Manyerere: Bunge Hili Ni Kama Mhuri Kwenye Hundi Ya Kughushi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Manyerere: Bunge Hili Ni Kama Mhuri Kwenye Hundi Ya Kughushi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Zed, Jul 11, 2010.

 1. Zed

  Zed JF-Expert Member

  #1
  Jul 11, 2010
  Joined: Mar 28, 2009
  Messages: 359
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35


  Source Kwanza: 9 July 2010 50 views No Comment
  Na Manyerere Jackton, Dodoma
  TANGU mwaka 1996 nimekuwa nikiripoti habari za Bunge. Muda huu si haba. Ndio maana nadiriki kusema kwamba sijawahi kuripoti habari za Bunge dhoofu kama hili la bajeti.
  Bunge hili limekuwa chombo cha kuidhinisha mambo yasiyochujwa wala kuchanganuliwa kwa kina. Ni kama mhuri unaotumika kuhalalisha hundi bandia!
  Kwa mara ya kwanza tumeshuhudia wizara mbili zikiwasilisha hotuba mbili za bajeti, hotuba mbili za Kamati za Bunge, na hotuba mbili za Kambi ya Upinzani!
  Fikiria, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inawekwa pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi! Zote zinajadiliwa na kupitishwa ndani ya saa kadhaa!
  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inaunganishwa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Zote zinasomwa na kuchangiwa na wabunge, kisha zinapitishwa!
  Kuna sababu kadhaa zilizotumiwa kuhalalisha hali hii. Mosi, wabunge wamejiaminisha kwamba kazi nyingi za Bunge zinakuwa zimemalizwa kwenye Kamati za Kudumu za Bunge, hivyo hotuba zinapotolewa na mawaziri, pamoja na hotuba za wenyeviti wa Kamati hizo, huwa zinajaribu kuwasilisha kile kilichokwishakubaliwa! Huu ni mzaha.
  Huu ni mzaha kwa sababu si kweli kwamba Kamati ya wabunge 20 inaweza kufanya kazi maridhawa kama ambayo ingeweza kufanywa na wabunge zaidi ya 300. Hapa napo wabunge wana kisingizio cha kwamba hakuna mbunge anayezuiwa kuingia katika Kamati yoyote kutoa mchango wake, ingawa anaweza asiwe na kura ya uamuzi. Sasa fikiria, wabunge wanaweza kuwa na muda mwingi kiasi gani wa kuhamia katika kamati hizo ili kutoa mawazo yao .
  Lakini hili la kila kitu kumalizwa kwenye Kamati si la kweli kwa sababu hata juzi tu, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Job Ndugai, hotuba ya Kamati yake ilisomwa, lakini hakuridhika. Akaamua kuchangia.
  Kwenye mchango wake alizungumzia athari za ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mto wa Mbu-Loliondo mkoani ARusha hadi Musoma mkoani Mara. Alipomaliza, Naibu Spika, Anne Makinda, alimshangaa! Akasema kwa kuwa mambo aliyozungumza ni makubwa, na yeye ni Mwenyekiti wa Kamati husika, kwanini hayakuingizwa? Akataka utaratibu ufanywe ili yaingizwe kwenye taarifa rasmi ya Kamati. Kwa hiyo utaona kuwa hili la kila kitu kumalizwa kwenye Kamati za Bunge si la kweli. Ushahidi mwingine ni kukwamishwa kwa Muswada wa Baraza la Usalama la Taifa uliowasilishwa na Waziri Sofia Simba. Kamati iliyoupitia iliridhia, lakini baada ya kupelekwa kwenye Kamati ya Bunge zima, wakongwe kama Mzee John Malecela na Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan
  Ngwilizi waliuchana chana kiasi cha kuukwamisha. Hiyo ndio raha na faida ya kulitumia Bunge zima!
  Pili, Bunge linapeleka mambo yake haraka haraka kwa sababu kuna habari kwamba hakuna fedha za kutosha kulifanya lidumu muda mrefu. Nakumbuka zamani Bunge la aina hii liliketi kwa miezi hadi mitatu. Hoja hii ni dhaifu, hasa kwa kuzingatia kuwa mambo ya nchi hayahitaji uamuzi wa zimamoto.
