EDO KUMWEMBE: Ukimuwaza Miquissone unaongeza heshima kwa Samatta

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
996
UNAPOANDIKA kitabu kinachohusu klabu ya Simba. Utaandika mwanzo, katikati, kisha kuna hizi kurasa za mwisho mwisho. Namaanisha hizi zama zetu za sasa. Utaandika sifa za baadhi za wachezaji. Utakutana na jina la Luis Miquissone.

Katika sifa rahisi zaidi kumwelezea Miquissone inabidi uandike tu ‘Mmoja kati ya wachezaji bora kuwahi kuvaa jezi ya Simba’. Ndiyo, unaweza kuwasahau baadhi ya wachezaji, lakini jina la Mmakonde huyu hauwezi kulisahau kiurahisi.

Aliikamata Simba miaka minne iliyopita. Kipi alishindwa? Hakuna. Alikuwa na kasi, alikuwa ana ubora mwingi wa kufunga, alikuwa na ubora mwingi wa kupiga chenga, pia alikuwa na ubora mwingi wa kupiga pasi za mwisho.

Akitokea pembeni Miquissone alikuwa hatari. Akicheza nyuma ya mshambuliaji mmoja anakuwa hatari. Alipoondoka hakukuwahi kuwa na mchezaji aliyefikia walau nusu ya ubora wake. Nani Peter Banda? Hapana. Pape Ousmane Sakho? Hapana. Walikuwa wachezaji wa kawaida tu ambao hawakuwahi hata kufikia ubora wa Hassan Dilunga wa Simba.

Waarabu Al Ahly walifika bei nzuri wakamchukua Miquissone. Haikushangaza sana. Bao alilowafunga katika Uwanja wa Benjamin Mkapa lilisisimua. Miquissone alikuwa katika ubora wake. Simba waliambulia pesa nyingi.
Nasikia amerudi tena Msimbazi. Majuzi ametangazwa kuwa mchezaji wao mpya baada ya klabu ya Al Ahly kuvunja mkataba wake. Kabla ya hapo walimpeleka kwa mkopo katika klabu ya Abha ya Saudi Arabia lakini nayo haikuamua kumchukua jumla.

Sasa hivi waliamua kumuita mezani na wamefikia makubaliano ya kuchana mkataba huku Simba wakimtangaza rasmi kuwa mchezaji wao. Ni hadithi ambayo kwa upande mmoja inasikitisha. Nini kimetokea kwake? Tulidhani safari ndio imeanza.

Mpira ambao Miquissone aliucheza katika misimu miwili aliyocheza nchini haujawahi kuchezwa na staa wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta wakati alipocheza katika Ligi yetu akiwa na African Lyon kisha Simba.

Miquissone kwa ubora ule tulidhani alikuwa anatuaga moja kwa moja kwenda mbali. Safari yake imekuwa fupi. Ameungana na mastaa wengi waliowahi kucheza Tanzania ambao tulikuwa tunasubiri kuwaona mbali lakini waliishia karibu.

Mmojawapo mwingine ni Emmanuel Okwi. Alicheza kiwango cha juu katika soka letu ambacho Samatta hakuwahi kuonyesha. Hata hivyo, Okwi alienda katika klabu ya kawaida Denmark, kisha pale Etoile du Sahel Tunisia, halafu Misri na sasa yupo Iran.

Hakuwahi kufika kule kwa kina Genk wala Napoli ambako tulimtazamia. Ni hadithi hii ya kina Miquissone. Ni hadithi hii ya wachezaji wengi wa ndani na wa nje ambao katika soka letu wanakuwa moto mkubwa lakini wanapoondoka huwa wanarudi kimya kimya.

Aliwahi kuniambia kiungo wa zamani wa Tottenham Hotspurs na timu ya taifa ya Kenya, Victor Wanyama kucheza soka Ulaya katika kiwango cha juu si jambo rahisi kama watu wengi wanavyofikiri. Ni mapambano ya machozi, jasho na damu.

Lakini kabla haujawaza sana kuhusu Ulaya, hata kucheza soka la Afrika katika kiwango cha juu kama ambacho Samatta alifanya na TP Mazembe kiasi cha kuwa mfungaji bora wa michuano ya Afrika na mchezaji bora wa ndani Bara la Afrika halikuwa jambo rahisi.

Haijashangaza sana hawa mastaa wengi kina Miquissone walikwenda katika klabu za juu za Afrika lakini maisha bado yamekuwa magumu kwao. Tulidhani wangeanza kutamba kwanza katika klabu hizo kabla ya kutorokea Ufaransa, Ubelgiji, Uturuki na kwingineko lakini mambo hayakuwa hivyo.

