Silaha nne za Afrika ya Kati zafikishwa Stars Send to a friend Wednesday, 23 March 2011 20:28
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
Sweetbert Lukonge na Jessca NangaweWAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiwataka wapenzi na mashabiki wa soka nchini kuacha tabia ya kuwabagua wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars kwa sababu ya klabu watokako katika mchezo wa Jumamosi, timu hiyo (Stars) imepewa majina ya wachezaji hatari wanne wa wapinzani wao, Jamhuri ya Afrika ya Kati na kutakiwa kuwachunga.
Kulingana na taarifa za mitandao na vyombo vya habari vya Jamhuri ya Afrika ya Kati, timu hiyo ambayo inaongoza Kundi D linaloundwa pia na Algeria na Morocco ikiwa na pointi nne, licha ya kushiriki mara chache michuano mikubwa ya Afrika, inaundwa na wachezaji wenye damu mchanganyiko ambao Stars haina budi kuwachunga.
Nyota hao chini ya kocha Jules Acorsi, raia wa Ufaransa wametajwa kuwa ni kiungo mshambuliaji Foxi Kethevoama (24) ambaye ndiye mfungaji wao tegemeo ambaye pia huichezea klabu ya Kecskeméti TE ya Hungary anayetajwa kuwa atasumbua mabeki wa Stars Jumamosi.
Wengine ni, Hilaire Momi, anayechezea Cotonsport ya Cameroon, viungo Romaric Linganzi wa US Bitam ya Gabon na Marcelin Tamboulas aliyekuwa katika benchi la akiba la TP Mazembe katika mechi dhidi ya Simba Jumapili.
Kwa kuangalia wastani wa umri wa wachezaji wa timu inao vijana wa umri wa kuanzia miaka 19 hadi mkongwe zaidi mwenye umri wa miaka 32, wote wakicheza soka katika nchi yao na nyingine Afrika na Ulaya. Wastani wa umri wao si zaidi ya miaka 24, jambo ambalo kwa soka la kisasa litawawasaidia.
Awali, akizungumza uzalendo kuelekea mechi hiyo , Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kuwa Watanzania wote wapenda soka wanatakiwa kushikamana na kuiunga mkono Stars katika mechi zake zote inazoshiriki bila kuangalia aina ya klabu wanakotoka wachezaji wanaounda kikosi hicho.
Stars itashuka uwanjani, Jumamosi Machi 26 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kupambana na Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwania nafasi ya kufuzu kushiriki fainali za Afrika mwakani.
"Nawaomba Watanzania wenzangu tushikamane na kuiunga mkono timu yetu ya taifa katika mchezo wake wa Jumamosi dhidi ya Afrika ya Kati.
"Umefika wakati wa kutanguliza kwanza utaifa na kuachana na tabia ya ubaguzi na kuwazomea wachezaji wetu kwa sababu tu kwamba kikosi kimeundwa na wachezaji kutoka klabu wasiyoshabikia," alisema Osiah.
Katika hatua nyingine kocha mkuu wa timu hiyo Jan Poulsen alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo yanaendelea vizuri na kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya kuhakikisha kinashinda mchezo huo.
Alisema mbali na hilo pia ana matumaini makubwa na wachezaji waliopo kwa sasa katika kikosi chake hata kama kiungo mshambuliaji wa Vancouver Whitecaps ya Canada, Nizar Khalfan asipotokea licha ya mchango wake kuhitajika kwenye kikosi hicho waliopo wataziba pengo lake.
Kumekuwepo na tetesi kuwa Nizar huwenda asijiunge na Stars kutokana na timu yake kuwa katika mikikimiki ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS ), jambo ambalo Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa taarifa hizo hazina ukweli na mchezaji huyo aanatarajia kutua nchi leo tayari kwa kuungana na wenzake kwa mechi hiyo ya Jumamosi dhidi ya Afrika ya Kati.
Kuhusu hilo, shirikisho hilo limesema endapo uongozi wa klabu hiyo ya Canada hautamruhusu Nizar Khalfan kwa ajili ya kushiriki mchezo wa kimataifa dhidi ya Afrika ya kati Jumamosi, klabu hiyo itashtakiwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Angetile Osiah alisema jana kuwa wao walitumia utaratibu na kumwombea ruhusa mapema mchezaji huyo ili aweze kuja kuungana na wenzake kwa ajili ya mchezo huo lakini inashangaza klabu hiyo kujibu kuwa hawana taarifa za mchezo huo na hadi sasa kushindwa kutoa jibu la kumruhusu mchezaji huyo.
"Sisi tulifuata taratibu na kutuma maombi kwa Whitecaps ili wamruhusu Nizar aje nchini kuungana na wenzake, lakini cha kushangaza wametuambia hawana taarifa za mchezo wetu wa kimataifa ndio maana mpaka sasa hajafika, lakini bado kuna muda anaweza kuwasili kesho (leo), kinyume na hapo tutaiarifu Fifa ili sheria na kanuni zichukue mkondo wake kwani Fifa wanatambua umuhimu wa mchezaji kuchezea timu ya taifa la nchi yake,"alisema Angetile.
Alisema kwa upande wa maandalizi yao yanakwenda vizuri na wapinzani wao, Afrika ya Kati tayari wamewasili nchini tangu juzi kwa ajili ya mchezo huo ambao mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi.
Kwa upande mwingine, Osiah alisema kufuatia na kubanwa katika michezo ya Ligi Kuu na ile ya kimataifa kwa timu za Simba na Yanga, walishindwa kucheza mechi za kimataifa za kirafiki ingawa tayari walipata mialiko katika nchi za Afrika Kusini na Afrika ya Magharibi.