Hekaheka za waimbaji Tamasha la Pasaka 2011
Makuburi Ally
SIKU 13 kabla ya kufanyika kwa tamasha la kimataifa la muziki wa Injili kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam, CCM Kirumba, Mwanza na Jamhuri Dodoma, maandalizi kwa waimbaji yameshika kasi.
Hili ni tamasha la Pasaka litakaloanzia Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam Aprili 24 na siku itakayofuata, litahamia Jamhuri Dodoma.
Aidha, baada ya waimbaji mahiri wa ndani na nje ya Tanzania kutikisa Dar es Salaam na Dodoma, Aprili 26, itakuwa zamu ya CCM Kirumba, Mwanza.
Kwa mujibu wa kamati ya maandalizi chini ya Mwenyekiti wake, Alex Msama, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, anasema maandalizi yanakwenda vizuri.
"Maandalizi yanakwenda vizuri, kilichobaki ni kuzidi kuwaombea wote wanaotamani kushuhudia tamasha hili ambalo mgeni rasmi ni Rais wetu mpendwa Jakaya Kikwete," anasema Msama.
Kuhusu waimbaji, Msama anasema tayari wapo kwenye maandalizi ya nguvu kuhakikisha siku hiyo wanatoa burudani ya kiwango cha hali ya juu ili kila atakayefika katika Diamond Jubilee, Jamhuri-Dodoma na Kirumba, asijutie muda wake.
"Kamati yangu imejitahidi kufanya kila iwezalo kuhakikisha tamasha hili linakuwa lenye kiwango cha ubora wa hali ya juu," anasema Msama.
Wakati Msama anayasema hayo, waimbaji nao kwa nyakati tofauti, wamezungumza kwa njia ya simu na kila mmoja ameahidi kufanya vitu vya uhakika katika matamasha yote matatu.
Rose Muhando, malkia wa muziki wa injili wa mwaka 2009, akizungumza kutoka mkoani Dodoma, anasema hawezi kuahidi mengi, isipokuwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili, wafike kwa wingi Diamond Jubilee, Jamhuri, Kirumba.
"Unajua, binadamu unaweza ukapanga hivi, lakini Mwenyezi Mungu akapanga vinginevyo…. niseme tu tuombe Mungu alie hai atujalie sote uzima na afya siku hiyo ili tuweze kuifurahia Pasaka kwa namna yake pale Diamond Jubilee.
Muhando ambaye alishirikishwa na Annastazia Mukabwa wa Kenya katika albamu ya ‘Kiatu,' inayotamba vilivyo kwa sasa, anasema Tamasha la Pasaka kwake ni kitu cha kipekee.
Rose aliyetamba na kung'ara na vibao mbalimbali katika anga ya muziki wa injili kikiwemo cha ‘Jipange Sawaswa', anasema ana sababu mbili zinazolifanya tamasha la injili kuwa la kipekee kwake.
Sababu ya kwanza, anasema Pasaka ni alama ya ushindi wa Yesu Kristo dhidi ya dhambi kwa niaba ya wanadamu, hivyo ni fumbo lenye maana kubwa kwa maisha ya kiroho.
Rose anaongeza kuwa, kwa vile Pasaka huadhimishwa mara moja tu kwa mwaka, hivyo uwepo wake katika jukwaa la Diamond Jubilee siku hiyo ni njia mojawapo ya kuisindikiza Pasaka.
"Sababu ya pili inayofanya Pasaka iwe ya kipekee kwangu ni kwamba siku hiyo nitakuwa nikishambulia jukwaa huku nikikumbuka siku ya ubatizo wangu" anasema Rose.
Mwimbaji mwingine aliyezungumzia tamasha hilo ni Mukabwa ambaye kwa sasa anatamba na albamu ya ‘Vua Kiatu' aliyomshirikisha Rose Muhando.
Akizungumza kwa simu kutoka Nairobi, Kenya, Mukabwa amesema tayari alishaanza mazoezi kwa lengo la kutoa burudani ya uhakika siku hiyo mbele ya mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete.
Mbali ya kibao cha Kiatu kilichobeba jina la albamu, vibao vingine vilivyomo kwenye albamu hiyo ni ‘Ee Mungu', ‘Tabu zangu', ‘Usiwe Manamba', ‘Nzizilela', ‘Nishike Mkono Bwana' na ‘Wanaokudharau' na Mfalme.
"Naomba Mungu anijalie uzima na afya siku hiyo, mimi binafasi, ninaitamani sana siku hiyo kwa sababu ni heshima ya aina yake kuimba mbele ya mkuu wa nchi, pia kukutana na waimbaji wengine kama dada yangu Rose," anasema Mukabwa.
Kuhusu tamasha, Mukabwa anasema ingawa itakuwa mara ya kwanza kwake kushiriki, anaamini litakuwa lenye mvuto wa aina yake kutokana na uzoefu wa Msama na Kamati yake.
