Mdau mmoja wa JamiiForums ameelezea kuwa watu wanaokunywa pombe kupita kiasi (Ulevi uliopindukia) wakiacha ghafla matumizi ya pombe wanaweza kufa.
Mdau huyu anaeleza kuwa pombe hupunguza utendaji wa akili kama yalivyo madawa mengine ya kulevya, pia huleta uraibu na utegemezi.
Amewashauri walevi sugu kuacha pombe taratibu ili wasipatwe na athari kubwa kwenye afya, ikiwemo kifo kutokana na kifafa.
Madai haya ni sahihi?
Amewashauri walevi sugu kuacha pombe taratibu ili wasipatwe na athari kubwa kwenye afya, ikiwemo kifo kutokana na kifafa.
Madai haya ni sahihi?
- Tunachokijua
- Kama ilivyo kwa aina nyingine za uraibu, unywaji wa pombe uliopindukia husababisha mabadiliko ya kemikali kwenye ubongo ambayo huleta utegemezi kwa mhusika. Ubongo unapotengeneza uraibu na utegemezi wa pombe, inakuwa karibu haiwezekani kwa mtumiaji kufanya kazi bila pombe.
Kwa mlevi, kunywa pombe kunaweza kuonekana kuwa muhimu kwa maisha yake ya kila siku kuliko kitu kingine chochote. Kusitisha ghafla unywaji huathiri ubongo kwa kusababisha dalili zenye maudhi madogo yanayovumilika au makali kiasi cha kuua.
Baadhi ya dalili za kujiondoa kwenye matumizi ya pombe (Alcohol Withdrawal Symptoms) ni kutetemeka, kukosa usingizi, kichefuchefu na kutapika, kukosa hamu ya kula, kuweweseka na maumivu makali ya kichwa. Kwa mujibu wa tafiti, 3% ya watu wanaositisha ghafla matumizi ya pombe hupatwa na aina kali ya kifafa inayoweza kuwa hatari kwa afya, hata kuua.
Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya kuaminika, ikiwemo taasisi ya IARC, JamiiForums imebaini kuwa usitishaji wa ghafla wa matumizi ya pombe kwa walevi wa kupindukia unaweza kuwaletea changamoto nyingi kwa afya, ikiwemo kifo, kutokana na kifafa kisichotibika kirahisi.
Katika hatua za kusitisha matumizi ya pombe, wataalam wa afya hushauri jambo hili lifanyie taratibu ili kuepusha maudhi na dalili kubwa zinazoweza kutokea.
Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na Vyakula ya Marekani (FDA) imepitisha matumizi ya dawa tatu zinazoweza kumsaidia mtu kusitisha matumizi ya pombe;
- Acamprosate husaidia kupunguza ukubwa wa maudhi baada ya kusitisha matumizi.
- Disulfiram husababisha maudhi kwa mhusika hasa kiungulia na kutapika ikiwa atakunywa pombe au hata kusikia harufu yake. Hii humfanya aanze kuiepuka.
- Naltrexone husaidia kupunguza hamu ya kunywa.