Mashimo ya Mfalme Suleiman

Baada ya hivi, hakukawia kupona, lakini Bwana Henry hakumwambia habari za vitendo vya Foulata mpaka alipokuwa karibu ya kupona. Bwana Good akasema, ‘Mwambie kuwa ameniokoa, nami sitasahau kabisa wema wake.’


Nikamwambia Foulata maneno aliyosema Bwana Good na Foulata akafurahi sana, akamtazama kwa macho ya mapenzi akasema, ‘Sivyo, bwana, labda bwana wangu amesahau kuwa yeye ndiye aliyeokoa maisha yangu, na mimi ni kijakazi wa Bwana.’


Baada ya siku chache Ignosi akafanya baraza kuu akakubaliwa na wakubwa wote wa nchi. Ikawa sherehe kubwa sana, na askari wale waliobaki katika jeshi lile la Wajivu waliwekwa mbele wakapewa shukrani za mfalme kwa kazi nzuri na ushujaa waliofanya katika vita.

Kila mtu alipewa zawadi ya ng’ombe na wote wakapandishwa kuwa wakubwa katika jeshi jipya ambalo vile vile liliitwa kwa jina la Wajivu.


Tena Ignosi alithibitisha maneno yale aliyotuahidi, mbele ya watu wote, yaani, watu hawatauawa tena bila ya kuhukumiwa, naya kuwa desturi ile ya kuwafichua wachawi itakoma mara moja.


Baraza ilipovunjika tulimsuburi Ignosi tukamwambia kuwa sasa tuna hamu ya kuzifichua siri zile za Mashimo yale ya Sulemani ambayo yalikuwepo mwisho wa Njia Kuu ya Sulemani; tukamuuliza kama amekwisha pata habari yoyote, akajibu, ‘Rafiki zangu, nimepata habari kuwa ni pale wanapokaa Wale Watatu Walio Kimya, ambao Twala alitaka kumuua Foulata awe ndiye mhanga wao.


Tena ni pale katika shimo kubwa wafalme wanapozikwa; ndipo mtakapoona maiti ya Twala amekaa pamoja na wale waliomtangulia. Na hapo lipo shimo lililokwenda chini sana lililochimbuliwa na watu wa zamani sana, labda kwa makusudio ya kutafuta mawe ya thamani uliyotaja.


Hapo ndipo Mahali pa Mauti, na humo kuna chumba ambacho hakijulikani. Ila na mfalme na Gagula. Twala alikijua lakini sasa amekufa, nami sikijui, wala sijui nini kilichomo.

Lakini imesimuliwa kuwa zamani mtu mweupe alivuka milima, akaongozwa na mwanamke mmoja, akaonyeshwa chumba kile cha siri, akaonyeshwa hazina.


Lakini kabla hawajaweza kuzichukua, akampitia kinyume na kuwaambia adui zake, akafukuzwa na mfalme wa wakati ule, na tangu siku ile hapana mtu aliyeingia katika mahali hapo.’


Nikasema, ‘Hadithi hiyo ni ya kweli Ignosi, maana tuliona maiti ya huyo mtu katika milima.’ Akajibu, ‘Ndiyo, tulimwona, na sasa nimeahidi kuwa kama mnaweza kukifikia chumba hicho, mna ruhusa kuchukua mawe yale ikiwa yapo.’

Nikasema, ‘Hicho kito unachovaa juu ya kipaji cha uso kila siku chathibitisa kuwa yapo.’ Akasema, ‘Labda, kama yapo mnayo ruhusa kuchukua kadiri mnayotaka, yaani ikiwa ni lazima mniache, ndugu zangu.

’Nikasema, ‘Lazima, lazima tukitafute hicho chumba .’ Akajibu, ‘Yupo mtu mmoja tu anayeweza kutuonyesha, naye ni Gagula.’

Nikasema, ‘Na kama hatakubali kutuonyesha itakuwaje?’
Akasema, ‘Basi atakufa. Nimemwacha hai kwa kusudio hilo tu. Tumwite tuone kama atakubali.’

Akatuma mtu kumwita. Baada ya kitambo akaletwa na askari huku akiwatukana. Mfalme akamwambia askari wamwache, na mara alipoachiliwa akakaa chini, na macho yake yakang’aa kama kito, akasema, ‘Wataka nini kwangu, Ignosi? Huthubutu kunigusa, ukinigusa nitakuua papo hapo ulipokaa. Jihadhari na uchawi wangu.’

Ignosi akajibu, ‘We mbwa jike, uchawi wako haukumwokoa Twala, wala hauwezi kunidhuru mimi.

Sikiliza, nataka utwambie habari za siri za mawe yale yanayong’aa’.
Gagula akacheka, akasema, ‘Ha!Ha! Hapana ajuaye ila mimi nijuaye siri hizo, nami sitakwambia kamwe.

Mashetani weupe hawa watakwenda zao mikono mitupu.’
Ignosi akasema, ‘Lazima utaniambia. Nitakushurutisha.’ Akajibu, ‘Kwa namna gani, Ewe mfalme? Wewe kweli ni mkubwa mwenye nguvu lakini nguvu zako zinawezaje kuukamua ukweli kutoka kwa mwanamke?’


Ignosi akajibu, ‘Najua ni vigumu, lakini nitafanya.’ Gagula akasema, ‘Ndiyo, lakini kwa namna gani?’ Ignosi akasema, ‘Hivi, ikiwa huniambii, utakufa kwa mateso ya pole pole.’
Gagula akalia, akasema, ‘Kufa? Hutothubutu kunigusa; wewe hujui mimi ni nani.


Umri wangu wadhani ni miaka mingapi? Mimi niliwajua baba za baba za baba zako. Nchi ilipokuwa mpya, mimi nilikuwapo; nchi itakapokuwa imechakaa mimi nitakuwapo. Siwezi kufa ila kuuawa kwa ajali, maana hapana anayethubutu kuniua.’


Ignosi akajibu, ‘Ndiyo, lakini nakwambia kuwa mimi nitakuua.’ Akashika mkuki wake akamsimamia juu tayari. Yule kizee akasema, ‘Sitakuonyesha kabisa; huwezi kuthubutu kuniua, huwezi kabisa. Atakayeniua mimi atalaaniwa milele.’


Pole pole Ignosi akashusha mkuki hata ncha yake ilimchoma kidogo, na mara Gagula akaruka juu kwa sauti kali, kisha akaanguka chini akagaagaa, huku akisema, ‘Basi, basi, niachilie niishi nami nitakuonyesha.’


Ignosi akasema, ‘Vema. Nilihisi’ kuwa nitapata njia ya kukufanya ukubali. Kesho utafuatana na Infadus na ndugu zangu weupe, kuwaonyesha hapo mahali, na uangalie sana usifanye makosa, maana usipowaonyesha, hakika utakufa.’


Yule kizee akajibu, ‘Sitakosa, Ignosi. Ni desturi yangu kutimiza niliyoahidi. Ha!Ha!Ha! Zamani mwanamke mmoja alimwonyesha mtu mweupe kile chumba na tazama! Alipatikana na maovu. Jina lake lilikuwa Gagula vile vile.


Labda mimi na huyo mwanamke ni mmoja.’ Na mcho yake maovu yalizidi kung’aa.
Nikasema, ‘Mwongo, hayo yalitokea zamani vizazi kumi nyuma.’


Akasema, ‘Labda, labda; mtu akiishi miaka mingi pengine husahau. Labda lilikuwa jina la mama yangu nayeye aliniambia, kwa hakika jina lake lilikuwa Gagula vie vile. Lakini, angalieni, nawaambia ya kuwa katika chumba kile yalipo hayo mawe, mtaona kifuko cha ngozi kimejaa mawe meupe.


Huyo mtu alijaza kifuko hicho, lakini hakuwahi kukichukua. Alipatikana na maovu , nasema alipatikana na maovu! Labda aliyeniambia alikuwa mama wa mama yangu! Itakuwa safari ya furaha.


Tutapita katika mahali walipopigana askari juzi, tutaona maiti waliokufa katika vita. Macho yao yatakuwa yamekwisha pofuka sasa, na mbavu zao zitakuwa zimekwisha bonyeka. Ha! Ha!Ha!’
 
SURA YA KUMI NA SITA


Giza lilikuwa limekwisha ingia siku ya tatu tulipofika mahali pa kupiga kambi chini ya ‘Vichawi Vitatu’ yaani ile milima mitatu iliyokuwa mwisho wa Njia Kuu ya Sulemani.

Katika safari yetu tulikuwa sisi watatu, na Foulata, na Infadus, na Gagula aliyechukuliwa katika machela, ambaye daima tulimsikia akitukana na kuguna, na askari wachache pamoja na viongozi na watumishi.

