Mara yatajwa kinara kilimo cha bangi

Influenza

JF-Expert Member
Jul 1, 2018
1,445
3,403
MATUMIZI ya dawa za kulevya aina ya bangi, yametajwa bado ni tatizo nchini, huku mkoa wa Mara ukiwa ni kinara katika kulima cha zao hilo ikifuatiwa na Tanga.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, ndiye aliyebainisha hayo bungeni jana, wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2018.

“Pamoja na jitihada zilizofanywa na serikali katika kupambana na dawa za kulevya nchini, bangi imeendelea kuwa tatizo kubwa nchini, mikoa ambayo inaonekana kuathirika zaidi na kilimo cha bangi ni pamoja na Mara, Tanga, Morogoro, Arusha, Kagera na Ruvuma,” alisema Mhagama na kuongeza:

“Kwa kipindi cha mwaka 2018 juhudi za vyombo vya dola kwa kushirikiana na wananchi zilifanikisha ukamataji wa tani 24.3 za bangi zikiwahusisha watuhumiwa 10,061.”
Alisema dawa za kulevya aina ya mirungi nayo imeendelea kutumiwa na watu wa rika mbalimbali, kwamba kwa mwaka 2018 vyombo vya dola vilikamata tani 8.97 za mirungi zikiwahusisha watuhumiwa 1,186.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2018, kesi 7,592 zikiwa na watuhumiwa 10,979, zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali, kesi 7,174 zilizowahusisha watuhumiwa 11,045 ziliendelea kusikilizwa.

“Serikali imeendelea kutoa huduma za tiba kwa watumiaji wa dawa za kulevya, jumla ya vituo sita vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Dodoma viliendelea kutoa huduma, hadi mwaka 2018 zaidi ya watumiaji 8,000 waliendelea kupatiwa huduma za Methadone katika vituo husika,” alisema Mhagama.
Mhagama alisema mwaka 2018, dawa za kulevya aina ya Cocaine kilo 8.9 zilikamatwa, na watuhumiwa 156 walifikishwa katika mikono ya sheria.

Alisema kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Tanzania ilipunguza uingizaji wa dawa za kulevya nchini aina ya Heroine kwa asilimia 90.

Naye, Kamishna wa Kinga na Tiba kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Dk. Peter Mfisi, alisema serikali hainunui dawa za Methadone bali zinanunuliwa na wafadhili kutoka Canada, thamani yake ni Dola za Marekani 1,500 kwa kilo moja.

Alisema India kilo moja ya Methadone ni Dola za Marekani 650 hadi 700, kwa mwaka matumizi ya dawa hiyo nchini ni kilo 300.
Dk. Mfisi alisema kilo moja ya Methadone inahudumia watu 600 hadi 700 kwa mwezi.

1573107744496.png

Chanzo: Nipashe
 
Back
Top Bottom