  Bunge, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , ndicho chombo kikuu cha uwakilishi wa wananchi. Ndipo mahali ambako wawakilishi wa wananchi wanatakiwa kuuliza na kujibiwa masuala yanayolihusu taifa. Tena si kujibiwa tu, bali kujibiwa kwa kina!
  Haiwezekani mambo muhimu yanayolihusu Taifa yakawa yanajadiliwa kwa zimamoto kwa kisingizio cha kutokuwapo fedha za kutosha. Watu wenye akili ya kawaida wanaweza kujiuliza, “Lipi bora? Kujadili mambo kijuu juu ili kuokoa fedha na hatimaye kuliingiza Taifa shimoni; au kutumia rasilimali za kutosha kupitisha mambo yenye manufaa na ustawi kwa Jamhuri yetu?” Bila hatuhitaji elimu ya ajabu kupata jibu.
  Tatu, Bunge hili linapelekwa haraka haraka eti kwa sababu mwaka huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Sawa, tuna Uchaguzi Mkuu, lakini hata kabla ya mwaka huu tumeshakuwa nao, mbona mambo hayakuwa ya aina hii? Mbona mijadala ilikuwa mizuri?
  Kwa mujibu wa Katiba, tuna Bunge, lakini kwa maslahi ya nchi ni kama hatuna Bunge. Ndio maana haishangazi kuona kuwa Bunge hili hili linajadili na kupitisha sheria (haraka haraka), kisha sheria hizo hizo zinarejeshwa bungeni tena kufanyiwa marekebisho hata kabla ya kutumika! Ni kama mtu kustaafu kabla ya kuajiriwa! Kama mijadala ingekuwa mirefu, ya wazi, na makini, tusingeshuhudia aibu hizi za kurejewa sheria kabla ya kuanza kutumiwa. Majaji na mahakimu nao wakisema wana kesi nyingi kwa hiyo kila kesi isikilizwe kwa nusu saa, hii itakuwa nchi ya namna gani?
  Mawaziri wamepunguziwa muda mno muda wa kusoma hotuba zao. Vivyo hivyo, wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, wasemaji wa Kambi ya Upinzani na wabunge wenyewe. Kanuni zimetenguliwa na kuwapa wabunge dakika 10 za kuchangia.
  Dakika 10 si haba. Lakini wabunge wetu dakika tano au zaidi kati ya hizo 10 ni za mipasho. Atasimama mbunge wa Chama Cha Mapinduzi ataanza kuwasimanga wapinzani weeee hadi anapigiwa kengele ya kwanza kabla ya kutoa mchango! Akimaliza atatoa pongeze weee hadi wasikilizaji tunakoma. Akimaliza ataanza kumsifu Rais Kikwete weee kana kwamba kaagizwa na wapiga kura kuwa hiyo ndio kazi yake. Atasimama mbunge wa upinzani ataanza kusema CCM haijafanya kitu! Ataorodhesha mambo meeengi wakati hakuna mwenye akili timamu anayeweza kukubali kuwa CCM haijafanya kitu, kama ilivyo kwa waungwana ambao hawawezi kukubali kwamba mambo yote ya Serikali ya CCM ni safi !
  Kwa hiyo tuna Bunge ambalo ni la mipasho na hadithi nyingi zisizokuwa na maana. Kuna muda wa kumwuliza maswali Waziri Mkuu. Badala ya wabunge kuuliza maswali magumu na ya maana, wamebaki kuuliza mambo yale yale yaliyochusha. Hata kama waziri kajibu swali jana, mbunge leo atamwuliza waziri mkuu hilo hilo kwa sababu hakuwapo bungeni, na aliporejea hakujisumbua kujua kilijadiliwa kitu gani.
  Wabunge wanasema muda hautoshi, lakini ni hao hao wanaotuma viji-karatasi vingi kwa Spika, Naibu Spika au Mwenyekiti ili wageni wao wasomwe! Wajulikane kuwa wapo bungeni! Sasa Bunge hili ni jukwaa la watu kujitafutia umaarufu. Mbunge anaweza kumchukua mpenzi wake na kumwambia ‘twende bungeni leo wakusikie redioni na wakuone kwenye televisheni’. Kweli ikawa hivyo! Huyo anaweza kutambulishwa kama “kada au mpiga debe mahiri” wa chama Fulani, kumbe ni mpenzi au rafiki tu!