Msama na kamati yake, ndio imechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki wa injili kupitia matamasha mbalimbali ya Pasaka, Krismasi au uzinduzi wa albamu kadha wa kadha tangu mwaka 2000.
Mwimbaji mwingine aliyezungumzia tamasha hilo na maandalizi yake, ni Solomon Mukubwa, mwimbaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo anayeishi nchini Kenya.
Mukubwa ambaye si mara ya kwanza kwake kutumbuiza kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, anasema yupo fiti licha ya kubaki na mkono wake mmoja wa kulia kwani huohuo unatosha kufanya vitu vya kumtukuza Mungu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.
Mukabwa anayetamba na wimbo wa 'Mfalme wa Amani', anasema hiyo ni nafasi muhimu kwake kushirikiana na wengine kushambulia Jukwaa la Diamond Jubilee mbele ya Rais Jakaya Kikwete.
"Pamoja na kubaki na mkono mmoja, haunizuii kumuimbia Mungu, hivyo wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili waje washuhudie na kupata baraka za Mungu kupitia uimbaji," anasema.
Mukabwa anayekiri kwamba kwenda kwake nchini Kenya ilikuwa ni kumfuata mwimbaji wa nyimbo za Injili Angela Chibalonza ambaye kwa sasa ni marehemu, anaamini kila atakayekuja kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, ataondoka na baraka za Mungu.
Mbali ya Mukabwa aliyetokea familia ya watoto tisa (saba wa kiume), waimbaji wengine watakaopamba tamasha hilo la kimataifa, ni Boniface Mwaitege na Pamela Wanderwa.
Mukabwa aliyemwoa Betty Japheth tangu Machi mwaka jana, ni kati ya waimbaji mahiri wa muziki wa injili katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wenye mapenzi makubwa na Tanzania.
Mwaitege ambaye kwa sasa aliyewahi kutamba na vibao mbalimbali kama ‘Mke Mwema' na ‘Utamtambuaje' kwa sasa anatesa na albamu yake ya Mama ni Mama iliyojaa vibao vyenye ujumbe wa kuvutia.
Akizungumzia tamasha hilo, Mwaitege amesema hana mengi ya kuzungumza isipokuwa amewataka wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili, kufika Ukumbi wa Diamond Jubilee kusikia ujumbe wa neno la Mungu kupitia vipawa vya uimbaji kutoka kwa waimbaji watakaohudumu siku hiyo.
"Nashukuru kupata nafasi hii ya kuimba kwenye Tamasha kubwa la Pasaka, ni nafasi ya kipekee kwangu kujumuika na waimbaji wengine kufurahia ushindi wa Yesu Kristo pale Msalabani," alisema Mwaitege kwa njia ya simu.
Kuhusu maandalizi, Mwaitege amesema tayari ameshaanza kujipanga kwa ajili ya tamasha hilo kwa lengo la kutoa burudani ya kutosha kwa kadri Mungu atakavyomjalia.
Naye Upendo Nkone ambaye ni kati ya waimbaji watakaopamba jukwaa la Diamond Jubilee mbele ya Rais Kikwete, anasema ni furaha kubwa kwake kujumuika na waimbaji wengine kwenye tukio hilo la aina yake.
Anasema, Pasaka ni alama ya ushindi wa Yesu Kristo dhidi ya dhambi baada ya kuteswa, kufa na kufufuka kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu kutoka katika vifungo vya dhambi, hivyo kujumuika na wengine siku hiyo, kwake ni siku ya kipekee.
"Nashukuru sana kupata nafasi hii ya kujumuika pamoja na waimbaji wengine na wananchi kwa ujumla bila kujali kama ni mkristo au vinginevyo kwa sababu sote tu wana wa Mungu," anasema Nkone.
Anasema, anamwomba Mungu amjalie uzima na afya ili siku hiyo aende Diamond kuchota baraka za Mungu kwa sababu wakusanyikapo wawili watatu kwa jina la Mungu, naye huwepo mahali hapo, hivyo Mungu atakuwepo Diamondi Jubilee.
Anasema pamoja na malengo mengine ya uwepo wa tamasha hilo kwa mfano sehemu ya kile kitakachopatikana kuwafariji yatima, wajane na wengine wenye shida, anatoa wito pia kwa kila atakayefika Diamond Jubilee, autumie nafasi hiyo kusamehe wengine.
"Natoa wito kwa wote watakaofika Diamond Jubilee kuwa na furaha pamoja na ufufuko wa Yesgu Kristo kwa kungua mioyo yao kwa kuwasamehe hata wale waliowakosea badala ya kuhama kiti kimoja hadi kingine kumkimbia mwenzako," anasema Nkone.
Christina Shusho kwa upande wake, hakuna na mengi ya kusema isipokuwa amewataka wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili wasikose kwenda Ukumbi wa Diamond Jubilee siku ya Aprili 24 kupata baraka za Mungu kupitia uimbaji.
