China inaendelea kuongoza katika masuala ya teknolojia ya akili mnemba (AI) ndani ya nchi za BRICS ikiwa na 47.2% ya tasnifu zilizotajwa zaidi za AI na kushika nafasi ya juu katika kuweka hataza za AI kimataifa. Ukiungwa mkono na zaidi ya dola bilioni 150 za ufadhili wa serikali, mkakati wa AI wa China umetoa muundo wa ushindani wa chip na lugha kutoka makampuni kama vile Huawei na Baidu.
India nayo pia inaendelea kusonga mbele na mpango wake wa "IndiaAI", unaogharimu dola bilioni 1.2 ambao ulizinduliwa mwaka 2023 ili kusaidia kutoa chanzo cha wazi na huru cha lugha ya Kihindi, pia kutoa zana za AI kwa ajili ya kilimo, elimu, na huduma ya afya, pamoja na muundo wa chipu wa nchi hiyo.
Kwa upande wa Urusi imefungamanisha AI na usalama wa taifa. "Mkakati wake wa Taifa wa AI 2030," uliotangazwa na Rais Vladimir Putin, umewekezwa dola bilioni 1.2 kwa ajili ya maendeleo ya AI inayolenga ulinzi.
Brazili na Afrika Kusini zinaibuka kama vitovu vya AI inayofuata maadili, hasa katika kilimo na afya ya umma. Embrapa ya Brazil inapeleka AI katika kilimo cha usahihi, huku CSIR ya Afrika Kusini ikitumia AI katika usafiri na huduma ya afya inayooungwa mkono na mchakato wa kidijitali (eHealth). Misri na Ethiopia pia zinawekeza katika utawala wa kutumia teknolojia za kidijitali na miundombinu inayofuata utafiti wa AI.
Lengo kuu la mkakati wa AI ya BRICS ni kuacha kutegemea watoa huduma ya wingu wa Magharibi na miundo ya kimsingi, ambapo wakosoaji wanasema inaonesha upendeleo wa nchi za Magharibi. China, India, na Urusi zinaunda modeli zao kubwa za lugha, ambapo mwaka 2024, Brazili na China zilizindua mradi wa pamoja wa kujenga modeli kubwa za lugha ya Kireno-Kihispania kwa ajili ya nchi za Amerika ya Kusini.
Katika Mkutano wa Kilele wa BRICS wa 2024 huko Kazan, wanachama walipitisha "Mkataba wa AI inayowajibika," ukihimiza maendeleo ya AI yenye ushirikishwaji na yanayojikita katika utamaduni, ambao unawekwa kama njia mbadala ya Sheria ya AI ya Umoja wa Ulaya, ambayo watu wengine wanaiona kama kikwazo kwa Nchi za Kusini.
Juhudi za nchi za BRICS zinafanikiwa kutokana na usaidizi wa kifedha kutoka Benki Mpya ya Maendeleo, ambayo mwaka huu ilizindua Mfuko wa “Ukuu wa Kidijitali” wa dola bilioni 5, ili kuimarisha miundombinu ya AI, yakiwemo maeneo ya utafiti, vituo vya data, na utengenezaji wa chip.
Juhudi za nchi hizi pia zinaendelea katika kuunda mkusanyiko wa hesabu wa BRICS yaani “BRICS-based compute stack”. SMIC ya China na CDAC ya India zinaendeleza uzalishaji wa chipu za 7nm, wakati nchi kama Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zinawekeza kwenye kompyuta ya quantum na mashirika ya kitaifa ya AI.
Kwa pamoja, mataifa ya BRICS yanaunda upya mandhari ya kimataifa ya AI, yakihamisha uwiano wa nguvu kutoka makampuni makubwa ya teknolojia ya Magharibi kuelekea mustakabali wa pande nyingi zaidi.