Mo Dewji akutana na kuteta na kocha Gomes

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,805
4,488
SIMBA leo wana jambo lao kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam wakati watakapotangaza ubingwa wao wa 22 katika Ligi Kuu Bara, lakini inaelezwa kipigo cha bao 1-0 ilichopewa na Yanga bado kimewavuruga mabosi wa klabu hiyo.

Simba leo itavaana na Coastal Union ikihitaji pointi moja tu kubeba ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo, lakini akili za mabosi wa klabu hiyo bado zipo kwenye mchezo wao ujao wa fainali za Kombe la Shirikisho (ASFC) wakilenga kufuta uteja dhidi ya watani zao.
Yanga iliwafunga Simba kwenye Kariakoo Derby iliyopigwa wiki iliyopita kikiwa kipigo cha pili msimu huu pamoja na cha Kombe la Mapinduzi 2021 na timu hizo zitakutana tena katika fainali ya ASFC itakayopigwa mjini Kigoma Julai 25 na Simba haitaki kupata aibu tena.

Katika kuhakikisha wanafanya vyema kwenye mchezo wa Kigoma, inaelezwa mapema Jumanne bilionea wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji aliamua kukutana na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mfaransa, Didier Gomes na kujifungia kwa muda wa saa tatu wakipeana dili za kijanja. Moja ya mambo yanayodaiwa kuwakutanisha wawili hao ni fainali ya ASFC, ambayo Simba inaitolea macho kinoma, ikitaka kuepuka aibu tena ya kuchapwa na watani zao, ambao kwa msimu uliopita waliwafumua kwenye nusu fainali kwa mabao 4-1, kitu ambacho Msimbazi wanataka kuendeleza tena Kigoma, ili kujifariji na kushindwa kuwatesa Yanga katika Ligi Kuu kwa misimu miwili sasa.

Chanzo makini kutoka ndani ya Simba, kinasema bilionea huyo kijana alifanya kikao kizito kisichopungua saa tatu na Gomes, ikiwa ni mara ya pili kwao kwani walishakutana mara moja tu mara Mfaransa huyo alipotua Msimbazi akitokea Sudan alikokuwa akiifundisha El Merreikh.

“Kipigo cha Yanga, kilimfanya Mo Dewji kukutana na Gomes na kuyajenga kwa lengo la kuona mechi ya fainali ya ASFC, Jangwani nao waugulie maumivu kwani kama ubingwa wa Bara tayari ni uhakika, ila kutowafunga watani ni kama doa Msimbazi,” kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, Mwanaspoti lilimtafuta Gomes na kuzungumza naye juu ya kikao hicho kilichofanyika na kumalizika usiku alikwepa ishu ya Yanga na kudai walijadiliana mambo mengi ikiwamo mpango wa Mo Dewji kutaka kumwaga mkwanja wa maana ili wavute majembe msimu ujao.

MSIKIE MWENYEWE
Gomes alianza kwa kumshukuru Mo kwa kuwa na nia ya dhati kuhakikisha Simba inafanya vizuri katika mashindano yote na kufikia mafanikio makubwa ambayo sio kazi rahisi.

Alikiri ni kweli kikao hicho na Mo kwake, kilikuwa cha pili na kusema amepata nafasi ya kufahamu mambo mengi kutoka kwake kama ambavyo naye imekuwa hivyo.

“Tulizungumza jambo moja baada ya jingine kuhusu timu, kuna ambayo naweza kuyaweka wazi, ila mengine yanabaki ndani kama siri ya klabu, kikubwa ambacho nataka Simba wafahamu chini ya Mo Dewji watafanya vizuri na kufikia malengo makubwa,” alisema
“Nimeamua kuliweka wazi hilo kutokana na mambo aliyonieleza pamoja na maoni yake ambayo anataka Simba ifike iwe klabu kubwa Afrika ndani ya muda fulani ambayo inajiendesha yenyewe.

“Kufanikisha hilo nimemhakikishia kupambana na kujitolea katika kila ambalo nalielewa ili ndani ya muda fulani tuweze kuwa timu kubwa Afrika hata kuchukua mataji.”

UBINGWA WA LIGI

Gomes alisema baada ya hapo, walizungumzia pia mashindano ya ndani wakianza na Kombe la ASFC, ambalo wanatakiwa kulichukua kama ilivyokuwa msimu uliopita, kisha walifanya tathmini ya pamoja katika ligi tangu pale alipoanza kazi hadi sasa na changamoto alizokutana nazo.

“Palipokuwa na changamoto katika ligi tulipata njia ya kusuluhisha na msimu ujao tutakuwa bora zaidi na pale tulipofanya vizuri tumeamua kuweka nguvu kwa pamoja ili kuwa bora zaidi,” alisema Gomes aliyeanza kuinoa Simba Januari 24, mwaka huu.
“Tulikubaliana malengo makuu ya timu ni kuchukua taji hilo la ligi katika kila msimu ili kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika na huko tuna malengo mengine makubwa zaidi.

“Ukiangalia namna ya kikosi chetu kilivyo na maboresha ambayo tutayafanya nilimuahidi hilo linawezekana na katika kuonyesha ukubwa wa Simba tulikubaliana katika kila shindano la ndani tupambane tutakavyoweza ili kuwa mabingwa pia.”

FAINALI YA MABINGWA
Juu ya michuano ijayo ya Afrika, Gomes alisema kama alivyoeleza awali katika kikao hicho na Mo Dewji, walikubaliana kufikia malengo makubwa ya kucheza fainali za Afrika ikiwezekana kuchukua taji hilo kabisa baada ya msimu huu kukwamia robo fainali mbele ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Gomes alisema ukiangalia mwenendo wa timu yao ulivyo katika mashindano hayo alikubaliana na Mo kuwa, katika kipindi ambacho kisizidi miaka mitano wafikie lengo moja kati ya hilo.

Anasema mbele yake alikubali kuwa ataandaa timu kulingana na wachezaji wake walivyo ili ndani ya miaka hiyo mitano Simba iweze kucheza fainali hiyo kubwa kwa ngazi ya klabu.

“Kama Simba ikifanikiwa kucheza fainali maana yake ni mafanikio makubwa lakini inaweza kutokea tunashinda mchezo huo mmoja na tukawa mabingwa wa kombe hilo.”

USAJILI
Juu ya usajili, Gomes alisema Simba itasajili mchezaji mmoja wa kigeni ambaye atakuja kuchukua nafasi ya Perfect Chikwende atakayetolewa kwa mkopo, lakini akiwa tayari hesabu zake zikinasa wazawa watatu wamenaswa.

Alisema kuna wachezaji wazuri wazawa ambao tutakuwa nao kulingana na mapungufu yao klwa msimu huu, lakini kuna nyota mwingine wa kigeni atakayetua Msimbazi.

“Mwenyekiti amenihakikishia kuwa tutapata mchezaji kweli huyo wa kigeni kulingana na shida ambayo ipo katika kikosi lakini hata wale wazawa watakuwa wenye kuongeza uimara wa kikosi,” alisema Gomes.

Japo Gomes aligoma kutaja wachezaji waliowajadili kwenye kikao chake na Mo, lakini Mwanaspoti linafahamu wazawa watatu walionaswa ni; beki Israel Patrick Mwenda kutoka KMC, kipa Jeremia Kisubi wa Tanzania Prisons na winga Jimson Mwanuke wa Gwambina, huku kwa nyota wa kigeni jina la Moses Phiri likitajwa mapema kutua Msimbazi kutoka Zambia.

VIONGOZI WAGUSWA
Gomes alidokeza pia yeye na Mo walipata nafasi ya kujadili namna gani anapata ushirikiano na viongozi wote wa Simba ambao hufanya nao kazi mara kwa mara na pia kukutana nao deile kazini.

Alisema alimueleza Mo Dewji amewahi kufundisha timu nyingi Afrika, ila Simba ni moja yenye viongozi wanaofuatilia katika kila maeneo na wepesi kutoa msaada pale anapokuwa na shida.

“Kiukweli napata ushirikiano wote kutoka kwa viongozi wa Simba tangu siku niliyofika kuanzia kazi hapa hadi sasa naendelea na majukumu yangu bila ya kuwa na shida yoyote,” alisema Gomes na kuongeza;

“Viongozi wote wa Simba kila mmoja kwa nafasi yake amekuwa akinipa ushirikiano hata pale ninapo washauri jambo wamekuwa wakilifanyia kazi kwa uharaka.”

KUIJENGA SIMBA
Gomes alimalizia kwa kufafanua kuwa, pia alipata nafasi ya kumshauri Mo Dewji katika maeneo ambayo anatakiwa kuyafanya ili kuendelea kuitengeneza Simba na kupiga hatua katika maeneo mbalimbali.

Alisema katika kumshauri kwake waligusia masuala ya timu ya vijana, kuboresha maeneo kama ya miondombinu pamoja na mambo mengine ya siri ambayo Mo Dewji ameyapokea.

“Natamani kuweka alama yangu hapa Simba katika kufikia mafanikio makubwa ya kuchukua mataji ya ndani na nje ya nchi lakini mafanikio yao yaendani na miondombinu yao,” alisema Gomes na kuongezea;

“Mwenyekiti amesema yupo tayari kuijenga Simba katika maeneo yote ya msingi jambo ambalo hata gharama za uendeshaji zitapungua pamoja na kujitoa katika maeneo yote ili klabu iendelee kuwa kubwa.

“Nimetamani kuyaongeza hayo kupitia Mwanaspoti kwani ni mambo makubwa ambayo klabu ya Simba inayo na mengine imepanga kuyafikia ili timu yao iweze kufikia hadhi ya klabu kubwa Afrika kama Al Ahly, TP Mazembe, Wydad Casablanca na nyinginezo nyingi.”

Credit: Mwananchi
 
Hii imechelewa wapi Mkuu? Maana Simba na Coast tayari matokeo yanajulikana.
 
Alisema katika kumshauri kwake waligusia masuala ya timu ya vijana, kuboresha maeneo kama ya miondombinu pamoja na mambo mengine ya siri ambayo Mo Dewji ameyapokea.
Katika yote waliyoongelea points muhimu zipo eneo hili. Ni eneo ambalo wafadhili wengi wa masuala ya michezo wanapenda kusikia ingawa utekelezaji wake unakuwa zero.
 
Back
Top Bottom