Matumizi ya Benki kuu yaishtua Serikali

GAMBLER

JF-Expert Member
Nov 22, 2009
303
11
*NI UJENZI WA MAKAZI YA GAVANA , YASITISHA MIKOPO YA WAFANYAKAZI

Leon Bahati na James Magai

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo amesema serikali imeshtushwa na taarifa kuwa Benki Kuu (BoT) imetumia zaidi ya Sh1 bilioni kujenga upya nyumba anayoishi Gavana Benno Ndulu na kwamba wizara yake inachunguza uhalali wa matumizi hayo.

Habari zaidi zinasema BoT imesitisha nyongeza ya mikopo ya nyumba ya asilimia 50 iliyoidhinisha kwa wafanyakazi wake, hatua ambayo imekuja siku chache baada ya kuidhinishwa na menejimenti ya taasisi hiyo kubwa ya fedha.

Taarifa za matumizi hayo makubwa ya fedha hizo za walipakodi katika kujenga makazi ya gavana ziliripotiwa na Mwananchi Ijumaa iliyopita katika habari iliyoeleza jinsi nyumba ya kigogo huyo wa BoT ilivyogharimu Sh1.4 bilioni kuikarabati, kabla ya Ndulu kutoa ufafanuzi kuwa nyumba hiyo ilijengwa upya na si kwamba ilikarabatiwa.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano juzi, Mkulo alisema pamoja na kushtushwa na taarifa hizo, jambo hilo ni kubwa na linahitaji umuhimu wa kipekee kuchunguzwa ili walipakodi wajue ukweli wa matumizi ya fedha wanazoilipa serikali.

"Lazima tuchunguze ukweli wa taarifa hizo, maana hili ni jambo kubwa na linamhusu mtu mkubwa," alisema Mkulo katika mahojiano na gazeti hili.

Mkulo alisema kuwa alikuwa safarini nje ya nchi na kwamba baada ya kurejea nchini juzi, ofisi yake itatumia wiki hii kufanyia uchunguzi suala hilo na wiki ijayo atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweka mambo yote hadharani.

Akitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo wiki iliyopita, licha ya kukiri matumizi hayo ya fedha, Profesa Ndulu alisema kuwa nyumba anayoishi ilianza kujengwa kutoka chini na kwenye kiwanja ambacho ni cha BoT.

"Nyumba haijakarabatiwa, imejengwa from the ground (kutoka chini)... ni tofauti kukarabati na kujenga nyumba mpya... huu ni upotoshaji wa wazi na kujaribu kuchafua mema," alilalamika gavana huyo.

Aliongeza: "Napenda taarifa sahihi ambazo hazipotoshi ukweli kwa maana taarifa kama hizo zinaharibu kila kitu, kizuri na kujenga taswira mbaya kwa wananchi, kitu ambacho si sahihi."

Mwananchi toleo la Desemba 23, mwaka huu iliripoti kuwa nyumba anayoishi sasa gavana huyo ilikarabatiwa kwa takriban Sh1.4 bilioni na kwamba ilikuwa kwenye mradi wa kukarabati nyumba za vigogo wanne wa BoT; ya Ndulu na manaibu wake watatu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyumba nyingine ni pamoja na aliyokuwa akiishi gavana wa zamani, marehemu Daudi Balali ambayo Prof Ndulu alidaiwa kuikataa kwa kuwa haina bwawa la kuogolea.

Licha ya tuhuma hizo, BoT inalalamikiwa kwa kujiidhinishia mamilioni ya fedha za mikopo yenye tofauti kubwa ya viwango baina ya wafanyakazi wa chini na vigogo.

Katika hatua nyingine, BoT imesimamisha nyongeza ya mikopo ya nyumba kwa asilimia 50, ambayo menejimenti hiyo iliridhia nyongeza yake ambayo watumishi wa kada ya chini wangejipatia mkopo wa hadi Sh30milioni na vigogo hadi Sh100milioni.

Habari zilizolifikia Mwananchi na kuthibitishwa na Gavana wa BoT, Profesa Ndulu zimethibitisha kusimamishwa kwa mikopo hiyo.

Kabla ya kusimamishwa kwa mikopo hiyo baadhi ya watumishi wa taasisi hiyo walikaririwa na vyombo vya habari (siyo Mwananchi), wakilalamika kuwa nyongeza hiyo ililenga kuwanufaisha zaidi vigogo.

Walidai kuwa matarajio yao yalikuwa wafanyakazi wa kawaida wangepewa kipaumbele zaidi, lakini hali ikawa kinyume.

Kusimamishwa kwa mikopo hiyo pia kumeibua mitazamo tofauti kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo, wengi wakionyesha mashaka kwa hatua hiyo wakidai inawaaminisha kuwa nyongeza hiyo ilikuwa na lengo la kuwanufaisha zaidi wakubwa.

"Hii inaleta mashaka kwani kama hapakuwa na tatizo ni kwa nini baada tu ya kuripotiwa kwenye vyombo vya habari ndipo ikasimamishwa?" alihoji mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo.

"Sina hakika sana juu ya sababu zilizofanya mikopo hiyo isimamishwe na hatua au marekebisho yanayokusudiwa kuchukuliwa, lakini hii inaweza kutoa picha kuwa kuna mambo hayakuwa sawa ndio sababu imesimamishwa baada ya vyombo vya habari kuiripoti."

Lakini juzi, Gavana Ndulu alisema lengo la kusitisha mikopo hiyo ni kutoa elimu zaidi kwa wafanyakazi hao kuhusu mikopo hiyo.

Alisema imebainika kuwa wafanyakazi hao hawakuwa na elimu ya kutosha kuhusu vyongeza hiyo ya viwango vya mikopo na kwamba ndio maana walikaririwa na vyombo vya habari wakilalamika.

Ndulu alifafanua kuwa upo umuhimu wa elimu hiyo kwa wafanyakazi ili wasije wakabeba mzigo wasiouweza kwa kuwa mikopo hiyo ina masharti mengi kwa mkopaji.

"Tumeongeza masharti mengi na hatutaki mtu abebe mzigo asiouweza. Tumegundua wafanyakazi wengi hawakuelewa na ndio maana tumeona kuna umuhimu wa kuelimishana kwanza," alisema Prof Ndulu.

"Pengine elimu ilipaswa itangulie kwanza. Mara nyingi hivi vitu ni kuelewana. Ilionekana wengi hawakuelewa ndio sababu wakalalamika kwenye vyombo vya habari. Kwa hali hiyo sasa tumeisimamisha mikopo hiyo kwanza na tayari nimewaagiza maofisa husika kusimamia utaoaji wa elimu hiyo."

Gavana Ndulu alisema mfuko huo wa mikopo kwa nyumba umekuwepo kwa muda mrefu na kwamba kilichofanyika ni kuongeza tu viwango vya mikopo ili kuendana na mabadiliko ya hali ya maisha.

Kuhusu chanzo cha pesa hizo, alisema si za serikalini bali zinatokana na operesheni mbalimbali za benki hiyo ikiwa ni pamoja na riba inayotokana na mikopo mbalimbali wanayoitoa kwa serikali na kwa mabenki mengine nchini.

Kuhusu masharti ya mikopo hiyo alisema inapotokea mtumishi amestaafu kabla ya kumaliza kurejesha mkopo huo, basi sehemu ya mafao yake hutumika kufidia kiasi kilichosalia.

BoT imekuwa ikiangaliwa kwa karibu tangu kuibuka kwa kashfa ya wizi wa zaidi ya Sh133 bilioni kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

Taasisi hiyo pia imekumbwa na kashfa nyingine kama za bima ya maghorofa yaliyo jijini Dar es salaam na Zanzibar, kuongeza gharama katika uchapishaji wa noti na matumizi mabaya ya madaraka katika ujenzi wa maghorofa pacha.

Wafanyakazi wa benki hiyo pia wamejikuta kwenye kashfa za kufanikisha njama za wizi, kuajiriwa kwa kutumia vyeti vya kughushi na tuhuma za watoto wa vigogo kupewa ajira za upendeleo.
 
Eti Serikali imestushwa leo hii baada ya zaidi ya wiki nzima ya mjadala huu kuwa hewani! Kweli hii ni ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya! Je, Ndullu atawajibishwa!? Au serikali baada ya kustushwa hakuna hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi ya Ndullu na manaibu wake. Ndullu mshahara wake ni $15,000 labda ukiweka na rupurupu anaweza kufika $20,000 au zaidi kuna haja ya kumpa onyo kali kwa ufujaji wa pesa na pia kukatwa mshahara wake kwa 50% kwa miaka mitano au kipindi kilichobaki katika mkataba wake na hastahili tena kupewa mkataba mwingine.
 
Wanajibaraguza tu..unajua hiki ni kipindi cha mpito..wanajua bila kuzichanga vizuri karata, kutakuwa hakuliki hakupakuliki 2010.
 
Mkuu hata kwenye EPA tuliambiwa hivyo hivyo na Luhanjo, serikali imeshtushwa na rais amekasirika sana, well yako wapi????????
 
Tatizo ni kwamba, I doubt kama hata kuna guidelines za kusema gavana anatakiwa kukaa nyumba ya gharama gani. Kwa hiyo at the end of the day huwezi hta kusema kwamba rules zimekuwa violated.

Ndiyo upungufu wa systems zetu, bado tunaendeleza oral tradition, nothing significant is written down.Halafu worse still, vitu kama hivi wala haviwezi kusababisha watu waanze ku establish hizi protocols.

Wakati huo huo wenzetu mama akinywa pombe na kuendesha watoto, halafu akapata ajali, anatungiwa sheria mahsusi within 3 months.
 
i can say jk administation is the worst......wanacheza na maisha yetu
 
Mkuu hata kwenye EPA tuliambiwa hivyo hivyo na Luhanjo, serikali imeshtushwa na rais amekasirika sana, well yako wapi????????

- Eti Rais aliwahi kukasirikia wizi wa hela za serikali? When was that? Rostam na Lowassa wanafanya nini bungeni kama Rais hapendi wizi? ahggrrrrrrr!

Respect.

FMEs!
 
Tatizo ni kwamba, I doubt kama hata kuna guidelines za kusema gavana anatakiwa kukaa nyumba ya gharama gani. Kwa hiyo at the end of the day huwezi hta kusema kwamba rules zimekuwa violated.

Ndiyo upungufu wa systems zetu, bado tunaendeleza oral tradition, nothing significant is written down.Halafu worse still, vitu kama hivi wala haviwezi kusababisha watu waanze ku establish hizi protocols.

Wakati huo huo wenzetu mama akinywa pombe na kuendesha watoto, halafu akapata ajali, anatungiwa sheria mahsusi within 3 months.

- Ndio maana mzungu mmoja alionyeshwa kushangazwa sana kusikia Mkapa amesoma Columbia University, na kwamba Chenge amesoma Havard alisema no way man! I hope you are not joking!

Respect.


FMEs!
 
Serikali inashangaa nini waache kutufanya sisi wajinga. Wakati hundi zinasainiwa wizara ya fedha ilikuwa haijui au BOT wanafanya mambo yao wenyewe bila kuhusisha wizara ya fedha naomba kuuliza swali la nyongeza mnijuze labda mwenzenu nipo bado kwenye enzi za TANU. Hii nchi kweli inaenda kama tractor lililokosa mafuta ilimradi liende.
 
Date::12/30/2009Uchunguzi gharama za ujenzi BoT ufanyike
broken-heart.jpg

HABARI za ujenzi wa nyumba ikiwamo ya gavana wa Benki Kuu (BoT), Benno Ndulu kutumia mamilioni ya shilingi wakati huduma za msingi za wananchi wa Tanzania zikiwa katika hali mbaya zimestua umma.

Habari hizo zinasema kwamba nyumba hiyo iliyojengwa na BoT kama makazi ya gavana imegharimu zaidi ya Sh 1 bilioni kiasi ambacho kingeweza kutumika katika kupanua huduma za afya, elimu kwenye maeneo ya vijijini.

Hatukatai kwamba gavana anapaswa kukaa katika nyuma nzuri, lakini tuna wasiwasi kwamba kiasi hicho cha fedha kinachodaiwa kutumika katika ujenzi wa nyumba hiyo ni kikubwa, lakini vilevile, magavana waliomtangulia huyu wa sasa walikuwa wana makazi ambayo umma unapaswa kuelezwa yamekwenda wapi hadi tuanze kujenga nyumba nyingine kwa sasa?

Tunaamini kwamba katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wanakosa vitabu vya kiada, wanakosa maabara kwa ajili ya kupata elimu kwa vitendo, kiasi hicho cha fedha kingesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hilo.

Tunatambua juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kuboresha sekta za elimu, afya na ujenzi wa barabara, lakini vilevile tunatambua kwamba kuna matumizi makubwa katika taasisi za serikali, ambayo yangeweza kumsaidia katika kuwaletea maisha bora wananchi.

Ndio maana tunaungana na kauli ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo kwa kusema kwamba wafanye uchunguzi kujua gharama halisi za ujenzi wa nyumba ya gavana na vilevile kuzuia mikopo kwa wafanyakazi wa BoT.

Benki Kuu ya Tanzania inapaswa kuwa kioo cha jamii katika kusimamia fedha za walipa kodi kwa kuwa ndio waliopewa kazi hiyo, hivyo basi tusingependa kuona uozo unatokea katika taasisi hiyo nyeti.

Tumeshuhudia hila nyingi zikidaiwa kufanywa katika BoT ikiwamo EPA, ujenzi wa majengo pacha na bima yake na mengine ambayo taasisi za dola zinachunguza. Ni maoni yetu uchunguzi utafanyika mapema iwezekanavyo ili ukweli wa matumizi ya ujenzi huo wa nyumba ya gavana ujulikane.
 
Back
Top Bottom