Hadithi ya Mwendapole na Madereva
Hawa ni vijana waliojipatia umaarufu mkubwa katika nchi ya Kusadikika kila mmoja kwa sababu zake tofauti.
Madereva alianza kupanda chati baada ya kusikika hadharani akiwatukana viongozi (hata wa chama chake) na akafika kilele pale alipoonekana wazi akitaka kuvuruga mchakato wa KATI BAR mpya ili juwafurahisha wakuu wake. Anakumbukwa kwa vurugu za pale kwenye LULU ya BULUU aliposemekana alimpiga Mzee War Iobber kwa chupa ya maji na mdahalo kuvurugika.
Kwa upande wa MwendaPole yeye alijipatia umaarufu kwa sababu zote chanya, kwanza alisimamia kile alichoamini kuhusu mchakato wa KATI BAR kuwa KATI BAR ya wananchi ndiyo mwarobaini wa kudumu kwa taifa la Kusadika.
Kwa vyovyote vile...vijana hawa kwa wakati ule hawakuwa marafiki wala kuwa na fikra sawa, mmoja akitetea genge lililomtuma akawa mpiga zumari wa mfalme na mwingine akitaka KATI BAR inayowapa wananchi nguvu zaidi na kumbana mfalme.
Zoezi la Kati Bar likafa kifo cha kimya kimya, likafuatiwa na uchaguzi wa kumpata mfalme mpya lakini kabla yule wa zamani hajaondoka akamteuwa Madereva kuwa mkuu wa WE-LIAR, wengi wakasema ni fadhila kwa kazi nzuri ya upigaji wa zumari. Kuelekea uchaguzi wa mfalme mpya, Mwendapole akaamua kumpigania mfalme mpya kutoka msitu wa kijani, akidhani huyu mpya atakuwa na tofauti na aliyemtangulia. Watu wakasema sana kuwa Mwendapole anataka kupewa mfupa...akakanusha na kujiapia kuwa hataki na anamwomba Mungu amwepushe.
Ukafika wakati mfalme mpya anatoa fadhila kwa wapiganaji wake....Mwendapole akapewa mfupa...watu wakamkumbusha viapo vyake, jamaa akala ngumu. Madereva naye akabadili gia angania akawa dam dam na mfalme mpya akabaki mjini. Yakatokea mabadiliko, Madereva akapandishwa cheo akawa mkubwa wa Mjini na Mwendapole akatolewa kijijini akaletwa mjini sasa yupo chini ya Madereva.
Mambo yamebadilika sana, Mwendapole aliamini na anajua kuwa anauwezo mkubwa kuliko Madereva, na anajua kuwa mfalme mpya hasimamii kabisa misingi ya ile KATI BAR aliyokuwa anaipigania, amejikuta katika wakati mgumu....si wa kumeza wala kutema, amebaki kuwa MWANAFALSAFA akiandika maneno magumu ambayo wadadisi na wachunguzi wa kusadikika wanadai kuwa hali sasa si nzuri kwa Mwendapole.
Wananchi wanamtaka Mwendapole afanye maamuzi na siyo kulalamika kwa mafumbo, achague mmoja awe mpiga zumari wa mfalme au aendelee kutetea KATI BAR ya wananchi iliyomjengea heshima kubwa lakini ajue kuwa, akichagua uamuzi wa pili akubali kujitoa, kujikana na katu hatafanikiwa asipohama katika msitu wa Kijani.