Siwezi kusahau milima ile namna ilivyokuwa katika mwangaza wa jua la asubuhi; ilikwenda juu sana hata kufika mawinguni.


Tulipotazama juu tuliona Njia Kuu ya Sulemani inakwenda moja kwa moja mpaka kilele cha katikati, mwendo wa kiasi cha saa mbili.


Afadhali nisijaribu kueleza mambo tuliyokutana nayo katika safari hii, msomaji na akisie mwenyewe.

Lakini sasa tunakaribia mashimo yale ya ajabu ambayo ndiyo sababu aliyofia Yule mzee Mreno zama za miaka mia tatu nyuma, na tena Yule mjukuu wake aliyekuwa rafiki yangu, na tena, labda hata na ndugu yake Bwana Henry.


Je, ajali yetu itakuwa ya namna hiyo hiyo? Wao walipatwa na maovu kama alivyosema Yule kichawi Gagula; na sisi je? Tulipokuwa tukienda katika ile njia nzuri sikuweza kujizuia nisiwe na hofu. Na tena nadhani Bwana Good na Bwana Henry vile vile walikuwa na hofu.


Kwa muda wa saa moja na nusu tulikwenda kwa miguu upesi upesi tukivutwa na tamaa, hata wale waliochukua machela waliona shida kufuatana nasi, na Gagula akatoa kichwa chake katika machela akasema, ‘Nendeni pole pole nyinyi watu weupe, nyinyi mtafutao hazina, mbona mnakwenda mbio kuonana na maovu ?’

Akacheka kicheko cha uhabithi kilichochukiza sana na kufanya mwili kunisisimka, na kwa muda kidogo tulipunguza mwendo wetu.


Basi tuliendelea kwenda mpaka tuliona shimo kubwa lililokwenda chini sana mbele yetu, katikati ya mahali tulipo na kile kilele. Nikamuuliza Bwana Henry, ‘Je, unajua shimo hili ni la nini?’

Yeye na Bwana Good wakatikisa vichwa vyao. Nikawaambia, ‘Ni dhahiri kuwa hamjapata kuona mahali panapochimbwa almasi.


Nadhani shimo hili ni shimo la kuchimba almasi.’
Basi tulifuata njia ili tupate kutazama vitu vitatu tulivyoona kutoka mbali kidogo, na tulipokaribia tuliona kuwa ni Wale Watatu Walio Kimya, wanaoogopwa na Wakukuana. Lakini hatukutambua vema ukubwa wao mpaka tulipofika karibu kabisa.


Hapo tuliona masanamu matatu, na baina ya kila sanamu na mwenzake ilikuwa nafasi ya hatua ishirini, na wote wanatazama uwanda wa Loo. Masanamu mawili yalikuwa ya wanaume na lile la tatu lilikuwa la mwanamke.


Basi tulisimama tukatazama sana masanamu yale, na baadaye kidogo Infadus akatujia, akainua mkuki wake kuyaamkia yale masanamu, akatuuliza kama tunataka kuingia Mahali pa Mauti sasa hivi, au tutangoja mpaka kwisha chakula cha mchana.
 
Ikiwa tunataka kwenda sasa hivi, basi Gagula yu tayari kutuongoza.

Kwa kuwa ilikuwa saa tano tu, nasi tulikuwa na hamu sana kupatazama mahali penyewe, tulisema kwamba tunataka kwenda sasa hivi, nami nikatoa shauri kama afadhali tuchukue chakula pamoja nasi, maana labda tutakawia katika mahali penyewe.
Basi machela ya Gagula ikaletwa, akatoka ndani.


Huko nyuma Foulata aliweka nyama na vibuyu viwili vya maji katika kikapu. Gagula alipotoka katika machela akacheka na akajikongoja kushika njia. Sisi tulimfuata, mpaka kwenye mlango wa pango.


Hapo Gagula akasimama akatungojea, na hata hivi sasa akicheka kicheko cha uhabithi. Akasema, ‘Sasa watu weupe waliotoka katika nyota, mashujaa wenye busara, mtayari?


Tazama mimi nipo hapa kufanya aliyoniamuru bwana wangu mfalme, yaani kuwaonyesheni hazina na mawe meupe yanayong’aa.Ha!Ha!Ha!’
Nikajibu, ‘Sisi tu tayari.’


Akasema, ‘Vema! Vema! Jipeni moyo mpate kuvumilia mtakayo yaona. Nawe Infadus, utakuja, wewe uliye mhaini bwana wako?’


Infadus akakunja uso kwa hasira, akajibu, ‘La, mimi siji, hayanihusu. Lakini wewe, Gagula, utawale ulimi wako, wangalie pia mabwana zangu.


Mimi ninawatia katika mikono yako, na ukiudhuru hata unywele mmoja, wewe Gagula, utakufa, hata ukiwa mchawi wa namna gani! Umisikia?’


Gagula akajibu, ‘Nasikia Infadus. Lakini usiogope, mimi maisha nafuata amri za mfalme tu. Mimi nimefuata amri za wafalme wengi Infadus, lakini mwisho wao walifuata amri zangu mimi.

Ha!Ha! Nakwenda kutazama nyuso zao mara moja tena, na vile vile nitatazama uso wa Twala. Haya twendeni, twendeni.’


Akachukua kibuyu cha mafuta akatia utambi kama taa. Bwana Good akamuuliza Foulata, ‘Unakuja, Foulata?’ Akajibu, ‘Naogopa, bwana wangu.’ Akasema, ‘Basi nipe kikapu.’

Akajibu, ‘La, bwana wangu, uendako nami nitakwenda.’ Basi Gagula hakungoja zaidi, akaingia katika ule mlango, tukaona kuwa ni kinjia cha kutosha watu wawili kwenda pamoja, tena giza tupu.

Tukamfuata Gagula huku tukiogopa na kutetemeka; tukasikia kishindo cha mbawa, na mara Bwana Good akauliza, ‘Je, nini kile, kitu kimenipiga usoni?’ Nikasema, ‘Haya twendeni, alikuwa ni popo tu.’


Basi tukaenda mbele na tulipokuwa tumekwisha kwenda kadiri ya hatua hamsini tuliona kuwa giza linapungua, na halafu tukajiona katika mahali pa ajabu.
 
Tumo katika pango kubwa lililo kwenda juu sana, hata kwa juu lilikuwa kadiri ya hatua mia moja. Kutoka pango hilo mapango madogo yaliingia katika mlima.

Basi tulitaka kutazama kila mahali, lakini Gagula hakutupa nafasi, yeye alikwenda mbele mpaka mwisho wa pango kubwa, tukamfuata.

Tulipofika huko tuliona mlango mwingine na Gagula akatugeukia akauliza, ‘Mko tayari kuingia katika Mahali pa Mauti?’

Tukajibu, ‘Haya tu tayari.’
Bwana Henry akasema, Mambo yanaanza kutisha sasa.’ Basi wakanipa nafasi mimi nitangulie, lakini katika roho yangu niliogopa, mpaka Bwana Good aliposema, ‘Haya, twende rafiki, au kiongozi wetu mzuri atatupoteza.’


Basi kuambiwa haya, nikaanza kuingia katika kinjia, na baada ya hatua ishirini hivi, nilijiona katika pango lingine.

Lilikuwa giza kidogo, lakini nilipozoea giza niliona meza ndefu na mwisho wa meza sanamu jeupe kubwa imekaa, na kuzunguka meza masanamu meupe mengine yenye kimo cha mtu.

Tena nikaona katikati sanamu jingine jeusi kidogo, na macho yangu yalipozoea giza nilitambua masanamu yale ni nini, nikageuka nikakimbia kutoka pango lile kadiri nilivyoweza kwenda mbio.


Kwa kawaida mimi siyo muoga sana, wala siogopi mambo ya kishetani, lakini nakiri kuwa niliyoyaona yalinitisha sana, na Bwana Henry asingalinizuia ningetoka pangoni upesi, na nisingekubali kuingia tena, hata kwa almasi zote zilizopo duniani.


Lakini Bwana Henry alinikamata baraabara, na kwa hivyo nilisimama, Lakini, mara na yeye macho yake yalizoea giza na yeye aliona yale niliyoyaona mimi, mara akaniacha akaanza kujifuta jasho usoni.


Bwana Good akashangaa kabisa, na Foulata akamkumbatia huku akilia tu. Gagula tu ndiye aliyecheka sana.

Mambo tuliyoyaona yakawa ya kutisha mno. Maana mwisho wa meza ile ndefu tuliona mifupa ya mtu mrefu sana, urefu wa futi kumi na tano au zaidi, naye ameshika mkuki mkononi, akawa kama sanamu za hayo Mauti yenyewe.

Nikasema, ‘Je, hi! Ni nini?’ Na Bwana Good akaonyesha wale waliokuwa wamekaa mezani akasema, ‘Na hawa ni nani?’


Na Bwana Henry akaonyesha Yule mweusi kidogo akauliza, ‘Na huyu ni nani?’
Gagula akacheka, ‘Hee!Hee!Hee! Maovu yanawajia wote waingiao Mahali pa Mauti. Hee! Hee!Hee!Ha!Ha! Njoo Ndovu, wewe uliye shujaa katika vita, njoo mtazame Yule uliyemuua.’


Na kizee huyu akamshika kwa vidole vyake vyembamba akamwongoza kwenye meza. Sisi tukafuata. Alipofika akasimama akamwonyesha Yule mweusi kidogo, Bwana Henry akastuka akarudi nyuma.

Maana pale mezani maiti yaTwala ilikuwepo, mfalme wa hivi karibuni wa Wakukuana, alikaa na kichwa chake amekipakata.

Na maiti huyo alifunikwa chumvi; tukasikia matone ya maji yakidondoka, tukafahamu kuwa maiti ya Twala inageuzwa kuwa jiwe, yaani kwa dawa iliyomo katika yale maji yanyodondoka.


Tukatazama masanamu yale mengine na tukafahamu Maiti za wafalme wa zamani zimekaa kuzunguka meza, na maiti ya mfalme Twala imekaa juu ya meza imepakata kuwa wale ni maiti wafalme wa zamani, na sasa wamekwisha geuka kuwa masanamu ya mawe kwa ile dawa.

Tukahesabu masanamu ishirini na saba, na ile ya mwisho ilikuwa sanamu ya baba yake Ignosi, na kila moja limegeuka jiwe.

Tukaona kuwa desturi hii ya kuweka maiti za wafalme hapa ni ya zamani sana. Lakini sanamu ile kubwa iliokaa mwisho wa meza tuliona kuwa ni kazi ya mikono ya watu wale waliochonga Wale Watatu Walio Kimya.
 
SURA YA KUMI NA SABA

Wakati ule tulipokuwa tukitazama kila kitu katika Mahali pa Mauti. Gagula alikuwa akifanya kazi yake. Alipanda mezani akaenda karibu na maiti ya Twala, na tena akampitia kila maiti akafanya kama anaongea na maiti.

Alipokwisha fanya hivyo akakaa kitambo kidogo chini ya ile sanamu kubwa akaanza kusema maneno mengi kama anasali.

Basi nikasema, ‘Haya Gagula, tuongoze katika chumba.’ Yule kizee akaondoka, akanitazama usoni, akasema, ‘Mabwana zangu hamuogopi?’
Nikajibu, ‘Tuongoze.’

Akasema, ‘Vema, mabwana zangu.’ Akazunguka nyuma ya ile sanamu ya Mauti, akasema, ‘Chumba kiko hapa. Afadhali uwashe taa kwanza.’


Akasimama ukutani. Basi nikawasha taa nikatazama nione mlango uko wapi, nisiuone; niliona ukuta tu. Gagula akacheka sana akasema, ‘Njia ni ile, mabwana zangu. Ha!Ha!Ha!’ nikasema, ‘Usifanye udamisi.’


Akajibu, ‘Mimi sifanyi udamisi, mabwana zangu, tazameni!’
Akatuonyesha ukuta. Tuliinua taa na alipokuwa akituonyesha, ukuta, kumbe ule mkubwa ulianza kupanda juu na kuingia katika sehemu ya juu ya pango.

Namna alivyo fyatua mtambo ulioinua ukuta ule, sisi hatukuona, maana alifanya hila za kutuficha.


Vile ukuta ulipanda pole pole mpaka ukaingia kabisa, tukaona mlango wa kuingilia katika pango la ndani. Sasa hatukuweza kusubiri tena, maana tupo hapo kwenye hazina, lakini mimi nilianza kuogopa na kutetemeka, sijui wenzangu walikuwaje.


Je, itakuwa ni hila tu, au yale maneno ya Da Silvestre yatatokea kuwa ya kweli? Kweli katika pango zimo hazina nyingi sana hata kutufanya kuwa matajiri kupita wote duniani? Punde tutajua.


Gagula akasema, ‘Haya ingieni nyinyi watu weupe mliotoka katika nyota, lakini kwanza msikilizeni mtumishi wenu, kizee Gagula.


Mawe yanayong’aa mtakayoyaona yalichimbuliwa katika shimo lile kubwa lililo chini ya Watatu Walio Kimya, nayo yaliwekwa hapa sijui na nani.

Mahali hapa pameingiliwa mara moja tu tangu wakati ule walipotoka kwa haraka sana wale walioyaweka mawe haya wakayaacha.

Habari za hazina zilijulikana na watu, maana zimekuwa zikipokezana kizazi baada ya kizazi, lakini hapana aliyejua chumba kiko wapi wala siri ya mlango wa chumba hicho.


Lakini mtu mweupe alitokea, akafika nchi hii kwa kuvuka milima ile, sina habari kama yeye alitoka katika nyota, akapokewa vizuri na mfalme wa wakati ule. Ilisadikika kuwa mwanamke mmoja wa nchi hii alisafiri pamoja naye, na Yule mwanamke akapata kujua siri ya ule mlango.


Basi Yule mtu mweupe aliingia pamoja na Yule mwanamke, wakaona mawe, akajaza mawe katika kifuko kidogo cha ngozi ya mbuzi alichokichukua Yule mwanamke ili kuwekea chakula chao.


Alipokuwa akitoka chumbani akainama achukue jiwe moja jingine lililokuwa kubwa, akalishika mkononi.’

Hapa Gagula akanyamaza . nikamuuliza, ‘Yapi yaliyompata Da Silvestre?’
Yule kizee akashtuka mno, akaniuliza, ‘Umejuaje jina la mtu huyo aliyekufa?

Hapana mtu anayejua yaliyotokea; lakini ilikuwa dhahiri kuwa Yule mtu mweupe aliogopa sana, akatupa kifuko kile cha mawe akatoka chumbani mbio huku kachukua jiwe moja tu.’
Jiwe lenyewe ni lile ulilolifungua wewe Makumazahn, katika paji la uso wa Twala.’ Nikamuuliza, ‘Je, hapana aliyepata kuingia tokea wakati huo?’


Akajibu, ‘Hapana, mabwana zangu. Lakini siri ya mlango ilisitirika na kila mfalme amefungua mlango, lakini hapana aliyethubutu kuingia.


Imesemwa kuwa atakayeingia katika chumba hiki atakufa katika muda wa mwezi mmoja, kama mtu Yule mweupe alivyokufa katika pango mlimani pale ulipomwona wewe Makumazahn, na kwa hivyo wafalme hawaingii.

Ha!Ha! maneno yangu ni ya kweli kabisa.’

Basi kusikia maneno hayo, tukatazamana, ghafula nikaona baridi na kuchafukwa na moyo. Kizee huyu alijuaje habari hizi zote?

Basi akasema, ‘Haya ingieni, mabwana zangu. Ikiwa nimesema kweli mtaona kifuko kile cha ngozi ya mbuzi kilichojaa mawe kimetupwa chini, na ikiwa ni kweli kuwa wale watakaoingia watakufa, basi haya mtapata kuyajua halafu!Ha!Ha!Ha!’
 
Akaingia mlangoni huku kachukua ile taa lakini lazima nikiri kuwa nilisita tena.
Bwana Good akasema, ‘Mimi nitaingia, hiki kishetani hakiwezi kunitisha mimi, ‘Akaingia na Foulata akamfuata na sisi tuliwafuata upesi.


Gagula alisimama mbele kidogo anatungoja, akasema, ‘Tazameni, mabwana zangu, wale walioweka hazina hapa walikimbia kwa haraka, wakafikiri kulinda siri, isijulikane na watu wengine lakini hawakupata nafasi.’

Akatuonyesha mawe makubwa yaliyoletwa tayari kusudi kuziba ile njia.
Basi tulikwenda mbele na Foulata akazidi kuogopa akasema kuwa hawezi kuendelea, basi tukamwambia akae atungojee, tukaweka kikapu karibu naye, tukaendelea.


Tulipokwisha kwenda kadiri ya hatua kumi na tano, tuliona mlango wa mbao umekaa wazi.

Yule aliyekuwa wa mwisho kutoka alikuwa amesahau kuufunga au labda alitishwa na kitu. Na pale mlangoni tuliona kifuko cha ngozi ya mbuzi kimejaa mawe! Gagula alicheka akasema, ‘Hee!Hee!


Watu weupe, niliwaambia nini? Sikusema kuwa Yule mtu weupe alifika hapa, akakimbia kwa haraka, akatupa kile kifuko cha mwanamke? Kitazameni!’

Bwana Good akainama akakiokota, akakiona kizito na akasema, ‘Lo! Kimejaa almasi.’
Bwana Henry akasema, ‘Haya twendeni mbele; nipe taa wewe kizee.’

Akatwaa ile taa akaingia chumbani, na sisi tulimfuata karibu na mara tukajiona katika chumba cha hazina za Sulemani.

Tulipozoea giza tuliona chumba kimechimbwa katika mlima. Tukaona pembe za ndovu nyingi sana, yapata mia nne au mia tano. Pembe hizi peke yake zilikuwa zinatosha kumfanya mtu kuwa tajiri maisha yake yote.

Katika upande mwingine wa chumba tuliona masanduku madogo yaliyo pakwa rangi nyekundu, nikasema, ‘Hizi ni almasi, lete taa.’


Bwana Henry akaleta taa akaiweka karibu na sanduku ambalo mbao zake za juu zilikuwa zimevunjika ; nikaingiza mikono yangu na kuitoa imejaa, si almasi bali sarafu za dhahabu. Basi nilirudisha dhahabu ile nikasema, ‘Hatutarudi mikono mitupu.’


Basi Gagula alitwambia, ‘Mabwana zangu mkitaka almasi na muende pale pembeni mtaona makasha matatu, mawili yametiwa muhuri na moja tayari limefunguliwa.’


Kabla sijatafsiri maneno haya kuwaambia Bwana Henry na Bwana Good, nilifikiri moyoni jinsi alivyopata kujua habari hizo huyu Gagula, yaani ikiwa hapana aliyeingia humu tangu Yule mtu mweupe alipoingia zamani, vizazi vingi nyuma.


Gagula alitambua mawazo yangu, akasema kwa maneno ya kunidharau, ‘Ah! Makumazahn, wewe unayekesha usiku, nyinyi mkaao katika nyota, hamjui kuwa wapo wanaoweza kuona hata ndani ya majabali? Ha!Ha!Ha!’

Lakini Bwana Good alikuwa amekwisha ona zile almasi, akasema, ‘Haya jamani, njooni mtazame.’ Tukaenda kwa haraka, tukaona pembeni makasha matatu, mawili yametiwa muhuri na moja limefunguliwa.

Tukatazama tukaona kuwa zimejaa almasi, nikasema kwa sauti ndogo, ‘Sisi ni matajiri kupita watu wote duniani.’

Bwana Henry akasema, ‘Ndiyo, lakini lazima tuzichukue kwetu kwanza!’ Tukasimama tunatazamana, na mara tukamsikia Gagula anacheka tena; Hee!Hee!Hee! Hayo ndiyo mawe meupe mnayopenda; yachukueni, myale, na myanywe, ha!ha!h!’


Basi hapo nilipomsikia akisema maneno hayo, nikaona ni maneno ya kuchekesha tu! Maana nani aliyesikia mtu akila na akinywa almasi! Nikaanza kucheka, na wenzangu nao wakaanza kucheka vile vile; tukacheka sana.


Gagula akasema, ‘Haya, mabwana zangu, chukueni kadiri mnavyotaka.’
Basi tukazidi kutazama almasi zile huku tumefurahi lakini hatukuona jinsi Gagula alivyotoka pole pole katika kile chumba na sasa anakaribia ule ukuta mkubwa wa jabali.

Mara tukashtuka sana kwa kusikia sauti ya Foulata.’Lo!Lo!Lo! Mwamba unaanguka!’
 
Tukasikia sauti ya Gagula, ‘Niachilie wewe! Niachilie. Na tena sauti ya Foulata, ‘Aa!Aa! Amenichoma kisu!’ lakini sasa tulikuwa tunakwenda mbio na tulipofika karibu, mwangaza wa taa ulituonyesha hivi:

Ukuta ule ukirudi pole pole katika mahali pake, na sasa nafasi iliyobaki kwa chini ni kadiri ya futi tatu tu.
Pale karibu na mwamba Foulata na Gagula wamekamatana wa kiviringishana. Damu ilikuwa ikimtoka Foulata, lakini hakukubali kumwacha kile kichawi kilichokuwa kikipigana kama paka wa mwituni.

Ah! Amemtoka! Foulata ameanguka chini na Gagula anatambaa chini ya ukuta wa jabali kama nyoka. Yupo chini sasa! Lo! Amechelewa! Amechelewa! Ukuta unamponda naye analia kwa maumivu. Chini, chini, ule ukuta mzito unazidi kumponda.

Analia vilio tusivyosikia maishani mwetu, kisha, tulisikia namna ukuta ule ulivyombinya mifupa yake, na mara tukafika kwenye ukuta, tumekwisha chelewa, tumekwisha fungiwa ndani!

Sasa tulimtazama Foulata, tukaona kuwa amechomwa kisu maungoni, naye yumo katika kukata roho.

Akasema, ‘Ah! Bwana wangu, nakufa! Gagula alikuwa akinyatia; sikumwona kwanza maana hakukuwa na mwangaza wa kutosha, na ukuta ukaanza kurudi chini; alirudi nyuma ili atazame mara ya pili, nikamwona, nikamshika, akanichoma kisu, na sasa nakufa!’

Basi akafa, na Bwana Good akasimama na machozi yakimtiririka, akasema, ‘Amekufa! Amekufa!’

Bwana Henry akasema, ‘Basi nawe usijisumbue rafiki, maana karibu utaweza kumfuata alipo. Maana huoni kuwa sisi tumezikwa tungali hai?’

Nadhani mpaka Bwana Henry aliposema maneno hayo, hatukutambua kwa hakika hatari itakayo tupata. Lakini sasa tulifahamu.

Jabali lile lililoshuka chini limekwisha kutufungia ndani ya chumba, na aliyejua siri ya kulifungua amekwisha kufa! Amepondeka chini yake! Kwa muda tulipigwa na mshangao, ikawa kama nguvu zimetuisha, na Bwana Henry akasema, ‘ Haya, tutafute siri ya mtambo unaoendesha huu ukuta, upesi.’


Tukapapasa papasa kila mahali tukijaribu kutafuta huo mtambo hatukuona hata alama. Nikasema, ‘Mimi naona kuwa mtambo haupo upande huu; kama ungekwepo kwa nini Gagula alijitia katika hatari ya kutambaa chini apate kutoka kabla ukuta haujashuka?
Alijaribu kutambaa chini kwa sababu alijua kuwa hapana njia nyingine ya kutoka katika chumba.’


Bwana Henry akasema, ‘Lakini Mungu amemlipa upesi, maana kufa kwake kulikuwa kubaya sana. Hatuwezi kuinua ukuta. Basi naturudi katika chumba cha hazina.’


Tukarudi na tulipokuwa tukimpita Foulata niliona kapu lile lenye chakula na vibuyu vya maji, nikalichukua katika chumba. Tukakaa juu ya makasha yale ya hazina, na Bwana Henry akasema, ‘Tugawanye hicho chakula tukitunze kadiri tunavyoweza.’


Tukakigawanya. Chakula kilikuwa cha kutosha kadiri ya siku mbili tu. Tulipokwisha kula kidogo tukaondoka tukatazama kila mahali kutafuta njia ya kutokea tusiione.


Taa ikaanza kuzimika, na mafuta yalikuwa karibu kwisha. Bwana Henry akauliza, ‘Je, Quatermain, sasa saa ngapi?’ Nikatazama saa yangu nikamwambia kuwa ni saa kumi na mbili, nasi tuliingia pangoni saa tano, nikasema, ‘Infadus atatukumbuka, na kama hatatutafuta leo, basi kesho ni lazima atatutafuta.’


Bwana Henry akajibu, ‘Ndiyo, lakini anaweza kututafuta bure. Yeye hajui siri ya kuinua ukuta huu, wala hana habari ya mlango ulipo.

Ni mtu mmoja tu alijua, naye ni Gagula, na hapana mtu mwingine anayejua. Hata akiuona, yeye hawezi kuvunja jabali lile, hata akileta jeshi zima la Wakukuana.

Rafiki zangu, mimi naona hatuna la kufanya ila kujiweka katika mikono ya Mungu. Kutafuta utajiri kumewaangamiza wengi; nasi tutazidisha hesabu yao.’

Hapo taa ikazidi kuzimika. Na mara moja ilipanda juu tena na tukaona pembe zote na makasha ya almasi naya dhahabu, na kifuko kile cha ngozi, na tukamwona maiti Foulata. Kisha taa ikazimika kabisa.
 
SURA YA KUMI NA NANE

Siwezi kabisa kueleza vitisho na taabu za usiku uliofuata. Zilipunguzwa kidogo kwa usingizi, maana hata katika hatari kama ile tuliyokuwa nayo, usingizi ulitujia kwa jinsi tulivyochoka.

Lakini sikuweza kulala sana, maana niliona mauti yananikaribia, kimya kikawa kingi hata sikuweza kupata usingizi. Tumezikwa ndani ya mlima wa theluji, na hata vishindo vya mizinga yote ya dunia haviwezi kutufikia.


Tumetengwa kabisa na kila sauti ya duniani, tumekuwa kama watu waliokwisha kufa. Ndipo nilipokumbuka mambo yote yaliyotupata. Hapo karibu nasi ziko fedha za kutosha kulipia madeni ya watu wote duniani, na kuunda meli zilizo bora, lakini hazitufai kabisa. Kweli, mali ambayo watu wengi huitafuta maisha yao yote, mwisho wake haina thamani hata kidogo.


Usiku ulipita. Baadaye, Bwana Henry akauliza, ‘Je, Bwana Good, unazo chembe ngapi za kibiriti?’ Akajibu, ‘Vijiti vinane tu.’


Akasema, ‘Vema, afadhali washa kimoja sasa tupate kujua ni saa ngapi.’
Akawasha kimoja, na kulikuwa giza totoro, hata alipokiwasha macho yaliingiwa na kiwi. Ilikuwa saa kumi na moja.


Akasema, ‘Afadhali na tule kidogo sasa tupate nguvu kidogo.’ Na Bwana Good akauliza, ‘Ya nini kula, si afadhali tukihimize kifo?’

Bwana Henry akajibu, ‘Kama maisha yapo, basi na tamaa ipo.’ Basi tukala, tukanywa maji kidogo; tukangoja. Kisha Bwana Good akasema, ‘Afadhali na tukae karibu na mlango tupate kumsikia atakayekaribia.’

Basi akakaribia mlangoni akaanza kupiga kelele, lakini wapi! Alifanya kelele nyingi sana, lakini zilitufaa nini? Baadaye akaacha kupiga kelele, maana tuliona kuwa zinatuzidishia kiu tu.

Basi tulikaa tena juu ya makasha yale ya almasi yaliyokuwa na hazina za thamani nyingi, na mimi nilikata tamaa nikaweka kichwa changu kwenye bega la Bwana Henry nikalia na kutokwa na machozi; na nadhani nilimsikia Bwana Good akilia vile vile.


Bwana Henry alikuwa mtu mwema sana! Hata tungalikuwa watoto wawili naye ni mlezi wetu, nadhani asingaliweza kutufanyia wema zaidi.

Alisahau sehemu yake ya taabu akajaribu kutuliwaza kwa kutusimuliwa hadithi za watu waliopatwa na mambo kama haya yaliyotupata sisi, na namna walivyookoka mwishoni.


Na alipoona hadithi zile haziwezi kutuliwaza akatwambia kuwa ni lazima watu wote wafe siku moja, basi sisi tumepungukiwa siku zetu kidogo tu. Alijaribu kwa kila namna kutuliwaza.

Alikuwa mtu mpole na mtaratibu wala hana makuu, lakini alikuwa mtu imara.
Basi mchana nao ulipita kama ulivyopita usiku, tukatazama saa tena tukaona kuwa ni saa moja, na tena tukala kidogo tukanywa, na tulipokuwa tunakula nikapata wazo nikasema, ‘Je, imekuwaje kuwa hewa iliyomo katika chumba hiki ni nzuri? Kweli ni nzito kidogo, lakini ni safi kabisa.’


Bwana Good akashtuka akasema, ‘Kweli! Sikufikiri hivyo. Hewa haiweze kuingia kwa mlangoni, maana pamezibwa kabisa,. Ingelikuwa hewa haingii siku zote, tulipoingia tungalihisi hewa mbaya. Tutazame.’


Basi ikawa ajabu namna tulivyochangamka kwa kupata cheche hizo za tamaa. Na mara sote watatu tulianza kutambaa chini na kupapasa kila mahali tupate kutafuta hata dalili ya hewa.

Kwa muda wa saa nzima na zaidi tulifanya hivi mpaka Bwana Henry na mimi tulikata tamaa tena, maana tuliumia mara nyingi kwa kujigonga na zile pembe na yale makasha, lakini Bwana Good hakukubali kushindwa, akasema afadhali kufanya hivi kuliko kukaa bure.

Baadaye kidogo akatuita, na mara tukamwendea, akasema, ‘Haya, Quatermain, weka mkono wako ulipowangu. Je, unaona kitu?’

Nikajibu, ‘Nadhani nasikia kitu. Nadhani nasikia kama baridi inaingia.’
Akasema, ‘Basi, sasa sikiliza.’ Akasimama akakanyaga chini kwa mguu mmoja, na mara ile tamaa yetu ndogo ikageuka na kuwa tamaa nyingi zilizotujaa maana palilia wazi.
 
nadhani ni vinjia vya mashimo yale ya kuchimbulia almasi.

Baadaye kidogo Niliwasha kibiriti kwa vidole vilivyotetemeka. Maana tulibakiwa na mishale mitatu tu, nikaona tupo katika pembe ya chumba

Kibiriti kilipoangaza nikatazama chini, nikaona kama ufa chini, na tena, Alhamdulilahi! Pale chini juu ya sakafu nikaona pete la mawe limefungwa chini. Hatukusema neno, mioyo zilitupiga kama nini sijui.

Bwana Good alitoa kisu chake akaanza kuchokoa pale penye pete, na baada ya kufanya kazi kwa taratibu na subira nyingi, akaweza kuliinua lile pete, akalisimamisha

Sasa alilishika kwa nguvu akajaribu kulivuta juu lakini hapana kilichojongea hata kidogo.
Basi sasa mimi nikaanza kuwa na hamasa, nikasema, ‘Haya na mimi nijaribu.’ Nikashika lile pete nikalivuta juu. Hakuna kilichonyanyuka. Bwana Henry vile vile akajaribu, na yeye vile vile alishindwa.

Basi Bwana Good akaanza tena kuchokoa pale katika ufa, pale tulipoona baridi inaingia, akasema, ‘Haya sasa Bwana Henry, jaribu kwa nguvu zako zote, wewe una nguvu za watu wawili.’

Akavua kitambaa alichofunga shingoni, akakipitisha katika pete lile, akampa Bwana Henry mkononi, akaniambia nimshike Bwana Henry kiunoni na sote tukavuta kwa nguvu zetu zote.

Bwana Henry akasema kwa sauti kubwa, ‘Haya! Vuteni! Vuteni! Inalegea!’
Nikasikia mishipa yake ikidata kwa nguvu alizotumia.

Mara tukasikia sauti ya kukwaruza, mara sote tulianguka nyuma na pande la jiwe kubwa likaruka juu. Nguvu za Bwana Henry zimetuokoa. Akasema, ‘Haya Quatermain, washa kibiriti.’

Tukajizoazoa na kupumzika kidogo; nikawasha kibiriti, na hapo tuliona ngazi ya mawe ya kushukia katika shimo! Bwana Good akauliza, ‘Je, sasa tutafanya nini?’

Nikasema, ‘Na tufuate ngazi. Tubahatishe.’ Lakini Bwana Henry akasema, ‘Ngoja kwanza, afadhali na tuchukue nyama na maji yaliyobaki, huenda tutakuwa na haja nazo.’

Nikatambaa chini niyapate, Tulikuwa tumekwisha sahau zile almasi kwa muda wa saa ishirini na nne; na hatukutaka hata kufikiri almasi kwa jinsi zilivyotuingiza katika taabu na shida; lakini nilifikiri afadhali tuweke kidogo mifukoni mwetu, maana huenda tutajaliwa kutoka katika taabu yetu.


Basi nikajaza almasi mifuko yote ya koti langu, na kwa bahati nilichukua nyingine kutoka katika kasha lenye zile zilizo kubwa.

Nikasema, ‘Haya, jamani, njooni mchukue almasi.
Mimi tayari nimejaza mifuko yangu.’ Bwana Henry akajibu, ‘Almasi nazipotelee mbali, natumai sitaona almasi tena mpaka kufa.’

Bwana Good hakujibu, nadhani alikuwa akimuaga Foulata, ambaye alikuwa akimpenda sana na ambaye alilala pale chini maiti.


