea?” aliuliza Theo huku akimwangalia daktari huyo ambaye alionekana kuwa na jambo zito moyoni mwake ila hakutaka kumwambia mahali hapo.
“Naomba twende ofisini kwangu,” alijibu daktari huyo.

“Subiri kwanza. Naomba uniambie! Amejifungua salama?” aliuliza Theo huku akianza kutetemeka kwa hofu, kijasho chembamba kikaanza kumtoka, mwili wake ulikuwa ukitetemeka kana kwamba alikaa sehemu iliyokuwa na baridi kali.
“Naomba twende tukaongee,” alisema daktari yule.

Hakuwa na jinsi, yeye na marafiki zake wakaanza kuelekea kule ofisini kwa daktari, aliogopa, alimuomba Mungu kusiwe na habari mbaya ya kupewa, aliujua moyo wake, kwa jinsi ulivyompenda Violeth, kama angeambiwa mke wake amekufa basi maumivu ambayo angeyasikia yangekuwa makubwa mno.

Walipofika ndani ya ofisi hiyo, wakakaa kwenye viti na kuanza kuangaliana. Moyo wa Theo ulikuwa kwenye maombezi mazito, hakukuwa na siku ambayo alikuwa akimuomba Mungu kama siku hiyo.

“Theo....tumejitahidi sana, mke na watoto wako wamekufa...” aliisikia sauti hiyo moyoni mwake, sauti ambayo ilimtisha mno.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane siku nyingine.
 
Nilikuwa naombea hii hadithi isiwe zile za drama za kusalitiwa na visasi kuwa ndo dhamira kuu...

Afadhali hii inaelekea direction nyingine.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom