Mauaji haya yamulikwe kwa makini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mauaji haya yamulikwe kwa makini

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, May 20, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 20, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  [​IMG]

  [​IMG]
  Maoni ya katuni.  Kuna mauaji yameripotiwa kutokea katika Kanda ya Ziwa yakihusu makada wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mauaji haya ingawa yanatajwa kama uhalifu wa kawaida, kwetu yameamsha hisia tofauti kabisa kwa jinsi yalivyotokea.
  Tukio la kwanza lilitokea katika Ofisi ya CCM Kata ya Isamilo ambako Katibu wa kata hiyo, Bahati Stephano, aliuawa kwa kuchomwa kisu ofisini kwake, tukio la pili lilitokea wilayani Bunda ambako kada mwingine wa CCM, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Salama A, Messo Kubuka, naye aliuawa kwa kukatwakatwa mapanga na watu wasiojulikana na maiti yake kuokotwa barabarani.
  Awali ya yote tunachukua fursa hii kutoa pole kwa ndugu, jamaa au marafiki walioguswa na misiba hii miwili; tunawapa pole huku tukiomba Mungu mweza wa yote awape moyo wa subira kukabili kipindi hiki kigumu cha kupoteza wapendwa wao tena katika mauaji ya kikatili mno.
  Ingawa hadi sasa hakuna ushahidi thabiti juu ya chanzo hasa cha mauaji haya, kuna dalili kwamba kuna nguvu za kisiasa nyuma yake. Sababu kubwa inayotusukuma kwenye hisia hizo ni ukweli kwamba taifa kwa sasa lipo kwenye nyuzi joto za juu kabisa kuhusu uchaguzi mkuu na waliouawa wana nafasi katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, walau kupitia vyama vyao.
  Hawa ni makada ambao kwa kawada wagombea ama ubunge au udiwani ndio huwatumia kufanikisha azma yao ya kupata ushindi iwe kwenye kura za maoni ndani ya vyama vyao au hata katika mpambano baina ya wagombea wa vyama. Kwa maana hiyo kusikia tu mtu anachomwa kisu au anapigwa mapanga bila wala kuporwa chochote tena wengine wakiwa wameshiriki mikutano ya kisiasa na mbunge wao, si jambo la kufumbia macho.
  Kwa kawaida taifa hili limekuwa na utamaduni wa muda mrefu wa kupingana bila kupigana katika siasa, watu wanatoka vyama tofauti wanapingana lakini mwisho wa siku wanabakia kuwa Watanzania, ndugu, jamaa, majirani wema na marafiki baada ya uchaguzi.
  Si vema kuruhusu siasa za chuki na uhasama kumea katika nchi yetu. Ni kwa maana hiyo tunasema ingawa hisia zetu hazijathibitika pasi na shaka yoyote, tungeomba vyombo vya usalama vijitahidi kadiri viwezavyo kuchunguza matukio haya mawili kwa undani ili kutambua msukumo nyuma ya mauaji haya.
  Itakumbukwa kwamba huko nyuma ilipata kuripotiwa kwamba kijana mmoja alipotea katika mazingira ya kutatanisha; huyu alikuwa kada chipukizi wa CCM, habari ambazo miaka ya 2000 vyombo vya habari viliandika kwa kina ni kwamba aliagizwa kupeleka barua Geita akitoka Mwanza mjini, lakini hadi leo hakurudi.
  Kadhalika, ni jijini Mwanza humo humo ambako miaka ya tisini tulishuhudia Mbunge wa Mwanza Mjini wakati huo, Shomari akimwagiwa tindikali ambayo ilimjeruhi vibaya shingoni mwake, mshambuliaji aliyetumwa alikuwa anakusudia kumjeruhi usoni; haya ni matukio ya kutisha ambayo yameripotiwa kutoka Mwanza au Kanda ya Ziwa kama ni kupanua wigo wa visa hivi vibaya.
  Kwa hali hii tunapozungumza habari za hisia za kisiasa hatuzungumzi tu kwa sababu ya kutaka kukuza mambo, tunaongozwa na mwalimu mkuu Historia, kwamba mambo huwa yana tabia ya kujirudia. Tunasukumwa na historia ndiyo maana tunataka vyombo vya dola kutafakari, kuchunguza na kuhakikishia wananchi kwamba taifa hili bado linaendelea kuendesha siasa za kiungwana, kupingana bila kupigana achilia mbali kuuana.
  Tunatoa wito huu tukitimiza wajibu wetu kwa jamii wa kutaka hadhari zichukuliwe ili kuzuia mabaya yasitokee katika taifa letu; tunasema haya kwa kuwa kukaa kimya wakati hali si salama hakutatuponya si sisi wa sekta ya habari, wanasiasa au wananchi kwa ujumla wao. Tunataka hadhari za kweli zichukuliwe.
  Kwa hiyo, tunaposema vyombo vya usalama vijikite katika uchunguzi wa masuala haya tunakusudia kwamba ukweli utakaofichuliwa uwekwe wazi ili jamii itambue wapi tulipo na ni changamoto gani mpya zinaibuka katika kuendesha shughuli zetu, ama za kisiasa au hata za kusaka kipato kwa njia ya uchuuzi au njia nyinginezo.
  Nia yetu ni nyeupe na wazi, kwamba tunataka taifa hili lizidi kuwa kisiwa cha amani kwa maana pana, kwanza jinsi tunavyoendesha mambo yetu kiungwana, lakini pia jinsi ambavyo tunajipanga kuepusha hatari zozote zinazotunyemelea kama Watanzania. Tuchukue hatua.  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...