WENYE kupanga mikakati ya kivita wanajua, kuwa matokeo ya ushindi wa kivita hufahamika kabla risasi ya kwanza kupigwa. Inahusu matayarisho, malengo, mbinu na mikakati.
Ninapoandika haya, zimebaki siku 30 kabla ya Watanzania wenye sifa za kupiga kura hawajapanga foleni ya kwenda kupiga kura, nchi nzima. Kuchagua madiwani, wabunge na Rais.
Zilipobaki siku 45 kabla ya Oktoba 31, 2010 nikaandika; Kama Uchaguzi Mkuu Ungefanyika leo
. Ilikuwa ni tathmini yangu kutokana na uzoefu wangu wa chaguzi zetu na hali halisi ninayoiona. Nikathubutu kuandika, kuwa mgombea wa kiti cha Urais kutoka Chama Cha Mapinduzi, Bw. Mrisho Jakaya Kikwete, angeibuka kuwa mshindi, na kwamba CCM ingepata wabunge wengi na madiwani. Kwamba Dr Wilbrod Slaa, mgombea urais kutoka CHADEMA angechukua nafasi ya pili.
Kwamba Chadema ingekuwa ya pili pia kwa idadi ya wabunge na madiwani kutoka bara. Nikabainisha, kuwa Profesa Ibrahim Lipumba, mgombea Urais kutoka CUF angechukua nafasi ya tatu.
Leo, zikiwa zimebaki wiki nne kabla ya siku ya uchaguzi naiona hali iliyobadilika katika uwanja huu wa mapambano ya kisiasa. Naiona hali ifuatayo kama uchaguzi ungefanyika kesho.
Mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete angeibuka kuwa mshindi. Profesa Ibrahim Lipumba angeshika nafasi ya pili na huku Dr Wilbroad Slaa angetoka akiwa mshindi wa tatu. Vivyo hivyo, CCM ingetoa wabunge na madiwani wengi ikifuatiwa na CUF na CHADEMA. Kwamba CUF ndio ingekuwa chama kikubwa cha upinzani bungeni na hivyo basi, kutoa kiongozi wa upinzani bungeni kama ilivyokuwa katika bunge lililopita.
Nafahamu kuwa hii ni tathmini itakayowakera baadhi humu mtandaoni, lakini najisikia huru na kuona umuhimu wa kuandika tathmini yangu hii kwa madhumuni ya kuchochea mjadala na kujifunza pia. Ni ukweli, kuwa ukweli mwingine unahuzunisha, lakini ni lazima usemwe. Maana, ukweli ni uhuru pia.
Ni nini basi tafsiri ya nilichokiandika? Kama tungekuwa na uchaguzi mkuu kesho, Jakaya Mrisho Kikwete angeunda Serikali huku yeye na chama chake wakikabiliwa na changamoto kama nilizozielezea katika makala yangu yaliyopita. Kwamba changamoto kubwa itatokana na upinzani utakaokuwa umeongezeka nguvu ndani na nje ya bunge kutokana na ujio wa Dr Slaa kama mgombea Urais katika uchaguzi wa mwaka huu. Na ziada hapo, ni kuibuka kwa CUF bara kama chama chenye wabunge kati ya 10 na 15 na idadi ya kutia moyo ya madiwani.
Huko nyuma nilibainisha, kuwa viashria vya jamii inayotaka mabadiliko vimeshaonekana. CCM itakuwa na mawili ya kuchagua; kuchukua jukumu la kuyaongoza mabadiliko hayo au kusubiri kuzamishwa na mkondo wa maji ya mabadiliko hayo.
Historia ni mwalimu mzuri. Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Oktoba mwaka jana yanaiweka CCM na mgombea wake Urais mahali pazuri zaidi kiushindi kulinganisha na CUF na Chadema. Angalia taarifa hii; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Oktoba mwaka jana ulimalizika kwa kukipa ushindi mnono Chama Cha Mapinduzi. Chama hicho kilipata ushindi wa asilimia 91.71 za kura, kikifuatiwa kwa mbali na CUF iliyopata asilimia 3.94 na Chadema asilimia 2.76.
Katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee, Chama hicho tawala kiliibuka na ushindi mnono kwa kupata viti 402 kati ya 448, sawa na asilimia 91, huku wapinzani wakiambulia viti 40, sawa na asilimia tisa tu. Katika mkoa wa Iringa ninakoishi, CHADEMA, ilifanikiwa kushinda mtaa mmoja wa Kihesa Kilolo B,. Ni kwenye Kata ya Mtwivila Manispaa ya Iringa.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. CCM na mgombea wake Urais waliibuka washindi. Jakaya Kikwete alipata zaidi ya kura milioni 9.2 . Alifuatiwa na Profesa Lipumba aliyepata kura milioni 1.3 na huku mgombea wa CHADEMA , Freeman Mbowe akiambulia kura laki 7.
Pamoja na Profesa Lipumba na chama chake cha CUF kuwa cha pili, hakikupata mbunge wa kuchaguliwa huku CHADEMA ikipata nafasi hiyo ya kuwa na wabunge wa kuchaguliwa zaidi ya watano katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Kwa hali ilivyo kwa sasa, CCM bado wanajivunia:
Kuwa ni chama kikongwe, kikubwa na kilichotawala kwa muda mrefu. Na nilibainisha huko nyuma, kuwa kuna hata wanaokipigia kura chama hicho Kwa mazoea tu. Na katika nchi zetu hizi; kukiondoa chama kilicho madarakani, Chama kilichopigania uhuru au kinachotokana na chama kilichopigania uhuru ni kazi ngumu sana. Kwa anayetaka kufanikiwa katika hilo, anahitaji kwenda ilipo mizizi ya chama hicho. Ni vijijini. Na huko vijijini kwa leo hii chama wanachokijua ni CCM. Naam. Ndio Zimwi wanalolijua.
Mwanakijiji atatembea kwa miguu kilomita kumi kwenda kuhudhuria mkutano wa CCM. Atakwambia amepewa taarifa ya mkutano na Balozi wake wa Nyumba Kumi. Hivyo basi, CCM wanajivunia mtandao wao wa kichama kuanzia ngazi ya Balozi wa Nyumba Kumi, shina, tawi na kuendelea. Na hata mtandao wa Kiserikali.
Nyongeza ya Udhaifu wa CCM:
Kwamba CCM inajivunia K zake tatu; Chama Kikongwe, Kikubwa na Kinachotawala, basi, kuna baadhi ya watendaji ndani ya Chama hicho walioshindwa kusoma alama za nyakati. Wanafanya kazi zao kwa mazoea. Jambo hilo limeigharimu CCM muda na rasilimali katika jitihada za kuziba mashimo. Matokeo ya Uchaguzi wa Oktoba 31 hayataiacha CCM na mfumo mzima wa uendeshaji nchi katika hali iliyozoeleka. Subirini, mtaona.
Mama Salma Kikwete na Ridhiwani Kikwete:
Wawili hawa wamekuwa kiini cha mijadala itakayoendelea huenda hata baada ya uchaguzi kwisha. Tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 uliomwingiza madarakani Jakaya Kikwete, Tanzania imeshuhudia aina mpya ya harakati na kampeni za kisiasa zenye kuhusisha mke wa mgombea na hata wana familia ya karibu kama hili la mke na mwana wa Rais, Ridhiwani Kikwete.
Inaonekana sasa, kuwa zama za First Lady kuwa Mama wa nyumbani Ikulu zimepita. Ni dhahiri, kuwa kwa mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, amenufaika sana na ushiriki wa karibu wa mkewe na mwanawe Ridhiwani. Na si kwa Jakaya Kikwete tu, CCM kama chama, wagombea ubunge wake wananufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa Mama Salma Kikwete na Ridhiwani kwenye kampeni.
Wote wawili, Salma Kikwete na Ridhiwani Kikwete wana mvuto wa kisiasa unaoongezewa nguvu na wao kuwa wanafamilia ya Rais aliye madarakani na ambaye bado, kiukweli, ana mvuto kwa Watanzania walio wengi.
Katika mazingira ya sasa, Salma Kikwete na Ridhiwani Kikwete wanafanya kile ambacho Jakaya Kikwete hawezi kukifanya kwa urahisi kwenye kampeni kutokana na kubanwa na itifaki. Mama Salma Kikwete anaweza kufanya mikutano ya ndani Lindi, Mtwara na kwingineko akiongea na kundi kubwa la wapiga kura, wanawake, kwa lugha yao. Amefanya hivyo 2005 na sasa ana uzoefu zaidi. Anaongeza kura za JK.
Vivyo hivyo kwa Ridhiwani Kikwete, naye ana ametokea kwenye Chipukizi wa CCM na kuingia kwenye Umoja wa Vijana wa Chama hicho na kushika nafasi za uongozi. Ridhiwani ana mtandao mpana wa kichama ndani ya jumuiya hiyo na hata nje. Ni karata muhimu kisiasa. Ingekuwa ajabu kama asingezunguka kumtafutia kura zaidi mgombea wa chama chao ambaye pia ni baba yake.
CHADEMA:
Ujio wa Dr Slaa:
Niliandika, kuwa ujio wa Slaa, sio tu umewashangaza CCM na mgombea wake urais, bali pia unaonekana kuwashangaza CHADEMA wenyewe wanaoonekana kutokujiandaa na namna Dr Slaa alivyopokewa na wananchi. Dr Slaa ameongeza msisimko kwenye siasa za nchi yetu. Watu wengi wana shauku ya kumsikiliza, kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa 1995 uliomwibua Augustino Mrema. Akijipanga vema, hata baada ya uchaguzi huu. Akafanya kazi ya CHADEMA nje ya Bunge na kutembea nchi nzima, basi, Dr Slaa anaweza kuwa tishio kwa ye yote ndani ya CCM atakayekuja kupambana nae.
Udhaifu wa CHADEMA
Unajidhihirisha kwenye eneo la oganaizesheni na kifedha. Hilo nililibainisha katika makala yangu yaliyopita. Bado CHADEMA haina uwakilishi mpana katika ngazi za mashina na matawi. Niliandika, kuwa Dr Slaa anaweza kutua na helikopta Pawaga Iringa, lakini mara ile akiruka, huku nyuma hakuna watendaji wa CHADEMA wa kufanya kazi ya CHADEMA. Kuna taarifa pia za wagombea wake ubunge na udiwani kukosa nguvu za kifedha kuendesha kampeni .
Zitto Kabwe bado ni kitendawili:
Niliandika, kuwa Zitto Kabwe n i kada nyota ndani ya CHADEMA, lakini sarakasi zake za kisiasa huenda zinachangia kukidhohofisha chama chake kuliko kukipa nguvu. Alipata kulipotiwa na magazeti kutamka hadharani kuwa anajiandaa kugombea urais 2015. Zitto Kabwe alituachia maswali; Kulikoni ndani ya CHADEMA? Je, Dr Slaa ni mgombea wa msimu tu? Au ndio sababu Zitto Kabwe hakuhudhuria Mkutano wa ufunguzi wa kampeni za CHADEMA? Niliandika, kuwa kuna watakaouliza. Na maswali yanaongezeka.
Inachojivunia CHADEMA:
Bado ni chama kinachoonyesha kuwa na mvuto kama kitajipanga vema. Kuna vijana wengi na hususan wasomi wenye kuvutiwa na CHADEMA. Hizi ni dalili njema kwa CHADEMA kwa siku zijazo, endapo zitabaini mtaji huo , kuuwekeza na kuutumia vema mbele ya safari.
CUF: CHAMA CHA WANANCHI
Leo naweza kukiri, kuwa nilikosea, nilipoandika, kuwa CUF ( Bara) safari hii kinaonekana zaidi kuwa jokeli katika karata za kisiasa. Kwa hali ilivyo sasa, CUF bado ni chama chenye nguvu na kilicho na mizizi kwenye baadhi ya maeneo ya nchi. Na kwa hakika, Profesa Ibrahim Lipumba bado anaonekana kuwa na nguvu katika kanda ya pwani na mikoa ya kusini.
Mathalan, kama Uchaguzi Mkuu utafanyika kesho, CUF ina hakika ya kunyakua kati ya viti 8 hadi 10 kutoka mikoa ya Kusini pekee; Lindi, Mtwara na Ruvuma. CUF ina nafasi ya kushinda viti vingi vya madiwani kutoka mikoa hiyo na hata kuweza kuongoza halmashauri moja au mbili. Tunduru ni moja ya majimbo ambayo CUF ina nafasi kubwa ya kutoa mbunge na madiwani.
Ndio, Profesa Ibrahim Lipumba bado ni tishio. Ana uzoefu na anautumia. Na siku ile CHADEMA na CUF watakapokubaliana kuunganisha nguvu na kutoa mgombea mmoja wa Urais, basi, CCM itakuwa shakani. Lakini si kwa sasa, zikiwa zimebaki siku 30 kabla ya Oktoba 31. Ninapoandika fikra hizi huru.
Maggid