  Wanatajwa wageni hadi wanaosoma Ulaya na Marekani alimradi tu kuwakonga kina yakhe ambao watoto wao wanasota kwenye shule za kata. Ndio maana watu makini wanapaswa wajiulize, hivi kuna sababu ya kupoteza dakika tano au 10 kwa ajili ya kusoma majina ya wageni bungeni? Kwanini muda huo usitumiwe na mbunge au wabunge kutoa mchango wenye maslahi kwa nchi? Hivi kweli kusema waziri fulani, au mbunge fulani ana wageni kutoka mahali fulani kuna maslahi gani kwa mtazamaji wa televisheni au msikilizaji wa redio? Je, si kweli kwamba mgeni wa Bunge ndiye anayestahili kutambulishwa kwa uzito wake? Bunge gani makini linalobadilishwa na kuwa kijiwe cha kujipatia umaarufu? Heshima ya Bunge inapelekwa wapi? Hili nalo tumeiga Commonwealth?
  Je, ni haki kukosa muda wa kutosha kujadili mambo ya nchi, badala yake tukawa na fedha za kulipa muda wa kutambulishana? Tena kutambulishana kunafanywa na Spika au Naibu Spika! Je, huku si kudhalilisha madaraka na hadhi ya mhimili wa Bunge? Jaji au hakimu naye akiamua kutambulisha maswahiba waliofika kuona anavyogawa miaka kwa washitakiwa tutamshangaa?
  Wakati muda wa kutambulishana ukiwa umetengwa, sasa kuna kauli iliyochusha katika kiti cha Spika. Mara kadhaa, hasa akiwa ameketi Naibu Spika, utasikia akimweleza mbunge au waziri, Uliza kwa ufupi…Waziri jibu kwa ufupi.” Ufupi huu unasaidia nini kwenye mambo mazito yanayohusu mustakabali wa nchi. Suala la nchi uliza au jibu kwa ufupi, lakini kumtambulisha mke au rafiki wa kwenye bia, tumia dakika utakazo!
  Mara kadhaa nimepata kusema kuwa miongoni mwa sababu zinazotukwaza Watanzania wengi ni matumizi mabaya ya muda. Bila kubadilika na kuanza kuheshimu matumizi sahihi ya kila dakika tuliyojaliwa, tutabaki kucheza na mambo madogo madogo tu. Ndio maana hotuba za wanasiasa zinakuwa ndefu kwa sababu tu ya kutambulisha. Wasikilizaji wanachoka. Wanaondoka.
  Kwa kuwa sisi ni taifa la uchaguzi, kila baada ya uchaguzi mmoja tunawaza uchaguzi mwingine. Uhai wa Bunge ni miaka mitano, lakini viongozi wetu wanajitahidi kuliua hata kabla ya mwisho wa uhai wake. Wabunge wapo Dodoma kimwili, lakini kiroho wapo majimboni. Wengi wanawaza namna ya kurejea bungeni. Wasiwasi wa nini? Kama mbunge kafanya kazi zake vizuri, anamhofu au anawahofu kina nani? Na kama kwa miaka mitano hakuweza kufanya mambo ya maendeleo jimboni mwake, atawezaje kuyafanya ndani ya mwezi mmoja?
  Nisema tu kwamba Mkutano huu wa Bunge ni moja ya mikutano dhaifu kabisa ambayo nimepata kuishuhudia ndani ya kipindi ambacho nimekuwa ripota wa Bunge. Wanaoipenda nchi yetu wanapaswa kuhoji na kuomba hali hii isiendekezwe. Kuwa na Bunge la zimamoto kwa mambo makubwa, mambo yanayohitaji maswali na majibu yanayojitosheleza, ni hatari kubwa.
  Bunge kushindwa kuwajadili wageni wanaoiba maliasili zetu katika hifadhi na mapori mbalimbali, Bunge linaloshindwa kuzungumzia hatma ya safari ya Watanzania katika dunia ya utandawazi, Bunge linaloshindwa kujadili na kuamua mbinu za kuwabana wezi waliokubuhu katika idara, wizara na halmashauri zote nchini, Bunge linaloshindwa kuhoji na kupewa majibu ya mambo mazito yanayoikabili jamii yetu, Bunge linaloshindwa hata kumpongeza William Lukuvi kwa kufumua majambazi na majangili wa viwanja Dar es Salaam; Bunge hilo ni dhaifu. Jambo la kuomba ni kwamba Bunge la aina hiyo lifikie tamati ili pengine tupate Bunge jipya litakaloweza kumsaidia Rais Jakaya Kikwete. Hatma ya Tanzania iko mikononi mwa Watanzania wenyewe.
  manyerere@hotmail.com
   
