Naomba kuuliza hivi, kwani waheshimiwa wawakilishi na wabunge wetu wanalipwaje kwa mwezi?
Unaulizia kwa mwezi? Uliza kwanza posho ya kikao kwa siku, utakapogundua ni sawa na huo mshahara wa mwezi wa huyo daktari wa Zanzibar usishangae! Hata mshahara ukiwa mdogo hapo hakuna mbunge atakayeulalamikia! Ukweli ni kuwa wafanyakazi wengi wa serikali huwa wana mishahara midogo, lakini wale wenye nafasi wanaridhika kutokana na hizo wanazoita "posho". Nilipokuwa mwalimu huko nilikuwa nashangaa sana, nilikuwa nalipwa kwa mwezi mshahara ambao nikiitwa semina Dar ya siku 3 tu nalipwa posho ambayo ni sawa na mshahara wa mwezi! Maana yake ni kwamba mshahara ulikuwa mdogo sana, kwani hata hiyo posho ya siku 3 nikijibana sana na kukaa kwenye hoteli "choka mbaya" nilikuwa nasevu pungufu kidogo ya nusu! Yaani ni kwamba nikiondoka mwenyewe na mshahara wangu wa mwezi kwenda kupumzika kwenye hoteli iliyochoka ya huko Sinza, huo mshahara ungenitosha (kula na kulala) siku 4 tu! Kwenye hoteli ya kati katikati ya Jiji(sio ya kitalii), ungenitosha siku 2, na kwenye zile hoteli za beach kule Bagamoyo (vile vyumba vya bei ya chini kabisa) mshahara wangu wa mwezi ungetosha tu bed and breakfast kwa usiku mmoja tu! Sasa ulipaji wa hivyo kwa kweli ni masikhara kabisa! Wale wenzangu waliokuwa walimu wenye bidii sana na ufundishaji ambao hawakuwa na mradi wowote nyumbani, muda wote wako na wanafunzi, kumalizia syllabus, kupanga lesson plans nzuri, wanatoa assignments na tests kibao (maana yake pia wana kazi nyingi za kusahihisha kazi za wanafunzi), walikuwa na matokeo mazuri sana ya mitihani ya kitaifa katika masomo yao, lakini wenyewe walikuwa "choka mbaya"! Walikuwa hawafundishi tuisheni (isipokuwa tu wakati wa likizo, tena kama wiki 2 tu maana muda mwingine waliutumia kusahihisha terminal exams kwa "makini"). Hawakuwa na "kitu" mfukoni, hata wanafunzi walikuwa wanawatania! Lakini majuzi (June) nilikwenda nyumbani nikawaona wawili, nilishangaa, wameacha kufundisha! Unajua wanafanya nini? Wameingia kwenye siasa za "chama cha walimu", wananiambia wameajiriwa huko, huyo mmoja alinipa lifti kwenye gari ya chama cha walimu akanipeleka hadi kijijini Muriet kuona ndugu na jamaa, kaniambia sasa hivi mambo "mswano", kwani naye anapata "posho" za vikao, na amejenga nyumba na kuanzisha mradi wa baa! Yule aliyekuwa bingwa wa hesabu kajiunga na idara ya takwimu naye mambo yake ni "bomba", ualimu ameacha. Yuko mmoja wanafunzi wa A level Biology walikuwa wanamwita "Vines", alikuwa "amemeza" yale mabuku makubwa mawili ya A'Level biology (nadhani ndio yanaitwa Vines), alikuwa anapendwa huyo! Alikuwa anaongea kwa sauti ndogo sana na hachapi mtu, lakini akiwa zamu, utashangaa wanafunzi wanavyomtii na kumsikiliza. Walikuwa wanadai yeye ndio "biology" yenyewe, maana alikuwa anaitoa neno kwa neno kinywani mwake bila kutumia kitabu wala notes, anaingia darasani na chaki tu, na soksi iliyochakaa ya kufutia ubao! Lakini naye alikuwa ameyumba sana kiuchumi, kila siku yuko na suruali yake ya khaki, shati la bluu na safari buti (vijana walikuwa wanaziita "mbwa"), na nadhani zilikuwa hazifuliwi, maana ni kila siku ziko mwilini. Lakini vijana walikuwa wanafaulu sana somo lake, na wako wengi ninaowafahamu ni madaktari. Sasa huyu nilikutana naye, nilimsahau kabisa! Amekuwa "sopsop", anang'ara, anaendesha "Range-Rover", nikamwambia "mwalimu naona sasa mambo yamekuwa matamu, kumbe mie naondoka na nyie ndio mambo yanawanyookea". Akacheka sana, kisha akaniambia ningepata utamu huu kwenye ualimu nisingeacha. "Kumbe umeacha?" nikamwuliza. Akajibu ameacha zamani, na amejiunga na shirika linalojihusisha na utafiti katika masuala ya wanyama pori, na ameajiriwa kwenye mradi ambao anasema akienda field porini kwa wiki 3 tu anapata malipo ambayo ni sawa na mshahara wake wa mwaka mzima alipokuwa mwalimu!
Kwa nini nimeyasema yote haya? Ni kwamba mfumo wa utawala uliopo unawakatisha tamaa wataalamu, na unawafanya wale wenye bidii na uaminifu kujuta kwa nini wanafanya kazi kwa kujituma, kwani haiwalipi! Matokeo yake ni kwamba wale walio wazuri wanakata tamaa na kuacha kazi na kutafuta njia nyingine au sehemu nyingine ambako utaalamu wao unaheshimika na kulipwa ipasavyo. Wale wanaobaki kazini wanaendeleza "usanii", wanakuwa "pretenders", kwa hiyo while the government pretends to pay, the employees pretend to work! Hakifanyiki kitu hapo! Na ninasema tatizo si la madaktari peke yao, ni kila mtu anayefanya kazi serikalini (isipokuwa wateule wachache wa huko BoT, TRA, PCB, TANROADS). Bahati mbaya kwetu ni kwamba madaktari "wametushika pabaya", wakigoma athari zinaonekana haraka na zinatisha, kwa hiyo wanasikilizwa haraka pia. Lakini wengine pia wana hali mbaya hivyohivyo!