Tangu naifahamu vyema Ligi Kuu ya Tanzania ni wachezaji wawili tu ambao wamewahi kucheza soka la ngazi za juu Ulaya. Wawili tu. Alianza Nonda Shabani ambaye mwaka 1995 akiwa na Yanga aliondoka kwenda kucheza katika klabu ya Vaal Professional.

Baadaye akaibukia FC Zurich ya Uswisi. Kisha Rennes ya Ufaransa, halafu akaibukia Monaco, kabla ya kwenda Blackburn ya Ligi Kuu England wakati huo, kisha AS Roma halafu akaenda Galatasaray. Umeona klabu ambazo alizurura?

Halafu akafuata huyu mdogo wetu Mbwana Samatta. Alienda TP Mazembe kisha akaibukia Genk ya Ubelgiji, baadaye Aston Villa ya England, kisha Fenerbahce, halafu Royal Antwerp na kisha akarudi Genk na sasa yupo zake PAOK ya Ugiriki. Maisha haya hayawi rahisi sana.

Kwa Nonda unaweza kudai labda kwa sababu alikuwa Mcongo. Wakati mwingine inaonekana kama vile damu yetu ya Watanzania. Kwamba labda kwa sababu Congo imeshawahi kutoa mastaa wengi wa soka Ulaya pamoja na wanamuziki wengi waliotamba Ulaya basi labda Nonda alitembelea nyota. Vipi kwa Samatta?
Amepambana haswa kufika alipofika. Unapoona kina Miquissone wanarudi kutoka Cairo kuja Dar es salaam halafu Samatta anatoka Genk anakwenda Athens basi ujue kazi imefanyika. Kazi ambayo sijawahi kuona mchezaji wa kizawa akiifanya. Kazi ambayo sijawahi kuona hata wageni wanaifanya.

Kucheza nje kunahitaji mambo mengi nje ya soka la uwanjani. Nimewahi kumtembelea Samatta mara kadhaa na ukweli ni unahitaji moyo mkubwa kutamba Ulaya katika maisha yale ya baridi na mahitaji makubwa ya utimamu wa mwili na akili. Sio kila mchezaji wa Kitanzania anaweza.

Haijalishi una kipaji kiasi gani, ukweli ni kwamba kucheza soka katika kiwango cha Ligi kuu Ulaya unahitaji kujitoa. Lakini haishangazi pia kuona kuna wachezaji ambao hapa wanachukuliwa kama mastaa lakini wakienda nje wanashindwa kutamba.

Kuna maeneo ambayo ligi yetu bado ni nyepesi na haina ushindani mkubwa kiasi cha kumwndaa mchezaji wa Tanzania kutamba moja kwa moja mbele ya safari yake. Kina Clatous Chama walitamba Tanzania kisha wakaenda nnje. Mambo yakawa magumu. Waliporudi wameendelea kuwa Wafalme.

CREDIT: MWANASPOTI
 
Huyu naye anadai ni mchambuzi wa soka!! Hajaweahi hata kucheza soka kwa kiwango cha kitaifa ngazi ya juu!! Hawa wakiwa ndio wanaochambua soka letu, kusubiri tupige hatua tutasubiri sana!!
 
Huyu naye anadai ni mchambuzi wa soka!! Hajaweahi hata kucheza soka kwa kiwango cha kitaifa ngazi ya juu!! Hawa wakiwa ndio wanaochambua soka letu, kusubiri tupige hatua tutasubiri sana!!
Poa poa tumekusikia, haya turudi kwenye mada husika.
 
Huyu naye anadai ni mchambuzi wa soka!! Hajaweahi hata kucheza soka kwa kiwango cha kitaifa ngazi ya juu!! Hawa wakiwa ndio wanaochambua soka letu, kusubiri tupige hatua tutasubiri sana!!
Ficha ujinga unazan akina mourinho wamewai hata kuwa mastaa wasoka, au unazan makocha nawachambuzi nguli duniani wanazo balloon Dior
 
1)Wamisri wenyewe kwenda ulaya ni kwa mbinde

2) bila kusahau nduvu ya wakala uliyenaye(mf Choupo Morning typo tu Bayern) na Salamba

3) Nafasi unayocheza uwanjani. Strike ni rahisi kutoboa. KWA vile takwimu zake hazina mbambamba. Magoli sana sana
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom