John Mnyika
JF-Expert Member
- Jun 16, 2006
- 713
- 1,241
Tamko la Vijana wa CHADEMA dhidi ya kauli ya Waziri wa Fedha Mhe.
Mustafa Mkulo kuhusu fedha za EPA
Mustafa Mkulo kuhusu fedha za EPA
Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tumeshtushwa na kusikitishwa sana na kauli iliyotolewa na Waziri wa Fedha Mhe. Mustafa Mkulo kama ilivyonukuliwa na vyombo kadhaa vya habari (Gazeti la Mwananchi na Habari Leo, Jumamosi tarehe 21.06.2008), tunanukuu;
Mkulo asema fedha za epa hazikuwa za Serikali wala BoT
Mkulo asema fedha za epa hazikuwa za Serikali wala BoT
Tunalazimika kutoa tamko hili kwa umma wa Watanzania na Serikali yake tukiamini kuwa kauli hii si ya kupuuzwa, si msimamo binafsi wa Mhe.Mkulo bali ni msimamo wa serikali kwa kuwa imetolewa na serikali kupitia Waziri wake wa Fedha. Kwa mantiki yake kauli hii inamaanisha kuwa;
- Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) hakustahili kukagua akaunti hiyo. Kwa hiyo alikagua kwa makosa.
- Fedha hizo zilikuwa za wafanya biashara na ziliingizwa BOT kwa makosa na sasa serikali imeamua kuwarudishia wafanya biashara hao fedha zao.
- Si lazima kwa fedha hizi kurejeshwa kwa kuwa si za serikali wala BOT.
Kauli ya Mhe.Mkulo kuwa fedha za EPA si za serikali wala BOT inaashiria mambo yafuatayo kwa umma wa Watanzania;
- Kauli hii ni moja ya vielelezo vya kuendelea kutawaliwa na serikali isiyokuwa makini hasa katika Wizara ya Fedha, licha ya Mhe. Raisi Kikwete kufanya mabadiliko kadhaa ya baraza lake la Mawaziri. Ukosefu wa umakini wa serikali katika suala hili kwanza unajibainisha kwa viongozi wa serikali moja na ya chama kimoja (CCM) kutofautiana katika kauli zao. Mhe. Raisi Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wamewahi kutamka moja kwa moja na kutoa kauli kadhaa ambazo kimantiki zilibainisha kuwa Fedha za EPA ni Fedha za Umma chini ya usimamizi wa Serikali lakini Mhe. Waziri Mkulo kana kwamba Wizara yake si sehemu ya serikali hii alidiriki kutoa kauli tofauti na viongozi wenzake. Waziri huyu huyu hivi karibuni akishirikiana na wafanyakazi wa Wizara yake aliandaa na kusoma hotuba ya Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2008/2009 ikiwa na mapungufu makubwa ya kitakimwu na akatoa hoja ya kulitaka Bunge liipitishe. Ukosefu huu wa umakini wa serikali hasa katika uendeshaji wa Wizara nyeti ya Fedha unadhihirisha kuwa hakuna tofauti yoyote kati ya baraza la mawaziri liliundwa mara tu ya uchaguzi na hili lililofanyiwa mabadiliko na Raisi ya Kikwete hivi karibuni. Vijana wa CHADEMA tunasikitika sana kuona kuwa Mhe. Raisi Kikwete, huu ukiwa ni mwaka wa tatu wa utawala wake, bado amekuwa akijifunza jinsi ya kuunda serikali yake bila mafanikio. Vijana wa CHADEMA tunamshauri tena Mhe. Raisi Kikwete kulitazama upya baraza lake jipya la mawaziri kwani bado lina idadi kubwa ya mawaziri wasiomakini na wanaohusika katika kashfa mbalimbali za ufisadi.
Tunamtaka Mhe.Raisi asione haya kulifanyie tena mabadiliko baraza hili la mawaziri, bali azingatie haja kupata mawaziri bora ambao angalau watamwezesha kuanza kutekeleza ahadi yake ya kuleta maisha bora kwa kila mtanzania kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010. - Kauli ya Mhe. Mkulo kwamba fedha za EPA si fedha za serikali wala BOT, ni kauli yenye kuwakatisha tamaa Watanzania kuwa serikali ya CCM inafanya usanii katika kushughulikia urejeshwaji wa fedha za EPA na kuwachukulia hatua waliohusika. Vijana wa CHADEMA tunasisitiza kuwa fedha za EPA ni fedha za umma na tunawataka waheshimiwa wabunge wote bila kujali itikadi zao waendelee kuibana serikali si tu katika kuhakikisha fedha za EPA zinarejeshwa bali pia katika kuhakikisha waliozichukua wanatajwa na kuchukuliwa hatua kali.
