Kado, Samatta kuifufua Vijana Stars
Imeandikwa na Zena Chande; Tarehe: 22nd February 2011 @ 23:59 Imesomwa na watu: 184; Jumla ya maoni: 0
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 ‘Vijana Stars', Jamhuri Kihwelo ‘Julio', jana alitangaza kikosi cha wachezaji 25 kitakachojiandaa na mechi dhidi ya Cameroon kuwania kufuzu michuano ya Olimpiki itakayofanyika Uingereza mwakani.
Katika kikosi hicho, Julio amemwita kipa wa Mtibwa Sugar na timu ya Taifa, Taifa Stars, Shaaban Kado pamoja na mshambuliaji Mbwana Samatta wa Simba na kiungo Omega Seme wa Yanga.
Mara ya mwisho Vijana Stars ilishiriki mashindano kama hayo mwaka 1999 kuwania kucheza Olimpiki ya mwaka 2000 iliyofanyika Sydney, Australia, wakati wa utawala wa Chama cha Soka Tanzania (FAT-sasa TFF), ikiwa chini ya Mwenyekiti Muhidin Ndolanga, Katibu Mkuu, Ismail Rage, Makamu Mwenyekiti Subira Mambo (sasa marehemu) na Katibu Msaidizi Amin Bakhressa ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).
Timu hiyo katika hatua hiyo ya awali ilicheza na timu ya Taifa ya Ghana, ambapo mchezo wa kwanza uliofanyika mjini Acca, Ghana, Vijana Stars ilifungwa mabao 2-1 na ziliporudiana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru), Vijana Stars pia ilifungwa mabao 2-1 mgeni rasmi akiwa Frederick Sumaye wakati huo akiwa Waziri Mkuu.
Baadhi ya wachezaji waliokuwepo kwenye kikosi hicho cha mwisho cha Vijana Stars, ambao baadaye walikuja kung'ara na timu mbalimbali ni Renatus Njohole, Steven Mapunda, Athumani Machupa, Wilfred Kidau, Omari Kapilima, Ngawina Ngawina, Adinani Mohammed (sasa marehemu), Amani Simba, Abdallah Sabebe, Mnenge Suluja, Ally Mayay, Omary Tamba, Abuu Mkangwa, Victor Kilowoko.
Wengine ni Kelvin Mhagama, Lameck Sichula, Ephraim Makoye, Jumanne Sabula, Zuberi Katwila, Hussein Mataka, Paschal Tungaraza, Mtindi Ally, Kassim Issa na Athumani Machepe (sasa marehemu).
Tangu wakati huo Vijana Stars haikuwahi kucheza mashindano yoyote, badala yake TFF imekuwa ikitumia timu mbili za vijana ambazo ni ile ya chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), hivyo kuitwa kwa Vijana Stars baada ya miaka 12 ni hatua mpya katika maendeleo ya soka.
Kulingana na Ofisa Habari TFF, Boniface Wambura wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema shirikisho hilo kwa kushirikiana na benchi la ufundi limepanga kuitafutia timu hiyo mechi mbili za kirafiki kabla ya kuikabili Cameroon.
Kwa upande wake akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Julio alisema kwa kushirikiana na kocha mwenzake Adolph Rishard wametafuta wachezaji hao ambao wanaamini watafanya vizuri na kwa vile wengi wao ni vijana, hakuna shaka kuwa ndio watakaounda timu ya taifa ya wakubwa siku zijazo.
"Tumemchagua Kado kwa sababu yuko chini ya miaka 23 na tunajua ni kipa mzuri na pia kocha Jan Poulsen anamtumia kwenye timu ya Taifa, lakini tunamuomba tumtumie kwetu," alisema.
Timu hiyo itacheza mechi ya kwanza dhidi ya Cameroon Machi 26 mjini Yaounde. Timu itaanza mazoezi leo kabla ya kuanza kambi rasmi Jumamosi.
Kikosi kamili kilichotangazwa na Julio na timu zao katika mabano ni makipa: Salehe Malande (TSA), Daudi Gabriel (Azam FC), Shaaban Kado (Mtibwa Sugar).
Mabeki wa pembeni: Salum Telela (Yanga), Hassan Kessy (Mtibwa/TSA), Issa Rashid (Mtibwa Sugar).
Mabeki wa Kati: Zahoro Pazi (African Lyon), Mbwana Hamisi (Simba), Louis Tumba, Omary Mtaki (Azam FC), Babu Ally (Morani).
Viungo: Godfrey Innocent (Simba), Ibrahim Juma, Himid Mao, Salum Abubakar (Azam FC), Frank Damayo (JKT Ruvu), Samwel Ngasa (African Lyon). Wengine ni Jamal Mnyate, Cosmas Freddy (Azam FC), Edward Shija (Simba).
Washambuliaji: Benedict Ngasa (Moro United), Atupele Green (Yanga), Samatta (Simba) na Thomas Ulimwengu.