Basi Bwana Henry akatuita, akasema kuwa yeye atatangulia kushuka. Nikamwambia, ‘Uangalie sana unapoweka miguu, pengine kuna mashimo.’

Basi tukashuka, na tulipohesabu daraja kumi natano tukaona kama tumefika chini. Sasa tukajiona tumo katika kinjia, tukakifuata, huku tumeelekea mahali inapotoka baridi.

Tulipokuwa tumekwanda kwa kadiri ya robo saa, (tulikuwa tukienda pole pole sana ) tuliona kinjia kinapinda, au kimekatwa na kingine.

Basi vivyo hivyo tukafuata kwa saa sijui ngapi. Vinjia hivi ni vya nini hatukufahamu, lakini tulisimama tumekwisha choka kabisa, tukala nyama iliyobaki na tukanywa maji yote yaliyobaki.

Ikawa kama tumeokoka katika kile chumba ili tupotee katika vinjia. Tulipokuwa tumekaa hivi, tukiwa tumekata tamaa kabisa, nilisikia kama sauti, lakini ikitoka kwa mbali sana, ikawa kama sauti ya maji yanayotiririka.
 
Basi tukajipa moyo; tukaendelea tena tukipapasa kuta zilizo kando ya kinjia. Tulipoendelea sauti ikasikika zaidi, mpaka tukaweza kusikia kama maji yanakwenda kwa nguvu.

Sasa tulikaribia sana, na Bwana Henry akasema, Nendeni pole pole, tunakaribia sana sasa.’

Mara tukasikia kishindo cha maji, na Bwana Good akapiga ukelele. Kumbe, ametumbukia majini! Tukafadhaika sana, tukamwita, akaitika, ‘Mimi nipo salama, kwa bahati nimeshika jabali, lakini washa kibiriti nipate kuona nipo wapi.’


Nikawasha mshale wa mwisho wa kibiriti. Na kwa mwangaza wake nikaona pale pale miguuni petu mto wa maji mengi yanapita kwa nguvu, na pale mbali kidogo Bwana Good ameshika jabali lililotokeza katika maji.


Mara tulisikia kishindo tena, kama anashindana na maji, na mara alitoa mkono na kumshika Bwana Henry, tukamvuta nchi kavu. Akasema huku akitweta, ‘Lo! Bahati yangu! Nisingeliweza kuogelea au kushika mwamba ule, ningalichukuliwa mbali kabisa. Mto huu unakwenda kasi sana.’

Tuliogopa kufuata ukingo wa maji tusije tukatumbukia ndani. Basi tulipumzika kidogo, tukanywa maji ya mto, maana yalikuwa matamu, tukajinadhifisha kidogo, tukaburudika. Lakini Bwana Henry akasema, ‘Ya nini kuhangaika, kinjia chochote kitatufaa, maana hatujui viendako wala hatuwezi kujua.’


Basi tukaendelea, na Bwana Henry aliongoza, na mara akasimama ghafla, nasi tuliokuwa tukimfuata tukagongana. Akasema, ‘Tazameni, je, nimeshikwa na kichaa?, au kweli ni mwangaza?’

Tukatazama na kule mbele tukaona mwangaza mdogo sana. Basi tuliingiwa na tamaa ya kuendelea. Baada ya mwendo wa dakika tano tukawa hatuna shaka tena, tuliona kuwa kweli ni mwangaza.


Na baada ya dakika nyingine tuliweza kuhisi upepo unatupiga usoni, tukaenda mbele moja kwa moja

Mara kinjia kikawa chembamba sana kikawa kama shimo la mnyama.
Bwana Henry akatambaa huku kajikunja, naye akatoka, na Bwana Good vile vile, na mimi vile vile, na tulipotupa macho juu tuliona nyota, na pia tukavuta hewa baridi safi kabisa.

Tulikuwa tumesimama hivi, na mara kitu kiliteleza na sote watatu tulianguka tukapinduka pinduka na kubiringika katika majani na vijiti.

Nikawahi kukamata kitu, nikasita kubiringika. Nikapiga kelele, na kwa chini yangu nilisikia Bwana Henry ananiita. Yeye alifika mahali pa sawa, alitulia. Na sasa ikawa kumtafuta Bwana Good, tukamwona karibu, alikuwa amejigonga na mti. Hakuumia sana, naye akaja juu upesi.


Basi sasa tulikaa juu ya majani tumejaa furaha jinsi hali yetu ilivyobadilika kwa ghafla. Kweli tumeongozwa katika kile kinjia ili tuokoke. Na tazama sasa kunaanza kupambazuka, nasi hatukufikiri ya kuwa tutaona tena mapambazuko.


Basi, polepole, jua likapanda na mwangaza wake ukaangaza nchi, tukaona kuwa tumo katika shimo lile kubwa lililo mbele ya pango lile tulimoingia. Na sasa tuliweza kuona yale masanamu matatu yaliyokuwepo ukingoni mwa shimo.

Tukakaa tukangoja mpaka jua likapanda juu zaidi, ndipo tulipoondoka tukaanza kupanda tutoke shimoni. Kwa muda wa saa nzima tulipanda kwa shida, tukajivuta juu kwa kushika majani na miti midogo midogo, mpaka tukafika juu.


Basi tukatoka na kusimama kuelekea yale masanamu matatu, na pale kando ya njia tuliona moto unawaka, na watu wamekaa karibu na moto.


Basi tukajikokota huku tukisaidiana, tukasimama kila hatua mbili tatu. Mara, mmoja katika wale watu alituona, akaanguka chini pale pale huku akipiga kelele kwa hofu.

Tukamwita, ‘Infadus! Infadus! Ni sisi rafiki zako.’ Akaondoka na kutujia. Akatukodolea macho huku akitetemeka. Akasema, ‘Enyi mabwana zangu, ‘kweli ni nyinyi mmefufuka?’ Na yule mzee askari akajitupa mbele yetu, akamshika Bwana Henry magoti, akalia kwa furaha ya kumuona tena.
 
SURA YA KUMI NA TISA

Baada ya siku kumi kutoka asubuhi ile tuliyookoka kwa namna ya ajabu, tulikuwapo tena nyumbani mwetu katika mji wa Loo; na kwa bahati hatukudhurika kwa mambo yaliyotupata, ila nywele zangu zilikuwa zimeingia mvi zaidi, na Bwana Good hali yake haikuwa kama zamani.

Nadhani alihuzunika sana kwa kifo cha Foulata. Nadhani sina haja kusema hatukuenda tena katika chumba cha hazina za Sulemani.

Lakini baada ya kupumzika kwa muda wa siku mbili tulishuka tena katika shimo lile refu tukitumai kuona kinjia kile tulichotokea, tusikione.

Maana mvua ilikuwa imenyesha na nyayo zetu zilifutika; na tena mteremko wa shimo ulijaa vitundu na vinjia vya wanyama. Ikawa haiwezekani kutambua kinjia kipi tulichotokea.

Siku ile kabla ya kuanza safari yetu ya kurudi Loo tuliingia tena katika Mahali pa Mauti tukatazama kila mahali.

Tukatazama tena ule ukuta wa jabali ulioshuka ukatufungia ndani ya chumba cha hazina, tukazikumbuka hazina zilizomo nyuma ya ukuta huo, na kile kizee cha ajabu kilichobonyezwa na ukuta, na Yule mwanamwali mzuri ambaye amezikwa ndani.

Tuliutazama sana tusione hata dalili ya namna unavyoinuliwa, ingawa tulijaribu sana kwa muda wa saa nzima. Kwa kweli siri yake ilisitirika sana, na kazi yake ilikuwa ya watu mastadi sana.

Mwisho tukaacha kutafuta kwa hasira, lakini naona kuwa hata ungaliinuliwa mbele ya macho yetu, hatungalidhubutu kuingia ndani tena, hatungalidhubutu kukiruka kiwiliwili cha Yule kizee Gagula, ingawa ilikuwa yamkini kupata almasi nyingi kupita kiasi.

Lakini niliona uchungu kuacha mali hiyo yote isiyomfaa mtu. Labda katika zama zijazo, msafiri mmoja atavumbua siri ya jabali hilo, lakini nadhani halitovumbuliwa. Naona kuwa hiyo mali itakaa pamoja na maiti ya Foulata mpaka mwisho wa dunia.


Basi tulianza safari yetu kurudi mji wa Loo. Msomaji atakumbuka kuwa mimi kwa bahati nilijaza mifuko yangu almasi, na kwa hiyo hatukuwa na haki ya kuona uchungu sana, Ijapokuwa nyingine zilitoka mfukoni nilipokuwa nikiporomoka katika shimo, lakini kwa thamani ya almasi ilivyo, nilikuwa na mali ya kutosha kutufanya matajiri sana.

Tulipofika Loo Ignosi alifurahi sana, naye alikuwa hajambo, akijaribu kutengeneza tena nchi yake, maana iliaribika sana katika vile vita.

Alisikiza habari zetu kwa makini na tulipomwambia habari za kufa kwake Gagula alianza kufikiri, akamwita mzee mmoja wa baraza lake, akamuuliza, ‘Wewe mzee sana, sivyo?’

Yule mzee akajibu, ‘Ndiyo. Bwana wangu mfalme! Babu yako na mimi tulizaliwa siku moja.’ Akamuuliza, ‘Niambie, wewe ulipokuwa mdogo ulikijua kile kizee kichawi Gagula?’

Akajibu ‘Nalimjua, mfalme wangu.’ Akamuuliza, ‘Wakati huo alikuwaje? Alikuwa kama wewe ulivyokuwa?’

Akajibu, ‘La, mfalme wangu! Alikuwa kama alivyo sasa na kama alivyokuwa siku za babu yangu kabla ya wakati wangu; alikuwa kizee wa kuchukiza amekauka na kujaa uovu.’

Ignosi akamwambia, ‘Basi, hayupo tena,’ tayari amekufa.’ Yule mzee akasema, Kweli Ewe mfalme! Basi na nchi imeondolewa baa kuu.’

Basi Ignosi akampa ruhusa naye akajibu, ‘Koom! Na kwenda, Ewe mfalme.Koom!’
 
Ingosi akatugeukia akasema, ‘Mnaona, ndungu zangu, huyo alikuwa kizee wa ajabu, nami nimefurahi kuwa amekufa.

Yeye alitaka nyinyi mfe katika pale Mahali pa Mauti na giza, na labda angalivumbua njia ya kuniua mimi vile vile kama alivyopata njia ya kumuua baba yangu na kumweka Twala, mahali pake.

Haya sasa, niambieni zaidi juu ya safari yenu; kwa hakika hapajatokea safari kama hiyo!’ basi nilipokwisha mwambia yote, nilimuuliza namna ya kutoka katika nchi ya Wakukuana.

Nikasema, ‘Na sasa, Ignosi, wakati wa kuagana nawe umewadia tupate kurudi katika nchi tuliyotoka.

Tazama, Ignosi, wewe ulikuja hapa ukitutumikia, na sasa tunakuacha hapa ukiwa mfalme mkubwa. Ikiwa unatushukuru basi tutendee kama ulivyoahidi.

Kutawala kwa haki, kushahi sheria, kutomuua mtu bila sababu ya haki, ndivyo utakavyo stawi. Kesho kutakapo pambazuka, Ignosi, twataka utupe walinzi wataotuongoza kuvuka milima tena. Sivyo mfalme?’

Ignosi akafunika uso wake kwa mikono yake kwa muda, akakaa kimya, kisha akasema, ‘Moyo wangu ni mzito sana; maneno yako yamenitia ufa moyoni, yameupasua katikati.

Nimewafanyia nini, ewe Ndovu na Makumazahn, na Boungwan hata mnataka kuniacha mpweke? Nyinyi mlioniunga mkono siku za vita, mnaniacha katika siku za amani na neema?

Mnataka nini! Je, ni wake? Chagueni katika wanawali wote! Mahali pa kukaa? Tazameni nchi hii ni yenu mpaka upeo wa macho yenu! Nyumba za Kizungu?

Mtawafundisha watu wangu nao watazijenga! Ng’ombe wa chakula na ng’ombe wa maziwa?

Kila mtu aliyeona atakuleteeni ng’ombe dume au ng’ombe jike! Mnataka kuwinda wanyama? Ndovu hawatembei katika mapori yangu?

Viboko hawalali katika matope kingoni mwa mito yangu? Mnataka kufanya vita? Majeshi yangu yanangoja amri zenu. Kama yapo mengine mnayotaka, hayo nitawapa .’

Nikajibu, ‘Sivyo, Ignosi, hatutaki kitu chochote katika vitu vyote ulivyotaja, tunataka kwenda kwetu tu.’ Ignosi akajibu kwa uchungu, ‘Sasa nimefahamu. Mnapenda mawe yale yanayong’aa kuliko mnavyonipenda mimi rafiki yenu.

Tayari mmepata mawe; sasa mnataka mwende kuyauza muwe matajiri kama ilivyo tamaa yenu watu weupe. Kwa ajili hiyo, mawe hayo meupe nayaangamie na aangamie pia atakayeyafuata.

Mauti yatamkabili atakayekwenda katika Mahali pa Mauti ili kuyafuata. Watu weupe, mnayo ruhusa ya kwenda.’

Basi niliweka mkono wangu juu ya mkono wake, nikasema, ‘Ignosi, twambie, wewe ulipotembea tembea katika nchi ya Amazulu, na miongoni mwa watu weupe huko Natal, moyo wako haukutamani nchi ile aliyokusimulia mama yako, yaani nchi ile uliyozaliwa, ulipocheza ulipokuwa mtoto, nchi ambayo ni kwenu?’
 
Akajibu, ‘Ndiyo, nilitamani sana, Makumazahn.’ Nikasema, ‘Ndivyo, Ignosi, mioyo yetu inavyotamani kwetu, nchi yetu.’

Basi, akakaa kimya kwa muda, kisha akasema, ‘Sasa nimefahamu kuwa maneno yako yana maana, nayo ni ya busara kama yalivyo siku zote.

Wale warukao hewani hawapendi kutambaa chini; watu weupe hawapendi kukaa wanavyokaa watu weusi.

Haya, kama lazima mwende, nendeni, mniache na moyo mnyonge, kwa sababu mkisha kwenda mtakuwa kwangu kama mliokufa, maana sipati habari zenu tena.

Infadus, mjomba wangu, atawachukueni na yeye mwenyewe pamoja na jeshi lake atawaongozeni. Nimesikia kuwa ipo njia nyingine ya kuvukia milima, naye atawaonyesheni.

Kwa herini, ndugu zangu, watu weupe mashujaa. Msinitazame tena, maana sina moyo tena.

Tazameni, natoa amri nayo itatangazwa kutoka milima mpaka milima, majina yenu, Ndovu, na Makumazahn, na Bougwan yatakuwa mwiko kutajwa tokea hivi leo, kama yanavyokuwa majina ya wafalme wanaokufa.

Atakayeyataja, atakufa, hivyo ndivyo majina yenu yatakavyo kumbukwa daima katika nchi hii.

‘Nendeni sasa machozi yasije yakanimiminika kama mwanamke.

Kila mkikumbuka mambo yaliyopita kumbukeni namna tulivyopigana bega kwa bega katika vita vikubwa ulivyoviongoza wewe, Makumazahn, au namna wewe ulivyokuwa mwisho wa askari wale waliozunguka upande wakalishinda jeshi la Twala, wewe Bougwan, au namna ulivyokaa katikati ya Wajivu na watu wakaanguka kama mavuno mbele ya shoka lako, wewe Ndovu; na namna ulivyozivunja nguvu za fahali Twala, ukakivunja na kukizika kiburi chake.

Kwaaherini, kwa heri milele, Ndovu na Makumazahn na Bougwan, rafiki zangu.’
Basi Ignosi akatutazama kimya kwa muda kidogo. Kisha akavuta ngezi ile aliyovaa akajifunika kichwa kujificha uso, Tukatoka kimya.

Kulipopambazuka tulitoka mji wa Loo, na rafiki yetu Infadus, naye vile vile moyo wake ulikuwa na huzuni kwa kuagana nasi.

Ingawa tuliondoka mapema sana, njia zote zilijaa watu, wakituamkia kwa maamkio ya kifalme tulipokuwa tukipita, na wanawake wakatushukuru kwa sababu tulimwondoa Twala, wakatutupia maua.

Tulipokuwa tukisafiri, Infadus alitwambia kuwa ipo njia nyingine ya kuvukia milima. Baada ya kusafiri kwa muda wa siku nne mwendo wa taratibu tulifika tena kwenye milima inayopakana na nchi ya Wakukuana na lile jangwa.


Hapa tuliagana na Infadus, askari shujaa, akatutakia mema katika safari yetu, na akawa karibu ya kulia kwa huzuni; akasema, ‘Mabwana zangu, macho yangu hayataona tena watu kama nyinyi.’

Nasi tuliona huzuni kuagana naye. Basi, baada ya kutazama kuwa chakula na maji na kila kitu cha safari yetu kiko sawa, tulipeana mikono na kuagana na Infadus, nasi tukaanza kushuka mlima. Ilikuwa kazi ngumu, lakini tulifika chini salama.

Asubuhi tulianza safari yetu ya taabu ya kuvuka lile jangwa, lakini tulikuwa na maji ya kutosha yaliyochukuliwa na wapagazi watano.
Saa sita, siku ya tatu tulifika kwenye mahali penye majani na miti.
 
SURA YA ISHIRINI

Na sasa nitasimulia habari zilizo za ajabu kupita zote za safari yetu, nazo labda zitaonyesha namna mambo yanavyotokea kwa ajali. (mambo yote hutokea kwa sababu)

Nilikuwa nikitembea pale tulipofika penye majani na miti, na mara niliona mambo ya kustajabisha. Mbele yangu, kadiri ya hatua ishirini, niliona banda limejengwa chini ya mti.

Nikasema kimoyomoyo, ‘Je, banda hili limekujaje hapa?’ Na mara niliona mtu mweupe anachechemea akitoka bandani amevaa ngozi, naye ana ndevu nyeusi ndefu.

Kwanza nilifikiri kuwa labda nimeshikwa na homa na nimo njozini. Maana, ilikuwa haimkiniki.

Hapana mwindaji aliyepata kufika hapa na hakika hapana mtu aliyepata kujenga nyumba hapa na kupafanya kwake.

Nikatazama tazama, na hapo Bwana Henry na Bwana Good wakaja, nikawaambia, ‘Haya jamani, huyu ni mtu mweupe au labda nimeshikwa na wazimu?’

Bwana Henry akatazama, na Bwana Good akatazama, ndipo Yule mtu mweupe alipotuona akatupigia kelelena akaanza kutujia anachechemea. Alipofika karibu, akaanguka kama kwamba amezimia.

Mara Bwana Henry upesi akamwinamia, akasema, ‘Alhamdulilahi! Ni ndugu yangu George!’

Kusikia kelele, mara mtu mwingine amevaa ngozi vile vile akatoka bandani kachukua bunduki, akatujia mbio.

Aliponiona, akasema, ‘Makumazahn, hunijui, bwana? Mimi ni Jim, mwindaji. Barua ile uliyonipa nimpe bwana wangu ilinipotea nasi tumekaa hapa hapa kwa muda wa miaka miwili.’

Na pale pale akaanguka penye miguu yangu akagaagaa na kupiga kelele kwa furaha. Nikasema, ‘Ee wewe, mzembe! Unastahili kupigwa sana.’

Huku nyuma Yule mtu mweupe akazinduka tena, akasimama, na yeye na Bwana Henry wakashikana mikono kwa nguvu kimya! Hawakuweza kusema hata neno. Ule ugomvi wa zamani ulisahauli kabisa.

Baadaye Bwana Henry akapata kauli akasema, ‘Mpenzi ndugu yangu, nilifikiri kuwa umekwisha kufa. Nimevuka milima ya Sulemani ili kukutafuta, na sasa ninakuona unakaa jangwani kama kunguru!’

Yule mtu akajibu, ‘Mimi nilijaribu kuvuka milima miaka miwili nyuma, lakini nilipofika hapa jabali liliniangukia likanivunja mguu, nami nikakaa hapa, sikuweza kwenda mbele wala kuru nyuma .’

Ndipo nilipokaribia mimi, nikasema, ‘Hujambo, bwana Neville? Unaweza kunikumbuka?’
Akanitazama akasema ‘Kumbe, Quatermain, na wewe Bwana Good vile vile. Ngojeni, rafiki zangu, naona kizunguzungu tena. Mambo haya ni ya ajabu na ya furaha tupu na hasa kwa mtu aliyekwisha kata tamaa.
 
Siku ile usiku Bwana George alitusimulia habari za safari yake. Kwa uchache ilikuwa hivi: miaka miwili nyuma alitoka mji wa Sitanda kujaribu kufika milima ya Sulemani.

Ile barua niliyompa Jim hakuipata, wala hakupata habari zake mpaka leo hivi. Lakini alisikia habari kwa wenyeji wengine.

Hakujaribu kufika kwenye maziwa ya Sheba bali alifuata njia ile nyingine tuliyorudia sisi, yaani njia iliyo bora kuliko ile iliyoandikwa katika ramani ya mzee Silvestra.

Yeye na Jim walipata taabu nyingi katika jangwa lile, lakini kwa bahati walifika hapa pahali penye majani na maji, ndipo Bwana George alipopatikana na ajali. Siku moja alikuwa kakaa kando ya mto na Jim alipanda juu kujaribu kutafuta asali.

Alipokuwa akifanya hivi, jiwe kubwa lililegea likaporomoka likamwangukia likamvunja mguu vibaya sana.

Basi tokea siku ile hakuweza kwenda vizuri, ikawa hawezi kwenda mbele wala kurudi nyuma, akaazimia kukaa pale pale.

Waliweza kupata chakula cha kutosha, maana walikuwa na risasi nyingi na wanyama huja penye majani na maji yale usiku usiku kila siku. Basi huwapiga wanyama, nakula nyama, na ngozi walizitengeneza ziwe nguo zao.

Basi Bwana George akamaliza kusimulia hadhithi yake, akasema, ‘Basi hapa tumekaa kwa muda wa karibu miaka miwili tukitumai kuwa labda wenyeji watapita na kutusaidia, lakini hawakuja.

Hivi jana usiku tulifanya shauri kuwa Jim aniache hapa naye ajaribu kufika mji wa Sitanda na kupata watu watusaidie. Tulikata shauri kuwa aondoke kesho, lakini hakika sikutumai kuwa ataweza kurudi tena.

Na sasa wewe, ambaye katika watu wote duniani sijakutumainia kabisa, wewe niliyekufikiri kuwa umenisahau na kukaa Uingereza kwa raha, umekuja bila ya kukutarajia.

Ni jambo la ajabu, tena bahati sana.’
Basi alipokwisha kusema, Bwana Henry akaanza kusimulia habari za mambo muhimu katika safari yetu, tukakaa sana usiku ule tukizungumza.

Nikamwonyesha almasi zile nilizopata, akasema, ‘Lo! Kweli mmepata kitu katika taabu zenu, si kama mimi nisiyestahili hata kuhesabiwa sasa.’

Bwana Henry akacheka, akasema, ‘Almasi hizi ni mali ya Quatermain na Good. Hivyo ndivyo tulivyopatana, ya kuwa watagawana mali yoyote tutakayo ipata.’

Basi, maneno yale yalinitia katika fikra, na nilipokwisha kumshauri Bwana Good, nilimwambia Bwana Henry kuwa sisi sote wawili tunataka hata na yeye ashirikiane nasi katika kugawanyana zile almasi, na kama yeye hakubali, basi sehemu yake tutampa ndugu yake aliyevumilia taabu nyingi kuliko sisi katika kujaribu kuzipata.

Mwisho akakubali namna tulivyopatana, lakini Bwana George hakupata habari mpaka baada ya siku nyingi. Basi, hapo nadhani nitamaliza hadithi yangu.

Safari yetu ya kuvuka jangwa mpaka mji wa Sitanda ilikuwa safari ya taabu nyingi, hasa kwa sababu ilitupasa kumsaidi sana Bwana George ambaye mguu wake wa kulia ulikuwa dhaifu sana, na ukamfanyia matata.

Lakini tulivuka, na kusimulia habari zake ingekuwa kukariri hadithi ile niliyokwisha isimulia.

Tulifika Sitanda, tukaona bunduki na vyombo vyetu vingine vipo salama, lakini nadhani Yule mzee aliyekuwa akivitunza hakupenda kutuona tena.

Baada ya miezi sita tulifika kwangu, katika mji wa Durban, na ndipo ninapokaa sasa na kuandika habari hizi. Na sasa nakupeni Kwaherini nyote mliosafiri pamoja nami katika safari hiyo ndefu na ya ajabu kuliko zote nilizosafiri.

MWISHO.
 
Kitabu kizuri sana.
Nilisoma kitabu hiki zaidi ya miaka 20 iliyopita kutoka maktaba ya shule.
King Solomon's Mines.
 
Mkuu bujibuji tafadhali naziomba hizi mambo naomba namna ya kuzipakua kwa maana nikiwa offline niwe naweza kuzisoma
 
Mkuu bujibuji tafadhali naziomba hizi mambo naomba namna ya kuzipakua kwa maana nikiwa offline niwe naweza kuzisoma
Ninayonya kingereza, Nina iataach, za kiswahili mcheki bjbj
 

Attachments

  • solomon.pdf
    397.6 KB · Views: 45

Similar Discussions

Back
Top Bottom