Matokeo ya uchunguzi wa samaki toka Japan yaonyesha hawana mionzi

Jiwe la Ukara

Member
Jul 15, 2011
44
31
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU USALAMA WA SAMAKI WALIOINGIZWA NCHINI KUTOKA JAPAN

1. Utangulizi
Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 24 Julai 2011, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitoa taarifa kwa umma juu ya samaki waliohisiwa kuchafuliwa na mionzi ya nyuklia kuingizwa nchini Tanzania kutoka Japan. Katika kufanyia kazi taarifa hizo, Serikali ilizuia mzigo wa samaki aina ya Marckerel waliongizwa nchini kutoka Japan na kampuni ya Alphakrust Ltd. ya Dar es Salaam.

Samaki hao waliingizwa nchini kwa kufuata taratibu zote za kisheria. Hata hivyo, baada ya kuenea mashaka kuwa samaki hao wamechafuliwa na mionzi ya nyuklia, Serikali ilichukua tahadhari ya kuzuia mzigo huo na kuutaka umma wa Watanzania kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa samaki hao hawatumiwi mpaka uchunguzi zaidi juu ya uwezekano wa samaki hao kuwa na mionzi ya nyuklia utakapofanyika na taarifa ya uchunguzi huo kutolewa.


2. Hatua zilizochukuliwa
Katika kufanya uchunguzi na uhakiki wa usalama wa samaki hao yafuatayo yalifanyika:-

a)
Tarehe 23 Julai 2011, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliiagiza Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kufanya ukaguzi na kuhakikisha kuwa samaki hao wanazuiliwa ili wasitumiwe. Hadi kufikia tarehe 2 Agosti 2011, Mamlaka kwa kushirikiana na Idara za Afya Mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro na Jeshi la Polisi zilimudu kukamata na kuzuia tani 123.908 (99.14%) kati ya tani 124.992 zilizokuwa zimeingizwa nchini na kampuni ya Alphakrust Ltd. Kiasi cha tani 1.084 (0.86%) zilikuwa zimekwishauzwa kwa watumiaji.

b) Taratibu na nyaraka mbalimbali zilizoambatana na shehena hiyo zilihakikiwa kwa kufanya mawasiliano na Mamlaka za kitaifa yaani Idara ya Uvuvi, Kamisheni ya Nguvu za Atomiki Tanzania, Mamlaka ya Mapato (TRA) na za kimataifa yaani Japan Frozen Foods Inspection Corporation ili kubaini uhalali wake pamoja na kupata uthibitisho wa usalama wa samaki hao. Tathmini hiyo imethibitisha kwamba samaki hao waliingizwa kwa kuzingatia sheria na taratibu.

c)
Ili kujiridhisha kuwa samaki hao ni salama, tarehe 25 Julai 2011 sampuli za samaki hao zilichukuliwa kutoka katika shehena iliyozuiliwa na kufanyiwa uchunguzi katika maabara ya Kamisheni ya Nguvu za Atomiki Tanzania ili kuhakiki endapo samaki hao wamechafuliwa na mionzi ya nyuklia.

Matokeo ya uchunguzi huo yalipatikana tarehe 29 Julai 2011 na yalionesha kwamba samaki hao hawajachafuliwa na mionzi na hivyo ni salama kwa matumizi ya binadamu. Majibu haya yanafanana na uchunguzi wa awali wa sampuli za samaki hao uliofanywa na Taasisi hii kabla ya kuruhusiwa kuingizwa nchini pamoja na yale yaliyotolewa na Japan Frozen Foods Inspection Corporation ya Serikali ya Japan.


d)
Hata hivyo, ili kujiridhisha zaidi, mnamo tarehe 22 Agosti 2011, TFDA ilichukua sampuli nyingine na kuzipeleka katika maabara ya Afrika ya Kusini ambayo ina ithibati (ISO 17025:2005) katika uchunguzi wa mionzi ya nyuklia. Sampuli hizo zilipokelewa na maabara hiyo tarehe 25 Agosti 2011 na kufanyiwa uchunguzi. Matokeo ya uchunguzi huo yalipatikana tarehe 05 Septemba 2011 ambapo pia yanaonesha kuwa samaki hao hawajachafuliwa na mionzi ya nyuklia.

e)
Uchunguzi huo wa kimaabara umezingatia viwango vya kimataifa vinavyotolewa na Taasisi ya kimataifa inayohusika na kuandaa viwango vya vyakula (Codex Alimentarius Commission); iliyo chini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

f)
Katika kipindi chote ambapo uchunguzi wa suala hili umekuwa ukiendelea, kulikuwepo mawasilianao na ushirikiriano wa karibu baina ya TFDA, Kamisheni ya Nguvu za Atomiki Tanzania na Idara ya Maendeleo ya Uvuvi ambazo ni taasisi za Serikali zenye majukumu yanayogusa suala hili ili kuweza kulihitimisha kwa ufanisi.

3. Hitimisho

3.1 Kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi uliofanyika, tunapenda kuufahamisha umma kuwa samaki aina ya Marckerel waliongizwa nchini kutoka Japan na kampuni ya Alphakrust Ltd. hawajachafuliwa na mionzi ya nyuklia. Samaki hao ni salama kwa matumizi ya binadamu na hivyo wameruhusiwa kusambazwa na kuuzwa.


3.2 Tunapenda kutoa shukrani kwa ushirikiano mzuri uliooneshwa na vyombo vya habari, Kampuni ya Alphakrust Ltd., Jeshi la Polisi na jamii kwa ujumla wakati wa uchunguzi wa suala hili.


3.3 Tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa pale wanapokuwa na mashaka kuhusu usalama, ubora na ufanisi wa bidhaa za vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.


Hiiti B. Sillo, Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Chakula na Dawa,
S.L.P 77150,
DAR ES SALAAM.
Simu: +255 22 2450512/2450751/2452108
Fax: +255 22 2450793
Email: info@tfda.or.tz
Website: TANZANIA FOOD AND DRUGS AUTHORITY

9 Septemba, 2011
 

Nyumisi

JF-Expert Member
Nov 10, 2010
10,829
14,409
WanaJF katika taarifa ya saa 2 usiku ITV mkurugenzi wa TFDA katoa majibu ya uchunguzi wa samaki toka Japan ambao walihisiwa kuwa na mionzi na kuthibitisha kuwa hawana mionzi. Mfanyabiashara aliyeingiza samaki hao naye kaonyesha relief ya hali ya juu na kutoa madai kwamba kuna watu walizusha ili kumhujumu katika biashara zake. Lakini ninachojiuliza hapa, labda na wenzangu mtanisaidia, hivi matokeo haya ya kiuchunguzi ni kigezo kwamba samaki watakaoingizwa kuanzia sasa kutoka Japan watakuwa safi na hivyo wanatakiwa waendelee kutumiwa au ni vipi? Nachele kuuliza hivyo kwa sababu uchunguzi wa mionzi umefanywa nje ya nchi, Afrika kusini, na majibu yamechukua takribani siku 40 kutolewa. Je mkurugenzi atatuhakikishia kuwa kila kontena la samaki litakaloletwa toka Japan litasubiri matokeo ya vipimo vya mionzi katika maabara za Afrika kusini kabla ya kutumiwa na walaji ili wasipate madhara ya mionzi? Ama, kutokana na eneo la bahari la Japan kuwa risky area kutokana na contamination ya mionzi, samaki kutoka huko inabidi wapigwe marufuku? Haya yote mkurugenzi hakuyaweka wazi labda kutokana kuwa na furaha ya matokeo ya kumsafisha mtu, Jairo type. Naombeni maoni yenu.
 

Mwita25

JF-Expert Member
Apr 15, 2011
3,836
1,164
Hii nchi tuna samaki wengi sana na wa kila aina, kulikuwa na umuhimu gani wa kuagiza samaki Japan?
 
0 Reactions
Reply
Top Bottom