Simba, Yanga zafyeka nyota wao
Send to a friend Thursday, 03 March 2011 20:13 0
Kocha wa Simba,Patrick Phiri
Clara Alphonce
SIKU moja kabla ya mahasimu, Simba na Yanga kucheza katika mechi ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa, uongozi wa klabu hizo umewaengua vikosini baadhi ya wachezaji kwa kile kilichoelezwa utovu wa nidhamu.
Mara kadhaa inapokaribia mechi zinazohusisha timu hizo ambazo mara nyingi ni za kulinda heshima, kumekuwa na ulinzi mkali huku wachezaji wakichungwa na wakati mwingine kunyang'anywa hata simu zao.
Habari ambazo Mwananchi imezipata ni kwamba Simba imekwenda Zanzibar huku ikimwacha kiungo wake, Mohamed Banka kutokana na utovu wa nidhamu.
Zilisema habari hizo kuwa mchezaji huyo ameachwa kwa kile kilichoelezwa kuwa kocha wa timu hiyo, Patrick Phiri na uongozi mzima wa Simba umechoshwa na tabia ya utovu wa nidhamu ya mchezaji huyo.
Banka aliondolewa kambini kwa sababu alitoroka siku moja kabla ya mechi dhidi ya Mtibwa, na alipoambiwa ajielezee alikanusha taarifa hizo hivyo viongozi kuamua kumuacha Dar.
"Nilicheza mechi ya mtaani, siku moja kabla ya mechi na Mtibwa na niliporudi kambini nilijihisi malaria, nikaenda hospitali na kugundulika na malaria...viongozi walinitaka nijieleze, nikawaambia hivyo na wapo walionielewa na wengine hawakunielewa nikaachwa," alisema Banka.
Kwa upande wa Yanga ambayo ipo mjini Bagamoyo, kocha Sam Timbe amesema amemuacha Dar es Salaam, Ernest Boakye baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu.
Timbe alisema amemuacha Boakye baada ya kulalamika kuwa kocha anawapa mazoezi magumu wakati ni jukumu lake kutekeleza mazoezi hayo.
Ernest Boakye ameachwa kwa mara ya pili kambini, awali alitimuliwa mjini Tanga wakati Yanga ilipokwenda kucheza na Azam.
Naye Vicky Kimaro anaripoti kuwa wachezaji wa Simba wamewatoa hofu mashabiki wao na kuwataka wajitokeze kwa wingi uwanjani wakiwa wamevalia jezi zenye rangi ya timu hiyo.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti baadhi ya wachezaji hao ambao wamejichimbia Zanzibar wakijiandaa kwa mchezo huo, walisema wana ari ya hali ya juu na kwamba watahakikisha Jumamosi wanawafunga mdomo watani wao, Yanga.
Mganda Emmanuel Okwi ambaye alikuwa ni majeruhi alisema, "Mashabiki watulie tena wawe na matumaini ya ushindi mnono, waone vile tutakavyowaonyesha kazi Yanga, si unajua damu si njano damu ni nyekundu."
"Kila shabiki wa Simba aje akiwa amevaa nguo nyekundu wala asiwe na hofu, sisi tupo kamili hatuna majeruhi na kila mchezaji ana ari ya hali ya juu," alisema Okwi
Wakati Okwi akisema hayo, kiungo mchezeshaji wa timu hiyo, Jerry Santo alisema: "Tumejiandaa vizuri, tumejipanga hatuna presha, tena mashabiki wetu waje wakiwa wamebeba vitambaa vyekundu kila mmoja kushangilia ushindi."
Mechi hiyo ya watani wa jadi ni ya 108 katika ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara na katika mzunguko wa kwanza Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Wakati huo huo, Sweetbert Lukonge alisema kocha mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Jan Poulsen amesema kuwa anatarajia kuona mchezo mzuri na wenye ushindani mkubwa kutokana na ukubwa klabu hizo hapa nchini.
Poulsen alisema kuwa anatarajia kuona mchezo mzuri na waushindani ambao pia utakuwa na tofauti kubwa na mechi nyingine za Ligi Kuu kutokana timu hizo kuwa katika nafasi nzuri ya kunyakuwa ubingwa wa ligi hiyo.
"Kama walivyo Watanzania wengine wengi ni matarajio yangu kuwa mechi baina timu hizo itakuwa nzuri na yenye ushindani mkubwa kutokana na historia iliyopo baina ya timu hizo kila zinapokutana.
"Jambo kubwa la msingi, wachezaji wa timu zote mbili wanatakiwa kutulia na kuonyesha uwezo wao wa kutandaza soka na kudhilisha kuwa ni moja kati ya timu zinazostaili kuwa wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kimataifa," alisema Poulsen.