BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,769
- 288,283
Mkapa anashitakika - Dk. Slaa
na Edward Kinabo
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
na Edward Kinabo
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeendelea kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete kumchukulia hatua za kisheria Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kwa kutumia vibaya madaraka yake wakati wa kipindi chake cha uongozi.
Chama hicho kimewataka Watanzania kutokubali kuendelea kupotoshwa na baadhi ya watu wanaokuwa wanadai kuwa Mkapa hawezi kushitakiwa hadi Bunge limwondolee kinga.
CHADEMA imesisitiza kuwa Rais Mkapa, sawa na rais yeyote mstaafu, hana kinga kikatiba inayozuia asishitakiwe dhidi ya makosa aliyoyafanya akiwa madarakani kama mtu binafsi.
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbrod Slaa, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Sokoni, Kawe, Dar es Salaam, juzi, ikiwa ni mfululizo wa mikutano ya kuimarisha chama hicho iliyopewa jina la Operesheni Sangara.
Alisema katiba ya sasa pamoja na kuwa na upungufu, haijatamka kuwa rais mstaafu hawezi kushitakiwa kwa makosa aliyofanya akiwa madarakani kama aliyoyafanya Rais Mkapa wakati wa kipindi chake cha uongozi.
Watanzania mpende kusoma. Mmekuwa mkipotoshwa kwamba Mkapa hawezi kushitakiwa kwa sababu ana kinga ya kikatiba. Tunasema kwa katiba yetu hii hii pamoja na upungufu wake, bado anaweza kushitakiwa kwa makosa aliyofanya akiwa madarakani
Ibara ya 46 ya katiba yetu inafafanua wazi kuwa iwapo kutakuwa na haja ya rais mstaafu kufunguliwa mashitaka kwa makosa aliyofanya, ataandikiwa notisi ya siku 60 kuhusu kusudio la kumfungulia mashitaka kabla ya shauri hilo kupelekwa mahakamani.
Watu wanapotosha kuwa hawezi kushitakiwa hadi aondolewe kinga bungeni. Kinga gani? Katiba yetu haizungumzii chochote kuhusu kinga dhidi ya mtu aliyetenda mambo binafsi wakati akiwa madarakani, alisema Dk. Slaa.
Akifafanua zaidi suala hilo, alisema matendo ambayo rais mstaafu hawezi kufunguliwa kesi hadi aondolewe kinga ni yale tu aliyoyafanya kama rais, katika madaraka yake kisheria kama kuwaachia huru wafungwa, kuidhinisha sheria na masuala mengine yaliyoainishwa kwenye katiba ya nchi.
Masuala kama ya Rais Mkapa kufanya biashara akiwa Ikulu hayahitaji kuondolewa kinga ili ashitakiwe, kwani aliyafanya nje ya mamlaka ya rais aliyopewa.
Rais Mkapa anapaswa kushitakiwa kama watu wengine kwa kutumia Ikulu kujimilikisha hisa katika mgodi wa makaa ya mawe, kupitia kampuni aliyoiunda ya Tan Power Resources Limited na kuiingiza nchi katika hasara.
Dk. Slaa alitoa msimamo huo kupinga kauli za baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hususan kauli ya Mbunge wa Singida, Lazaro Nyalandu, ambaye hivi karibuni kupitia kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na kituo cha TBC1, alisema Mkapa aachwe ampumzike, kwani amelitendea taifa mambo mengi mazuri badala ya kuendelea kuandamwa na wanasiasa.
Akielezea kushangazwa kwake na kauli hiyo, alisema hakutarajia mtu kama mbunge huyo kutoa kauli kama hiyo.
Sikutarajia kumsikia mbunge akitoa kauli kama hiyo. Hivi mtu akifanya mambo mema mia moja lakini akafanya kosa moja, polisi haimkamati? alihoji Dk. Slaa.
Alisema kwa sababu ya Mkapa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lililazimika kuilipa Tan Power Resources Limited sh milioni 300 kwa siku, kiasi alichosema ni kikubwa kuliko kile kilichokuwa kikilipwa kwa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond ya Marekani.
Mkataba wa TANESCO na Richmond kabla ya kuvunjwa ulikuwa ukililazimisha shirika hilo kuilipa Richmond na mrithi wake, Dowans, sh milioni 152 kila siku hata kama hazikuzalisha umeme.
Aliwaambia wananchi hao kuwa familia ya Mkapa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini katika serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, walijimilikisha hisa za asilimia 85 za mgodi wa Kiwira.
Kutokana na Mkapa kuhusika kwa kiasi kikubwa na ufisadi, hatua zinazochukuliwa na serikali za kuwashitaki watuhumiwa wa ufisadi bado haziridhishi, hadi hapo Mkapa na watuhumiwa wengine walioachwa watakapokamatwa na kushitakiwa.
Kama serikali ingesimamia vizuri rasilimali za taifa, Tanzania isingehitaji hata senti moja kutoka nchi wahisani. Ameishutumu serikali ya Rais Kikwete kwa kushindwa kukusanya kodi.
Alisema kama serikali ingekusanya vizuri mapato yatokanayo na sekta ya mifugo na uvuvi, ingeweza kupata mapato ambayo ni karibu mara tatu ya mapato yatokanayo na dhahabu.
Dk. Slaa aliwataka wananchi hao kuiunga mkono CHADEMA na kukiimarisha chama hicho katika maeneo yao, ili kuipatia viongozi wa serikali za mitaa katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu.
Kwa muda mrefu sasa baadhi ya watu wamekuwa wakidai kuwa Rais Mkapa hawezi kushitakiwa kwa makosa anayodaiwa kufanya akiwa madarakani, kwa sababu ana kinga ya kikatiba ya kutoshitakiwa kwa makosa aliyotenda akiwa rais.
Watu hao ambao baadhi yao ni wasomi, wamekuwa wakipendekeza kuwa ikiwa kuna haja ya rais huyo mstaafu kushitakiwa, basi kinachopaswa kufanywa ni Bunge kuondoa kinga hiyo.