Mkapa anataka azomewe vipi zaidi?

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,148
Mkapa anataka azomewe vipi zaidi?






HIVI karibuni jina la Mkapa lilirejea kupamba tena kurasa za magazeti yetu kadhaa nchini.

Mara ya kwanza ilikuwa ni kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 33 ya CCM huko Singida ambako Spika Samwel Sitta alinukuliwa akiusifia utawala wa awamu ya tatu wa Ben Mkapa.

Sifa hizo kemkem zililifanya gazeti moja nchini kuibuka na kichwa cha habari kilichosomeka hivi: Sitta ambeba Mkapa.

Sikuitilia sana maanani kauli hiyo ya Sitta ya huko Singida; kwa sababu siku ya pili yake Sitta mwenyewe alitoa taarifa nyingine ya ufafanuzi kwamba hambebi Mkapa, na kwamba mwandishi aliyeandika habari zile alimnukuu vibaya.

Nikiri kwamba nilishusha pumzi siku iliyofuata niliposoma habari za Sitta za ufafanuzi wa kauli yake hiyo ya Singida. Hiyo ni kwa sababu, katika hali ya kawaida, nilidhani Sitta angekuwa ni mtu wa mwisho Tanzania kummwagia sifa kemkem Mkapa.

Nasema hivyo kwa sababu katika kipindi cha zaidi ya miaka minne ambacho Sitta amekuwa Spika, Bunge lake lilitawaliwa zaidi na mijadala ya ufisadi uliotendwa wakati wa kipindi cha utawala wa Mkapa.

Sote tunajua kwamba katika miaka ya karibuni hakuna kipindi ambapo Bunge letu lilitawaliwa na mijadala kuhusu ufisadi kama katika kipindi hiki cha Spika Sitta. Na kama nilivyosema mwanzo, ufisadi mwingi unaojadiliwa ni ule uliotendwa wakati wa utawala wa Mkapa.

Ndiyo maana ingeshangaza kama Spika wa Bunge ambalo limetawaliwa na mijadala ya ufisadi mkubwa uliotendwa na utawala wa Mkapa amsifu tena Mkapa huyo huyo kwamba alikuwa kiongozi mahiri.

Hata kama wanasiasa wetu ni watu vigeugeu na wenye hulka ya kusema wasichokiamini, siamini Spika Sitta angekwenda that low. Ungekuwa unafiki wa kiwango cha juu kabisa!

Kwa hiyo, kama nilivyosema mwanzo, sikulitilia sana maanani tukio hilo la Singida kama ambavyo nimelitilia maanani tukio la pili la huko Kilolo ambako Mkapa alitamba kwamba haogopi kuzomewa na wananchi!



"Mr Clean", Benjamin Mkapa
Akihutubia wafanyakazi wa Hospitali Teule ya Kilolo huko Iringa, Jumatano iliyopita, Mkapa (“Mr Clean”) alitamba kwamba haogopi kuzomewa na wananchi. Alinukuliwa zaidi akisema hivi: “Hawa jamaa zangu wanahabari wamekuwa wakiandika kuwa sijitokezi kuzungumza kwa kuwa naogopa kuzomewa. Siogopi kuzomewa mimi… hivi mmeona nani kanizomea leo hapa?”

Na si hivyo tu; bali “Mr Clean” aliendelea kusema kwamba haonekani mara kwa mara hadharani kwa kuwa yuko busy na masuala ya kimataifa.

Mkapa hakueleza ni masuala gani hayo ya kimataifa yanayomfanya awe busy kiasi cha kutokuwa na muda na nchi yake Tanzania, lakini nisema tu kwamba kauli yake hiyo ilinikumbusha kauli iliyopata kutolewa na Rais wa zamani wa Marekani, George H.W. Bush, Julai 1988.

Bush, akiwa amebanwa kwa maswali mazito na mwandishi mmoja wakati akijiandaa kuingia kwenye helkopta yake, alisingizia kwamba kelele ya helkopta ilikuwa ikimfanya asiyasikie vyema maswali ya mwandishi yule wa habari; japo kabla ya kuulizwa maswali hayo walikuwa wakisikilizana vyema tu!

Hilo lilimfanya Rais huyo, baadaye, akejeliwe na Wamarekani kwa kijembe kile maarufu kilichoanzishwa Julai 18, 1988 na mwanamama Ann Richards cha; “he cannot hear our questions over the noise of the helicopter” (hawezi kuyasikia maswali yetu kwa sababu ya kelele ya helkopta).

Kwa maneno mengine, Mkapa naye, kwa kauli yake mwenyewe ya huko Kilolo, hawezi kutusikiliza kwa sababu yuko busy na masuala ya kimataifa! Mwenzake alisingizia kelele za helkopta, yeye anasingizia u-busy na masuala ya kimataifa!

Vyovyote vile; kilichogusa fikra zangu si kisingizio hicho cha Mkapa cha kutoonekana hadharani mara kwa mara; bali kutamba kwake kwamba haogopi kuzomewa na wananchi.

Kabla ya kujadili tambo yake hiyo, nikiri kwanza kwamba kuna kitu kuhusu Mkapa ambacho nimeshindwa kukielewa. Kitu hicho ni ile hulka yake ya kutoa kauli nzito nzito zinazohusu urais wake akiwa mikoani (vijijini).

Sijui ni kwa nini (kwa mfano) aliamua kuitoa kauli hiyo nzito ya kutokuogopa kuzomewa akiwa huko Kilolo na si Dar es Salaam ambako kuna vyombo vingi vya habari.

Wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka kwamba Mkapa aliwahi kutoa kauli kama hiyo (ya defiancy) akiwa kijijini kwake Lupaso (Masasi) na si Dar es Salaam.

Sielewi vilevile ni kwa nini Mkapa hupendelea pia kutumia makanisa kutoa kauli hizo za defiancy dhidi ya wanaomshutumu kwamba aliulea ufisadi mkubwa akiwa Ikulu.

Kwa kuwa hapendi kufanya mahojiano maalumu na chombo chochote cha habari hapa nchini, pengine hatutakuja kuelewa ni kwanini aliamua kutumia makanisa au safari za huko vijijini kutoa kauli hizo nzito za defiancy.

Vyovyote vile; kauli yake hiyo ya hivi karibuni, huko Kilolo, kwamba haogapi kuzomewa, inafikirisha. Je, ni kweli kwamba Mkapa haogopi kuzomewa au anaogopa kuzomewa, na ndiyo maana anajihami mapema kwa kutamba hivyo?

Kuna aya moja katika Biblia inayosema kwamba kinywa hunena yale yaujazayo moyo wa mtu. Kama hivyo ndivyo, basi, Mkapa anawatambia wananchi kwamba haogopi kuzomewa kwa sababu ndani ya moyo wake kuna hofu kubwa ya kuzomewa na wananchi.

Hata hivyo, huwa najiuliza moyoni; hivi Mkapa anataka kuzomewa vipi tena zaidi? Nauliza hivyo kwa sababu, kwa mtazamo wangu, kudhihirika huku kwa sasa kwa ufisadi wa serikali yake, ni ‘kuzomewa’ tosha kunakochoma zaidi moyoni kuliko pengine kuzomewa kwa sauti na kikundi cha watu mahali fulani nchini!

Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba; ni kweli Mkapa hazomewi kwa sauti, na yeye haogopi kuzomewa kwa sauti, lakini kila siku ya Mungu watuhumiwa wale wa ufisadi wa EPA (wakiwemo mawaziri wake wawili) wanapofikishwa mahakamani, Mkapa anazisikia moyoni mwake sauti za ‘kuzomewa’; japo hakuna mtu anayeonekana kwa macho akimzomea!

Uingereza inapokiri kwamba mauzo yale ya rada kwa Tanzania yalikuwa ya kifisadi na Watanzania wanapokumbuka kwamba Waziri wa Uingereza, Claire Short alimtahadharisha Mkapa kuhusu ufisadi huo lakini akapuuzwa, Mkapa ‘anazomewa’ kimya kimya japo haoni wanaomzomea!

Nimedokozwa kwamba kuna asasi moja hapa nchini inapanga kumtuza Mama Claire Short kwa kuitetea mno Tanzania wakati wa mauzo yale ya kifisadi ya rada. Kama hilo likitokea, Mkapa atakuwa ‘amezomewa’ tena kimya kimya.

Isitoshe, Watanzania wanapofahamishwa kwamba Mkapa alinunua mgodi wa umma wa Kiwira wakati akiwa Ikulu, na kwamba sasa Serikali ya Rais Kikwete imeurejesha tena mgodi huo mikononi mwa serikali, huko ni kuzomewa ‘kimya kimya’ kwa Mkapa.

Niulize tena: Mkapa anataka azomewe vipi tena zaidi? Ni kuzomewa kupi kunakopaswa kumsononesha Mkapa? Ni huku kunakohusu matendo ya ufisadi wa serikali yake kuanikwa hadharani na nchi kama Uingereza, au ni huku kwa kelele na matusi ya vikundi fulani vya watu?

Kama ni huko kwa kwanza, basi, Mkapa ‘anazomewa’ kimya kimya kila kina Yona na Mramba wanapofikishwa kortini, na ‘kuzomewa’ huko kimya kimya kunaitafuna nafsi yake! Vivyo hivyo kila Watanzania wanapokumbushia skandali za rada, Meremeta, Twin Towers, Kiwira nk.

Nihitimishe kwa kusema kwamba Mkapa anaungua moto kimya kimya (man on fire) kila matendo yake hovyo aliyoyafanya akiwa Ikulu yanapoanikwa hadharani.

Nimshauri (kama anasikiliza; maana kuna kelele za helkopta na u-busy wa masuala ya kimataifa!) kwamba namna ya kuuzima moto huo si kukimbilia vijijini (Lupaso, Kilolo nk) au makanisani kutoa kauli hizo za defiancy.

Anaweza kuuzima tu moto huo kwa kuitisha Press Conference mjini Dar es Salaam na kuwaeleza Watanzania ukweli wote kuhusu EPA, Kiwira, rada, Meremeta, mauzo ya NBC, uuzaji wa nyumba za serikali nk, na kuwaomba wamsamehe kwa yale mabaya aliyoyafanya.

Nina hakika Watanzania watamsamehe tu; maana kuna mengi mazuri aliyoyafanya kama vile kuanzisha TRA, kujenga barabara kwa pesa zetu wenyewe, kuanzisha TASAF na hata mradi wa maji wa Ziwa Victoria nk.

Nisisitize kwamba kuomba msamaha na kuonyesha remorse (majuto) ndiyo njia pekee ya kutuliza fukuto ndani ya kifua cha Mkapa.

Njia hiyo aliyoichagua Mkapa ya kutoa kauli za defiancy wakati Watanzania sasa wanaujua ukweli wote kuhusu (kwa mfano) skandali za Kiwira na rada, hakika haitamsaidia kuuzima moto huo unaoitafuna nafsi yake.
 
Back
Top Bottom