Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
MGENI KARIBU, JUISI YA PILIPILI.
MWENYEJI:
Karibu mzee Chali, ukaribie nyumbani,
Uketi upige wali, upoze chango tumboni,
Kisha tujalie hali, za wenzetu Kinondoni.
Karibu wetu mgeni, juisi ya pilipili.
MGENI:
Loo! msinite Chali, jina langu Abuduni,
Nina njaa kwelikweli, ninawapa shukurani,
Hali zao afadhali, watia gia angani.
Ni mwenyeji si mgeni, asante kwa pilipili.
MWENYEJI:
Somo la uliberali, tulo nao Buguruni?
Sema wamelikubali, bila kinyongo rohoni,
Ama hawajakubali, wamelitupa jaani?
Karibu wetu mgeni, juisi ya pilipili.
MGENI:
Naona wamekubali, watazame visogoni,
Wakiliwa na ugali, wanachoma ulimini
Ni michicha kwelikweli, wenye miba vikonyoni,
Ni mwenyeji si mgeni, asante kwa pilipili.
MWENYEJI:
Ya kwao ulo kubali, yatupie barazani,
Tupate kuyajadili, na kuyapima mzani,
Tuyabebe yalo kweli, tuyatumie kundini,
Karibu wetu mgeni, juisi ya pilipili.
MGENI:
Sina nilo yakubali, hamuwezi kuamini,
Tumewazidi akili, maono na umakini,
Nyumbu wamelala chali, wamevimbiwa majani,
Ni mwenyeji si mgeni, asante kwa pilipili.
MWENYEJI:
Kibopa wetu Munduli, naye ana hali gani?
Bado apiga msuli, wa kuwa bosi nchini?
Lile wazo kabadili, kuchunga ng'ombe porini?
Karibu wetu mgeni, juisi ya pilipili.
MGENI:
Tetesi kila mahali, 'taenda Ujerumani,
Ila hayana ukweli, yu mzima si utani,
Tatizo ni utapeli, uchungaji siuoni.
Ni mwenyeji si mgeni, asante kwa pilipili.
MWENYEJI:
Hatutaki kadi mbili, ichome ya msituni,
Kichwa na kiwiliwili, vyote virejee ndani,
Mazito yatukabili, hasa kule visiwani.
Karibu wetu mgeni, juisi ya pilipili.
MGENI:
Nimesharudi madhali, nina moja mkononi,
Ninaapa kwa Jalali, nisemayo ya moyoni,
Mengine tutajadili, kwa idhini ya Manani.
Ni mwenyeji si mgeni, asante kwa pilipili.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
0622845394 Morogoro.