Tanzania Daima linasema, 'Mbowe agoma kuipigia magoti mahakama'
WENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amekataa kujisalimisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha iliyoamuru akamatwe kwa kosa la kutotii amri ya kufika mahakamani hapo. Bila kumung'unya maneno, Mbowe alisisitiza kutojisalimisha akisema, "Ni bora nife nikiwa nimesimama kuliko kuishi nikiwa nimepiga magoti!"
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, alisema walishatoa ombi mbele ya Hakimu Mkazi Charles Magesa la kuruhusiwa kushiriki vikao vya kamati ya Bunge kwa mujibu wa nafasi zao, ambalo lilikubaliwa na mahakama hiyo.
Alisema katika ombi hilo, waliomba dhamana yao iendelee wakiwa nje jambo ambalo pia mahakama hiyo ililiridhia, hivyo kuwa na uhuru wa kushiriki vikao vya kamati ya Bunge la bajeti litakaloanza Juni 7, mwaka huu.
Alisema kutokana na maombi hayo, mahakama iliamuru wabunge wote waendelee na majukumu yao ikiwemo kushiriki vikao vya kamati za Bunge lakini baada ya siku chache alishangaa kusikia anatakiwa kukamatwa.
"Siwezi kuzuia hali hii, najua kuna jambo vyombo vya usalama vinataka kufanya ikiwemo kuwadhoofisha wabunge wa vyama vya upinzani hasa katika kipindi hiki cha kuelekea bajeti ya nchi.
"Kwa nafasi yangu ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni ni mjumbe wa Kamati ya Fedha ya Bunge, na ninasimamia serikali kivuli katika kuandaa maoni ya kambi ya upinzani, sasa kama wao wanaona wana haki ya kunikamata wafanye hivyo, lakini ni bora nife nikiwa nimesimama kuliko kuishi nikiwa nimepiga magoti… sitafanya hivyo kama wanavyotaka hata kidogo," alisisitiza Mbowe.
Alisema yeye na chama chake hawawezi kukaidi amri ya mahakama ila kinachotakiwa ni mahakama yenyewe kutanguliza busara kuliko kutanguliza utashi na shinikizo la kisiasa kutoka kwa watawala.
Hivyo, alisema kilichofanyika dhidi yake na watu waliomdhamini ni udhalilishaji hasa kwa nafasi yake kama Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Kwa upande wake Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, alisema kambi yao imepokea kwa mshtuko, masikitiko na mshangao mkubwa taarifa za Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Arusha kutoa amri ya kumkamata Mbowe.
Alisema kiongozi wao hakuhudhuria mahakamani mara mbili kwa kuwa alikuwa akihudhuria vikao vya kamati mbalimbali za Bunge vilivyoanza Mei 23 mwaka huu.
"Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshtushwa na amri ya kumkamata Mheshimiwa Mbowe kwa vile inakiuka moja kwa moja sheria, mila na desturi za miaka mingi zinazohusu kinga, haki na mamlaka ya Bunge na ambazo ni msingi mkuu wa demokrasia yetu ya kibunge.
"Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua na kulinda uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.
"Uhuru huu wa Kikatiba umetiliwa mkazo katika vifungu vya 5, 6 na 11 vya Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge ya mwaka 1988 vinavyokataza mbunge kukamatwa au kupewa amri ya kuhudhuria mahakamani wakati akiwa ndani ya eneo la Bunge au wakati Bunge limekutana bila kuwepo kwa kibali cha Spika," alisema Lissu ambaye ni mwanasheria kitaaluma.
Alisema maneno ‘eneo la Bunge' yametafsiriwa na kifungu cha pili cha sheria hiyo kumaanisha "ukumbi ambao hutumiwa kwa vikao vya Bunge, pamoja na ofisi, vyumba, vibambaza, maeneo ya wageni, bustani na maeneo mengine yaliyowekwa kwa ajili ya matumizi au malazi ya wajumbe, maafisa au wageni wa Bunge pamoja na njia zinazounganisha maeneo hayo na maeneo mengine yanayoweza kutangazwa na Spika kuwa ndani ya maeneo ya Bunge.
Alisema kwa maana hiyo, mbunge anapokuwa anahudhuria vikao vya Bunge au kamati zake au anapokuwa mahali pengine popote kwa kuitikia wito wa kuhudhuria vikao hivyo vya Bunge hawezi akakamatwa ili kutekeleza amri ya mahakama au ya chombo kingine chochote nje ya Bunge.
Akigusia kile alichokiita ‘upendeleo', Lissu alisema inashangaza kuona wabunge wa upinzani wakikamatwa na polisi bila kuomba kibali kwa Spika, lakini wanapotaka kuwakamata wabunge wa CCM hufanya hivyo.
Alisema wabunge wa kambi ya upinzani waliokamatwa kinyume cha sheria ni Freeman Mbowe (Hai), Godbless Lema (Arusha Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Meshack Opulukwa (Meatu), Ester Matiko (Viti Maalum CHADEMA) Felimon Ndesamburo (Moshi Mjini), Joseph Selasini (Rombo) na Madgalena Sakaya (Viti Maalum CUF).
Akitoa ushahidi wa vibali vinavyoombwa pindi polisi inapotaka kuwakamata wabunge wa CCM, alionyesha barua ya mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Mwanza SP B.M. Wakulyamba kwenda kwa Katibu wa Bunge, ambayo ilimwomba ruksa ya kumhoji Mbunge Dk. Titus Kamani (Busega, CCM) kuhusiana na njama za kutaka kumuua aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dk. Raphael Chegeni.
Kutokana na hali hiyo alisema hakuna mbunge hata mmoja wa CHADEMA au chama kingine cha upinzani ambaye kwa taarifa zao amewahi kuombewa kibali cha kukamatwa na polisi kama inavyoonekana kwa wabunge wa CCM.
Alisisitiza kuwa hali hiyo inadhihirihisha upendeleo wa wazi wa Jeshi la Polisi kwa wabunge wa CCM na uonevu kwa wapinzani.
"Tutapinga kwa nguvu zetu zote kitendo chochote cha kumtishia au kumkamata kiongozi wa kambi ya upinzani," alisema.
Alisema wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha inatoa amri ya kumkamata Mbowe, kiongozi huyo tayari analindwa na kinga ya Bunge.
"Mbowe ataendelea kulindwa na kinga hiyo kwa kipindi chote cha Mkutano wa Nne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pamoja na muda muafaka na wa kutosha kama unavyotambuliwa katika mila na desturi za Mabunge ya Jumuiya ya Madola hadi baada ya kwisha mkutano huo," alisema mnadhimu huyo.