Misri yatekeleza adhabu ya kifo kwa watu 11 baada ya kukutwa na hatia ya mauaji

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Mamlaka nchini Misri zimetekeleza adhabu ya kifo watu 11 siku ya Jumanne baada ya kuwakuta na hatia ya mauaji, chanzo kimoja ndani ya vyombo vya usalama vya Misri kimeiambia Shirika la Habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina.

Adhabu hiyo ya kifo imetekelezwa katika gereza la Borg al-Arab karibu na mji wa Alexandria, ikiwahusisha watu waliopatikana na hatia kwa makosa ya mauaji waliyoyatekeleza katika majimbo ya Alexandria na Beheria miaka ya hivi karibuni.

Huu ni mwendelezo wa utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa wafungwa nchini Misri, baada ya watu watano kuuawa siku ya Jumamosi, wakiwamo wanawake watatu kutokana na kukutwa na hatia kwa makosa yanayofanana na waliouawa siku ya Jumanne.

Shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International limelaani ongezeko la vitendo vya utekelezaji wa adhabu za vifo kwa wafungwa nchini Misri chini ya utawala wa Rais Abdel-Fattah al-Sisi.

Sisi aliingia madarakani mwaka 2013 baada ya mapinduzi yaliyomwondoa madarakani kiongozi anayeungwa mkono na Udugu wa Kiislamu, Mohamed Morsi, na utawala wake unalaumiwa kwa ukandamizaji wa haki za binadamu.

Amnesty inasema kuwa takriban wafungwa 57 wamenyongwa kati ya mwezi Oktoba na Novemba mwaka jana, ikizilaumu mamlaka za Misri kutoa adhabu ya kifo katika mazingira yenye ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo watu wengi kupelekwa mahakamani na kuhukumiwa kunyongwa kwa pamoja.

Misri inalaumiwa pia kwa kutoweka wazi idadi ya watu walionyongwa hadi kufa au wafungwa wanaosubiri kunyongwa. Shirika la Human Rights Watch limeitaka Misri kusimamisha mara moja utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa wafungwa.

Chanzo: AFP
 
Back
Top Bottom