Mbinu nyingi leo Madrid v Barcelona Send to a friend Wednesday, 20 April 2011 11:51
MADRID, Hispania
KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho anatakiwa kutatua tatizo la mbinu wakati timu yake itakapokutana leo na Barcelona kuwania kombe la Mfalme wa Hispania katika pambano litakalofanyika kwenye Uwanja wa Valencia unaoitwa Mestalla.
Mourinho ambaye anafahamika kwa vituko vingi Jumamosi iliyopita aliwezesha timu yake ya Real Madrid kuilazimisha Barcelona sare ya bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Hispania, La Liga.
Raisi wa heshima wa Real Madrid, Alfredo Di Stefano amemtaka kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho kuja na mbinu mpya kama anataka kushinda mechi dhidi ya Barcelona leo na kuifananisha Barcelona kama mnyama Simba.
"Mechi tuliyocheza siku ya Jumamosi dhidi ya Barcelona inatakiwa itupe muelekeo wa kufahamu tutaikabili vipi Barcelona katika mechi ya leo,"alisema Distefano mwenye miaka 84.
"Barca wanauchezea mpira kwa heshima, wanaupenda na wanaringa nao, kwao mpira mahesabu, ukiwaangalia wanavyocheza inafurahisha,"alisema Di Stefano.
Katika mechi iliyozikutanisha timu hizo Jumamosi iliyopita Mourinho aliichezesha timu yake kwa kutumia mbinu ya kujilinda zaidi na kuzuia kocha wa Barcelona, Pep Guardiola kutengeneza rekodi ya kushinda mechi sita katika mechi sita alizokutana na Real Madrid akiwa kocha wa Barcelona.
Pia katika mechi hiyo Mourinho aliweza kuepuka kichapo cha aibu cha mabao mengi kama Barcelona ilivyoichapa Real Madrid bao 5-0 Novemba mwaka jana.
Katika mechi ya Jumamosi iliyopita, Real Madrid ikiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya mchezaji mmoja kutolewa kwa kadi nyekundu pia ikiwa nyuma kwa bao 1-0, iliweza kusawazisha bao na kufanya mashabiki wa Real Madrid kulipuka kwa furaha,ambapo sare ilionekana kama ushindi.
Katika mechi hiyo Mourinho alitumia mbinu ya kumchezesha Pepe kwenye nafasi ya kiungo wakati Pepe ni beki wa kati, pia alikuwa na viungo wakabaji wawili hali iliyomsaidia kuweza kupunguza kasi ya viungo wa Barcelona.
Katika mechi ya leo Mourinho anatarajiwa atamchezesha Mesut Ozil kuanzia kipindi cha kwanza, lakini beki Raul Albiol hatacheza kwa sababu kwa sababu alipewa kadi nyekundu wikiendi kwa maana hiyo Sergio Ramos anatarajiwa kuanza sambamba na Ricardo Carvalho.
Real Madrid ambayo inaonekana kukata tamaa katika harakati za kuwania ubingwa wa Hispania, inataka kutwaa taji la kombe la Mfalme ambalo kwa mara ya mwisho ililitwaa mwaka 1993, pia wiki ijayo itacheza mechi ya nusu fainali ya Ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Barcelona.
Kocha wa Barcelona, Pep Guardiola ambaye alitwaa makombe yote matatu 2009 yaani kombe la ligi kuu, kombe la mfalme la ligi ya mabingwa barani Ulaya, anatarajiwa pia atabadilisha mbinu na kuja na mfumo mpya katika mechi hiyo.
Kiungo wa Barcelona na Argentina, Javier Mascherano hivi sasa amerudi uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu na anaweza kusaidia katika safu ya ulinzi kama Carles Puyol atakuwa bado hajapona.
Alipoulizwa kama Barcelona itafanya mabadiliko yoyote katika uchezaji wake baada ya kushindwa kuifunga Real Madrid, kocha Pep Guardiola alisema,"kila timu inacheza kwa jinsi inavyoamini na kutumia wachezaji wao bora, sisi tunayo falsafa yetu ya kucheza soka na aina yetu ya uchezaji soka na siku zote tunaheshimu falsafa yetu na aina yetu ya uchezaji soka."
Akilizungumzia pambano la leo, mchezaji wa zamani wa Barcelona, Johan Cruyff alisema kwamba Barcelona inatakiwa kuwa makini inapokutana na mtaalamu wa kutwaa makombe, Jose Mourinho.
Alisema,"hata kama wanaipenda staili yao ya uchezaji soka iliyojaa pasi nyingi wanatakiwa kuongeza ubora wao ili waweze kuifunga Real Madrid."