Miaka Minne Kizuizini bila ya Amri ya Rais | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Miaka Minne Kizuizini bila ya Amri ya Rais

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by kwamwewe, Apr 22, 2012.

 1. kwamwewe

  kwamwewe JF-Expert Member

  #1
  Apr 22, 2012
  Joined: Jul 15, 2010
  Messages: 1,313
  Likes Received: 118
  Trophy Points: 160
  [FONT=&amp]Katika mwaka 1968 Hakimu Seaton, Hakimu wa Mahakama Kuu; alitembelea gereza la Mwanza. Nilimuuliza kama kuna uhalali wowote juu ya kuwekwa kwetu kizuizini. Mkuu wa gereza akamwambia Hakimu kuwa hakuna karatasi zozote zilizoletwa pamoja na mawaziri wa zamani wa Zanzibar. Hakimu akaahidi kulifuatilia suala hili. Baada ya miaka minne tangu wakati huo, nikiwa katika gereza la Bukoba, Katibu wa Mkuu wa Mkoa alitoa shauri kuwa nimuombe Raisi anitoe kizuizini. Nalimwambia kuwa kwa vile sijui nini kosa langu la kuwekewa kizuizini naona sina hoja za kimsingi juu ya ombi langu. [/FONT]

  [FONT=&amp]Alinijibu, "Hapana shaka ulipotiwa kizuizini ulisomewa amri ya kutiliwa kizuizini." [/FONT]

  [FONT=&amp]Nilimwambia kuwa, vile ninavyo kumbuka mimi hapakuwepo amri ya mimi kutiwa kizuizini. Suprintendent wa magereza akanambia kuwa ilikuwepo amri, hapo akanisomea hio amri ambayo ikionesha kuwa inatokana na Raisi na ambayo imeandikwa kwa lugha ya kisharia. Amri hio inasema kuwa Raisi baada ya kutoshelezeka kuwa, fulani na fulani; akiwataja mawaziri wote wa Serikali ya Muhammad Shamte, kuwa walikhusika na vitendo vya uchochezi wa kukhatarisha salama ya nchi, alitoa amri tutiwe kizuizini. Nalipomuuliza amri hio ilitiwa sahihi lini, ilidhihiri ilikuwa ni mwaka wa 1968, baada ya muda mchache tangu pale nionane na yule Jaji Mkuu, Seaton kwenye gereza la Mwanza![/FONT]

  [FONT=&amp]Sisi tulivamiwa nchi yetu na kutiwa vizuizini katika mwaka wa 1964. Najuwa kulikuwa na mapinduzi (mavamizi) huko Zanzibar, na hicho kitendo cha kiharamia iwe kimetokea huko. Lakini tangu kati ya mwaka wa 1964 pale tulipotiwa vizuizini mpaka hii 1968 ambapo hii amri ya kutiwa kizuizini kutolewa na kutiwa sahihi; wakati huo wote - miaka minne - kuwekwa kwetu kizuizini na yeye Raisi Nyerere ambae ndie aliekuwa na hukumu yote huko Tanzania bara basi hakukuwa kisharia hata katika hio sharia ya kidhaalimu ya Tanzania. Kwa muda wa miaka minne kabla ya kutiwa sahihi hii amri ya kuwekwa vizuizini sisi tulikuwa basi ni wafungwa wake yeye Nyerere. Je, ndio inayumkinika katika muda huo iwe yeyote miongoni mwetu sisi tuweze kufanya vitendo vya uchochezi wa kukhatarisha salama ya taifa? Tujaalie kuwa inakusudiwa ule muda kabla ya kukamatwa na kutiwa kizuizini. Wakati huo sisi tulikuwa ni mawaziri wenye mas-ulia kwa vile tulichaguliwa kulingana na sharia ya kikatiba iliokuwepo nchini - Zanzibar - wakati huo. Je, sisi wakati huo tutaweza kuwa tutende kama vile ilivyoelezwa katika hio amri iliotiwa sahihi na Julius Nyerere? Kama itakavyokuwa, hilo taifa linalo elezwa kuwa ni Tanzania; halikuwepo kabla ya sisi kukamatwa na kutiwa vizuizini. Huyo ndio mkuu wa nchi, anaejigamba kuwa yeye ni mwenye kuweka haqi, anafika kuzuwa na kupanga uwongo kama huo; ni jambo la kushangaza sana; lakini kwa watu kama yeye sio ajabu kulitenda. Baada ya kupata hoja hizi ndipo nilipomwandikia Raisi, bila shaka maandishi yangu yalikuwa ni ya upole na kweli za hakika. Sikupata majibu. Kwa hakika sikupata hata mara moja jawabu au hata kuarifiwa kuwa zimefika, baruwa zangu kadhaa wa kadhaa nilizompelekea Nyerere, tangu niko kizuizini na hata baada ya kutoka. Utaritibu wa hishima kama hio Tanzania inaonekana ni mpango wa kikoloni uliokwisha pitwa na wakati.[/FONT]

  [FONT=&amp]Dr. Kleru alikuwa ni Mkuu wa Mkoa aliepigwa risasi na mkulima, Abdulla Saidi Mwamindi; siku ya krismasi mwaka 1971. Mkulima huyu, Abdulla Saidi, alikuwa ni miongoni mwa watu kadhaa wa kadhaa walionyang'anywa mashamba yao kwa kuwanzishia vile vijiji vya ujamaa. Jeuri ya Mkuu wa Mkoa huyu ilifurutu ada. Waliokuwa wakiteswa na kudhulumiwa na Mkuu wa Mkoa huyu walishitaki kwa wakuu wa chama. Kila wakishitaki huambiwa wakashitaki polisi; na wakifanya hivyo. Kamanda wa Polisi, Abubakar aliwaonya wakuu huko Dar es Salaam juu ya vitendo viovu na vya kuudhi vya Mkuu wa Mkoa huyu na juu ya ile tabia yake ya ulevi kufika kuanguka na kuingiliwa na wahuni. Baada ya kupigwa marisasi na kuuliwa, wale jamaa wote waliokuwa wakipeleka mashtaka yao Polisi walikamatwa na kuwekwa kizuizini mpaka Abdulla Saidi Mwamindi ahukumiwe na kunyongwa. Hata kabla ya kesi kumalizika, magazeti na vyombo vyote vya khabari vya Serikali na vya Chama, vyote vilianza shutuma zao, sio tu dhidi ya Mwamindi, bali dhidi ya wakulima wote, huku wakisemwa, "mabepari", "wanyonyaji", "wakoloni" na makhaini". Mudhahara uliopangwa na Sirikali ukaingia njiani kupita kuwashutumu na kuwalaani watu hawa. Kwa hali hii ikawa Mwamindi kesha hukumiwa na vibaraka vya Sirikali hata kabla ya kufikishwa mahakamani. Mashahidi wote wale ambao wangeliweza kutowa ushahidi japo kuthibitisha juu ya vitendo vya uchokozi vya yule Mkuu wa Mkoa walizuiliwa mpaka pale kesi kumalizika. Khatuwa hii ilikusudiwa kumtia khofu yeyote yule aliekuwa na fikra ya kutaka kutowa ushahidi upande wa mshitakiwa. Hivi ndivyo sharia inavyo firigiswa katika nchi kama hivi Tanzania wakati ambapo sharia ya kumtia mtu kizuizini bila ya kupelekwa mahakama inatumika. Watu kumi na mbili wa Iringa pamoja na yeye Mwamindi mwenyewe walikuwa pamoja na mimi gerezani Dodoma. Kamanda wa Polisi Abubakar, na yeye vilevile aliwekwa na sisi siku mbili gerezani akiwa yumo katika pirika za kuhamishwa kutoka gereza hii na kupelekwa gereza jengine.[/FONT]

  [FONT=&amp]Ilani nyingi zilitolewa na kutangazwa ulimwenguni juu ya maafa na mateso katika magereza ya Zanzibar na Pemba. Lakini hapana lililosemwa na kuelezwa walimwengu kukhusu mateso yanayowapata wazuiwa katika magereza ya Tanzania bara. Sio kuwa uwovu na mateso wanayotendewa wazuiwa magerezani huko Tanzania bara hayajuulikani; mengi yake hayafiki ulimwenguni basi kwa sababu ya kukosekana demokrasia na heshima ya haki za binadamu juu ya haki ya kueleza na kujieleza. Kutokana na hali hii, mateso na vitendo vya kikhabithi havielezwi nje kwa walimwengu kukhofia hao watakaoeleza kuadhibiwa na utawala wa kidikteta. Niliona kwa macho yangu nilipokuwa gereza la Mwanza, wakati ambapo Superintendent Odenyo ndie aliekuwa mkuu wa gereza wakati huo; niliona wafungwa walipozuiliwa chakula na maji kwa muda wa siku nne, kisha wakapelekwa hospitali (nusu maiti) na ripoti kuwa (ati) walikuwa wamegoma kula. Nilipokuwa Dodoma nilikuwa nikisikia kadhia kama hizo. Nikisikia, kwani baina yetu ilikuwa ni kuta, baina ya chumba niliokuwemo na vile vyumba vya mateso. Katika gereza la Dodoma aliekuwa katili hivyo ni Ofisa Mkuu, aliepangwa jina "Iron Face" (Uso wa Chuma), kwa vile akijuulika kuwa hajapata kuwa na huruma. Mkuu wa magereza hapa, alifika kuwa hajishughulishi tena na kazi yake; hivi ni kwa sababu kwa hichi cheo chake cha juu na daima kuwemo katika vikao na sherehe za kisiyasa, takribani alimuachilia uendeshaji wote wa gereza mikononi mwa msaidizi wake - huyu Ofisa Mkuu. Mabwana wawili hawa waliyafanya maisha ya gerezani hapa hayastahamiliki hata kidogo. [/FONT]

  [FONT=&amp]Ile mikutano ya kawaida ya kila Jumamosi ambapo ofisa mas-uli hutarajiwa asikilize malalamiko ya wafungwa ikawa haifanywi tena. Ziara za kila mwezi gerezani za Mahakimu mbalimbali nazo pia zikasita. Wafungwa hutiwa gerezani na kufika kutolewa bila ya kujuwa kuwa wanahaki ya kuwasiliana na watu wao. Inafaa ifahamike kuwa hivi kuharibika hali kiwango hichi, sio tu katika gereza la Dodoma. Niliiona hali kama hiyo katika gereza la Mwanza. Gereza la Bukoba ilikuwa haijambo pale nilipoondoka. Lakinibasi, wakuu wa kisiasa; kama vile Mkuu wa Mkoa na Mawaziri dhaahir shaahir walikuwa wakijiepusha kuyazuru magereza na kujuwa hali za wafungwa na wazuiwa waliomo humo magerezani. Ama Raisi na Makamu wa Raisi, si dhani kama iko siku wamewahi kuzuru gereza lolote lile katika Tanzania bara, licha kuzungumza na mabwana au mabibi waliowatia humo magerezani. Hali katika gereza la Dodoma ilizidi kufanywa kuwa mbaya kwa ukhabithi wa huyu "Uso wa Chuma" na kulemaa kwa ulevi wa marungi Msaidizi wa Superintendent.[/FONT]

  [FONT=&amp]Mpango ulifanywa kumuuwa "Uso wa Chuma". Mmoja wa wafungwa aliweza kupata kisu na akataka kumpiga nacho huyo "Uso wa Chuma", kwa bahati akaanguka kifudifudi, kichwa chake mbali na yule mfungwa ambae alikuwa na pingu za chuma miguuni mwake na yeye vilevile akaanguka upande wake. Wakati huo mfungwa aliweza basi kuipata miguu ya "Uso wa Chuma" na kuanza kumpiga visu vya miguuni mpaka pale ilipowezekana kuzidiwa nguvu akanyang'anywa hicho kisu. Hapo tena akaingiliwa mfungwa huyo kupigwa marungu mpaka akawahijiwezi ndipo alipotiwa pingu za mikono. Askari wa gereza akaamrishwa kumpiga marisasi ya miguu. Hivyo ikawa kafungwa kila upande na marisasi miguuni mwake, hapo tena akasukumizwa katika chumba cha adhabu. Baadae kidogo msaidizi wa superintendent akaja na yeye akaanza kumpiga vile alivyopenda. Vilio vyake tukivisikia kutokea katika hicho chumba cha adhabu alimokuwemo na tukamuona askari aliekuwa zamu kwenye kidungu akigeuza uso na kupiga ukelele: "Wanamuuwa huyu mtu!" Binadamu huyu akavurumishwa tena humo chumbani kisha bomu la kutowa machozi likatupwa katika hicho chumba ambacho sehemu yake ya kupitia upepo ni ndogo kabisa. Usiku uleule akajifia.[/FONT]

  [FONT=&amp]Asubuhi yake wafungwa wote wakasimamishwa kwenye uwanja na maiti ikaletwa mbele yao uchi kama alivyozaliwa. Hapo tena msaidizi wa superintendent akawa anamchocha maiti kwa gongo huku akimwambia yule maiti: "Inuka uwaambie wenzio vipi ulivyokuwa hodari, na nini mwisho wa uhodari wako?" Baada ya hivyo tena akawahutubia wafungwa kwa kuwaambia kuwa hivihivi ndivyo tutakavyomfanya yeyote yule miongoni mwenu asiposhika adabu yake. Hapo tena wafungwa wote wakafungiwa vyumbani mwao kisha mabomu ya kutowa machozi yakatupwa humo vyumbani mwao. Haya yalifanywa kwa makusudio ya kuwataka watajane wale waliokhusika na mpango huu. Haukupita muda isipokuwa wengi wakatajana na kukiri makosa yao. Lakini adhabu na mateso yaliendelea kwa wiki kadhaa wa kadhaa. Chakula kikapunguzwa, hata kwetu sisi wazuiwa. Kila mtu alitaraji mauwaji haya yatafanyiwa uchunguzi na hukumu ya haki kupitishwa. Askari wa gereza ikawa wanasema hadharani kuwa ukifanywa uchunguzi watawaambia askari Polisi hakika ya mambo ilivyo. Lakini hapana lilokuwa. Tulisikia katika redio, kama maneno ya kupita tu yaliosemwa Bungeni - kwa woga - na mmoja wa Wabunge kuwa kulikuwa na askari makhabithi walio waadhibisha wafungwa mpaka kufika kuwauwa. Kubwa lililotokea ni uhamisho wa kawaida wa maofisa wa magereza wa vyeo vya juu kutoka magereza mbali mbali nchini. Khabari ikamalizikia hapo.

  Katika nchi yenye sheria ya kutiwa watu vizuizini bila ya kupelekwa mahakamani, kelele zozote zile ni sawa na mbwa mwenye kubweka hazina athari yoyote ile, na sharia basi ni kwa kumtumikia bwana mtawala aendelee katika utawala wake na atende vile anavyopenda.[/FONT]
   
Loading...