Wadau,
Ndugu zangu wa JF ambao mnaishi kwenye Jiji la Dar es Salaam mnalifahamu vema tatizo (ambalo sasa ni janga halisi) la msongamano wa magari barabarani. Tatizo hili limejidhihirisha wazi zaidi hususan kwenye siku za muda mfupi uliopita, wakati wa msimu wa mvua ndefu (masika) ambao uliungana na msimu wa mvua fupi (vuli) kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ya kidunia (Global Climatic Change).
Mojawapo ya mapendekezo ya iliyokuwa Kamati ya Uchambuzi juu ya Tatizo la Msongamano wa Magari, iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, lilikuwa ujenzi wa barabara zinazopita juu ya ardhi, maarufu kwa jina la fly-overs.
Lengo kuu la fly-overs ni kuwezesha magari kupita juu ya barabara moja kwa moja kwenye kila sehemu ya makutano, hivyo kuondoa haja ya kusubiri magari yanayoruhusiwa kupita (kwa zamu) na taa za kuongoza magari (traffic lights). Kwa mfano, iwapo kungekuwa na fly-over kwenye makutano ya Barabara ya Ali H. Mwinyi na Barabara ya Kawawa (Morocco), magari yaendayo Kinondoni kutokea Msasani yangepita moja kwa moja, na yale yaendayo Msasani kutoke Kinondoni nayo pia yangepita moja kwa moja, huku yale yaendayo Jijini kutokea Mwenge, Mbezi Beach, na Tegeta (na sehemu nyinginezo) yangepita moja kwa moja, na yale yatokeayo Jijini kwenda Mwenge, Mbezi Beach, Tegeta, na sehemu nyinginezo, vile vile yangepita moja kwa moja.
Kwenye fly-over hiyo, iwapo gari ingetaka kwenda Msasani kutokea Mwenge, kungekuwa na sehemu (mstari) maalum ya kuliwezesha gari hilo kuingia pole pole kwa kutumia utaratibu wa kisheria unaojulikana kama "yielding". Utaratibu huo ungetumika pia kwa wale ambao wangetaka kwenda Kinondoni kutokea Mwenge, hivyo kuwezesha magari kutembea kwa kasi zaidi bila kusimama, na hivyo kufanikiwa kuondoa kabisa tatizo la msongamano wa magari.
Watanzania wasingelazimika kuamka saa 9 alfajiri (kwa wale wanaoishi Mbezi Beach, Tegeta, Bunju, Boko, n.k.) ili waweze kuondoka nyumbani kwao saa 10 alfajiri ili kuwahi ofisini saa 1 au 1.30 asubuhi, tayari kwa kazi, kwa wale ambao wana ajira kwenye Serikali Kuu, kwani, badala ya kutumia muda wa saa 3 au 4 barabarani, wangeweza kutumia muda wa saa 1 au 2 tu!
Ujenzi wa fly-over si kitu cha ajabu wa kitu kigeni. Ujenzi huu unatumika sana nchi za ulaya, na umeondoa na kupunguza kabisa tatizo la msongamano wa magari kwenye nchi nyingi. Tukumbuke pia kwamba, tunapotumia muda mwingi kwenye msongamano wa magari, sio tu kwamba hasara kubwa inatokea kutokana na
(a) matumizi makubwa ya mafuta ya petroli, na
(b) upotevu mkubwa wa muda ambao ungetumika katika shughuli za uzalishaji, bali pia
(c) sisi wenyewe tunaathirika kiafya kutokana na kuvuta hewa iliyochanganyika na moshi wa magari ambao huwa na sumu na kemikali zenye madhara kwa afya zetu.
Niliwahi kujikuta kwenye msongamano wa magari nikitokea Mbezi-Luguruni, nikiwa Ubungo-Kibo. Sehemu ambayo, kwa kawaida, kufika kwenye makutano ya Barabara ya Morogoro na Barabara ya Sam Nujoma huchukua muda wa dakika 2 au 3, nililazimika (pamoja na watu wengine kadhaa) kutumia muda wa saa 2! Nilikuwa ninatokea Mbezi-Luguruni kurudi nyumbani Mbezi Beach. Nilipofika nyumbani nilishindwa kabisa kuona, nikalazimika kuosha macho yangu kwa maji, lakini sikupata nafuu, nikaenda kulala. Siku hiyo ilikuwa Jumamosi, nilifika Ubungo-Kibo saa 12.30 jioni, ilipofika saa 1.30 usiku ndio nilifanikiwa kuvuka makutano ya Barabara hizo, hatimaye kufika nyumbani saa 3.30 usiku! Nilikuwa nimealikwa kwenye sherehe ya harusi ya jamaa wa familia; sikuweza tena kwenda kutokana na kuumwa macho. Nimdai nani?
Swali langu, baada ya kutoa hoja, ni, je, Watanzania wenzangu mliopo nje ya nchi mnaonaje kama mtachukua jukumu la kuongea na makampuni ya ujenzi wa barabara ili yaweze kuja Tanzania na kuingia ubia na, ama
(a) Serikali Kuu au
(b) Watanzania wenye uwezo wa kushirikiana nao ili kuweza kujenga hizi fly-over na kuondoa kabisa hili tatizo?
Serikali Kuu tayari imekwishaweka mkakati wa ujenzi unaojulikana kama Build-Operate-and-Transfer (BOT), ambao unamwezesha mjenzi kukopa pesa kwa minajili ya kurejeshewa alichowekeza kwa njia ya kutoza kodi za moja kwa moja au "indirect taxation". Ninaamini kwamba Watanzania waliopo nchini(hususan Dar es Salaam) hawatapinga nyongeza ya kodi kwenye mafuta ya petroli kuwarejeshea wajenzi wa fly-over kile walichowekeza, ili mradi fly-over zinajengwa na tatizo la msongamano linaondolewa kama si kupunguzwa kwa kiwango kikubwa.
Naomba kuwasilisha hoja.
./Mwana wa Haki