Moyo Ulioonja Maumivu

SEHEMU YA 35

Ilikuwa taarifa mbaya mno kwake, ilimuumiza kupita kawaida, alibadilika na kukosa tumaini kabisa moyoni mwake, alimpoteza mtoto wake mmoja na aliamini kabisa alikuwa njiani kumpoteza mtoto wake mwingine.

“Naye atakufa?” aliuliza Theo huku akimwangalia daktari.

“Theo! Ni vigumu sana kukwambia hili!” alijibu daktari.
“Niambie tu. Hata kama kuniumiza zaidi, niumize tu,” alisema Theo.

Tatizo hilo lilikuwa kubwa, kitaalamu hujulikana kama Acute decompensated heart failure (ADHF) ambapo mtu analipata mwisho wa siku anakuwa na ugumu katika mfumo wa upumuaji.

Moyo utakaposhindwa kufanya kazi yake vizuri, kutakuwa na tatizo jingine kwenye misuli yake hivyo kutampelekea mgonjwa kuwa na maumivu makali mwilini mwake.
Kwa kawaida tatizo hilo mara nyingi huwakuta watu wazima lakini kitu cha kushangaza kabisa, lilimpata mtoto mdogo kama Rachel.

Hilo liliwachanganya madaktari, walihisi kabisa uhai wa mtoto huyo haukuwa wa muda mrefu, mwaka huohuo kulikuwa na uwezekano wa kufariki dunia.

“Kwa hiyo atakufa?”
“Ila si leo!”
“Lakini atakufa?” aliuliza Theo huku akimwangalia daktari ambaye kulijibu swali hilo kwake kulikuwa na ugumu mkubwa.

Ukimya wake ulikuwa jibu tosha kwa Theo kwamba ni kweli mtoto wake angekufa kwani kwa jinsi hali ilivyoonekana, hakukuwa na ujanja wowote wa kuweza kuokoa maisha yake, na kama wangetaka kufanya hivyo basi wangetumia kiasi kikubwa cha pesa.

“Ni lazima apatiwe matibabu makubwa zaidi,” alisema daktari.
“Nitatumia hata utajiri wangu wote ilimradi mtoto wangu apone,” alisema Theo.

Kilichofuata ni kutoka humo na kwenda katika chumba alicholazwa mke wake, alikaa katika kiti cha pembeni huku akimwangalia tu jinsi alivyokuwa kimya kitandani.

Alikumbuka namna mke wake huyo alivyokuwa na hamu ya kutaka kuzaa watoto wenye afya njema, alijua ni kwa jinsi gani alikuwa na hamu ya kuwaona, je, nini kingetokea kama angemwambia kuwa mtoto wake mmoja alifariki dunia na huyu aliyebaki naye alikuwa kwenye hatari ya kufa?
 
SEHEMU YA 36

Maumivu aliyokuwa ameyapata yalikuwa ni mara tano ya yale ambayo angeyapata mke wake. Aliumia, hakutamani kuona mke wake huyo akiumia kama atakavyoumia, alitamani kuona akiishi maisha ya furaha, yasiyokuwa na maumivu hata kidogo.

Siku ya kwanza ikapita, Theo hakuondoka hospitalini, taarifa zilianza kuzagaa mitandaoni kwamba Violeth alijifungua usiku uliopita lakini hakukuwa na mtu aliyepata taarifa kuwa mtoto mmoja alifariki dunia.

Theo hakutaka kumtaarifu mtu yeyote yule, na hata alipoongea na ndugu zake aliwaambia kwamba alijifungua salama kabisa. Alihitaji kumuona mke wake akifumbua macho na kuzungumza naye, ampe taarifa hiyo ili wajue ni kwa namna gani wangewaambia wananchi.

Siku hiyo ndiyo ambayo Violeth alipoyafumbua macho yake kitandani pale. Alionekana kuchoka mno, kitu cha kwanza kilichokuja kichwani mwake ni watoto wake, alijua alijifungua, alihitaji kuwaona wote wawili.

Akaangalia pembeni, kulikuwa na mtoto mmoja wa kike, lakini upande mwingine hakukuwa na mtoto. Haraka sana Theo akasimama na kumfauata mke wake mahali pale.

“Mume wangu! Nimejifungua....tumepata watoto mapacha mume wangu...wa kiume ataitwa Harry na wa kike ataitwa Rachel...” alisema Violeth kwa sauti ya chini, hakujua kilichotokea, badala ya Theo kumjibu, machozi yakaanza kumtoka hali iliyoanza kumtisha Violeth kitandani pale. |
|
|

Je, nini kitaendelea?
Tukutane siku nyingine.
 

Similar Discussions

14 Reactions
Reply
Back
Top Bottom