Mashujaa wa uhuru waliosahauliwa: Makala ya Al Haj Abdallah Tambaza

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,217
30,582
Mashujaa wa Uhuru Waliosahaulika

Na Alhaj Abdallah Tambaza


u_9cKzY1A_6rahWNDIDhQOLGWRPGJZy8iKkgMs8zhOjP=w737-h553
Abdallah Tambaza
KATIKA taifa lolote duniani, kuna watu huwa wanaenziwa, wanatukuzwa na kutajwatajwa, kama namna ya kukumbuka michango yao katika uhai wa taifa husika, hata kama hawakuwahi kuwa viongozi wa juu. Kwa mfano, leo hii huwezi ukazungumzia taifa la India bila kugusa habari za kina Nehru na Mahatma Gandhi. Hali kadhalika, huwezi kuzungumza habari za Malawi, bila kuwataja akina Kanyama Chiume, Kamuzu Banda, na Yatuta Chizisa.Vivyo hivyo, historia ya Kenya, haiwi sawa usipowataja akina Deedan Kimathi, Kungu Karumba, Bildad Kagia, Njenga Karume, Jaramogi Oginga, Tom Mboya, Mbiyu Koinange na Ronald Ngala wa chama cha KADU.Wamarekani nao wanao watu wao waliowafanyia mambo makubwa mno siku za mwanzo za uhai wao. Mwaka 1776, kule Philadelphia waliketi kwenye chumba chenye joto kali sana na kuandaa mikakati ya kujitangazia uhuru Julai 4, 1776. Wamarekani wanawaita watu hao, ‘the framers of Independence’ (waliobuni na kuandaa mipango ya Uhuru). Majina ya Jefferson, Hamilton, Madison, Washington na Lincoln yanapatikana kwenye mitaa ya miji yote, katika kila jimbo la Marekani ili kudumisha kumbukumbu, kuenzi na kufundisha vizazi umuhimu wa watu hao.

Hapa kwetu hali haiko hivyo. Mashujaa wetu wanabakia kuwa Mwalimu Nyerere peke yake na watu wachache sana ambao viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wamewateua.Kwa hivyo basi, wakati huu tukiadhimisha kumbukumbu ya miaka 53 ya Uhuru wa taifa letu, ni vizuri basi, pamoja na mambo mengine, tukawakumbuka watu ambao nchi imewasahau na kuwaweka kando (marginalized) ambapo pengine kama si wao historia ya nchi yetu ingeandikwa kwa namna nyingine. Orodha yao ni ndefu sana, na kwa kweli siyo kusudio la makala haya kuwaorodhesha wote hapa chini, lakini tujiulize inakuwaje leo hii watu kama John Rupia, Mwinjuma Mwinyikambi, Jumbe Tambaza, Zuberi Mtemvu, Haidar Mwinyimvua, Dossa Aziz na Mshume Kiyate wawe ni watu wa kawaida tu kwetu?

Katika siku za mwanzo za harakati za kudai uhuru, chama cha TAA na baadaye TANU hakikuwa na fedha za kujiendesha kufanikisha shughuli zake kubwa na ndogo za kila siku. Katika kufanya hayo, chama kiliwategemea watu wachache ambao walikuwa na uwezo wa kifedha kwa wakati huo. Miongoni mwa watu hao ni Mzee John Rupia, Dossa Aziz, Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate, Mwinjuma Mwinyikambi, Haidar Mwinyimvua pamoja na familia ya kina Sykes. Hawa wote kwa wakati huo walikuwa ni Waafrika wazalendo wenye kumiliki mali kama mashamba, majumba na biashara mbalimbali.

Pamoja na kazi nyingine ngumu walizozifanya usiku na mchana, mabwana wakubwa hawa walijitolea mali zao nyingi sana kwa ajili ya harakati za kupigania uhuru bila kujali kama watapata hasara ama kufilisika kwa kufanya hivyo. Mzee Haidar Mwinyimvua alikuwa akiishi Wadigo street Kisutu, jijini Dar es Salaam, jirani na mahala alipozaliwa mwandishi huyu. Mzee Haidar alikuwa fundi cherehani lakini pia alimiliki majumba (landlord) yaliyotapakaa jijini Dar es Salaam wakati huo. Alikuwa pia Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU kwenye miaka ya 50. Habari zinasema alipata kuuza nyumba yake na fedha kuzipeleka katika harakati za ukombozi wa taifa hili kutoka minyororo ya ukoloni. Mzee Haidar, alikuwa na watoto wasiopungua 12 hivi waliohitaji kula, kulala na kusoma; lakini kwa mapenzi ya nchi hii na kuuchukia ukoloni, aliona bora awalaze njaa wanawe lakini nchi yetu iwe huru. Mtoto mkubwa wa Mzee Haidar ni Sheikh Ahmed Haidar, Imam Mkuu wa Msikiti wa Mwinyikheri pale Kisutu, Dar es Salaam.

Mmoja wa Waafrika waliokuwa na pesa nyingi kabla ya Uhuru ni Mzee John Rupia. Huyu alimiliki mashamba jijini Dar es Salaam pamoja na nyumba kadhaa, ikiwamo ya ghorofa (Rupia Building) pale mtaa wa Kitchwele (sasa Uhuru street). Huyu alikuwamo tokea TAA na wakati TANU ilipoanzishwa alikuwa Makamu wa Rais. John Rupia alitoa fedha zake nyingi sana kwa chama kama vile kilikuwa cha kwake binafsi na Julius Nyerere ni mfanyakazi tu. Alimnunulia suti na kumkatia tiketi ya ndege Nyerere kwenda UNO kuelezea azma ya Watanganyika kutaka kujitawala wenyewe. Fedha nyingine za kufanikisha safari zilitolewa na kina Dossa na Sykes. Mzee Mwinjuma Mwinyikambi na Jumbe Tambaza hawa ni babu zangu katika ukoo wetu. Jumbe Tambaza anakuwa binamu ya babu yangu mzaa baba. Kwa hiyo nawafahamu vizuri sana wazee hawa wa Kimashomvi. TANU likuwa ni wao na wao ni TANU. Hawa wazee wawili walikuwa na nafasi za kudumu (permanent seats) katika Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya TANU siku hizo; siyo kwa kupigiwa kura na mtu, bali kwa heshima na nyadhifa zao tu.

Mzee Mwinjuma alilitoa bure shamba lake lote la inayojulikana Kinondoni kwa Mwinjuma kwa TANU, kama zawadi yake ya uhuru pale ulipopatikana mwaka 1961. Vivyo hivyo kwa Mzee Tambaza; yeye alitoa sehemu kubwa ya shamba lake pale Upanga kwa Tambaza, iwe sehemu ya kuzikia Waafrika bure kwani wakati huo makaburi ya Kisutu walikuwa wanazikwa watu wenye asili ya Kiarabu tu. Zamani haikuwa rahisi ‘mwenzangu mimi’ kuzikwa pale kama ilivyo sasa. Fedha zake nyingi nyingine alizitumia kwa kazi ya TANU. Kama hiyo haitoshi, mahala ilipojengwa hospitali kubwa ya Waafrika pale Muhimbili—Wazungu walitengewa European Hospital (sasa Ocean Road) na Wahindi, Hindu Mandal— ilitolewa na Jumbe Tambaza mwaka 1957 tukiwa bado tunatawaliwa na kufa ovyo kwa kukosa tiba bora.

Mshume Kiyate, yeye pamoja na mambo mengine, alichukua jukumu la kumlisha Nyerere kila siku akipeleka kapu kubwa lililosheni kila aina ya chakula nyumbani kwa Mwalimu pale Magomeni, ili kazi ya kutafuta riziki isimwondoe Nyerere kwenye kufikiria kazi za chama. Aliifanya kazi hiyo kwa muda wote wa kudai uhuru na mpaka mwaka 1961 ulipopatikana, alitaka kuendelea kumpelekea Nyerere chakula pale Ikulu, lakini Nyerere akamwambia ‘Mzee Mshume sasa basi tena pumzika’. (Rejea kitabu cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes cha Mohamed Said). Alipokufa hakuna mtu yeyote aliyejua miongoni mwa wakuu wa nchi na maziko yake yalikuwa ya kawaida tu pale Mtaa wa Matumbi, jirani na maeneo ya Faya, Kariakoo, nyumbani kwa mdogo wake Mzee Maguno. Kwa kulipa fadhila na kuonyesha shukrani zake, kwa kipindi fulani, Nyerere alikuwa anamlea pale kwake Msasani, mjukuu wa Mzee Mshume aitwaye Mwinyi Kiyate, baada ya babake na babu kufariki.

