Mimi, Sal Davis na Kitabu Chetu

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,268
MIMI, SAL DAVIS NA KITABU CHETU
Kwa mara ya kwanza hiki ndicho kitabu changu kilichochapwa na Amazon.

Amazon sifa zao hazihitaji kuelezwa na mimi.

Walianza na uuzaji wa vitabu na kukufikishia hadi kizingitini kwako nchi yoyote ulipo kiwe ndiyo kwanza kimetoka kuchapwa au cha zamani sana hakipatikani wao watakupatia.

Mchapaji vitabu Abdullah Saiwad wa Readit Books siku moja katika mazungumzo yetu kuhusu vitabu nilimwonyesha mswada wa kitabu cha maisha ya Sal Davis ambao nilikuwa nimeumaliza miaka 14 iliyopita.

Akaniuliza kwa nini sijauchapa.

Nikamueleza matatizo ya kuchapa kitabu Afrika mahali ambako watu wameshughulishwa zaidi na kutafuta chakula kiasi kusoma kitabu si kipaumbele.

Akaniambia kuwa siku hizi kuchapa kitabu ni kazi ndogo sana kupitia Amazon.

Hakika sidhani hata mwezi mmoja ulitimia akawa kaupitia mswada kwa uhariri na akauwasilisha Amazon na kitabu kikachapwa.

Kila kizuri hakikosi kasoro.

Kitabu kikachapwa na kuwekwa sokoni kupitia mtandao wa Amazon lakini Tanzania hawawezi kukifikisha na hii naamini itakuwa pia katika baadhi ya nchi nyingine za Dunia ya Tatu.

Sababu yake sijui.

Baadhi ya wasomaji Marekani na Canada wakaniletea taarifa kuwa wanacho kitabu cha Sal Davis wameshakinunua.

Mimi na mchapaji, yaani publisher, Saiwad tukabakia kurushiana picha.

Leo nimetembelewa na mmoja wa vijana wangu kutoka Marekani ambae anatafiti historia hapa nchini kaniletea zawadi ya kitabu cha Sal Davis.

Kwa mara yangu ya kwanza nikawa nimeshika kazi ya mikono yangu katika mikono hii yangu iliyoandika kitabu hiki.

Nani huyu Sal Davis?

Sal Davis nimemwandika sana hapa na ikiwa unataka kumjua Sal Davis ni nani ingia Google ingia YouTube utamjua.

Sal Davis amejuana na Muhammad Ali London 1963 wakati Muhammad Ali anajulikana kama Cassius Clay na bado hajawa bingwa wa dunia wa masumbwi.

Sal Davis amejuana na Cliff Richard anapanda jukwaani kutumbuiza mwingine anashuka katika miaka hiyo ya mwanzoni 1960s.

Ikiwa humjui Cliff Richard ingia YouTube.
Sal Davis amejuana na Sidney Poitier, Paris na wakawa marafiki wakubwa.

Sal Davis ana mengi ya kueleza katika uhusiano wake na Harry Belafonte na Miriam Makeba.

Hawa wote ninaokutajia hapa ni watu waliowika katika ulimwengu wa watu maarufu katika michezo, muziki na filamu.

Kijana huyu Mswahili Salim aliyezaliwa Zanzibar na kukulia Mombasa Old Town siku hizo akijulikana kama Salim Abdallah mtoto wa Shariff Abdallah Salim aliwajuaje na kuwa rafiki na watu hawa maarufu ulimwenguni katika miaka kama ile?

Sal Davis alizaliwa na kipaji ambacho hakikuwa cha kawaida.

Akisimama jukwaani na nyuma yake kuna wapiga ala Wazungu na wengine wakubwa kwa umri kumpita (Sal Davis alikuwa mtoto mdogo ndiyo kwanza anakimbilia miaka 18) ukamsikia akiimba ilikuwa tabu kuamini kuwa ni kijana wa Kimombasa na si Muingereza au Mmarekani siku zile wakiitwa, "Negros."

Sal Davis anaimba ukimsikiliza utasema huyu ni kijana wa Kiingereza labda katokea Finsbury Park hapo hapo London.

Hiki ni kitabu cha maisha yake.

1696330678312.png

1696330716141.png

1696330744701.png

1696330789344.png
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom