Masomo 21 Kwa Ajili ya karne ya 21: Ukweli Kinyonga, Kuna Ukweli Bandia Unaodumu Milele

Mama Amon

JF-Expert Member
Mar 30, 2018
2,021
2,478
1617257767830.png

Dr. Yuval Noah Harari, Mwandishi wa Kitabu kiitwacho, "Masomo 21 Kwa Ajili ya Karne ya 21 (2018)

Mwaka 2018, mwanahistoria wa huko Israel, Profesa Yuval Noah Harari, aliandika kitabu kiitwacho, “Masomo 21 Kwa Ajili ya Karne ya 21,” yaani “21 Lessons for the 21st Century.” Kitabu hiki kimechapwa mwaka 2018 kupitia kampuni ya Spiegel & Grau huko Marekani na kampuni ya Jonathan Cape huko Uingereza.

Katika kitabu hiki, chenye sura 21 na kurasa 253, Profesa. Harari (2018) anajadili changamoto 21 katika karne ya 21, kupitia sura 21 zenye vichwa vya maneno yafuatayo:

Kuwapa watu matumaini; Kazi; Uhuru; Usawa; Jumuiya; Ustaarabu; Utaifa; Dini; Uhamiaji; Ugaidi; Vita; Uvumilivu; Mungu; Usekulari; Ujinga; Haki na amani; Ukweli wa kubumba; Riwaya za Kisayansi; Elimu; Maana; na Tafakari.

Sura ya 17 yenye kujadili “Ukweli bandia” na inayotetea rai kwamba,”baadhi ya habari bandia hudumu milele,” inatuhusu zaidi katika siasa za milenia ya tatu.

Katika sura hii Profesa Harari (2018) anasema kwamba, hadithi za ukweli wa kubuni zenye kukubalika kwa watu wengi kwa mpigo, na hasa zile zinazotufikia kupitia kwenye vyombo vya habari, dini, riwaya, michezo, kamari, hata matangazo ya kibisahara, zinachukua sehemu kubwa ya maisha yetu ya kila siku; na kwamba, hilo ni jambo la kawaida, kwani ni imani hizi za pamoja ambazo zimewasaidia wanadamu kushirikiana na kuitiisha sayari ya dunia.

Kwa sababu ya unyeti wake kwa siasa za leo, sura hii ya 17 inatafsiriwa na kuwekwa hapa chini, bila kuongeza wala kupunguza neno.

Lakini pia nimeambatanisha kitabu kizima kwa wale wanaopenda kusoma kwa kina.


================KIAMBATANISHO===================

Masomo 21 Kwa Ajili ya Karne ya 21
"Somo la 17: kweli Bandia: Huwa Kuna Ukweli Bandia Unaodumu Milele."

Hii n i sura ya 17 ambayo imenukuliwa kutoka katika kitabu cha Yuval Noah Harari, "Masomo 21 Kwa Ajili ya karne ya 21," cha mwaka 2018. Kitabu kizima kimeambatanishwa. Endelea kujisomea....


1617258211899.png

Profesa Noah Hariri in 2017

Tunaambiwa mara kwa mara siku hizi kwamba tumeingia kwenye enzi mpya ya kutisha yenye kutawaliwa na hadithi za ukweli feki, ambamo inawezekana, sio data pekee zinaweza kupikwa, bali pia historia nzima inaweza kukarabatiwa na hivyo kufanywa kuwa bandia.

Lakini ikiwa ni kweli kwamba hizi ni zama za ukweli bandia, ni lini hasa zikuwa zama za ukweli halisi? Na ni nini kilisababisha tuhame kutoka kwenye zama za ukweli halisi na kuingia katika ezama za ukweli bandia? Ni mtandao wa intaneti? Mitandao ya kijamii kama vile facebook, whatsapp na twitter? Au ni kuibuka kwa Putin wa Urusi na Trump wa Marekani?

Upekuzi wa haraka wa kumbukumbu za kihistoria unaonyesha kwamba, propaganda zinazofanyika kwa njia ya upotoshaji wa habari sio kitu kipya hapa duniani.

