Afrika ya Kati yaja kamili kuivaa Stars
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 11th March 2011 @ 23:55 Imesomwa na watu: 132; Jumla ya maoni: 0
WAZIRI wa Michezo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Aurelien Zingas, ataongoza msafara wa timu ya Taifa ya nchi hiyo itakayokuwa na watu 32 kwa ajili ya mchezo dhidi ya Taifa Stars.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema kuwa wamepata taarifa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Jamhuri ya Afrika ya Kati (FCF) msafara huo utakuwa na wachezaji 23 watakaotokea Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Gabon, Ufaransa, Morocco, Congo Brazzaville na Singapore.
"Wachezaji hao ni Prince Samola, Delphin Gbazinon, Audin Boutou, Nicaise Ozingoni, Mamadi Saoudi, Hilaire Momi, Geoffroy Lembet, Euloges Enza, Manasse Enza, Foxi Kette-Vouama, David Manga, Habib Habibou.
"Wengine ni Josue Balamandji, Fernander Kassai, Salif Keita, Freddy Lignanzi, Amores Dertin, Eudes Dagoulou, Vianney Mabide, Charly Dopekoulouyen, Emmanuel Yezzouat, Onassis Kemo na Franklin Anzite," alisema Wambura. Mchezo utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 27 mwaka huu.
Wakati huohuo, Wambura alisema mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Mohamed Adolf ameteuliwa kuwa Meneja wa timu ya Taifa ya wachezaji wenye umri chini ya umri wa miaka 23 inayoshiriki michuano ya mtoano ya Michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwakani jijini London, Uingereza.
Pia Adolf kitaaluma ni mwalimu wa mpira wa miguu. Timu hiyo ambayo inafundishwa na Jamhuri Kihwelo akisaidiwa na Mohamed Ayoub itacheza mechi ya mchujo ya michuano hiyo dhidi ya Cameroon.
Mechi hiyo ya kwanza itachezwa Machi 27 mwaka huu jijini Yaounde. Timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam wiki mbili baadaye.