WAZEE%2BWA%2BTANU.jpg
Kushoto Mohamed Jumbe Tambaza na Kulia ni Mshume Kiyate

Dossa Azizi, ni mtu mwingine aliyekuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere wakati huo. Dossa ni mtoto mkubwa wa Mzee Azizi Ali wa Mtoni Dar es Salaam. Wengine mashuhuri ni Hamza na Ramadhani Azizi. Azizi Ali, alikuwa Mwafrika tajiri wakati wa ukoloni akimiliki magari na majumba mjini. Mwanawe, Dossa Azizi hakuwa tu mfadhili mkubwa wa TANU, lakini pia ndiye aliyetoa gari yake binafsi iwe gari ya mwanzo kabisa kwa matumizi ya chama na Nyerere wakati huo. Ilikuwa gari ya Dossa Azizi aliyopanda Nyerere siku aliporudi kutoka safari yake ya kihistoria ya Umoja wa Mataifa alikotoa hotuba ya kusisimua, kuhusu mustakabali wa watu wa Tanganyika na kujitawala wenyewe, hotuba ambayo— habari zinasema— ilikuwa imeandikwa mapema na Abdulwahid Sykes.

Siku hiyo gari ya Dossa ilikwenda mpaka mahala iliposimama ndege (apron) na ‘kumbeba’ Nyerere mpaka mjini akipungia watu mkono huku gari likisukumwa kwa wimbo maarufu wa “baba kabwela Uno” (yaani kwa Kizaramo baba karudi UNO). Dossa Azizi alikufa na kuzikwa mpweke shambani kwake Mlandizi. Nyerere hakuhudhuria wala chama alichokitumikia katika nyadhifa mbalimbali wakati wa uhai wake pia hakikutuma mwakilishi. Inasikitisha sana. Pengine ndio sababu za misukosuko na kutoelewana kunakotokea nchini sasa hivi ni matokeo ya laana hizo. Siku zote Mungu huwa hawaachi hivi hivi madhalimu; anazo namna zake nyingi za kutoa adhabu hapahapa.

WAZEE%2BWA%2BTANU%2B%282%29.jpg
Waziri Dossa Aziz Kama Alivyokuwa 1955
Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu, ni mwanaharakati mwengine wa kupigiwa mfano katika mapambano ya ukombozi wa nchi hii kutoka katika madhila na makucha ya ukoloni wa ‘Ulaya Ingereza’. Kwa ujinga tu na sababu wanazozifahamu wao, watu wengi wamekuwa wakiuchukulia utawala wa Kingereza kama vile halikuwa jambo baya—wazungu walitutesa sana! Ma-PC na Ma-DC walikuwa wanachapa watu wazima viboko. Utawala wa Kiingereza haukuwa na jema lolote kwetu kwani ulituweka sisi Waafrika— wenye nchi hii— katika daraja la chini kabisa kibaguzi. Ukoloni uliwatukuza Wazungu kama daraja la kwanza; Wahindi daraja la pili; Waarabu daraja la tatu na Weusi wote daraja la mwisho; kwenye masomo, tiba, ajira na makazi.

Mzee Saleh Abdallah Tambaza, ni babu ya mwandishi huyu, ambaye pamoja na kaka yake Mzee Kidato Tambaza, walikuwa wanamiliki ardhi kubwa sana Upanga, jijini Dar es Salaam wakati wa ukoloni na kabla ya hapo. Eneo hilo lilianzia Selander Bridge, mahala walipokuwa wakivua samaki, Palm Beach, Sea View na kuzunguka mpaka maeneo ya Mahakama ya Kisutu, maeneo ya Diamond Jubilee, makao makuu ya Jeshi na Hospitali ya Tumaini. Miembe mikubwa ya miaka mingi, minazi, mikungu na mizambarau ambayo ipo bado hadi sasa ni kielelezo tosha (classic example) ya dhulma ya wazungu. Wakoloni waliwataka babu zangu wahame hapo kwa sababu tu hapafai kukaa mtu mweusi tuwaachie Wahindi upepo wa bahari. Wazungu nao peke yao wakawa wanaburudika kule Oysterbay (sasa Masaki). Ukionekana huko mtu mweusi ni mpishi au mkata majani (house nigger).

Babu alichachamaa sana, akapambana sana na DC wa kizungu wakati huo; lakini alishindwa na shamba likaenda kwa malipo kiduchu waliotaka watawala kutoa. Mzee Saleh alihamia eneo la Mabibo External kumalizia uhai wake, lakini alipokufa mwaka 1949 alirudishwa kuzikwa Upanga, na kaburi lake liko pale ulipojengwa Msikiti wa Maamur sasa hivi. Msomaji, hebu tafakari kidogo inawezekana vipi leo hii mtu akamsahau Zuberi Mtemvu (baba wa Abbas Mtemvu, mbunge wa sasa wa Temeke), mtu ambaye ndiye aliyekuwa katibu mkuu wa kwanza wa TANU? Vipi historia ishindwe kumtaja mtu huyu ambaye baada ya kuhitilafiana na Nyerere alianzisha chama chake cha siasa – African National Congress—kwa kazi ileile ya kudai uhuru? Vipi asitajwe, wakati chama chake kilimweka kwenye kinyang’anyiro (ballot box) cha kugombea urais mwaka 1962 na kama angeshinda ndiye angekuwa rais wetu?

Mtemvu alipata kura nyingi sana kwenye majimbo ya Bukoba na kuipiku TANU. Alizunguka sehemu nyingi duniani, hasa nchi za kisoshalisti wakati huo na kupendwa kuliko chama cha TANU. Makao makuu ya ANC yalikuwa mtaa wa Nyamwezi, Kariakoo Dsm, kwenye ghorofa iliyoitwa Kiruka Building ya Mzee Nassor Kiruka. Uhuru haukuletwa na Nyerere na TANU tu. TANU ilikuwa na ushawishi mkubwa tu na hivyo ikashinda uchaguzi kwa kupata viti vingi, lakini vyama vilikuwa zaidi ya TANU kwenye mapambano. Pamoja na Congress cha Zuberi Mtemvu, kilikuwapo chama maarufu cha UTP— United Tanganyika Party— kilichoongozwa na Sheikh Hussein Juma na nduguye Hassan Juma. Kilikuwapo pia chama cha AMNUT—All Muslim National Union of Tanganyika, nacho kiliweka mgombea. Hawa wote ni mashujaa wetu, kwani walifanya kazi ileile ya kudai uhuru. Mtume Muhammad (S.A.W) alipopewa utume kule Mecca, alipata taabu sana. Hakuweza peke yake kukubalika kirahisi bila ya msaada wa masahaba akina Abubakar, Omar, Ali, Bilal ibn Rabah, Othman bin Afan na wengine wengi.

Sasa kwa kuthamini michango ya watu hao, Mtume Muhammad na dini kwa ujumla inaenzi na kuthamini mchango wa akina Abubakar kupita kiasi mpaka imefika mahala wametabiriwa pepo kabla ya kufa wakiwa bado wapo hapa hapa duniani. Bilal Ibn Rabah alikuwa mtumwa wakati fulani lakini alikuwa akiteswa sana na bwana wake aliyekuwa kafiri kwa sababu ya kuukubali kwake Uislamu. Ilikuwa ni Sayiddna Abubakar aliyemgomboa kwa kitika kikubwa cha fedha ili awe huru.

Hadithi imepokewa kwamba kwa kitendo hicho Sayiddna Omar alimwita Abubakar hivi:

“Abubakar Sayiddna; attaka Sayidduna!!”
Maana yake ni kwamba Abubakar ni mtukufu wetu, lakini leo ametuokolea mtukufu wetu mwingine!

Sasa nyie Watanzania, watu waliokufanyieni hayo vipi muwaone kama vile wa kawaida? Tena mnapinga na kukataa kwamba hawakufanya chochote. Ni wizi wa fadhila huo. Historia ya Tanganyika kabla ya uhuru inakuwa si sahihi kama hukuwataja au kutambua mchango wa familia ya kina Sykes.Mzee Kliest Abdallah Sykes, alizaliwa Pangani mkoani Tanga mnamo mwaka 1894 wakati wa utawala wa Ujerumani hapa Tanganyika. Mzee Kliest Sykes alikuja kuwa askari shujaa wa Wazungu wa Kijerumani ambao walikuwa na kambi kubwa ya kivita eneo hilo.Katika uhai wake alijaaliwa watoto watatu wa kiume akiwamo Abdulwahid, Ali na Abbas. Alifariki dunia jijini Dar es Salaam mwaka 1949 baada ya kuwa amefanya kazi kubwa ya kuanzisha 1929, taasisi ya African Association iliyounganisha Waafrika wote. Historia ya nchi yetu itakuwa imechakachuliwa kama haitazungumza mchango wa mzee huyu pamoja na ule wa watoto wake katika mapambano dhidi ya ukoloni.

AA ndiyo iliyokuja kuzaa chama cha TAA na baadaye TANU. Jina la TANU lilibuniwa na Abdulwahid na Ali Sykes vitani Burma mwaka 1945 wakiwa na usongo wa kuja kuanzisha mapambano ya kukomboa watakaporudi nyumbani.Katika kitabu chake kuhusu maisha ya Abdulwahid Sykes, mwanahistoria maarufu nchini Alhaj Mohamed Said anaandika:

“…ilikuwa hapa siku ya mkesha wa Krismas 1945 Abdul na askari wengine pamoja na mdogo wake Ali na James Mkande, walifanya makubaliano ya kuunda chama cha siasa kudai uhuru wa Tanganyika mara tu watakaporudi nyumbani baada ya vita.’’ (Angalia Said Uk. 62).

20140910_144400.jpg
Abdulwahid Sykes Kama Alivyokuwa 1960

Mwaka 1954 wakati TANU ilipoasisiwa, Ali Sykes ndiye aliyebuni na kugharimia ununuzi wa kadi za chama kipya yeye mwenyewe akiwa na kadi namba 2. Kakake Abdulwahid namba 3, Dossa namba 4 na kadi namba 1 ikiwa ya Nyerere. Vipi taifa makini linaweza kuwafanyia hiyana watu wa namna hiyo? Watu waliohatarisha uhai wao ili leo ili sisi tuwe huru; haiingi akilini kwamba nchi inaweza kuwasahau kiasi hiki. Mimi bado nakumbuka, pale mchana ule wa Jumamosi, Oktoba 12, 1968 mji wa Mzizima ulipozizima baada ya habari kuzagaa kwamba Abdul Sykes ameaga dunia. Alikuwa mtu mashuhuri sana jijini Dar es Salaam, si tu kwamba alikuwa mwanasiasa lakini kipenzi na rafiki wa watu wengi akiwemo baba wa mwandishi huyu. Alizikwa na maelfu ya watu Jumapili Oktoba 13, katika makaburi ya Kisutu katika mazishi ambayo yalihudhuriwa pia na Mwalimu Nyerere na waasisi wengine wa taifa hili.

Lakini Waswahili wana msemo kwamba ‘maji hufuata mkondo’. Mtoto wa Abdulwahid, aitwaye Kliest Sykes damu ilipomchemka mwanzoni mwa mwaka 2000 alikuja kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.Moja ya kazi zake za kujivunia ni kubuni huu mradi mkubwa kabisa wa mabasi ya mwendo kasi BRT kwa jiji la DSM ambao viongozi kadhaa sasa wanajinasibisha (attributed) nao. Balozi Abbas Sykes ni mmoja kati ya waasisi wa TAA baadaye TANU. Huyu ni mdogo wa mwisho wa Abdulwahid Sykes lakini kwa namna ya pekee kabisa alikuwa na mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa nchi yetu. Mara baada ya Tanganyika kuwa huru 1961, Abbas Sykes, akiwa kijana mdogo wakati huo, ndiye aliyekuwa Provincial Commissioner wa kwanza mwafrika wa Jimbo la Dar es Salaam. Katika kipindi kirefu sana Balozi Sykes aliiwakilisha Tanzania nchini Canada, Italia na Sudan mpaka alipostaafu kazi hiyo kwa umri. Kwa hiyo Watanzania tufungue ukurasa mpya tuiandike tena historia ya mapambano ya ukombozi wetu kama inavyostahili—tunachekwa.

image%2B%281%29.jpg
Kushoto Kwenda Kulia: Hussein Shebe, Abdallah Awadh, Balozi Abbas Sykes, Mohamed Said na
Kleist Sykes Msikiti wa Kipata Katika Hawli ya Marehemu Ally Sykes 2014

Simu : 0715 808 864/0784 808 864. Barua pepe: atambaza@yahoo.com
 
Nakukubali sana Mzee MoSa kwa uchambuzi wa historia,ngoja Yericko Nyerere apitie atupe naye mtizamo wake.

Huyo atasubiri watu wasahau sahau hii nyuzi aanzishe yake abadili para na maneno aseme yeye ndiye aijuwae historia na hakuna zaidi yake.

Kishayafanya hayo humuhumu, na mwingine ajiitae Mzee Mwanakijiji wana plagiarize wakijifanya wao ndio wenye kuwajuwa wote waliotajwa humu, kumbe wameyakokotoa kwa Al Alama Mohamed Said.
 
Nmeangalia kwa makini picha ya Kamanda Abdulwahid, kumbe miaka ya 60 huko watu walishastaarabika! Ukiangalia picha tu unajua jamaa ni mjanja,yaani ni mtoto wa mjini!

Kuna nia fulani( OVU) inayosababisha wazee hawa waliojitolea kwa hali na mali kusahaulika. Bibi Titi kabakia jina tu pale makutano ya barabara ya Morogoro! . Ifike magali tuwaenzi wazee hawa!
 
Huyo atasubiri watu wasahau sahau hii nyuzi aanzishe yake abadili para na maneno aseme yeye ndiye aijuwae historia na hakuna zaidi yake.

Kishayafanya hayo humuhumu, na mwingine ajiitae Mzee Mwanakijiji wana plagiarize wakijifanya wao ndio wenye kuwajuwa wote waliotajwa humu, kumbe wameyakokotoa kwa Al Alama Mohamed Said.
Kaka hapa utakesha.mada zinazowataja wenye majina hayo tena zikionyesha walikandamizwa mahali flani unachangamkaga sana..by the way, unadhani kwanini hawajatajwa kabisa kama one of heroes?
 
Na changia leo but sijutii keani mimi mwenyewe nimukuwa nukijiuliza medali wanaxopewa watu pale ikulu kwa nini wasipewe madhujaa kama haws badala yake wanapewa wapika chips,jamani Tanzania Tanzania!...
 
Historia nzuri sana. Mwandishi angegusia na wazee wa bara ambao pia wana mchango wao mkubwa tu, kwani uhuru haukuletwa na watu wa pwani tu
 
Historia nzuri sana. Mwandishi angegusia na wazee wa bara ambao pia wana mchango wao mkubwa tu, kwani uhuru haukuletwa na watu wa pwani tu

Row,
Nakushauri usome kitabu changu, "The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924 - 1968) The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika (1998)."

Humo utakutana na maashujaa wengi kutoka bara.
Kwa kuanzia hebu ingia hapa: KIPINDI MAALUM MIAKA 53 YA UHURU WA TANGANYIKA: HISTORIA ILIYOSAHAULIKA YA SHUJAA HARUNA TARATIBU - Mohamed Said
 
Kama hujui ulikotoka huwez kujua unakokwenda hili linawafuatilia walio jifanya hawajui kina nanani wamewafksha pale
 
Mzee unaweza kofautisha jinsi wakoloni wa kiingereza na wale wa kiarabu walivyotofautiana katika kuwadhalilisha mababu zetu waafrika?
 
Mwandishi Mbona hujazitaja familia mbili? Bomani na Mbowe (baba wa Freeman) mengine nayakubali hasa laana iliyopo CCM ambayo kimsingi laana hiyo imeasisiwa na Nyerere mwenyewe.
 
Back
Top Bottom