Kwa kweli, siku zote wanadamu wengi wameishi katika zama za ukweli bandia. Binadamu ni kiumbe chenye hulka ya kubuni hadithi za ukweli bandia, ambaye aliitiisha sayari ya dunia kwa sababu ya uwezo wake wa kipekee wa kuunda na kueneza hadithi za ukweli bandia kama wafanyavyo watunzi wa vitabu vya riwaya.

Sisi ndio mamalia pekee ambao tunaweza kushirikiana na wageni wengi kwa sababu ni sisi pekee tunaweza kutunga hadithi za ukweli wa kubuni, kuzieneza, na kuwashawishi mamilioni ya wengine kuziamini. Kadiri hadithi hizo zinavyoaminiwa na kila mtu, ndivyo sisi sote tunajikuta tukitii kanuni zile zile za kifikra na kwa hiyo kuweza kushirikiana vyema katika miradi mbalimbali.

Tafadhali, kumbuka kuwa sikatai ufanisi wa kiuchumi, kisiasa na kijamii au baraka zinazoweza kutokana na dini – la hasha. Ninachosema hapa ni kwamba, hadithi za ukweli wa kubuni ni miongoni mwa zana bora zaidi katika sanduku la vifaa vya kuustarabisha ubinadamu na kuutiisha ulimwengu.

Kwa mfano, karne nyingi zilizopita, mamilioni ya Wakristo walijifungia ndani ya tufe la hadithi za kale za ukweli wa kubuni juu ya viumbe na ulimwengu, yaani visasili, bila kuthubutu kuhoji ukweli halisi wa masimulizi ya kibiblia, wakati mamilioni ya Waislamu waliamini masimulizi ya Kurani bila kuhoji kitu chochote katika masimulizi hayo.

Hatuna ushahidi wa kisayansi kwamba Hawa alijaribiwa na nyoka, kwamba roho za watenda dhambi zote zinachomwa motoni baada ya kufa kwao, au kwamba muumba wa ulimwengu hapendi Wakristo waone na Waislamu. Lakini mabilioni ya watu wameamini katika hadithi hizi kwa maelfu ya miaka hadi leo.

Huu ni ushahidi kwamba, baadhi ya hadithi za ukweli wa kubuni hudumu milele. Ninajua kuwa watu wengi wanaweza kukasirishwa na uamuzi wangu wa kujaribu kulinganisha habari za kidini na habari kweli wa kubuni , lakini huo ndio mfano mzuri wa kutusaidia kueleza maana ya ukweli bandia.

Watu elfu moja wanapoamini hadithi ya ukweli wa kubuni kwa mwezi mmoja, hiyo ni habari feki. Lakini, watu bilioni moja wanapoiamini adithi ya ukweli wa kubuni kwa miaka elfu moja, hiyo ni dini, na tunashauriwa tusiite "habari feki" ili tusiumize hisia za waamini au kupata kipigo kutokana na hasira zao.

Tafadhali, kumbuka kuwa sikatai ufanisi wa kiuchumi, kisiasa na kijamii au fadhila inayoweza kutokana na dini – la hasha. Kwa wema au ubaya, ukweli wa kubuni ni miongoni mwa zana bora zaidi katika sanduku la vifaa vya kustaarabisha ubinadamu.

Kwa kuwaleta watu pamoja, imani za kidini zinafanya ushirikiano mkubwa wa kibinadamu uwezekane. Viongozi wa dini wanahamasisha watu kujenga hospitali, shule na madaraja pamoja na majeshi na magereza.

Sehemu kubwa ya Biblia inaweza kuwa ya kutunga, lakini bado inaweza, na kwa hakika, imeleta furaha kwa mabilioni na bado inaweza kuwahimiza wanadamu kuwa na huruma, ujasiri na ubunifu.

Ni kama ambavyo hadithi zingine kubwa zenye ukweli wa kubuni, zilivyo na nafasi kubwa katika maisha ya watu. Mfano ni kama vile vitabu saba vya hadithi za ukweli wa kubuni vinavyosimulia habari ya wachawi awanaoongozwa na mhusika mkuu aitwaye “Harry Potter.”

