Uchaguzi 2020 Mambo 20 muhimu wakati wa kupiga kura, kuhesabu, na kutangaza matokeo

Bashir Yakub

Member
May 27, 2013
84
1,562
MAMBO 20 MUHIMU WAKATI WA KUPIGA KURA, KUHESABU, NA KUTANGAZA MATOKEO.

Na Bashir Yakub, WAKILI
+255 714 047 241.

1. Sifa za mpiga kura ni mbili, moja hakikisha umo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura(yaani umejiandikisha),mbili hakikisha unafika kwenye kituo cha kura na kadi yako ya mpiga kura. KIFUNGU CHA 13 (a)SHERIA YA UCHAGUZI.

2. Namna ya kupiga, utakwenda kituo ulichojiandikisha, utaonesha kadi ya mpiga kura, jina lako litaangaliwa kwenye daftari la kudumu, utapewa karatasi tatu za kura zenye muhuri, utaingia kwenye kijumba na kuweka alama kwa unaowachagua, utafunga karatasi zako zisionekana, utamuonesha afisa tume alama za tume zilizo nyuma ya karatasi ya kura, utaweka kwenye maboksi matatu tofauti kila karatasi(Rais,Mbunge,Diwani), kidole chako kitatiwa wino, utatoka nje na kuondoka.KIFUNGU CHA 61(3) SHERIA YA UCHAGUZI.

3. Mpiga kura asiyeona(blind) au mlemavu atakuja na msaidizi wake, isipokuwa msaidizi mmoja atamsaidia mlemavu mmoja tu, lakini kama nyumba moja ina mlemavu zaidi ya mmoja basi msaidizi mmoja atawasaidia wote, wakala au afisa tume haruhusiwi kumsaidia mlemavu kupiga kura. KIFUNGU CHA 61(9) SHERIA YA UCHAGUZI.

4. Asiyejua kusoma na kuandika hatakuja na msaidizi, bali afisa tume na wakala ndani ya kituo watamuonesha alama,picha, au rangi za vyama ili achague,hata hivyo hawatamwambia amchague nani.KIFUNGU CHA 61( i ) SHERIA YA UCHAGUZI.

5. Kura yako itahesabika imeharibika iwapo baada ya kuweka alama kwa mgombea utakunjua karatasi na kuonesha kwa waliopo kuwa umempigia fulani.KIFUNGU CHA 61( J) SHERIA YA UCHAGUZI.

6. Mtu aliyebadilisha majina kwasababu ya ndoa ama sababu nyingine anaweza kupiga kura kwa kutumia kadi yake yenye jina la zamani kama haikubadilishwa.KIFUNGU CHA 14 SHERIA YA UCHAGUZI

7. Afisa anayesimamia uchaguzi,askari anayesimamia usalama siku ya uchaguzi, na mgombea, wanaweza kupigia kura kituo chochote ndani ya jimbo ambacho hawakujiandikisha, kwa kutumia cheti maalum kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi. KIFUNGU CHA 13(4&5)SHERIA YA UCHAGUZI.

8. Tume inaweza kuahirisha siku ya kupiga kura na kutangaza siku nyingine iwapo kutatokea tukio linalozuia upigaji kura kufanyika.KIFUNGU 46(4) SHERIA YA UCHAGUZI.

9. Muda wa kufungua vituo vya kura ni Saa mbili kamili asubuhi na kufunga saa 12 jioni,au mapema zaidi kama itakavyoelekezwa.KIFUNGU CHA 47(3) SHERIA YA UCHAGUZI.

10. Pamoja na wakala kuteuliwa na chama lakini lazima awe ameridhiwa na mgombea.KIFUNGU CHA 57(1)SHERIA YA UCHAGUZI.

11. Mpiga kura aondoke kituoni baada ya kupiga kura. KANUNI 2(2.3.2)( c ) KANUNI ZA MAADILI YA UCHAGUZI.

12. Msimamizi wa kituo ni lazima aoneshe kwa mawakala na maafisa wengine kituoni kuwa sanduku la kura halina kitu ndani na alifunge kwa alama ambayo haiwezi kutoka kabla ya kuanza kupiga kura. KIFUNGU CHA 58(2) SHERIA YA UCHAGUZI.

13. Ni lazima wakala awepo wakati kituo kinapofunguliwa. KIFUNGU CHA 61(1) SHERIA YA UCHAGUZI.

14. Kama wewe si mpiga kura au umeshamaliza kupiga kura, si afisa tume,si mgombea,si afisa usalama,huruhusiwi kuonekana kituoni. KIFUNGU CHA 63(2) SHERIA YA UCHAGUZI.

15. Kura zote lazima zihesabiwe kituoni zilikopigiwa. KIFUNGU CHA 70A SHERIA YA UCHAGUZI.

16. Ikiwa wagombea watapata idadi ya kura sawa na hakuna mshindi, kura zitahesabiwa tena,kama zitalingana tena zitehasabiwa tena mara ya pili, zikilingana tena msimamizi wa kituo atamtaarifu msimamizi wa uchaguzi wa wilaya, na ndani ya siku 30 baada ya uchaguzi utaandaliwa uchaguzi mwingine kwa waliofungana tu. KIFUNGU CHA 77 SHERIA YA UCHAGUZI.

17. Wakala anayekataa kusaini matokeo aweke kwa maandishi kuwa amekataa na sababu za kukataa, vinginevyo mgombea wake atakosa haki ya kufungua kesi mahakamani. KIFUNGU CHA 79A(3) SHERIA YA UCHAGUZI.

18. Ulazima wa kurudia kuhesabu kura ni mara mbili tu hasa kama mara ya pili imerudisha idadi ile ile ya mwanzo, ya tatu ni hiari ya msimamizi wa kituo,si lazima.KIFUNGU CHA 78 SHERIA YA UCHAGUZI.

19. Mpiga kura ambaye hakuridhishwa na mchakato wa upigaji kura, atamuomba msimamizi wa kituo ampatie fomu namba 15 aeleze malalamiko yake na amkabidhi msimamizi wa kituo. KANUNI YA 53, KANUNI ZA SHERIA YA UCHAGUZI.

20. Waangalizi hawaruhusiwi kutoa maoni yao, ama kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea. KANUNI YA 22( i)( j ) KANUNI ZA SHERIA YA UCHAGUZI.
 
Mtu hafuati KATIBA atafuata vijisheria yeye ni Vifaru na kutesa
 
Back
Top Bottom