Nimekaa na Method Mogella pale TCA ingawa tulikuwa tukisoma field tofauti. Tulishuhudia jinsi STAR anavyozaliwa katika dunia ya michezo. Jamaa alianza kubadilika ghafla kwa kila kitu mara baada ya kuchukuliwa kutoka timu fulani ya Namanga na kuanza kuchezea AICC.
Kabla ya hapo, alikuwepo kijana mwingine ambaye na yeye ni Merehemu Salehe Sonda (Mpare mwenye asili ya Kisukuma). Huyu jamaa alikuwa na shabaha sijawahi kuona. Katika mechi zote nilizoona akicheza, sikuwahi kuona mpira wowote aliopiga zaidi ya mita 1 kutoka kwenye nguzo ya goli. Haikujalisha yupo mbali kiasi gani na hii ikiwa na maana magoli yake yote, alifunga yakiwa yameingia si mbali sana kutoka kwenye mlingoti wa goli. Marehemu Sonda kabla hajaja Tech. College Arusha, alikuwa mchezaji wa SIMBA SPORT CLUB enzi Husein Tendwa anakufa.
Marehemu Method Mogella pamoja na kuja kuwa STAR, alibaki kuwa mtu yuleyule tuliyekuwa tunamfahamu. Nakumbuka mara mbili kuonana naye Dar baada ya kuwa amemaliza Chuo. Mara ya kwanza nilimuona Ilala akitokea Kariakoo akielekea Buguruni, na nikasikia mtu ananiita kwenye Bus. Mwanzo sikujali sana nani ananiita ila mwisho niliposikia jina langu ndiyo nikaangalia na kucheck vizuri nikamuona Mogella.
Mara ya pili ilikuwa kwenye jengo la Simba. Alitoka juu na kunikimbilia kuja kunisalimia. Nilishangazwa sana na hii kitu na hasa ukichukulia jamaa alikuwa tayari ni STAR pale Tanzania. Jamaa alikuwa BINADAMU na alibaki kuwa BINADAMU ingawa tayari alishakuwa mtu maarufu sana. Nimekutana na watu wengi sana wakisema "jamaa alikuwa best wangu sana."
Jamaa kwa habari nilisozisikia ni kuwa alienda Uarabuni na huko akarudishwa kwa matatizo ya afya na kutoka hapo ndiyo ukawa mwisho wa STAR wetu Method Mogella. Lazima nikiri kuwa pana wakati nilikuwa Dar na nikaishiwa pesa, nilisikia uchungu sana kumkosa huyu jamaa. Nilikuwa na imani kuwa angelikuwa hai, basi ningelimtafuta walau akanipa nauli ya Daladala.
Wee unayemfahamu nduguye, basi mwambie kuwa ni wengi tutamkumbuka sana Kaka yake Method na lazima wawe PROUD na ndugu yao ingawa ni siku nyingi hatunaye tena.
RIP SALEHE SONDA. RIP METHOD MOGELLA.