 2. Zak Malang

  Zak Malang JF-Expert Member

  #2
  Jul 11, 2010
  Joined: Dec 30, 2008
  Messages: 5,410
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 0
  Kama ni huyo Manyerere wa Habari Corporation, basi hana credibility or moral authority kuyasema haya!
   
 3. H

  Hekima Ufunuo JF-Expert Member

  #3
  Jul 11, 2010
  Joined: May 28, 2009
  Messages: 220
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Marksman angalia hoja achana na mtoa hoja.

  Hoja ni za msingi sana kujadiliwa, naamini ni wajibu wetu sote kuliangalia bunge letu kama linaleta matunda tarajiwa.
   
 4. Zed

  Zed JF-Expert Member

  #4
  Jul 11, 2010
  Joined: Mar 28, 2009
  Messages: 359
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  Kama ulivyojitambuisha hapa JF yaani Hekima Ufunuo na ndivyo ulivyo na hekima! Nadhani Marksman anatupa mwana na maji aliyomwogea. Kiutu uzima Jackton anapoint hapa hata kama msimamo wake kwa ujumla ni tumikia kafiri - aka RA - upate mradi wako...hilo tulisahau kwa hoja hii. Bunge la wakati huu halina tija na ni ufujaji wa fedha za Watanzania. Lazima libadilike kama tunata kuwa na maendeleo
   
 5. Andrew Nyerere

  Andrew Nyerere Verified User

  #5
  Jul 11, 2010
  Joined: Nov 10, 2008
  Messages: 3,025
  Likes Received: 1,206
  Trophy Points: 280
  Hii makala ni perfect,inaonyesha clarity of thinking,inaonyesha habitual thinking. Press reporters wa Tanzania wanapaswa kuandika hivi.
   
 6. PhD

  PhD JF-Expert Member

  #6
  Jul 12, 2010
  Joined: Jul 15, 2009
  Messages: 3,819
  Likes Received: 818
  Trophy Points: 280
  manyerere kaandika vema, alichosahau kueleza ni kuwa sio Bunge lililoamua kuwa na kikao kifupi namna hii isipokuwa ni serikali na ccm kwa ratiba yao ya uchaguzi wa kura za maoni wamelazimisha kamati ya uongozi ya Bunge kupunguza muda wa vikao ili wabunge hasa wa ccm wawahi ratiba yao ya primaries.
  however ishu ya kutokuwepo fedha za kutosha kuendesha mkutano huu wa Bunge imesemwa na Serikali, so my conclusion over here ni kwamba , sio Bunge dhaifu ila ni Serikali ya CCM ndio imeleteleza haya yote, nawasilisha.
   
Loading...