Mithali 31
² Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu?
³ Usiwape wanawake nguvu zako; Wala moyo wako usiwape wale wawaharibuo wafalme.
☆ Mwanamume umeonywa juu ya kumpa mamlaka yako mkeo, kwani wanawake huendeshwa na hisia zaidi na hivyo ni rahisi kupotoka na kupotosha njia. Hapo inaposema moyo wako, kimsingi ni njia zako ndio tafsiri halisi, hivyo usimwache mwanamke akuongoze njia. Wewe ndio umepewa mamlaka yote ya uongozi wa familia.
¹⁰ Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani.
☆ Hizi ndizo sifa za mke mwema: thamani yake yapita thamani ya rubi. Neno marijjani ni madini ya rubi. Tena Ayubu 28:18 inasema hekima inapita thamani ya rubi, hivyo mke mwema ni mwenye hekima kuu.
¹¹ Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.
¹² Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake.
☆ Sifa kuu ya mke mwema ni UAMINIFU. Neno hili ni pana sana, linajumuisha uaminifu kwenye mahusiano (asiwe mchepukaji), uaminifu kwenye matunzo ya familia (awe mlezi bora wa baba na watoto), uaminifu kwenye mali (asiwe mwizi, mfano anajenga kwa siri) n.k. Mambo haya yatafanya moyo wa mwanamume umwamini. Tena mke mwema humtendea mema mumewe, si mwenye kumteta kwa marafiki, hamwendei kwa waganga, hatoki nje ya ndoa n.k.
¹³ Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo.
¹⁴ Afanana na merikebu za biashara; Huleta chakula chake kutoka mbali.
¹⁵ Tena huamka, kabla haujaisha usiku; Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; Na wajakazi wake sehemu zao.
☆ Hufanya kazi za mikono kama ufumaji nguo, ususi n.k. na kwa mapato yake yatokayo mbali, yaani yatokanayo na kujishughulisha kwake kuliko kusubiri tiho pesa za mahawara. Huweza kuchangia uendeshaji wa familia kwa mapato hayo. Mke mwema anajua eneo lake la majukumu ni malezi ya familia, huamka asubuhi mapema kupanga majukumu kwa wasaidizi wake, tena yeye ndiye mpishi wa vyakula. Wanaume wengi siku hizi wanaumizwa na mahouse girl kwenye vyakula, uchawi unawekwa humo, huku wake zao wakiwa busy kuchat , instagram na facebook. Ni aibu house girl kuwa mpishi mkuu wa familia huku mke amejinyoosha kwenye kochi tu. Unaoa msaidizi wa kukusaidia mambo ya nyumbani, halafu unaajiri mfanyakazi wa kuyatekeleza hayo hayo.
¹⁶ Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.
¹⁷ Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi; Hutia mikono yake nguvu.
¹⁸ Huona kama bidhaa yake ina faida; Taa yake haizimiki usiku.
¹⁹ Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia.
☆ Mke mwema hufanya shughuli za kuleta kipato cha familia, kazi zake ni zile zisizomtenga na familia. Atafanya kazi za mikono kama ufumaji, atapata mapato na kuyatumia kufungua biashara nyingine, mfano shamba, ataajiri wafanyakazi huko (kwa mapato ya mikono yake). Kama ni biashara ataweka wafanyakazi, yeye atapita kukusanya mapato, sio kushinda huko saa 12 asubuhi mpaka saa 4 usiku.
²⁰ Huwakunjulia maskini mikono yake; Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake.
²¹ Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; Maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu.
²² Hujifanyia mazulia ya urembo; Mavazi yake ni kitani safi na urujuani.
☆ Ni mtu mwenye kusaidia maskini. Watu wa nyumbani mwake huvikwa mavazi yenye thamani kubwa (nguo nyekundu - scarlet - mavazi ya matajiri na wafalme zamani za kale)
²³ Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi.
²⁴ Hufanya nguo za kitani na kuziuza; Huwapa wafanya biashara mishipi.
☆ Sifa njema za mke humwinua mumewe, hupata heshima kati ya wazee wa eneo lake. Afanyapo kazi za mikono yake huwauzia wafanya biashara waka peleka sehemu tofauti.
²⁵ Nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake; Anaucheka wakati ujao.
²⁶ Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake.
☆ Mke mwema hujiandaa kwa wakati ujao, hujiwekea akiba. Amejaa hekina na ni mwema kwa mumewe na watu wa nyumbani mwake
²⁷ Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; Wala hali chakula cha uvivu.
²⁸ Wanawe huondoka na kumwita heri; Mumewe naye humsifu, na kusema,
²⁹ Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.
☆ Familia yote humpenda na kumsifu daima. Mumewe hukosa mwanamke wa kumlinganisha naye, hivyo hawezi ona haja ya kuchepuka kwa sababu moyo wake umetekwa na mkewe.
³⁰ Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa.
³¹ Mpe mapato ya mikono yake, Na matendo yake yamsifu malangoni.
☆ Mke mwema hapimwi kwa uzuri, kwani huu ni wa muda tu unapotea. Mwanamke mwenye hofu ya Mungu ndiye atakayesifiwa, kwa sababu sifa zote hizo huzipati kwa mke asiye na hofu ya Mungu. Kumcha bwana ni chanzo cha maarifa. Mke mwema husifiwa kwa matendo yake na si sura yake.