Amedokeza kuwa, ni furaha kubwa watu kujumuika pamoja wakipata burudani ya nyimbo za kumsifu na kumwinua Mungu kwa matendo yake makuu ya kumleta mwanaye Yesu Kristo kuzifia dhambi msalabani ili wanadamu wapate ukombozi.
Hizi ni kauli za waimbaji waliopo kwenye maandalizi makali ya kufanya mashambulizi kwenye matamasha matatu; kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam; Jamhuri, Dodoma na CCM Kirumba, Mwanza.
Je, viongozi wa kiroho wanayaonaje matamasha haya?
Kwa mujibu wa Askofu wa Kanisa la Mungu mkoani Dodoma, Donald Mhango, anasema matamasha hayo yanaonekana kuwagusa wengi kwani mbali ya kueneza ujumbe wa neno la Mungu kwa njia ya uimbaji, pia sehemu ya mapato kusaidia wenye shida.
Anasema, kusaidia wenye shida kama vile yatima, wajane na waathirika wa mabomu ya Gongo la Mboto, ni jambo jema linalopaswa kuungwa mkono na kuwataka wapenzi na mashabiki wa nyimbo za injili na Watanzania kwa ujumla, kujitokeza kwa wingi.
"Nawasihi wapenzi na mashabiki wote wa muziki wa injili na wananchi kwa ujumla, tujitokeze kwa wingi kushiriki tamasha kama hili la Jamhuri, kwa lengo la kusaidia wenye mahitaji," anasema Askofu Mhango.
Kiongozi mwingine wa kiroho aliyezungumzia matamasha hayo matatu ni Mchungaji wa Kanisa la KKKT mkoani Dodoma, Timothy Holela, aliyetoa pongezi kwa waratibu kuandaa kitu kizuri kama hicho na kuwataka kujitokeza kwa wingi.
Mchungaji Holela anasema anaamini kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Jamhuri, Kirumba na Diamond, kutawafanya waandaaji wa tamasha hilo kufikiria kuendelea na jambo hilo jema na maana kubwa.
Anasema kitendo cha sehemu ya mapato kusaidia wajane, yatima na waathirika wa Gongo la Mboto, ni jambo jema mbele za wanadamu na Mungu.
Zaidi ya hapo, ametoa wito pia kwa Kampuni ya Msama Promotions kufanya matamasha hayo kila mwaka ili kufikisha ujumbe wa neno la Mungu kupitia uimbaji na kusaidia wenye matatizo ambao ni wengi nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi wa matamasha hayo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama, amewashukuru viongozi wa kiroho kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwake.
"Najisikia faraja kubwa kusikia viongozi wa kiroho wakitoa sapoti katika harakati hizi za kamati yangu katika kuandaa matamasha haya ambayo mbali ya kufikisha ujumbe wa neno la Mungu kupitia uimbaji, pia kile kitakachopatikana kwenda kwa wenye makundi maalumu," anasema Msama.
Kuhusu wito wa matamasha hayo kuwa endelevu kwa maana ya kufanyika kila mwaka, Msama anasema lengo ni kufanya kila mwaka, ingawa wakati mwingine wanafanya hivyo katika mazingira magumu kutokana na kuhitaji gharama kubwa.
Anasema unapotumia gharama kubwa kwa maandalizi ikiwamo kuwaalika waimbaji kutoka nje, gharama huwa ni kubwa na ili walau urudishe gharama, unaweza kufikiria kiiingilio kiwe kikubwa, lakini kwa kufanya hivyo, ni wachache watakaomudu.
Waimbaji wa Tanzania ambao wamethibitisha hadi sasa ni Rose Mhando, Upendo Nkone, Bony Mwaitege na Christina Shusho.
Kutoka nje, ni Ephraem Sekeleti wa Zambia, Annastazia Mukabwa, Solomoni Mukubwa na Pamela Wanderwa, wote kutoka Kenya.
Baada ya waimbaji hao kutikisa Diamond Jubilee, siku inayofuata yaani Aprili 25, wote watahamia Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kisha kuruka hadi mwanza kwa ajili ya mashambulizi ya nguvu ya hapo Aprili 26, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Msama anasema kiingilio cha Diamond ambapo Rais Jakaya Kikwete atakuwa mgeni rasmi, kitakuwa sh 4,000 kwa viti vya kawaida; viti vya maalumu (B) sh 10,000 na viti maalumu (A) sh 20,000.
Kwa tiketi za viti maalumu vya VIP A zitakazokuwa kama meza za familia, watakaohitaji watalazimika kupiga simu selula 0713 383838, 0786 383838 na 0786 373737 kwa ufafanuzi zaidi.
Kwa upande wa matamasha yatakayofanyika Jamhuri na Kirumba, kiingilio kitakuwa cha aina moja ambacho ni sh 3,000 kwa lengo la kuwawezesha wengi kuingia kupata baraka za Mungu kupitia uimbaji na kuwaona ‘live' waimbaji mahiri.