francis jn
Member
- Oct 9, 2012
- 11
- 12
Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hali ya kisiasa hapa nchini imekuwa ni ya vuta nikuvute ndani ya vyama vya siasa ikiwemo CCM na CHADEMA. Kabla ya Mwaka 2013 kuisha, tumeshuhudia viongozi waandamizi wa CCM wakijaribu kujisafisha kwa kuwatoa kafara wale wanaowaita mawaziri mizigo ili kukinusuru chama chao wanapoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Pia, tumeshuhudia mawaziri wanne wakifukuzwa ambaye mmoja kati yao alijiuzulu kutokana na kile kinachosemwa ni ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu katika kuendesha Operation Tokomeza Ujangili.
Hivi karibuni pia tumeshuhudia CHADEMA ambacho ni chama kikuu cha upinzani kinachowapa matumaini watanzania wengi katika kuleta mabadiliko ya kidemokrasia na maendeleo, nacho katika kujiweka sawa na kujiimarisha kisiasa kinapoelekea uchaguzi mkuu kimewafukuza viongozi wake watatu kwa kile kinachosemwa ni wasaliti wa chama. Viongozi wawili katika yao wamevuliwa uanachama na mmoja wao aliyesalia ni Mbunge wa Kigoma kaskazini, Zitto Kabwe ambaye aliweka pingamizi katika Mahakama kuu kuwa uanachama wake usijadiliwe na Kamati kuu mpaka liitishwe Baraza Kuu la chama kusikiliza rufaa yake, leo hii Mahakama kuu imekubali pingamizi lake.
Wakati kesi ikiendelea katika Mahakama kuu kwa takribani siku tatu, kumetokea matukio mbalimbali ya kupigwa kwa watu wanaosemakana ni wafuasi wa Zitto (mamluki) ambao walikuwa wakifika mahakamani kumuunga mkono mtu wao. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa bungeni alishawahi kusema maneno haya "sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine... maana tumechoka. Pia Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Temeke, Josephat Yona alipigwa na watu wasiojulikana, kwa kile kinachosemwa alikuwa ni mmoja wa viongozi waliopinga maamuzi ya Kamati Kuu ya kuwavua uanachama viongozi hao. Hata hivyo CHADEMA kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano, imekemea kwa ukali tukio hilo la kikatili la ukiukwaji wa haki za Binadamu na kulitaka jeshi la polisi lichunguze tukio hilo ili lijue ukweli na haki itendeke ili sheria ifuate mkondo wake.