Mapinduzi na wapiga viboko wa Soko la Kasa, Pemba

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,263
MAPINDUZI YA ZANZIBAR NA WAPIGA VIBOKO WA SOKO LA KASA PEMBA

Sijapata kukutana na Mzanzibari nje ya Tanzania asiwe na historia ya mateso yaliyoifika familia yake au watu anaowafahamu baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964.

Historia ya watu kupigwa viboko hadharani kwa mara ya kwanza niliisikia Muscat nyumbani kwa Sheikh Ali Muhsin mwaka wa 1999.

Tulikuwa tumekaa pamoja na mdogo wake Sheikh Abdallah Muhsin na watu wengine tunazungumza ndipo Sheikh Abdallah akanieleza kuhusu adhabu za kudhalilisha za watu Pemba kupigwa viboko hadharani bila ya sababu ya maana.

Sheikh Abdallah Muhsin akanihadithia kisa cha bwana mkubwa mmoja mwenye heshima zake katika jamii iliyomzunguka kupigwa viboko hadharani Pemba.

Huyu bwana alikuwa mtu mzima na baada ya kupigwa viboko vile hakuweza kutembea ikabidi wanae wambebe hadi nyumbani kwake akiwa hoi.

Bwana huyu kwa ile fedheha iliyomfika hakutoka ndani kuanzia siku ile hadi mauti yalipomfika akatolewa nje ya nyumba yake akiwa maiti ndani ya jeneza kwenda kuzikwa.

Sheikh Abdallah Muhsin hakunitajia majina ya waliokuwa wanatoa amri za kupiga watu viboko naamini ni kwa ajili ya ule uungwana aliokuwanao kwani alijua kama atanitajia watu hao mimi nitawafahamu.

Hata hivyo nilikuja kutajiwa majina ya watu hao na mtu mwingine kabisa.

Laiti kama majina yale angenitajia mtu wa hivi hivi ningepata tabu kuamini kwani hawakuelekea kuwa watu waovu.

Nilitajiwa majina hayo na mtu ambae alikuwapo na alishiriki katika mapinduzi ingawa yeye alikuwa katika kundi la makomredi.

Mmoja katika hawa nilimfahamu vizuri nikimjua kama Muislam wa vitendo na akida.
Haya yake ya nyuma ya kupiga watu sikuyajua.

Nikaiambia nafsi yangu huyu mtu bila ya shaka amejuta, ametubu na Allah bila ya shaka yoyote amemsamehe.

Mpiga viboko mwingine nilikuja kukutananae na nikajulishwa kwake kama mtu muhimu katika historia ya mapinduzi.

Tukazungumza mengi na moja ambalo alinieleza na likanigusa sana ni kuwa aliniambia kuwa yeye alifungwa baada ya kuuawa Mzee Karume na alihukumiwa kifo akasema kuwa juu ya mateso yote aliyoyapata jela faida kubwa aliyopata kifungoni ni kuwa kwanza alijifunza kusoma Qur’an akiwa jela.

Kutokana na kifungo kile na alimjua Allah.
Akasema anashukuru kuwa alipotoka kifungoni hakutizama nyuma.

Huyu bwana kama mwenzake na yeye alijuta kwa yake aliyotenda baada ya mapinduzi.
Naamini na yeye kwa majuto yale Allah amemsamehe.

Hawa wote sasa ni marehemu.
Nini kiliwafanya watu hawa kuwa wanyama?

Wenyeji wangu Pemba wamenifikisha Wete wakanipekeka Soko la Kasa kiwanja ambacho ndicho watu walikuwa wakipelekwa na kupigwa viboko hadharani.

Uwanja huo wa mateso hivi sasa haupo ni majumba matupu ya biashara.

Jina hili ''Soko la Kasa,'' linatokana na kuwa hapo kulikuwa na soko na kasa wakiuzwa hapo pamoja na samaki wengine.

Wenyeji wangu hawakuwa wanajua kuwa historia hii ya viboko nilikuwa naijua kwa miaka mingi wakawa sasa wananieleza yaliyopitika pale baada ya mapinduzi.

Soko la Kasa hivi sasa halipo ninayoona ni maduka ya kisasa yakiuza bidhaa mbalimbali maarufu katika miji yote – nguo, viatu, vipodozi nk.

Wakazi wa jiji la London wana msemo wao wanasema, ‘’Ukisimama Piccadilly Circus utawaona watu kutoka mataifa yote duniani.’’

Piccadilly Circus ni sehemu maarufu London ni kama vile Darajani Unguja.

Miaka mingi imepita lakini na hapa Wete lilipokuwa Soko la Kasa ukisimama utamuona aliyepata kupigwa viboko uwanjani hapo baada ya mapinduzi.

Picha hiyo hapo chini ni mmoja wa watu hao akinieleza mkasa wake wa viboko wakati huo akiwa kijana mdogo.

Nilitangulia mwanzoni kusema kuwa historia hizi za kutia majonzi nimezisikia nyingi kutoka vinywa vya Wazanzibari wenyewe.

Iko siku nilialikwa kuzungumza katika semina ya wanafunzi State University of Zanzibar, Beit Ras na wenyeji wangu walinipangia hoteli karibu sana na Forodhani.

Ilikuwa mwezi wa Ramadhani.

Jua lilipokaribia kutua nikatoka hotelini nikawa nimesimama karibu ya ufukwe nikiangalia mashua za wavuvi wakirejea na mapema pwani kuwahi kufuturu.

Mimi nilikuwa nimesimama pale kuangalia bahari na hawa wavuvi huku nikisubiri adhana nifungue kisha nikasali msikiti wa jirani.

Akanijia kijana mmoja labda miaka 20 hivi akanitolea salamu kisha akaniuliza, ''Wewe ni Mohamed Said?"
Nikamwitikia.

''Nimepata kukusikia ukihadithia historia ya mzee mmoja aliyepigwa viboko wakati wa mapinduzi ambae hakutoka ndani hadi siku ya kufa kwake.''

Nimepigwa na mshtuko nimeduwaa.
''Nakushukuru sana kwa kukieleza kisa kile.

Huyu mzee aliyepigwa viboko mimi ni babu yangu.''
Nimeshusha pumzi tukawa tunatazamana mimi sina la kusema.

Kisha nikampa pole baada ya ule ukimya.
''Nakufatilia sana katika makala zako unaziandika.''

Miaka mingi ilikuwa imepita na naamini huyu kijana wala hakupata kumjua babu yake ila amehadithiwa.

Hakika miaka mingi imepita na wala kijana hakumjua babu yake lakini nilihisi machungu yaliyokuwa ndani ya moyo wa yule kijana.

Alinishukuru akaniaga akiniacha mimi nimesimama palepale fikra zangu zikienda nyuma na nikijiuliza vipi watu hawa watapata sulhu na wakasameeana na kusahau machungu yaliyopita?

Nakumbuka kisa cha mtesaji wa mapinduzi mmoja ambae mimi nilikutanishwanae miaka ya hivi karibuni.
Sababu ni kuwa alikuwa anataka kuandika historia ya maisha yake.

Hiki ni kisa In Shaa Allah iko siku nitakieleza kwa kirefu.

Katika mazungumzo yetu ya kwanza nyumbani kwake nje ya Dar es Salaam akanieleza kisa mashuhuri cha wachunga ng'ombe waliouliwa kwa kushutumiwa walipanga kupindua serikali ya mapinduzi.

Huyu bwana ndiye alikuwa kiongozi wa operesheni ile.

Allah ana maajabu yake.

Kisa hiki alinieleza pia Sheikh Abdallah Muhsin iweje muhusika mwenyewe anitafute kunisadikishia kwa ulimi wake mwenyewe ule unyama uliopitika?

Huyu bwana siku moja alikabiliwa na kijana mdogo akamwambia, "Mimi huwezi kunikumbuka lakini mimi nakukumbuka ulipokuja nyumbani kwetu kumchukua baba yangu nilikuwapo lakini nilikuwa mtoto mdogo.

Sura yako haijanitoka akilini kwangu."
Yule bwana alipigwa na mshtuko mkubwa yule bwana aliyemchukua hakurejea tena nyumbani kwake.

Hakika alitishika.
Mbele yake kasimamiwa na yatima aliyempoteza baba yake.

Hakuitegemea siku hii wala hakujua kama itaweza kutokea au kumfikia.
Tulikuwa tumekaa nje ya nyumba yake kwenye mkeka kivulini chini ya mti.

Mwenyeji wangu alikuwa mgonjwa.
Huyu ndugu yetu sasa ni marehemu Allah amsamehe.

Nilikuwa kimya nakifikiria kitabu cha maisha ya mtu huyu katili.
Hakika Allah Muweza.

Pemba ina historia yake ya pekee sana katika historia ya mapinduzi na historia ya sasa ya Wazanzibari kutafuta mwelekeo mpya kupitia sanduku la kura.

Nimepita vijiji vya Pemba ambavyo vimepata kuhamwa na wakazi wake na ukisikia yaliyotokea pengine huenda usiamini.

Nina kitabu alinipa Prof. Ibrahim Lipumba sasa robo karne, ''Mauaji ya Kutisha ya Elfu Mbili na Moja.''

Ndani ya kitabu hiki Prof. Lipumba kaniandikia maneno akiniomba ninyanyue kalamu niandike historia bora na ya kueleweka zaidi ya yale yaliyotokea Pemba mwaka wa 2001:

PICHA:
Soko la Kasa, Wete Pemba
Kitabu

1694276991765.png

1694277039101.png

1694277073762.png
 
Mzee wangu Mohamed Said unawaelezeaje wale watu waliopigwa viboko kwa Karne kadhaa kabla ya mapinduzi?
 
Bora umeandika wewe legend mwenye heshima zako, maana wapemba ni jamii ya watu wa hovyo sana.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom