na Salehe Mohamed
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema watu wanaotaka kumtisha kwa kutumia deni lenye utata ambalo moja ya kampuni zake ilikopa miaka 18 iliyopita, wanajidanganya na kamwe hawawezi kusababisha akatetereka.
Mbowe alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wanahabari kujibu tuhuma dhidi yake zilizoripotiwa na vyombo kadhaa vya habari wiki iliyopita, vikimhusisha yeye na wakurugenzi wenzake wa wa Mbowe Hotels Ltd, kukwepa kulipa deni alilokopa kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) mwaka 1990.
Alisema ukiangalia kwa makini habari hiyo ambayo kwa mara ya kwanza iliandikwa katika gazeti la kila wiki la Rai linalochapishwa kila Alhamisi, utaona dhahiri kuwapo kwa mkakati wa makusudi wa kundi fulani la watu ambao hakuwataja wanaolenga kumchafua na kumpaka matope wakitumia mzozo wake wa kibiashara na NSSF.
Ninaamini kwamba habari hizi zinakuja leo hii, si kwa bahati mbaya au kwa sababu ni habari muhimu na za kulisaidia taifa hili. Kwa hakika habari hizi zinalenga kuzima moto tuliowasha dhidi ya mafisadi wa EPA, Richmond, Buzwagi na wale wote wanaotafuna rasilimali za taifa hili. Ni wazi kwamba taarifa hizi zinakusudia kupotosha mwenendo mzima wa namna wapinzani na hususan CHADEMA tunavyotaka serikali iwashughulikie wezi wa EPA na wale wa Richmond.
Watu hawa wenye nia mbaya na taifa hili, kwa makusudi mazima wameamua kuvitumia vyombo vya habari kutimiza malengo yao maovu ya kuzima uzalendo wetu juu ya rasilimali za Tanzania na mapambano yetu dhidi ya ufisadi, alisema Mbowe.
Akitoa ufafanuzi kuhusu deni hilo la hoteli yake, Mbowe aliyekuwa ameongozana na mkewe, Dk. Lillian Mtei, ambaye pia ni mkurugenzi wa Mbowe Hotels Ltd, alikiri kukopa shilingi milioni 15 kutoka iliyokuwa NPF (sasa NSSF) mwaka 1990, kwa ajili ya kuendeleza mradi wake wa hoteli hiyo kama mjasiriamali.
Alisema hadi kufikia hivi sasa, hoteli yake hiyo tayari imelipa kiasi cha shilingi milioni 75, kiasi ambacho ni mara tano ya deni la msingi alilokopa na hivyo utata uliobaki sasa ni riba inayotokana na deni hilo.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA, ambaye katika mkutano huo alikuwa ameandamana pia na uongozi takriban wote wa juu wa chama hicho ukimuacha Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, alisema hesabu walizokokotoa kwa kuzingatia utaalamu wa kisheria na kihasibu, zinaonyesha kuwa kiasi cha deni kilichobaki kulipwa hadi hivi sasa hakiwezi kuzidi shilingi milioni 43 na si shilingi bilioni 1.2 kama ilivyoripotiwa katika vyombo vya habari wiki iliyopita.
Alisema si kosa wala fedheha kwa mjasiriamali au kampuni yoyote kupata mkopo kwenye taasisi za serikali au benki, lakini ni jambo la kusikitisha kuona watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri, hasa wale wa vyombo vya habari, wakiwa tayari kutumiwa na watu wachache wenye nia mbaya na taifa.
Mwenyekiti huyo katika kauli iliyoungwa mkono pia na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, aliyekuwa katika mkutano huo, alisema watu wanaoeneza taarifa hizo hawafanyi hivyo kwa bahati mbaya, bali wanataka kuona joto la walilopandisha la kutaka mafisadi wachukuliwe hatua kali za kisheria likizimwa.
Mbali ya Zitto, viongozi wengine wa CHADEMA waliokuwapo kwenye mkutano huo wa Mbowe kwa kile walichokielezea kuwa ni kuonyesha mshikamano wao kwa mwenyekiti wao, ni Makamu wa Mwenyekiti, Chacha Wangwe, Mbunge wa Mpanda Kati, Said Alfi, John Mnyika na John Mrema.
Katika hatua nyingine, Mbowe alisema wanasiasa wa upinzani wanaofanya biashara kama yeye, mara kwa mara wamekuwa wakilazimika kukabiliana na adha na vikwazo vya namna hii kimsingi vinavyolenga kuwakatisha tamaa.
Kuna wakati, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, alipata kusema kuwa mfanyabiashara yeyote atakayejiunga na CCM mambo yake yatamnyookea, alisema Mbowe.
Akiigeukia NSSF, Mbowe aliilaumu kwa kutokujua uchungu wa kutafuta fedha kibiashara, hali aliyosema ndiyo iliyosababisha wataalamu wake kuendelea kuibana kampuni yake ambayo siku zote imefanya biashara kihalali.
