Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) yaonya ongezeko la joto

moyafricatz

JF-Expert Member
Nov 27, 2015
2,900
4,865
Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameshauri wakazi wanaoishi katika mikoa 15 inayotarajiwa kuwa na kiwango cha juu cha joto kuzingatia ulaji, unywaji, uvaaji na mtindo wa maisha unaofaa ili kupunguza kero itakayowakabili.

Jana, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ilisema mikoa hiyo inatarajiwa kuwa na joto la kati ya nyuzi 33 hadi 34 hali itakayosababisha fukuto hasa nyakati za usiku katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Unguja na Pemba, Kaskazini mwa Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Kagera, Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara.

Ili kukabiliana na hali hiyo, wataalamu hao wamezitaja dondoo kadhaa ikiwamo kunywa maji ya kutosha, kula matunda yenye majimaji na mbogamboga kwa wingi wakati vile vya wanga na mafuta wakitumia kwa kiasi kidogo.

Rose Senyangwa, mtaalam wa mamlaka hiyo alitangaza utabiri wa ongezeko la joto jana hilo kutokana na kuwapo kwa unyevunyevu mwingi angani.

“Usiku kutakuwa na joto kutokana na kuwapo kwa kiwango kikubwa cha unyevunyevu ambacho ni zaidi ya asilimia 80. Ongezeko hilo limesababisha baadhi ya maeneo hutunza joto litokanalo na mionzi ya jua na kusababisha fukuto,” alisema Rose.

Kutokana na utabiri huo, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Pedro Pallangyo alisema ili kuuweka mwili sawa katika msimu huu inashauriwa kunywa wastani wa lita tatu mpaka sita za maji.


“Tunashauri vyakula vyepesi ili kuepuka kuchoka ghafla ni vema chakula kikawa laini hasa kwa kuzingatia kiwe ni chenye majimaji au mchuzi wa kutosha na matunda yanayoshauriwa zaidi ni tikiti, tango, machungwa na mengine yenye majimaji ya kutosha,” alisema daktari huyo wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) huku akishauri watu wavae nguo nyepesi kuruhusu ngozi kupumua vizuri.

Lakini daktari bingwa wa ngozi, Andrew Foi alisema joto linapozidi linaweza kuleta madha kutegemea umri na maumbile ya mhusika.

“Watoto chini ya miaka mitano huathirika zaidi kwa kuwa matezi yao yanayohusika kutoa jasho yanakuwa hayajakomaa vya kutosha. Watoto hao watapata vipele vingi wakati mwingine mwili mzima,” alisema Dk Foi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Alisema hali hiyo hutokana na kuwepo kwa jasho jingi na utaratibu wa kupooza mwili hushindikana kwa kuwa tezi hazijakomaa vya kutosha.

“Wenye maumbile makubwa wanaweza kupata fangasi, kutoa harufu mbaya wakati watoto na watu wazima wakipata majipu,” alisema.

Hata hivyo, alisema ili kuukinga mwili kupoteza kiasi kikubwa, inashauriwa kunywa maji mengi, kuacha kufanya shughuli kwenye joto na jua kali na kuepuka kutumia mafuta mazito.

“Tusiwaache watoto wacheze juani, wapakwe mafuta ya nazi au lotion, tuangalie nguo wanazovaa na watoto wachanga wasiwafunikwe sana...waachwe wapate hewa ya kutosha,” alisema

Kwa upande wake, Dk Maghuha Stephano wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), alisema unywaji maji mengi wakati wa joto kali ni njia rahisi ya kuepuka saratani ya ngozi.



Kujikinga

“Hata watu wazima epuka nguo nyeusi, nzito, suti, tai, labda uwe na gari na ofisi yenye kiyoyozi, acha kuvaa nguo nzito. Makazi yetu nyumba zetu tumezijenga kwa msongamano yasiyo rasmi kwa makazi, huku mzunguko wa hewa katika nyumba huwa mdogo hivyo waweza kufungua madirisha.”

Dk Foi alishauri watu kula mlo kamili wenye matunda yenye majimaji na mbogamboga kwa wingi, wanga na mafuta kwa kiasi kidogo ili kupunguza kero ya joto.
 
Sio lazima kujiongelesha ongelesha ndiyo uonekane unafanya kazi watuambie kwanza mafuriko yalipoenda ndiyo waje kutuletea hizi nahau hapa
Mbona kwa wenzetu utabiri wa hali ya hewa huwa ni effective zaidi ya 90%
Elimu ya bongo nadhani ina shida lakini hata kujiongeza tu imekuwa mzigo kwao
 
Kwanini wanasema watu wenye maumbile makubwa si waseme watu wanene.
Unene ni subjective.. ni sifa.. kwa mtu mwenye umbile dogo au umbile kubwa.

Mtu mwenye Urefu wa mita 1.55 akiwa na kilo 70 ni mnene ila hana umbile kubwa ..
Mtu mwenye urefu wa mita 2 mwenye mwili wa kawaida asiye na mafuta mengi (body fats) Huyo anaweza asiwe mnene ila ana umbile kubwa.

Kwa Hapa nadhani walitaka kumaanisha wafu wanene.. na sio wenye maumbile makubwa..

Japo sijui kama.kusema "wanene" inaruhusiwa kipindi hiki PC Culture.. tusije Kuwa blacklisted mitandaoni.. :)
 
Sio lazima kujiongelesha ongelesha ndiyo uonekane unafanya kazi watuambie kwanza mafuriko yalipoenda ndiyo waje kutuletea hizi nahau hapa
Mbona kwa wenzetu utabiri wa hali ya hewa huwa ni effective zaidi ya 90%
Elimu ya bongo nadhani ina shida lakini hata kujiongeza tu imekuwa mzigo kwao
Kweli mkuu wiki kama mbili nyuma walitabiri kunyesha mvua kubwa mikoa kadhaa ila cha ajabu mvua ni kidogo kweli 😄😄
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom