Elias Msuya
Senior Member
- Dec 23, 2011
- 173
- 672
Wajumbe wa mkutano mkuu wa dharura wa Chama cha Wananchi (CUF) wamemchagua Mirambo Camil Yusuf kuwa Mwenyekiti wa chama hicho akichukua nafasi iliyoshikiliwa na Profesa Ibrahim Lipumba tangu mwaka 1999.
Mirambo, ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kigoma Mjini, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa nne wa chama hicho, akipata kura 257 amewashinda Othman Omar Dunga aliyepata kura , 177 na Nkunyunyika Siwale, aliyepata kura 6.
Uchaguzi huo uliofanyika katikaukumbi wa hoteli ya Lekham Buguruni jijini Dar es Salaam ulihudhuriwa na wajumbe 456, ambapo kura halali zilikuwa 448, huku kura sita zikiharibika.
Akizungumza baada ya kuchaguzuliwa, Mirambo amesema atahakikisha kunakuwa na matumizi sahihi ya fedha za chama na kwamba kipaumbele chake kitakuwa ni kuhakikisha watumishi wanalipwa kwa wakati ili kuongeza ari na morali ya kazi, pamoja na kuimarisha ngazi za chini za chama.
“Nataka kujenga taasisi inayoaminika na kupata wadau sahihi watakaosaidia chama kupiga hatua kwa kupata rasilimali fedha,” amesema.
Ameeleza pia kuwa siasa za Tanzania zinapaswa kuwa siasa za ukombozi kwa kujenga mtandao wa ngazi za chini utakaopanua wigo wa kura, badala ya kujikita zaidi katika siasa za upinzani.
“Mimi ni muumini wa siasa za ukombozi na ninaamini zinaweza kutuvusha kutoka hapa tulipo na kutufikisha hatua nyingine. Nitakuwa kiongozi bora kupitia fursa nitakayopata ili tufikie maendeleo endelevu,” amesema.
Vilevile, amesema amejipanga kutatua migogoro ndani ya chama kwa kuanza kuchunguza chanzo chake ili kupata suluhu ya kudumu kupitia njia sahihi zitakazowezesha kufikia hatua bora.
Mirambo ambaye ni mkazi wa Kigoma na alizaliwa mkoani Tabora mwaka 1971. Kitaaluma, ni mwandishi wa habari na mtaalamu wa lugha za Kiswahili, Kifaransa na Kiarabu. Pia ni mwalimu wa mpira wa miguu.
Aidha, amekuwa Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kigoma Ujiji kwa miaka 10, ambapo alikiongoza chama katika vuguvugu la Muungano wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ulioshirikisha vyama vya Chadema na NLD.
Mirambo Yusufu (mwenye shati la Kitenge) akipongezwa na baadhi ya Wanachama.
Nafasi nyingine
Kwa upande wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Miraji Mtibwiliko alipata kura 264 na kuwashinda Mohammed Ngulangwa aliyepata kura 88 pamoja na Mussa Mbarouk aliyepata kura 82.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar imechukuliwa na Haroub Mohamed Shamsi aliyepata kura 256, akimshinda Mbarouk Seif Salim aliyepata kura 171, huku Amina Rashid Salim akijitoa kabla ya upigaji kura.