Mwizi na fisadi siku zote hajui uchungu wa fedha. Mimi sina kiwanda cha kuzalisha fedha, sitoi wala kupokea rushwa na kila fedha ninayotoa nahakikisha lazima iende kwa haki na kwa wale walioifanyia kazi
kinyume na hapo itakuwa ngumu kuipata fedha yangu.
Mimi si mwendawazimu hata nikatae kulipa deni nililokopa. Nimekopa fedha kutoka katika benki mbalimbali kwa mamilioni, tena kiasi kikubwa kuliko kile nilichokopa NPF na nimekilipa. Kwa nini nishindwe kuilipa NSSF? Deni hili lina utata na hata leo katika gazeti la The Citizen mkurugenzi wa NSSF amekiri kutojua kiasi hasa wanachotudai, alisema Mbowe.
Kuhusu madai ya gazeti la Rai kwamba yeye anaifilisi NSSF, Mbowe alisema kamwe shirika hilo haliwezi kufilisika kwa mkopo wa shilingi milioni 15 alizokopa, bali kutokana na mabilioni yaliyokopwa na wakopaji wanaotajwa na ripoti mbalimbali za mfuko huo ambao hawajawahi kutajwa, kushitakiwa wala kukamatwa.
Alipotakiwa kueleza ni kwa nini basi deni hilo halijalipwa kwa miaka yote hiyo, Mbowe alisema wakati wanakopa deni hilo mwaka 1990, hali ya kiuchumi hasa mfumuko wa bei vilikuwa vikipanda, hivyo mwaka mmoja baadaye walilazimika kuomba mkopo wa ziada kwa ajili ya kumalizia mradi huo wa Mbowe Hotels uliokuwa haujakamilika.
Alisema katika mazingira ya kushangaza, NSSF walikataa kutoa mkopo wa ziada kwa Mbowe Hotels Ltd, hata baada ya shirika hilo kukiri kuwa mradi huo ulikuwa ukihitaji fedha zaidi kukamilishwa.
Mwenyekiti huyo alisema kutokana na uamuzi huo wa NSSF ulioigharimu kampuni yake, walilazimika kwenda kukopa fedha hizo katika Benki ya CRDB walikopata mkopo ambao tayari wameshaulipa.
Kuhusu taratibu za ukopaji, Mbowe alisema ni jambo la kawaida kupitia na kutathimini upya mikataba ya biashara baina ya mkopaji na mkopeshaji, ili kuangalia mazingira ya biashara kulingana na uchumi wa nchi na mradi wa mfanyabiashara husika kama ambavyo Mbowe Hotels wamekuwa wakitaka ifanyike kila siku.
Alisema kutokana na kulitambua hilo, ndiyo maana wao waliamua kuwasilisha maombi ya kutaka kuongeza mkopo ili waweze kumaliza mradi waliokusudia, lakini hawakuweza kupata na badala yake wakafikishwa katika fedheha hii iliyofanywa kwa makusudi na kwa malengo maalumu.
Ninaamini umakini wa utaalamu wa kibenki haukutumika katika maamuzi haya sambamba na mlolongo wa kushughulikia suala hilo haukuwa na dhamira njema, lakini pia ninahoji uwezo wa kitaaluma wa mfuko kujishughulisha na biashara ya ukopeshaji, alisema Mbowe.
Alisema tangu mwaka 2003 wawakilishi wa Mbowe Hotels Ltd wamekuwa wakiwaandikia barua za kuwaomba NSSF wakubali mapendekezo ya kumaliza deni hilo. Juni mwaka jana, shirika hilo la umma lilikubali wito wa majadiliano ya kumaliza deni hilo, lakini hadi hivi sasa hawajaandika barua ya kuwataka kukutana na uongozi wa kampuni yake.
Katika kile alichokieleza kuwa ni mazingira ya ajabu, Mbowe alisema wakati mawasiliano yakiendelea, Januari 27, 2004, NSSF iliamua kwenda mahakamani kuomba wakurugenzi wa Mbowe Hotels Ltd wakamatwe kwa kushindwa kuheshimu amri ya kulipa deni, ombi lililokubaliwa.
Alisema Januari 8, 2007, mke wake alikamatwa na akapelekwa Mahakama Kuu Februari 20, mbele ya Jaji Amiri Manento ambako shauri hilo linaendelea.
Kama hiyo haitoshi, Mbowe alitumia mkutano huo kumponda Mwenyekiti wa taifa wa chama cha Sauti ya Umma (SAU), Paul Kyara, aliyekaririwa na gazeti la Majira akitaka kukamatwa kwake (Mbowe) na wakurugenzi wenzake kwa kushindwa kulipa deni hilo.
Mbowe alisema Kyara alipata kuwa CHADEMA kama Mweka Hazina na baada ya hapo akatoka na kuanzisha chama chake cha SAU. Siku zote amekuwa akiendesha kampeni za kuwapinga kama alivyomwekea pingamizi mwaka 2005 wakati yeye (Mbowe) alipogombea urais na katika uchaguzi wa hivi karibuni wa Kiteto akasimamisha mgombea aliyefanya kampeni sambamba na CCM.