Na Zahoro Mlanzi
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba, Mbwana Samatta nyota yake inazidi kung'ara baada ya Klabu yake mpya ya TP Mazembe kumpeleka kufanya majaribio katika timu za Arsenal ya Uingereza na Anderletch ya Ubelgiji Desemba mwaka huu.
Samatta ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa 'Taifa Stars', alisaini mkataba wa miaka mitano hivi karibu wenye thamani ya sh. mil. 150 na mabingwa wa hao wa Afrika kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mlezi na Mshauri wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo alisema wameshamalizana na TP Mazembe na sasa Samatta ni mchezaji halali wa mabingwa hao wa Afrika.
"Namshukuru Mungu safari ilikuwa ya mafanikio na tumerudi salama, rafiki zetu walitupokea vizuri wakiongozwa na Mwenyekiti, Katanga Musa Katumbi na Meneja, Fredrick ambapo tulisaini mkataba bila matatizo yoyote," alisema Kasongo.
Alisema wamesaini mkataba wa miaka mitano, ambao kila baada ya miaka miwili lazima wakae tena chini kuzungumza ambapo pia suala la marupurupu limeachwa kutokana na timu hiyo kutoa marupurupu mengi kwa wachezaji wake.
Kasongo alisema mbali na kukamilisha suala hilo, pia klabu hiyo imewaambia wana mkataba na timu za Arsenal na Anderletch ambapo kila mwaka hupeleka wachezaji wanane kwenda kufanya majaribio na kwa mwaka huu, Samatta ni miongoni mwa wachezaji watakaokwenda huko.
"Unajua TP Mazembe wana mkataba na Arsenal na Anderltch wa kupelekeana wachezaji kufanya majaribio, Samatta atakwenda huko na atakaa kwa muda fulani na klabu hizo zikivutiwa na kiwango chake, yeye mwenyewe ndiye atakayeamua klabu atakaoichezea," alisema Kasongo.
Wakati huo huo, Kisongo alisema timu hiyo inatoa marupurupu ya kutosha kwa wachezaji wake ndiyo maana wachezaji wengi wanashindwa kwenda kucheza Ulaya kutokana na fedha za ziada wanazozipata.
Alisema timu hiyo hupewa maslahi makubwa, jambo ambalo linazidi hata mishahara wanayopata na ndiyo maana klabu nyingi za Ulaya zinashindwa kuchukua mchezaji kutoka katika timu hiyo.