Vitabu hivyo ni: Philosopher's Stone, Chamber of Secrets, Prisoner of Azkaban, Goblet of Fire, Order of the Phoenix, Half-Blood Prince, na Deathly Hallows. Vitabu hivi vilitungwa na mwandishi wa Kiingereza aitwaye J. K. Rowling kati ya mwaka 1997 na 2005.

Tena, watu wengine wanaweza kukerwa na uamuzi wangu wa kuwalinganisha wahusika wa Biblia na wahusika kama vile Harry Potter.

kiwa wewe ni Mkristo mwenye mawazo ya kisayansi, unaweza kusema kwamba kitabu kitakatifu hakikukusudiwa kusomwa kama simulizi ya kweli, isipokuwa kama hadithi ya sitiari iliyo na hekima ya kina. Lakini ukweli huo si ndio pia unazihusu hadithi za Harry Potter?


1617258790281.png

Profesa Noah Hariri mwaka 2020

Dini za zamani sio pekee zilizotumia hadithi kadhaa zenye ukweli wa kubuni kuimarisha ushirikiano kati ya watu. Hivi karibuni, kila taifa limeunda hadithi zao za kitaifa zinazoanzia kwenye majina na mawazo na matendo ya waasisi wa Taifa, yaani visasili vya kitaifa.

Kwa kweli, sio visasili vyote vya kidini vimekuwa vizuri. Mnamo 29 Agosti 1255, mwili wa kijana wa Kiingereza mwenye umri wa miaka tisa anayeitwa Hugh ulipatikana kwenye kisima katika mji wa Lincoln.

Uvumi ulienea haraka kwamba Hugh alikuwa ametekwa na kuuawa kwa kutolewa kafara katika ibada za kichawi zilizokuwa zinaendeshwa na Wayahudi wa hapo. Hadithi hiyo ilisambaa sana kwa njia ya mdomo na baadaye kwa njia ya maandishi ikitoa picha kwamba Wayahudi wa hapo walikuwa wanawatoa kafara watoto kwenye ibada zao za kishirikina.

Mmoja wa waandishi maarufu wa Kiingereza wa siku hizo, Matthew Paris, alitoa maelezo marefu juu ya jinsi Wayahudi mashuhuri kutoka kote Uingereza walivyokusanyika huko Lincoln ili kumkamata, kumtesa, na mwishowe kumsulubu mtoto huyo wakati wa ibada ya kishirikina.

Kwa sababu ya maelezo haya ambayo ni kashfa ya umwagaji damu wa Hugh kupitia ibada ya kishirikina, Wayahudi 19 walikamatwa, kushitakiwa, kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa madai ya mauaji.

Hili ni simulizi moja kati ya masimulizi mengi yenye kujikita katika hadithi za umwagaji wa damu kupitia ibada za kishirikina yaliyosikika sana katika miji mingine ya Kiingereza, na kusababisha msururu wa mauaji ambayo yalizilenga jamii za Kiyahudi kama watuhumiwa wakuu .

Mwishowe, mnamo 1290, Wayahudi wote wa Uingereza walifukuzwa kwa sababu ya tuhuma hiyo inayohusiana na kashfa ya umwagaji damu kupitia ibada za kishirikina.

Hadithi hii haikuishia hapo. Karne moja baada ya kufukuzwa kwa Wayahudi, Geoffrey Chaucer alijumuisha kashfa ya umwagaji damu kupitia ibada za kishirikina katika muundo wa "Hadithi ya Hugh wa Lincoln (1246 –1255)" iliyoandikwa katika kitabu cha “Ngano za Canterbury,” ngano nyingine ikiwa ni “Ngano ya Prioresia,” yaani "The Prioress's Tale."

Ngano hiyo ya Prioresia iinahitimishwa kwa kusimulia habari ya kunyongwa kwa Wayahudi kutokana na kashfa ya umwagaji damu kupitia ibada za kishirikina. Masimulizi ya kashfa ya umwagaji damu upitia ibada za kishirikina kama haya baadaye yalikuwa mdomoni mwa kila harakati dhidi ya Wayahudi kuanzia Uhispania ya zamani hadi katika Urusi ya sasa.

Baadaye Hugh wa Lincoln (1246 –1255) alizikwa katika Kanisa Kuu la Lincoln na kutangazwa mtakatifu. Alisifika kwa kufanya miujiza anwai, na kaburi lake liliendelea kuteka mahujaji hata karne nyingi baada ya kufukuzwa kwa Wayahudi wote kutoka Uingereza. Ulikuwa ni mradi mzuri kwa kiuchumi ulionufaika na hadithi ya ukweli wa kutunga uliogharimu maisha ya Wayahudi wengi wasio na hatia.

Ni mnamo 1955, miaka kumi baada ya mauaji ya halaiki ya Wayahudi iliyofanywa na Dikteta Hitler wa Ujerumani, uongozi wa Kanisa Kuu la Lincoln ulikanusha hadithi ya kashfa ya umwagaji damu kwa njia ya ibada za kishirikina iliyokuwa inawaandama Wayahudi, kwa kuweka kibao karibu na kaburi la Hugh wa Lincoln kilichosomeka hivi:

"Hadithi zenye ukweli wa kubuni kuhusu ibada za kishirikina zilizodaiwa kufanywa na jamii za Wayahudi zikihusisha mauaji ya kuwatoa kafara wavulana wa Kikristo zilikuwa za kawaida huko Ulaya wakati wa Zama za Kati na hata baadaye sana. Hadithi hizi ziligharimu maisha ya Wayahudi wengi wasio na hatia. Hugh wa Lincoln (1246 –1255) alikuwa na hadithi yake na mtu huyu anayedaiwa kuwa mwathiriwa wa ibada hizo alizikwa humu katika Kanisa Kuu mnamo mwaka 1255. Hadithi kama hizo zisizokuwa na ukweli wowote zimeutia doa kubwa Ukristo. ”

Sawa, hadithi za ukweli bandia kama hizi zimeweza kudumu kwa miaka mia saba. Dini za zamani sio pekee zilizotumia hadithi za ukweli wa kubuni kuimarisha ushirikiano. Katika nyakati za hivi karibuni, kila taifa limeunda hadithi zao za kitaifa, wakati harakati za watu kama vile wakomunisti, mafashisti na waliberali hutengeneza kanuni za imani kwa ajili ya kujiimarisha.

Kwa mfano, Joseph Goebbels, kiranja mkuu wa propaganda za Hitler na kiongozi wa chama cha Nazi cha Ujerumani, alidaiwa kuelezea mbinu yake hivi: "Uwongo unaosemwa mara moja unabaki kuwa uwongo, lakini uwongo unaosemwa mara elfu unakuwa ukweli."

Katika kitabu cha Wasifu binafsi wa Hitler kilichotumika kama Manifesto ya chama cha Nazi, kiitwacho “Mein Kampf,” Hitler aliandika kwamba, "Mbinu bora zaidi ya mwenezaji wa propaganda haitaleta mafanikio isipokuwa kama itazingatia kanuni moja ya kimsingi kila wakati , yaani: inapaswa kujielekeza kwenye hoja chache na kuzirudia hoja hizo mara kwa mara."

Je, mtu yeyote ambaye ni kuwadi wa habari za ukweli wa kubuni wa siku hizi anaweza kuboresha kitu chochote katika kanuni hii ya Hitler? Uhakika ni kwamba, ukweli haujawahi kuwa kipaumbele cha kwanza kwenye ajenda ya binadamu ngulu mbili. Endapo utashikilia na kufungamana na ukweli ambao haujakarabatiwa kwa kiasi fulani, ni watu wachache watakufuata.

Makampuni ya kibiashara pia yanategemea habari za ukweli wa kubuni na taarifa bandia. Kutangaza chapa ya biashara mara nyingi hujumuisha kurudia hadithi ile ile ya kutunga tena na tena, mpaka watu watakapoonekana kuanza kuiamini kwamba ni hadithi ya kweli.

Ni picha gani zinazokuja akilini mwako wakati unafikiria kuhusu Coca-Cola? Je! Unafikiria juu ya vijana wenye afya wanaojihusisha na michezo na kufurahi pamoja? Au unafikiria juu ya wagonjwa wenye ugonjwa wa kisukari waliolala kitandani hospitalini?