I. Commodity Import Support (CIS)
Kunako miaka ya 1978/1980 na kuendelea nchi yetu ilikuwa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni.Uhaba huo ulisababisha wafanya biashara waliokuwa wakiagiza bidhaa kutoka nje kushindwa kulipia bidhaa hizo. Hivyo nchi ikajikuta ina deni kubwa kutokana na bidhaa ambazo hazijalipiwa.Katika kulinda heshima ya nchi yetu serikali iliomba msaada/mkopo kutoka kwa wafadhili wa nje ili zipatikane fedha za kigeni kulipia mrundikano wa madeni.
Baada ya kupata msaada/mkopo serikali ilianzisha mfuko uitwao COMMODITY IMPORT SUPPORT (CIS), ambapo wafanya biashara waliokuwa wanadaiwa bidhaa walizoagiza kutoka nje walikopeshwa na kulipia deni kwa fedha za kigeni. Masharti yalikuwa kwamba wafanya biashara hao watakuwa wanalipa kwa Shillingi ya Tanzania wakati serikali ikiwalipia kwa fedha za kigeni kwa MKOPO kutoka mfuko huo wa CIS.
II. External Payment Arrears (EPA)
Ili kusimamia vizuri fedha hizo za CIS na kwa kuwa wafanya biashara wengi walikuwa wateja wa National Bank of Commerce (NBC), Benki kuu (BOT) iliagiza NBC ifungue akaunti iitwayo EXTERNAL PAYMENT ARREARS (EPA) kwa ajili ya kukusanya marejesho yaliyokuwa yakifanywa na waliokopa kwenye mfuko wa CIS. Marejesho hayo yalikuwa yakitumwa benki kuu kila mwezi ili kwenda kufidia kwenye mfuko waliokopa. NBC ilisimamia akaunti hiyo ya EPA kwa muda lakini baadae ilifungwa na kuhamishiwa BOT.
Kwa lugha ya uhasibu akaunti ya EPA ilikuwa ni SUSPENSE ACCOUNT kwa maana kwamba ni akaunti inayotumika kwa muda ili baada ya kukamilisha vipengere fulani fedha hizo zitaingizwa katika akaunti sahihi inayohusika.
Kwa mantiki hiyo fedha za EPA kama Suspense Account zilitakiwa zirudishwe kufidia kwenye mfuko zilikotoka/kopwa.
III. Debt Conversion Program (DCP)
Utaratibu uliobuniwa na serikali kuwakopesha wafanya biashara fedha za kigeni kwa ajili ya kulipia bidhaa zao chini ya mpango wa Commodity Import Support (CIS) na baadaye kuwataka warejeshe kwa Shillingi ya Tanzania kupitia akaunti ya External Payment Arrears (EPA) ulikuwa mpango mahususi wa kuwasaidia wafanya biashara wasikwamishwe katika uagizaji wa bidhaa kutoka nje.
Hata hivyo pamoja na ukweli kwamba wafanya biashara waliwezeshwa kupunguza madeni yao bado serikali ilibakia na mzigo wa madeni kwa wafadhili waliotukopesha chini ya mpango wa CIS. Hivyo sambamba na mpango wa CIS na EPA ilibidi serikali ibuni mkakati au mpango mwingine wa kulipa madeni yake ya nje. Ndipo ulipobuniwa mpango uitwao DEBT CONVERSION PROGRAM (DCP).
Chini ya mpango wa DCP serikali iliwataka WAFANYA BIASHARA WENYE FEDHA ZA KIGENI NDANI NA NJE YA NCHI KUNUNUA MADENI hayo kwa fedha za kigeni na serikali (BOT) kuwalipa kwa shillingi ya Tanzania.
Iwapo kwa huruma ya wafadhili deni lililotokana na mfuko wa CIS limefutwa, Mh. Mkulo hawezi kutuambia kwamba fedha za marejesho kwenye akaunti ya EPA hazina mwenyewe kwa sababu wafadhili wamekwisha kutufutia deni. Taratibu za uhasibu haziendi hivyo.
Iwapo wafadhili wametusamehe deni basi hapana budi fedha hizo ziingizwe kwenye vitabu vya serikali kama mapato ili zipangiwe matumizi.Vinginevyo zinaweza kuingizwa Kwenye vitabu kama malimbikizo (General Reserve). Hivyo siyo sahihi kabisa kusema kwamba fedha za EPA hazina mwenyewe.
Umuhimu wa kulinganisha hesabu za EPA na CIS (Reconciliation of accounts)
Pamoja na msaada mkubwa uliotolewa na serikali kuwakopesha wafanya biashara ili waweze kulipia bidhaa zao kwa fedha za kigeni na kuwataka walipe kwa shillingi ya Tanzania kuna wengine waliokopeshwa chini ya mpango huo lakini hadi leo hawaja fanya marejesho kwa shillingi ya Tanzania kama walivyotakiwa. Pia kuna wengine waliorejesha na kupitishia kwenye akaunti ya EPA kama ilivyotakiwa lakini baada ya kugundua kwamba fedha hizo bado zimelala tu katika Suspense Account ya BOT walishirikiana na wajanja wachache na kudai kuwa fedha hizo hazina wenyewe na hivyo wakaweza kuchota kiasi cha shs. 133bn.
Wakati wale waliochota kwenye EPA wamejulikana wapo wale ambao deni lao kwenye mfuko wa CIS hatujaambiwa ni kina nani na wanadaiwa kiasi gani.
Hapana budi kumwomba tena Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) afanye kazi ya ziada ya kulinganisha hesabu hizo na kutuambia ni kina nani bado wanadaiwa .
Inahitajika kauli ya Serikali kuondoa utata.
Pia iundwe Kamati teule/Tume ya Bunge kuchunguza fedha za CIS
Vijana wa CHADEMA tunataka serikali kupitia kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu (CAG) ituambie kama kweli fedha za EPA si za serikali au BOT kama anavyodai Mhe. Mkulo. Kwa kuwa haijaundwa tume/kamati ya kuchunguza fedha za Commodity Import Support (CIS) ni vyema sasa ikaundwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza fedha hizo zilivyotumika ili kubaini wale wote ambao bado wanadaiwa. Tunahangaika kutafuta fedha kufidia nakisi kwenye bajeti wakati fedha ziko hapa hapa karibu mifukoni mwa mafisadi wachache.
Kutokana na mfano mzuri ulioonyeshwa na kamati ya Mwakyembe inaonekana ni Tume/kamati Teule ya Bunge pekee ndiyo inaweza kufanya uchunguzi wa kuridhisha kwenye jambo zito kama hili. Tume nyingi zimewahi kuundwa kufuatilia mambo mbali mbali lakini taarifa za tume zimekuwa ni siri ambapo wananchi hawajulishwi matokeo yake. Tunawataarifu wadau kuwa kuna nyaraka BOT zinazoeleza taratibu zote za CIS, EPA na DCP hivyo ni uongo mkubwa kwa Waziri Mkulo kuzidi kuupotosha umma na kusizitiza kwamba fedha za EPA siyo za serikali au BOT.
Vijana wa CHADEMA tunamtaka Waziri Mkulo ajiuzulu haraka iwezekanavyo kwa kulidanganya Bunge na umma wa Watanzania na kuonesha ukosefu mkubwa wa umakini katika kuiwakilisha serikali kwenye kikao cha Bunge cha Bajeti kinachoendelea.
Mwisho, tunawataka vijana wote wa Tanzania kujiunga na harakati za vijana wa CHADEMA katika kutetea haki na maendeleo ya vijana wa kitanzania na hasa kuhakikisha kuwa suala la EPA na ufisadi kwa ujumla vinashughulikiwa ipasavyo. Haiwezekani vijana wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga kukosa mitaji, na vijana wa vyuo vikuu kukosa mikopo huku mabilioni ya umma yakiwa yameachwa mikononi mwa wachache huku serikali ikiendelea kusisitiza kwamba fedha hizo si za umma.
Kwa kuwa imebainika fedha zimetolewa toka kwenye EPA kwa kutumia nyaraka za kughushi; huo sio wakati wa kujiuliza fedha ni za nani, ni wakati wa kuwakamata wezi walioiba fedha za EPA na kuhakikisha fedha zinarejeshwa katika mkondo unaostahili. Waziri Mkullo asitafute kisingizio cha kukwepa ama kuchelewa kuwachukulia hatua watuhumiwa wa ufisadi wa BOT.
Imetolewa na;
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa
25/06/2008
Mjadala mwema
JJ