Morogoro: Aliyemuua dada yake alishawahi kumuua bibi yake

John Haramba

JF-Expert Member
Feb 4, 2022
365
1,373
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema kuwa kijana Shomari Malima anayedaiwa kumuua kwa kumcharanga na mapanga dada yake aitwaye Faidhat Ibrahimu (13) kutokana na ugomvi wa kifamilia, inadaiwa pia ameshawahi kumuua bibi yake kutokana na imani za kishirikiana ambazo zimemfanya asishiriki tendo la ndoa.

Kamanda wa Polisi wa Morogoro, SACP Fortunatus Muslimu, ameyasema hayo ikiwa ni siku chache baada ya mwanafunzi Faidhat aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mwenge iliyopo Kingolwira, Manispaa ya Morogoro kuuawa na kaka yake huyo.

Inaelezwa kuwa mara baada ya kuhusika na tukio la kwanza la bibi yake, familia yake ilificha juu ya tukio hilo kwa kuogopa atashughulikiwa na mamlaka za sheria.

Hadi kufikia leo Februari 22, 2022, Jeshi la Polisi bado linaendelea kumsaka mtuhumiwa ambaye ametoroka na hajulikani alipo.

Kutokana na tukio hilo Kamanda Muslimu, amewataka wananchi mkoani humo kuhakikisha wanashirikiana na Jeshi hilo kutoa taarifa za migogoro kwenye familia ili kudhibiti vitendo vya mauaji.

Muslim.jpg


=================

MWANAFUNZI ADAIWA KUUAWA KWA MAPANGA NA KAKA YAKE

MWANAFUNZI wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mwenge, Manispaa ya Morogoro, Faidhat Ibrahim (13) anadaiwa kuuawa kwa kukatwa na mapanga na kaka yake, Shomari Malima.

Faidhat anadaiwa kufanyiwa kitendo hicho kilichompotezea uhai wake nyumbani kwao, mtaa wa Tambukareli, kata ya Kingolwila, huku sababu ikitajwa ni ugomvi wa kifamilia kati ya mama wa marehemu na wa mtuhumiwa.

Akisimulia mkasa huo, mama wa marehemu, Zawadi Kidukulu, alisema tukio hilo lilitokea juzi huku akilihusisha na ugomvi wa kifamilia kwa sababu awali aligombana na dada yake baada ya yeye na mume wake kulima mihogo katika shamba la dada yake kwa kuwa alikabidhiwa kulinda eneo wakati hayupo.

Zawadi alisema wakati mazao hayo yamekuwa tayari kuvunwa, dada yake ambaye alikuwa akiishi Ngerengere, alirudi na kuvuna mazao hayo bila kumjulisha na alipohoji ndipo ugomvi ukazuka kitendo ambacho anaamini kiliingiza chuki hata kwa mtoto wake hadi kufikia hatua ya kutekeleza mauaji hayo.

"Ni kweli tulikuwa na ugomvi mimi na dada yangu. Itakuwa ndiye kapandikiza chuki hadi kwa mtoto wake kwa sababu hata mwanagu alikuwa akikutana naye akimsalimia haitikii. Lakini sikujua kama itafikia hatua ya kumtoa roho mwanangu kwa sababu ugomvi haukuwa mkubwa kiasi hicho," alisema Zawadi.

Ibrahim Gaddafi, baba wa marehemu, alisema mara ya mwisho kuzungumza na mtoto wake ilikuwa juzi baada ya kutoka shuleni ambapo alimuomba dada yake aende kumfuata mama yake ambaye alikuwa kazini.

Alisema baada ya kumfuata mke wake ambaye anafanya kazi ya kupasua kokoto, alipigiwa simu kuwa mtuhumiwa ameleta vurugu kwa mama yake lakini kabla hawajafika akapigiwa simu kuwa mtuhumiwa amempiga mtoto wake na yuko katika hali mbaya.

"Wakati tuko njiani tunaenda kwa shemeji yangu, ndipo nikapigiwa tena simu na kuambiwa nirudi nyumbani kwangu Faidhat amepigwa na kaka yake, yaani baada ya kutoka kwenye ugomvi na mama yake ndipo akaja huku kwangu," alisema Gaddafi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Tambukareli, Juma Muitano, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12:30 jioni. Alisema baada ya kupata taarifa, wakazi wa mtaa huo walianza msako wa kumtafuta mtuhumiwa bila mafanikio.

Aliwataka wakazi wa mtaa huo kuwa na utamaduni wa kuripoti taarifa za migogoro hasa ya kifamilia pindi inapotokea ili kupatiwa ufumbuzi kisheria na kuondokana na madhara makubwa yanayoweza kutokea.

Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi (ACP), Ralph Meela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba Jeshi la Polisi linamshikilia mama wa mtuhumiwa baada ya uchunguzi wa awali kuonyesha ni mgogoro wa kifamilia baada ya mtuhumiwa kukimbia.

Alisema jeshi hilo linaendelea kumtafuta mtuhumiwa ili kubaini sababu hasa za mauaji hayo na kwamba pamoja na mambo mengine pia mtuhumiwa huyo anadaiwa aliwahi kuhusika na mauaji katika kijiji cha Ngerengere miaka ya nyuma.

“Ziko sababu nyingi zinazohusishwa na mauji haya, kubwa likiwa mgogoro wa kifamilia pamoja na ushirikina kwamba mtuhumiwa na mama yake wamekuwa wakimtuhumu mama wa marehemu kuwaroga,” alisema.
 
Huyo ni kichaa awekwe kwenye ulinzi salama vinginevyo naye atauawa kwa kisasi
 
Back
Top Bottom