Kunywa Coca-Cola nyingi hakutakufanya uwe mchanga, hakutakufanya uwe na afya nzuri, na hakutakufanya uwe mwanariadha. Badala yake, itaongeza nafasi zako za kuugua unene na ugonjwa wa sukari. Hata hivyo kwa miongo kadhaa Coca-Cola amewekeza mabilioni ya dola kwa kujiunganisha na vijana, afya, na michezo - na mabilioni ya wanadamu wanaamini katika uhusiano huu.

Uhakika ni kwamba, ukweli haujawahi kuwa kipaumbele cha kwanza kwenye ajenda ya binadamu. Ikiwa utashikilia na kufungamana na ukweli ambao haujakarabatiwa kwa namna yoyote, ni watu wachache watakufuata. Hadithi za ukweli wa kubuni zina faida zake dhidi ya hadithi za kweli halisi, hasa linapokuja suala la kuunganisha watu wengi.

Ikiwa unataka kupima uaminifu wa kikundi, kuwahitaji watu hao waamini hadithi za ukweli wa kubuni ni jaribio bora zaidi kuliko kuwataka waamini katika hadithi za ukweli halisi. Kwa mfano, ikiwa chifu atasema jua linachomoza magharibi na kutua mashariki, ni wale watu ambao ni waaminifu kwake tu ambao watapiga makofi. Vivyo hivyo, ikiwa majirani zako wote wanaamini na kuikubali hadithi ya ajabu ajabu kama wewe unavyofanya, unaweza kuwategemea kusimama pamoja nawe wakati wa shida.

Ikiwa watu hao wako tayari kuamini hadithi ya ukweli uliothibitishwa pekee, na mchakato wa kuithibitisha bado haujafanyika, imani hiyo itawasaidia lini? Unaweza kusema kuwa wakati mwingine inawezekana kuwapanga watu vyema kupitia makubaliano ya hiari kwa kutumia hadithi za ukweli wa kubuni kama zile zinazopatikana kwenye riwaya na tamthiliya.

Katika uwanja wa uchumi, vitu vilivyobuniwa na binadamu kama vile fedha na mashirika huwaweka watu pamoja kwa ufanisi zaidi kuliko anavyoweza kufanya mungu yeyote au kitabu kitakatifu chochote.

Kuhusu habari ya kitabu kitakatifu, muumini wa kweli angesema, "Ninaamini kuwa kitabu hicho ni kitakatifu," wakati katika suala la sarafu ya dola, muumini wa kweli angesema tu, "Ninaamini kuwa watu wengine wanaamini kuwa sarafu ya dola ni yenye thamani. ”

Ni dhahiri kuwa sarafu ya dola imebuniwa na wanadamu tu, lakini watu kote ulimwenguni wanaiheshimu. Ikiwa ni hivyo, kwa nini wanadamu wasiache hadithi zote za ukweli halisi na kushirikiana kwa mujibu wa vigezo vilivyobuniwa kutokana na makubaliano ya hiari kama ilivyo kwa sarafu ya dola?

Yaani, tofauti kati ya vitabu vitakatifu na pesa ni ndogo sana kuliko inavyoweza kuonekana. Watu wengi wanapoona noti ya dola, wanasahau kuwa ni kitu kilichobuniwa kwa mujibu wa makubaliano ya wanadamu. Wanapoona kipande cha kijani kibichi chenye picha ya yule mzungu aliyekufa, wanaona ni kitu chenye thamani inayoanzia ndani mwake.

Hawajawahi kujikumbusha kwamba, "Kwa kweli, hii ni karatasi isiyo na thamani, lakini kwa sababu watu wengine wanaiona kama karatasi ya thamani, ninaweza kuitumia kufanya manunuzi ya vitu mbalimbali."

Kama ungeangalia ubongo wa mwanadamu kwenye mashine ya kufanya skana na kuonyesha picha ya ubongo huo, utaona kwamba mtu anapopewa begi lililojaa noti za dola mia mia, sehemu za ubongo ambazo huanza kuchangamka kwa msisimko sio sehemu za kutilia shaka mambo bali ni sehemu zenye kuonyesha tamaa.

Kinyume chake ni kwamba, kwa sehemu kubwa sana, watu huanza kutakasa Biblia au Kurani tu baada ya kukutana kwa muda mrefu na mara kwa mara na watu wengine ambao wanaiona kuwa kitu takatifu. Tunajifunza kuheshimu vitabu vitakatifu kwa njia ile ile tunayojifunza kuheshimu sarafu ya karatasi.

Hauwezi kucheza michezo au kusoma riwaya kabla ya kuyapiga kisogo mashaka uliyokuwa nayo juu yake. Kwa mfano, ili kufurahia mpira wa miguu, lazima usahau kwa dakika tisini kwamba sheria zake ni uvumbuzi wa kibinadamu tu.

Kwa sababu hii, katika utendaji wa kila siku, hakuna mgawanyiko mkali kati ya kujua kwamba kitu fulani ni chenye thamani iliyotokana na uvumbuzi tu wa wanadamu na kuamini kuwa kitu fulani ni chenye thamani asilia. Mara nyingi, watu wanaona utata au wanasahau kuhusu mgawanyiko huu.

Kutoa mfano mwingine, katika majadiliano ya kina ya kifalsafa juu ya mashirika, karibu kila mtu angekubali kuwa mashirika ni hadithi za kutunga zilizoundwa na wanadamu. Shirika la Microsoft sio watu wanaoajiriwa na Microsoft, au wanahisa wanaohudumiwa na Microsoft au majengo yanayomilikiwa na Microsoft.

Badala yake, Shirika la Microsoft ni hadithi inayosimulia ukweli wa kisheria iliyotungwa na kusukwa kupitia mikono ya wabunge na wanasheria. Lakini bado, asilimia 99 ya muda wote, hatujishughulishi na majadiliano ya kina ya kifalsafa, na tunayachukulia mashirika kana kwamba ni vitu halisi kama vileo duma au wanadamu.


1617258996026.png

Profesa Hariri akiwa katika pozi

Kufifisha mstari kati ya hadithi za ukweli wa kubuni na hadithi za ukweli kunaweza kufanywa kwa madhumuni mengi, ikiwemo kujifurahisha na kutafuta maisha.

Hauwezi kucheza michezo au kusoma riwaya kabla hujayapiga kisogo mashaka uliyokuwa nayo juu yake. Ili kufurahia sana mpira wa miguu, lazima ukubali kanuni zake na usahau kwa dakika tisini kuwa kanuni hizo ni ubunifu wa wanadamu tu.

Usipofanya hivyo, utafikiria ni ujinga kabisa kwa watu 22 kwenda mbio wakikimbiza mpira kwa dakika 90. Mchezo wa soka unaweza kuanza kama njia ya kujifurahisha tu, lakini unaweza kuwa jambo zito zaidi, kama ambavyo mhuni yoyote wa Kiingereza au raia wa Ajentina anayetafuta kitu cha kuliunganisha taifa atathibitisha. Soka inaweza kusaidia kuunda utambulisho binafsi, inaweza kuunganisha jamii kubwa, na inaweza kuwa sababu ya vurugu.

Wanadamu wana uwezo wa ajabu wa kujua mambo na kutojua mambo kwa wakati mmoja. Au, kwa usahihi zaidi, wanaweza kujua kitu wakati wanapokuwa wanafikiria juu yake, lakini wakati mwingi wanakuwa hawafikiri juu yake, na kwa hivyo wanakuwa hawajui. Ikiwa utatazama kwa umakini, utatambua kuwa fedha ni hadithi ya kutunga.

Lakini kawaida hufikiri juu yake namna hii. Ukiulizwa juu yake, unajua kwamba soka ni uvumbuzi wa mwanadamu. Lakini wakati joto la mechi linapopanda, hakuna anayeuliza. Ikiwa utatumia wakati na nguvu kufikiri vizuri, unaweza kugundua kuwa mataifa yamejengwa kama maorofa marefu. Lakini katikati ya vita, huna wakati wala nguvu za kufikiria haya.

Wasomi katika historia yote wamekumbana na mtanziko huu Je, Wanapaswa kulenga kuwaunganisha watu kwa kuhakikisha kila mtu anaamini hadithi ile ile, au wanapaswa kumruhusu kila mtu autafute ukweli wake hata kama jambo hili litazalisha utengano wa kijamii?

Ukweli na madaraka ni ndugu wawili wanaoweza kusafiri pamoja kwa muda mfupi sana. Baadaye kidogo kila mmoja hutembea kupitia njia yake tofauti. Ikiwa unataka madaraka, wakati fulani italazimika kueneza habari za kutunga.

Ikiwa unataka kujua ukweli juu ya ulimwengu, wakati fulani italazimika kuyakataa madaraka. Itabidi ukubali vitu ambayo vitawakasirisha rafiki zako, vitawavunja moyo wafuasi wako, au kudhoofisha mshikamano wa kijamii. Vitu hivyo ni pamoja na vyanzo vya madaraka yako mwenyewe.

Wasomi katika historia yote wamekumbana na mtanziko huu: Je, Wanadamu hutumikia madaraka au ukweli? Je, Wanapaswa kulenga kuwaunganisha watu kwa kuhakikisha kila mtu anaamini hadithi ile ile moja, au wanapaswa kuwaruhusu watu waujue ukweli kutokana na hadithi tofauti hata kama tofauti hizo zitaleta utengano?

Taasisi zenye nguvu zaidi za wasomi, kama vile makuhani wa Kikristo, mandarini wa Konfuchio au makada wa Kikomunisti, zilikweza umoja dhidi ya ukweli na kutweza ukweli dhidi ya umoja. Ndiyo sababu walikuwa, na bado wana nguvu sana.

Kama tabaka moja, wanadamu hupendelea madaraka kuliko ukweli. Tunatumia muda mwingi na juhudi kubwa kujaribu kudhibiti ulimwengu kuliko kujaribu kuelewa. Na hata tunapojaribu kuelewa, kawaida tunafanya hivyo kwa matumaini kwamba kuelewa ulimwengu kutafanya iwe rahisi kuudhibiti.

Ikiwa unaota juu ya ujenzi wa jamii ambamo hadithi za ukweli halisi zinatawala sana na hadithi za ukweli wa kubuni zinapuuzwa, huwezi kutarajia jambo lolote kubwa kutoka kwa binadamu walio katika jamii hiyo. Bora kujaribu bahati yako katika jamii ya sokwe.

HISANI: Sura hii imetafsiriwa kutoka kwenye kitabu chenye jina, “Masomo 21 kwa ajili ya Karne ya 21” kilichoandikwa na Dkt. Yuval Noah Harari, kilichochapishwa na kampuni ya Spiegel & Grau, chapa ya Penguin Random House, LLC, mwaka 2018. Yuval Noah Harari ni mhadhiri wa historia katika Chuo Kikuu cha Wahebrania,“Hebrew University,” kilichoko Yerusalem. Kitabu kizima kimeambatanishwa hapa chini.

1617259127031.png

Profesa Hariri akihutubia watu ukumbini
 

Attachments

  • yuval-noah-harari-21-lessons-for-the-21st-century.pdf
    1.3 MB · Views: 67
Kwanini umeamua kutafsiri sura hii??

unataka kutuaminisha nini?? Kwamba hakuna Mungu? dini zinatudanganya??

ACHA NIAMINI YUPO NIKIENDA NIMKOSE
KULIKO KUAMINI HADITHI ZAKO NIKACHOMWE MILELE.

ZAB. 14:1​

Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema.
 
Kitabu kimenipunguza uree kiasi kikubwa,niliacha mitungi nikahamia soda na sasa naacha soda nitakunywa chai bila sukari.
 
Kwanini umeamua kutafsiri sura hii??

unataka kutuaminisha nini?? Kwamba hakuna Mungu? dini zinatudanganya??

ACHA NIAMINI YUPO NIKIENDA NIMKOSE
KULIKO KUAMINI HADITHI ZAKO NIKACHOMWE MILELE.

ZAB. 14:1​

Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema.
Uende umkose? Hii sasa ni paradox, kama hakuna Mungu unadhani ukifa utakwenda wapi? Kama hayupo basi ukifa hauendi popote, unakua haupo tena mahala popote, kama tu ilivyokuwa kabla haujazaliwa.
 
Mimi nimekuwa advocate wa dhana ya kusema Mungu (muumba) yupo lakini mengi ya yanayo zungumzwa kwenye dini ni batili, ni hadithi za kubuni.

