Funga hao
Imeandikwa na Amir Mhando; Tarehe: 4th March 2011 @ 23:59 Imesomwa na watu: 152; Jumla ya maoni: 0
Hekaheka wakati wa mojawapo ya mechi za Simba na Yanga.
FUNGA hao! Leo hawatoki, mmekwisha, lazima kieleweke, hatuwakosi, leo mwisho wa hadithi.
Haya yote ni baadhi ya maneno yanayosemwa na mashabiki wa soka nchini inapofikia mechi ya watani wa jadi kwenye soka hapa nchini Simba na Yanga.
Leo alasiri kama ilivyokuwa nyakati zingine, timu hizo zinavaana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mchezo huo utamaliza ile hadithi tamu inayohusiana na maandalizi pamoja na mbwembwe ama hofu zinazohusiana na mchezo wa miamba hiyo, ambapo katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Simba ilifungwa bao 1-0, mfungaji akiwa Jerry Tegete.
Filimbi ya kumaliza mpira itakayopulizwa na mwamuzi Oden Mbaga, baada ya dakika 90 za waungwana hao kumenyana, ndipo kila upande utakapojua ulichovuna.
Ni mchezo ambao huvuta hisia za mashabiki wengi wa soka, ambao huwa hautabiriki hata kama moja kati ya timu hizo inaonekana uwezo wake ni mdogo kulinganisha na nyingine.
Yanga inaingia uwanjani ikiwa na nguvu kubwa, huku ikiongoza ligi hiyo kwa pointi 38 na imefungwa mechi moja na kushinda 11 na sare tano ikiwa imecheza mechi 17, wakati Simba yenyewe inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 37 imeshinda mechi 12, sare moja na imefungwa tatu.
Yanga inaingia ikiwa na safu inayotisha ya ushambuliaji ikiongozwa na Mzambia Davies Mwape na Jerry Tegete ambao katika siku za karibuni wamekuwa tumaini kubwa la timu hiyo katika ufungaji.
Lakini timu hiyo inayonolewa na Mganda Sam Timbe ambao huo utakuwa mchezo wake wa kwanza kukutana na Simba tangu akabidhiwe timu karibu mwezi mmoja sasa inao nyota wengine katika safu ya ushambuliaji, ambao ni Idd Mbaga na Nsa Job.
Safu ya kiungo Yanga itakuwa naye Athumani Idd 'Chuji' aliyerejea tena uwanjani baada ya kujichuja kwa muda kutokana na kutofautiana na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mserbia Kostadin Papic.
Pia itamtegemea Juma Seif na Omega Seme hasa kufuatia taarifa kuwa Nurdin Bakari ni mgonjwa. Safu ya ulinzi itakuwa na Nadir Haroub 'Cannavaro', Nsajigwa Shadrack, Stephano Mwasika na Chacha Marwa ambao watahakikisha kipa Yaw Berko hapati madhara.
Kwa upande wa Simba inayonolewa na Mzambia Patrick Phiri, safu yake ya ushambuliaji itawategemea Waganda Emmanuel Okwi, Patrick Ochan, Shija Mkina na Mussa Mgosi'.
Lakini miamba hao wanayo lulu mpya katika upachikaji mabao huyu ni Mbwana Samatta ambaye ameanza kuichezea timu hiyo duru la pili kutokana na kutoanza mzunguko wa kwanza baada ya uongozi wa Simba kushindwa kumtekelezea baadhi ya ahadi walizokubaliana.
Samata amekuwa tumaini la mashabiki wa Simba ambao jina lake hivi sasa lipo mdomoni mwao kama lilivyo la Mwape kwa mashabiki wa Yanga.
Samatta msimu uliopita alikuwa African Lyon. Upande wa kiungo inao Amri Kiemba, Jerry Santo na Nico Nyagawa, huku kwenye ulinzi ikiwategemea Kelvin Yondani, Juma Jabu, Juma Nyoso na Haruna Shamte wamlinde kipa Juma Kaseja asipate madhara.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Januari 12 mwaka huu Uwanja wa Amaan Zanzibar katika mchezo wa fainali Kombe la Mapinduzi, ambapo Simba ilishinda mabao 2-0.
Rekodi zao kwa mwaka jana timu hizo zilikutana mara tatu, ambapo katika ligi Simba ilishinda mara moja mabao 4-3 Aprili 18 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga nayo ikashinda kwa penalti 3-1 Agosti 21 katika mchezo wa Ngao ya Hisani na Oktoba 16 Yanga ikashinda bao 1-0.
Mwaka juzi Oktoba 31 Simba ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Mgosi, wakati Aprili 21 mwaka huo zilifungana mabao 2-2, ambapo katika sare hiyo mabao ya Yanga yalifungwa na Bernard Mwalala na Tegete, wakati yale ya Simba yalifungwa na Ramadhani Chombo na Haruna Moshi ‘Boban;.
Aprili 27, 2008 timu hizo zilifungana bao 1-1 na Oktoba 26 mwaka huo Yanga ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Ben Mwalala, hivyo kuhitimisha unyonge wa Yanga kwa Simba baada ya kushindwa kupata ushindi karibu miaka sita.
Awali miamba hiyo baada ya mechi ya Aprili 27, ilikuwa ikutane Julai 27 mwaka huo Uwanja Mkuu wa Taifa, lakini mechi hiyo haikufanyika kutokana na Yanga kutopeleka timu uwanjani, katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu Kombe la Kagame.
Mwaka 2007 zilikutana mara mbili na zote Yanga ilifungwa, ambapo mara ya kwanza ilikuwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro katika fainali ya Ligi Ndogo na Simba kushinda kwa penalti 5-4 na kisha Yanga kufungwa tena bao 1-0 Oktoba Uwanja wa Jamhuri, Morogoro katika mchezo wa raundi ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara.