Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
MISAADA YA MAREKANI NA UHURU WETU KAMA TAIFA.
Marekani kupitia MCC imeridhia kuinyima Tanzania fedha za msaada zaidi tirioni na pia nchi yetu imetolewa kabisa kwenye orodha ya nchi ambazo zilikuwa zinanufaika na miradi ya MCC. Sababu hasa ni sheria ya makosa ya kimtandao na uchaguzi wa wazanzibar.
Watanzania hasa wapinzani wametumia hili kama kuonesha uhalali wa kile ambacho wanakipagania na ya kwamba ni sawa kwa nchi kunyimwa misaada hiyo.
Baadhi ya vifungu vya sheria za mtandao siviafiki, na mimi ni mmoja watu wengi wanao amini uchaguzi wa awali wa Zanzibar hakufutwa kwa mujibu wa sheria na pia haukuwa na mapungufu ya kuhitaji kufutwa na kurudiwa.
Pamoja na kuamini hayo, siafiki hata kidogo kuwa sheria ya makosa ya mtandao ifanyiwe marekebisho na matokeo ya uchaguzi wa awali wa Zanzibar yatangazwe kisa tu MAREKANI anataka hivyo. Kama taifa huru hatuwezi kukubali hilo hata kidogo.
Tunaweza kuweka sawa jambo lilopotoshwa kwa kutumia mifumo iliyopo ndani ya nchi yetu. Kuhusu sheria iliyopitishwa na bunge, kama tunaona sheria hiyo imekiuka katiba ya nchi, yaani kama kuna haki za msingi za kiraia na za kibinadamu zinakiukwa na sheria hii, jambo jepesi ni kwenda mahakamani kwa mtu yeyote au taasisi yoyote ambayo inaona haki hizo zimekiukwa, na si kunyimwa misadaa kama ni njia.
Kuhusu uchaguzi wa zanzibar mara kadhaa tumewasikia wanasheria wakifafanua vizuri kwa kuonesha kwa namna gani Jecha kama mwenyekiti wa ZEC hakuwa na mamlaka ya kisheria ya kufuta uchaguzi, na mambo mengine mengi yaloonesha uchaguzi wa awali ulikuwa halali na ulifutwa kimakosa. CUF wakasusia uchaguzi wa marudio na CCM ikaingia uwanjani bila mpinzani wake mkubwa.
Najua wengi wetu tulitaraji kufanyika mazungumzo kati ya CUF na CCM yenye tija kabla ya uchaguzi ule. Mazungumzo hayakuwa na tija sababu CUF ilitaka matokeo yatangazwe na CCM ilitumia kete ya kuheshimu maamuzi ya ZEC.
Kama hawa wawili wamekaa na wameshindwa kuelewana chini ya mwavuli wa siasa, kwa vyovyote vile iliyohitajika kuchukua mkondo ni SHERIA, na kwa sababu hiyo nilitaraji CUF kwenda mahakamani kuomba tafasiri ya kisheria juu ya vifungu ambavyo ZEC ilivikiuka wakati ikiamua na kutekeleza uamuzi wa KUFUTA matokeo ya uchaguzi.
Kimsingi baada ya mazungumzo ya kidugu kutofaa njia nyingine ya kidugu ya kutatatua mkwamo ule ilikuwa ni kufuata mkondo wa sheria. KINYUME NA HIVI NI MACHAFUKO NA GHASIA ama kuingilia uhuru wa nchi kujiendesha kwa mifumo yake ya ndani.
Huenda ni kweli mahakama zetu haziaminiki, na hasa ukizingatia kitendo cha Jaji Mkuu mstaafu kwenda kugombea urais kupitia CCM, lakini mahakama zetu hizihizi ambazo tumeona serikali ikishindwa kesi nyingi tu, na mahakama zetu hizihizi ambazo ndio ziko juu ya mihimili mingine ya dola na juu ya kila ya tasisi na mtu.
Marekani na dunia ione na kutambua, kuwa nchi yetu ni dola huru na ina mihimili mitatu, na wananchi tunajua nini serikali inatakiwa kufanya na nini hautakiwi kufanya kwa mujibu wa katiba, na kama tukiona mambo yanayo fanywa na serikali na vyombo vilivyo chini yake yanakanyaga katiba na sheria, ni wajibu wetu kuikosoa na kuielekeza nini ifanye kwa kupitia bunge, lakini isipokaa sawa na tukiona makosa yake yanakiuka katiba yanaendelea bila woga hatuhitaji MAREKANI itusaidie kuirekebisha serikali yetu midhali mahakama ZIPO na mara nyingi Mtikila alikuwa anaibwaga serikali mahakamani.
kwa vitabia hivi, vitisho hivi vya kunyimwa misaada kisa tu hatutaki kwenda kama waendavyo wakubwa, ndio naona umuhimu wa kujitegemea kwa % 100 kama taifa, na hapa ndipo ninapo muelewa na kumkubali Magufuli.
Hoja yangu, yaani turekebishe sheria ya makosa mtandao sababu MAREKANI inataka hivyo? au sababu kuna makosa yanayo hitaji marekebisho? Hivi yale matokeo ya uchaguzi wa awali yangetangazwa sababu ni sawa kufanya hivyo kisheria au kwasababu MAREKANI anataka yatangazwe?
Nchi yetu ina mfumo wa kikatiba na mfumo wa nchi yetu una majawabu yote juu ya kadhia iliyotokea Zanzibar na juu ya kasoro katika sheria ya makosa ya mtandao. Hatuwezi kuacha kufuata njia ya mfumo wetu kisha kama taifa tukubali kuendeshwa kwa mhemko wa MISAADA YA MCC.
Njano5
0622845394