Mungu siyo katili wa kuchoma watu kama wasemavyo siku ya hukumu ikija(hii haitakuja sababu ukifa ndiyo basi hakuna lolote tena, no pain, no feelings, no memory).

Dini ni mpango wa kustaarabisha watu kinguvu kupunguza ukaidi na aggressiveness ya binadamu.

Dini ni mpango wa kuleta utiifu (order), ni mpango wa kuwatawala watu kama watumwa wa fikra na mwili.

Watu wengi wanaamini mambo mengi ya kubuni tu. Dunia inatawaliwa na uongo na propaganda, na brainwashing ya watu dhaifu kifikra au waoga, au emotionally unstable people.

BTW, nimekuwa nikijiita mkristo mkatoliki, nilibatizwa nikawa muumini mzuri tu lakini miaka ya karibuni nimefunguka kifikra sikubaliani na mengi ya dini za kikristo, kiislam na kiyahudi.
Hata baadhi ya dini zetu za asili za kiafrika.
Ninacho amini kwa sasa Mungu yupo lakini hana hayo mashariti yote ya hizi dini tajwa hapo juu, hana mpango wowote wa kuchoma au kutesa watu.

Fight only for a good cause, not for religions....
Support a politician only for a good cause, not for a political party he/she is in...
 
Daahh hiki kitabu simchezo jamaa ameiweka dunia nzima uchi ...sijui kwanini nilichelewa kuiona hii thread

Muandishi kaandika ukweli mtupu kuhusu maisha tunayoishi na hizi tamaduni zetu ..looohh Dunia imejaa uongo hii
 
Nimependa ulivyotafsiri.

Halafu nahisi hiki kitabu hakijatafsiriwa chote kwa Kiswahili. Ningependa kujua kama una mpango wa kufanya hivyo.

Hapana, sina mpango wa kukitafsiri kitabu chote kwa sababu kadhaa.

Kwanza, sipendi na sikubaliani na kila kitu kilichoandikwa mle.

Na pili, ni suala la gharama. Muda, breakfast, lunch, dinner, umeme, kodi ya pango la ofisi, etc etc ni vikwzo tele.

Hiyo sura ya kitabu niliipa kipaumbele kwa vile ilikuwa inahitajika sana kueleza wazo langu muhimu: vita dhidi ya disinformation in post-truth era.

Kwa hakika, disinformation ni tatizo mtambuka kuanzia serikalini mpaka kwenye azaki, kuanzia chama tawala hadi vyama vya upinzani, kuanzia taasisi za kidini hadi kwenye taasisi za kisekulari.

Hiki ni kilema chenye ndugu wanne, yaani:

  • Kusambaza taarifa potofu kwa kujua na kwa nia ovu ya kutafuta faida ya kiuchumi, kisiasa au kijamii (disinformation);
  • Kusambaza taarifa potofu bila nia ovu na bila kujua kwa imani kwamba usambazaji huo utamnufaisha mpokeaji (misinformation); na
  • Kusambaza taarifa za watu binafsi lakini ambazo ni za kweli kwa watu wasiohusika na kwa nia ovu ya kuwachafua watu wengine wasiokubaliana naye (malinformation).
  • Kuwapotosha watu kwa kusambaza taarifa zenye ukweli nusu nusu kwa makusudi ili kutafuta maslahi binafsi (deception by omission). (Tazama kiambatnisho)
Something urgent needs to be done some where by someone.

Napendekeza kuwa, utafiti kuhusu kiwango cha disinformation ndio hatua ya kwanza.

Wenzetu huko nje ya Tanzania wako mbele sana.
 

Attachments

  • Information Disorder Syndrome--3.pdf
    303.7 KB · Views: 19
Kwa kweli sina mpango wa kukitafsiri chote.
Muda, breakfast, lunch, dinner, umeme, kodi ya pango la ofisi, etc etc ni vikw\zo tele.
Hiyo sura niliipa kipaumbele kwa vile ilikuwa inahitajika sana kueleza wazo langu muhimu: vita dhidi ya disinformation in post-truth era.
Jitahidi kadri ya utakavo barikiwa mkuu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom