Maovu ya Howard Elkins yanapofichuka na kuamsha machungu upya

Intelligent businessman

JF-Expert Member
Sep 6, 2022
26,107
52,832
HAKUNA DHULMA YA MILELE, ISIYO LIPWA.

‘Mwili uliolala milele hauwezi kuamka, lakini unaweza kuzungumza ukweli kuliko mwili unaoamka kila siku’ – Pragya Santra.

Kila nyumba ina stori yake, ndoto zake, siri zake na matumaini ya watu wanao ishi na walio wahi kuishi humo. Nyumba moja mjini New York ilikuwa na siri nzito iliyotunzwa kwa miaka zaidi ya 30. Kuna mtu aliamini siri hiyo haitafichuka kamwe kwa sababu mwili wa mtu aliyemuua kwa siri umelala na hauzungumzi. Hakujua kuwa miili iliyolala inazungumza, tena ukweli zaidi kuliko miili isiyolala.

Siku ya Tarehe 2, mwaka 1999 familia ya Bw. Ronald Cohen ilikuwa inahama kutoka nyumba moja kwenda nyumba nyingine huko jijini New York. Katikati ya shughuli ya kutoa vyombo nje, Bw. Cohen aligundua kuna pipa ndani ya nyumba hiyo ambalo alilikuta miaka tisa iliyopita wakati akihamia ndani ya nyumba hiyo. Pipa hilo lilihifadhiwa kwenye stoo ndogo iliyokuwa chini ya ngazi za kupandia ghorofani. Bw. Cohen hakuwahi kulifungua pipa kwa sababu lilikuwa limefungwa kisawasawa na pia lilikuwa na lebo ya kemikali. Baba huyo wa familia hakujua kuna kemikali gani ndani ya pipa lile, na hakuona haja ya kufungua kemikali zisizomuhusu, kwa hiyo aliamua kuliacha kama alivyolikuta miaka tisa iliyopita. Lakini wasaidizi wake waliamua kulitoa nje, lichukuliwe na wazoa taka. Waliamini hakuna kitu cha maana ikiwa mmiliki wa awali wa nyumba hiyo aliliacha na hakuwahi kulitafuta kwa miaka tisa.

Kwa mshangao kidogo, wakati wakianza safari ya kuhama makazi hayo, Bw. Cohen aligundua kuwa takataka zote zilibebwa na wazoa taka isipokuwa lile pipa zito walilotoa wasaidizi wake. Kutazama vizuri kwenye pipa hilo kulikuwa na karatasi ya maelezo ambayo bila shaka iliachwa na wazoa taka. Bw. Cohen alishuka kwenye gari na kwenda kusoma karatasi ile.

‘Mpenzi mteja, tumeshindwa kubeba pipa hili kwa sababu ni zito mno. Tafadhali piga simu idara ya mazingira wafanye mpango maalum wa kuliondoa’ – Ulisomeka ujumbe kwenye karatasi ile.

Hapo ndipo Bw. Cohen alipohamasika kutaka kujua kuna nini ndani ya pipa lile. Alitafuta kisu na kukata utepe mgumu ulioshikiza mfuniko wa pipa lile na kisha akatumia chuma kuumegua mfuniko huo uliokuwa umeshikana sawasawa na pipa lile. Punde tu alipofanikiwa kulifungua, Bw. Cohen alikutana na harufu kali. Kutazama vizuri, aliona kitu kama kiganja cha mtu na kiatu cha kike. Polisi wa kitongoji cha Jericho waliitwa na kuchukua pipa lile hadi kwenye kituo kikubwa cha uchunguzi wa kimahakama.

Kila kitu kilitolewa kutoka ndani ya pipa lile. Mwili wa mwanamke uliooza kana kwamba ume hifadhiwa humo kwa miaka mingi. Pia kulikuwa na vipande vingi vya plastiki vyenye umbo la mfano wa punje za mchele, na mkoba mdogo wa kike, na mfano wa majani yaliyotengenezwa kwa plastiki.

Chini kabisa kulikuwa na majimaji ya ajabu yenye rangi ya ugoro, labda ni majimaji yaliyotoka kwenye mwili wa mwanadamu huyo aliyeoza. Ndani ya mkoba kulikuwa na karatasi zilizoharibika kabisa kiasi kwamba hazikuweza kusomeka. Yale majimaji yaliharibu kabisa zile karatasi ambazo labda zingetoa muelekeo wa kumtambua mtu huyo.

Wachunguzi wa kimahakama waliobobea katika taaluma ya patholojia wali uchunguza mwili ule na kugundua mambo kadhaa; moja, baadhi ya meno ya marehemu yalionesha kuwa yaliwahi kufanyiwa ukarabati wa kitabibu na kuwekewa nakshi maalumu. Utaratibu huo haukuwa ukifanyika nchini Marekani bali maeneo ya Amerika ya Kusini. Pili, wataalamu waligundua ni mwili wa mwanamke tena alikuwa mjamzito. Uchunguzi wa mionzi ya Xray ulionesha kichanga chenye ukubwa wa inchi 17, karibu kabisa kujifungua.

Reyna-newspaper.jpg
Howard-Elkins-e1487921504205-150x150.png
 
Pipa nalo lilichunguzwa. Mojawapo ya ugunduzi muhimu kutoka kwenye pipa hilo ni namba za pipa – 52766 – na jina la kampuni iliyotengeneza pipa hilo; kampuni ya OILWAY Gaf. ya mjini London, New Jersey. Polisi walifuatilia kumbukumbu za kampuni hiyo na kugundua kuwa pipa lile lilitengenezwa mwaka 1965. Na sasa miaka 34 baadaye pipa lile limekuwa kama jeneza la mtu ambaya hakuwahi kuzikwa.

Maofisa wa upelelezi walizigeukia nyaraka zile zilizokuwamo ndani ya mkoba ambazo zilikwisha haribika sana. Wachunguzi wa nyaraka walitamani kujua kilichoandikwa kwenye nyaraka hizo ingawa macho ya binadamu yasingeweze kuona. Ndani ya maabara ya kuchunguza nyaraka, watalamu waliziweka nyaraka zile kwenye oven maalum na kuziacha kwa muda wa siku saba ili zikauke. Baada ya kukauka nyaraka ziliwekwa kwenye mashine maalumu ijulikanayo kama Video Spectral – Comparator au VSC, ambayo kazi yake ni kusoma alama za siri kwenye nyaraka, maandishi yaliyofutwa na maandishi yaliyoharibiwa kwa maji au kwa kukaa muda mrefu. Teknolojia hii hutumika pia katika utengenezaji na usomaji wa vitambulisho mbalimbali kama hati za kusafiria na leseni za udereva.

Baada ya kazi kubwa na subira ya muda mrefu ya kujua kilichomo kwenye nyaraka hizo, matokeo hayakufurahisha. Mashine ya VSC haikuona kitu. Lakini wachunguzi wa nyaraka hawakukata tamaa. Siku baada ya siku walijitahidi kutumia Kompyuta zenye uwezo mkubwa wa kusoma maandishi yaliyofutika, si tena kwa kutegemea rangi ya wino ambao haupo, bali kwa kutegemea alama za mgandamizo wa kalamu wakati nyaraka hizo zikiandikwa.

‘Wakati karatasi inapoandikwa, na hasa ikiwa imeegemezwa juu ya meza ya mbao au kitu kingine kigumu, alama za maandishi hutokea kwa namna mbili; kwa rangi ya wino na kwa mgandamizo wa kalamu. Maana yake ni kuwa hata kalamu isiyo na wino inaweza kuacha alama za maandishi kutokana na mgandamizo kati ya kalamu, karatasi na meza.

Hatimaye wataalamu wa nyaraka walianza kuona maandishi kadhaa. Kwanza walipata jina moja na namba za simu kwenye karatasi iliyoonekana kuwa ni mkataba wa biashara. Lakini namba hiyo ya simu haikuwa ikitumika na mtu yoyote wakati huo.

Upelelezi uliendelea. Maofisa wa upelelezi waliamua kumtafuta mmiliki wa nyumba lilipokuwa pipa lile aliyeishi kabla ya Bw. Collin. Mmiliki huyu aliitwa Howard Elkin, mmiliki mwenza wa kampuni ya kutengeneza urembo wa aina mbalimbali kwa kutumia plastiki; majani na miti ya plastiki, vikombe vya plastiki, midoli ya plastiki nk. Je! majani ya plastiki yaliyokutwa kwenye pipa lilohifadhi mwili wa marehemu kwa miaka mingi yalihusiana na Bw. Howard Elkns?

Wakati maofisa wa upelelezi wakipanga kumfanyia mahojiano Bw. Howard Elkns, wataalamu wa nyaraka walipata taarifa zingine kwenye karatasi zilizoharibiwa. Jina la mwanamke mmoja na namba za simu ya nyumbani ambayo ilikuwa bado ikifanya kazi wakati huo.

Wapelelezi pia walifika kwenye kampuni iliyokuwa ikitengeneza bidhaa zile za plastiki kabla ya kukutana na Bw. Howard Elkin. Wafanyakazi wa kampuni hiyo hawakuweza kuwa na uhakika kama majani yale ya plastiki yalitengenezwa na kiwanda chao, lakini walisema kuhusu majimaji yale ya rangi ya ugoro, kuwa ni rangi maalumu ya kupakia bidhaa za plastiki. Hata hivyo wataalamu wa kampuni hiyo walisema, rangi hiyo haikuwa ikitumiwa tena kwenye kiwanda chao na haikuwa kutengenezwa tena tangu mwaka 1971.

Vyombo vya habari navyo havikubaki nyuma. Gazeti moja la kila siku liliandika habari zote zilizotolewa na polisi kuhusu tukio lile na kuweka picha ya pipa lile kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti. Mwanamke mmoja akapiga simu polisi baada ya kuona picha ile.

Akasema, anajua pipa lile ni aina ya mapipa yaliyokuwa yakitumiwa na kampuni ya Meryrose ya kutengeneza urembo wa plastiki. Mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo alikuwa Howard Elkins. Mtoa taarifa akaongeza kuwa anamjua Howard Elkins na anajua kuwa alikuwa na mahusiano na mwanamke mmoja mwenye asili ya kispaniola nje ya ndoa yake, na anajua mwanamke huyo alikuwa mjamzito na alikuwa akifanya kazi kwenye kampuni ya Howard Elkins. Mtoa taarifa huyo alipoitwa polisi kujaribu kuutambua mwili ule, hakuweza kuutambua na kujua kama ni mwili wa mwanamke aliyemfahamu miaka zaidi ya 30 iliyopita.

Kufikia hapo, maofisa wali ona haja ya kumtafuta Howard Elkin ambaye wakati huo alikuwa akiishi Florida. Kwa bahati mbaya Howard hakutoa ushirikiano wa kutosha kwa maofisa wa upelelezi. Howard alikataa kulijua pipa lile akisema hawakuwahi kuwa na pipa la aina ile kwenye biashara zao, alikataa kujua yale majani ya plastiki na hakutaka maswali zaidi. Maofisa wa upelelezi walijitahidi kumuomba ushirikiano lakini Howard aliwataka waondoke kwani mkewe anapiga simu na hawezi kuongea naye wakiwepo.
‘Tulijua anatudanganya’ – alisema mpelelezi Robert Edwards.

Maofisa wa upelelezi walimsisitiza Howard atoe ushirikiano lakini hakutaka. Waliendelea kumuuliza maswali bila yeye kujibu.

Ulikuwa na mahusiano yoyote nje ya ndoa miaka 30 iliyopita? Unaweza kueleza huyo mchepuko wako alikuaje? alikuwa mrefu, mfupi, mweupe au mweusi? alikuwaje?

Wapelelezi hao walimuomba Howard msaada wa mwisho wa kuchukua sampuli ya mate yake kwa ajili ya vipimo vya DNA, lakini Bw. Howard hakukubali na hakutaka kujibu swali lolote aliloulizwa. Baada ya kukosa ushirikiano, maofisa wa polisi walimuaga Howard kwa maneno haya;

“Tunaondoka, lakini tutakwenda mahakamani kuchukua kibali, tukipata kibali cha mahakama tutakuja kuchukua sampuli ya damu yako kwa nguvu, na tutalinganisha DNA yako na ya mtoto aliyekutwa tumboni mwa yule msichana, na hapo maisha yako yote yataishia gerezani”.

Kwa namna Howard alivyokataa kutoa ushirikiano kwa maofisa wa upelelezi ilikuwa ni ishara kwamba yeye ndiye muhusika wa tukio lile. Lakini maofisa wa upelelezi wasingeweza kumkamata kwa sababu ya kutokutoa ushirikiano, bali walihitaji ushahidi wa kushikika. Lakini Howard alikuwa ameshafanya maamuzi yake moyoni. Hata kabla wapelelezi hawakurudi na kibali cha mahakama, Howard Elkins alichukua bunduki yake aina ya Shortgun, akaingia kwenye gari yake, akailenga bunduki kwenye kidevu chake na kuifyatua. Howard aliamua kujiua ili kukwepa aibu na adhabu kubwa ya kifungo cha maisha au pengine kunyongwa.

Wataalamu walichukua sampuli ya damu ya marehemu Howard Elkins, wakafanya DNA na kulinganisha na DNA ya kichanga kilichokutwa kwenye tumbo la msichana aliyeuawa miaka zaidi ya 30 iliyopita. Ingawa tishu za kichanga hicho zilikuwa zimeharibika sana, lakini wataalamu walitumia mbinu ya kimaabara ijulikanayo kama Polymerizing Chain Reaction au PCR ili kupata majibu sahihi ya DNA. Matokeo ya vipimo yalionesha DNA ya Howard Elkins na DNA iloyopatikana kwenye mabaki ya kichanga zilifanana kwa silimia 93.5.

Hakuna shaka kwamba Howard alikuwa baba wa kichanga kile.

Reyna-newspaper.jpg
 
Wapelelezi hao walimuomba Howard msaada wa mwisho wa kuchukua sampuli ya mate yake kwa ajili ya vipimo vya DNA, lakini Bw. Howard hakukubali na hakutaka kujibu swali lolote aliloulizwa. Baada ya kukosa ushirikiano, maofisa wa polisi walimuaga Howard kwa maneno haya;

“Tunaondoka, lakini tutakwenda mahakamani kuchukua kibali, tukipata kibali cha mahakama tutakuja kuchukua sampuli ya damu yako kwa nguvu, na tutalinganisha DNA yako na ya mtoto aliyekutwa tumboni mwa yule msichana, na hapo maisha yako yote yataishia gerezani”.
Fikiria wangekuwa hawa wa kwetu wangefanyaje zaidi ya kumfanya mhusika mtaji kwa rushwa
 
Back
Top Bottom