Mambo 10 usiyoyajua kuhusu Richard Mabala

Ado Shaibu

Member
Jul 3, 2010
99
108
mabalaa.jpg
MAMBO KUMI USIYOYAJUA KUHUSU RICHARD MABALA

KWA watu wengi waliofika ngazi ya elimu ya sekondari, jina Richard Mabala linapotajwa, jambo la kwanza watalolikumbuka ni vitabu vyake maarufu vya fasihi vya Mabala The Farmer na Hawa the Bus Driver. Wengine watamkumbuka kwa mashairi yake ya Kiingereza yaliyomo kwenye vitabu vya Summons: Poems From Tanzania na Selected Poems.

Richard Mabala ni mtu wa namna gani hasa? Kwenye makala haya tunakuletea mambo 10 ambayo pengine ulikuwa huyajui kuhusu Richard Mabala, mwandishi maarufu wa vitabu, mwanafasihi, mkereketwa wa elimu ya Tanzania, mhamasishaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya kufundishia nchini, mwanasafu kwenye magazeti mbalimbali na mwanaharakati kupitia Asasi ya TAMASHA. Mambo hayo ni yafuatayo:

1. MNYAMWEZI MKOROGO!

Jambo moja ambalo baadhi ya wasomaji wa vitabu na makala zake wanaweza wasilijue kuhusu yeye, hasa kutokana na anavyokimudu Kiswahili kwa uweledi wa hali ya juu, ni kwamba Richard Mabala ni mzungu. Richard Mabala alikuja nchini mwaka 1973 akiwa miongoni mwa Wafanyakazi wa kujitolea chini ya mpango wa Wafanyakazi wa kujitolea (Voluntary Service Oversea-VSO).
Chini ya VSO, utaratibu ulikuwa Wafanyakazi kutoka uingereza walikuwa wanalipwa mshahara ule ule waliokuwa wanalipwa Wafanyakazi wa Tanzania. Mabala ambaye amewahi kufanya kazi kwa muda mrefu mkoani Tabora hupenda kujiita kwa jina la utani la Mnyamwezi Mkorogo.

2. TOKA RICHARD SATTERTHWAITE HADI RICHARD MABALA

Alipofika Tanzania, Richard Mabala anasema jina lake la asili lilikuwa ni Richard Satterthwaite. Kutokana na kuwawia vigumu wenyeji kulitamka jina hilo, aliamua kubadili jina na kujiita Mabala. Jina hilo Mabala limetoka wapi? Mwenyewe anasema, Nilijiunga na kwaya ya Ipuli kule Tabora, mwishoni na baada ya kuzoeana wanakwaya wenzangu walisema kuwa hawawezi kulitamka jina langu na kwamba watanipa la kwao; Mabala. Nilipowauliza lina maana gani wakasema eneo kubwa la nje kutoka Uingereza hadi Tabora. Kwa kweli nilianza kulitumia jina hili kwa wasiwasi kidogo nikiona watu wanaweza kuniona najitia kimbelembele kulia kuliko mfiwa, lakini kila mtu akalipenda. Kwa hiyo baada ya kunogewa na kupata uraia nikaliongeza na kuwa jina rasmi.

3. URAIA NA FAHARI YA UTANZANIA

Baada ya kuvutiwa na Tanzania, Mabala alikata shauri kuwa raia kamili wa nchi hii adhwimu. Harakati zake za kusaka Uraia alizianza rasmi mwaka 1979 ambapo Richard Mabala alipeleka maombi ya uraia kwa mamlaka zinazohusika na hilo, maombi yake hayo yakaridhiwa miaka miwili baadaye na akawa Mtanzania kamili. Mabala anasema kuwa hajawahi kamwe kujutia uamuzi wake wa kubadili uraia licha ya kulazimika kupitia mlolongo mrefu wa kuomba Viza kila anapotaka kwenda kumjulia hali mama mzazi yake aliyeko Uingereza.

Mabala anasema kamwe rangi yake haijawahi kuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli zake mbalimbali hapa nchini.

4. MWALIMU WA MA-NGULI

Kwa vipindi tofauti Mabala amefundisha kwenye shule na vyuo mbalimbali nchini. Baadhi ya shule na vyuo alivyofundisha ni Mirambo, Mzumbe, Korogwe, vyuo vya ualimu Changombe na Marangu. Pia amewahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . Mabala analikumbuka zaidi darasa lake la kwanza la Shule ya sekondari ya Wavulana Mirambo ambalo lilikuwa na wanafunzi ambao sasa ni wanasiasa na wanazuoni nguli.

Baadhi yao ni Marehemu Profesa Jwani Mwaikusa, Mwanazuoni wa Sheria aliyebobea na Wakili katika Mahakama ya Kimataifa Maalum ya Mashtaka ya Jinai juu ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda, ICTR, iliyoko Arusha, Profesa Abdallah Njozi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro na Mwanafasihi Mbobezi wa Lugha ya Kingereza na Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Uchukuzi.

5. MWALIMU MSIKIVU

Baada ya Uhuru, uchapishaji wa vitabu mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili ulishika kasi. Uchapishaji wa vitabu kwa lugha ya Kiingereza hasa vile vya fasihi vilivyoandikwa na waandishi wa kitanzania ulidorora. Kitabu cha Summons: Poem from Tanzania kilikuwa kati ya diwani za mwanzo kabisa za ushairi wa Kiingereza kuchapishwa nchini baada ya uhuru. Kazi hii ambayo inajumuisha mashairi ya waandishi mbalimbali wa Kitanzania kama Kajubi Mukajanga, Isaac Mruma, Kundi Faraja, Jwani Mwaikusa na Mabala mwenyewe ilikuwa ni zao la ushirikiano wa Mabala na waliokuwa wanafunzi wake wa sekondari. Mabala anasema kuwa wanafunzi wake walikuwa wakimpatia changamoto ya kuandika kazi zake mwenyewe badala ya kuishia kuchambua na kuzikosoa kazi za wengine.

Mabala anasema Kajubi Mukajanga (ambaye sasa ni Katibu wa Baraza la Habari-MCT) ndiye aliyenishawishi kuandika mashairi wakati yeye alikuwa mwanafunzi na mimi nilikuwa mwalimu wake. Eti kazi yangu ilikuwa kukosoa wengine kwa nini na mimi nisiandike ili nao wapate nafasi ya kunikosoa.

Mabala aliifanyia kazi rai ya wanafunzi wake na kuandika mashairi na vitabu vingine vya hadithi.

6. KUTOKA UHADHIRI HADI MWANAHARAKATI

Baada ya miaka mingi ya ualimu, Mabala aliamua kujikita kwenye harakati za Asasi za Kiraia (AZAKI). Yeye ni miongoni mwa wanachama waanzilishi wa AZAKI maarufu kama Haki Elimu na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na mwishowe kwa kushirikiana na vijana, akaanzisha asasi ya TAMASHA yenye makao makuu jijini Arusha.

Mabala anasema Nillifundisha Milambo, Mzumbe, Changombe TTC, Marangu TTC, Kibosho Girls na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kisha nikatambua kwamba mimi ni mwanaharakati kuliko mwanataaluma (mhadhiri) ndiyo maana nikaingia AZAKI kwa lengo la kuwawezesha vijana. Nimeanzisha TAMASHA (Taasisi ya Maendeleo Shirikishi) tukihimiza vijana wapate nafasi yao katika jamii

Kati ya mwaka 1999 hadi 2007 Mabala alifanya kazi kwenye shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) kwenye programu ya kuwakomboa vijana wasio shuleni. Mabala alifanya kazi na Unicef kama mwandishi wa mfululizo wa vitabu vya Sara ambavyo vilitafsiriwa kwa Kiswahili. Vitabu vilivyowahi kutolewa katika mfululizo huo ni pamoja na The Special Gift (Zawadi Maalum), Daughter of Lioness (Binti Simba), The Empty Compound na Who is the Thief?

7. SAUTI YA VIJANA

Vitabu vingi vya Mabala vinahusu watoto na vijana. Mabala anasema kuwa watoto ni kundi lililosahauliwa. Anasisitiza kuwa kamwe haiwezekani kujenga utamaduni wa kupenda kujisomea vitabu kama jitihada hazielekezwi kwa watoto wadogo kwa sababu ni vigumu kuwa na ari ya kupenda kujisomea wakiwa ukubwani.

8. MTETEZI WA KISWAHILI.

Licha ya kuwa kazi zake nyingi zimeandikwa kwa Kiingereza, Mabala ni miongoni mwa watu wanaopigia chapuo kutumika kwa Kiswahili kama lugha ya kufundishia tangu shule ya msingi hadi chuo kikuu. Mabala anasema Kama mwalimu moyo unaumia sana kuingia darasani siku ambayo wanafunzi wamebahatika kupata mwalimu na kukuta sura zilizofadhaika maana hawaelewi wanachofundishwa. Au fanya jaribio la kufundisha kwa Kiingereza lakini uwape kazi ya kujadili katika vikundi. Angalia watakavyochangamkia mada na kujadili kwa kina kwa kiswahili lakini huku wakitumia neno la Kiingereza hapa na pale hasa ya istilahi na wataelewana vizuri sana.

Mabala anaongeza juu ya hayo kwa kusema, Msingi wa elimu ni ubunifu na uelewa ndiyo maana nchi zilizo nyingi sana duniani wanahakikisha kwamba wanafundisha watoto wao kwa lugha wanayoielewa. Waholanzi, Waswidi na wengineo wana uwezo wa kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia lakini hawafanyi hivyo maana wanajua kwamba msingi wa elimu na ubunifu, ni uelewa. Na wanajua pia kwamba mara nyingi wanasayansi ndio wabovu kabisa katika kujifunza lugha.

Kisha anaendelea kusema kuwa Iwapo tunatengeneza mazingira yanayofaa watoto wetu wanaweza kujua Kiingereza vizuri sana pamoja na kuwa na uelewa wa mambo yote muhimu katika elimu. Mimi nilikuwa sijui Kihispania kabisa lakini kwa muda wa miaka miwili tu, ndani ya shule tu, niliweza kupata 'B' katika A Level. Kwa sababu ya ufundishaji vizuri, mipango makini na pia juhudi yangu. Kwa hiyo hakuna linaloshindikana. Elimu kwanza si lugha kwanza.

9.BWANA MAKENGEZA NA MWANDISHI WA AYA
Ili kufikisha ujumbe kwa mtindo wa kipekee, Mabala anaendesha safu mbili kwenye magazeti ya Mwananchi (Bwana Makengeza) na Raia Mwema (Aya za Ayah Binti Hidaya). Makala hizo, licha ya kuwasilishwa kwa mtindo wa ucheshi, zimebeba ujumbe mkubwa sana wa hali halisi kwenye jamii. Mathalani, kwenye safu yake ya Aya za Ayah Binti Hidaya, anamtumia mhusika wake mkuu Hidaya ambaye ni mtumishi kwenye nyumba ya Waziri (Waziri wa Mikiki na Makeke) kuonyesha maovu na ghiliba zinazofanywa na wanasiasa.

10. MWANDISHI WA USIKU

Mabala anasema uwingi wa shughuli za Asasi za Kiraia na zile za uandishi kamwe haujawahi kumletea matatizo kwenye familia kwa sababu mkewe anamuunga mkono kwenye kazi zake.Mke wangu ni muelewa sana kwa sababu kazi zangu za kuandika nazifanya kati ya saa tisa usiku na saa kumi na mbili asubuhi. Ananiunga mkono sana isipokuwa pale kitanda kinapokuwa cha baridi sana anasema Mabala kwa utani.



mabalaa.jpg
Pichani ni Mwalimu Richard Mabala (katikati mwenye miwani) akiwa na Wanafunzi wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari Mirambo mwaka 1974.Kwa maelezo ya Mabala kwenye picha hii kuna angalau profesa mmoja wa UCLAS, 2 wa UDSM (mmoja marehemu) wakubwa wa BRELA na SUMATRA, generali 1, waziri 1 waandishi maarufu angalau 2 (1 marehemu), kiongozi wa usalama wa taifa. Aidha kuna mkubwa wa bandarini. Unamtambua nani kati yao?
 
Asante mleta mada kwa kumwelezea huyu mtaalamu wa lugha kwa kutumia aya 10.Kipindi fulani nilihudhuria
semina moja huyu mwalimu akawa anachangia mada kwa njia ya ucheshi nilioupenda sana.Nikauliza ni nani nikaambiwa anaitwa Richard Mabala, mwingereza aliyefall in love na Tanzania. Nafurahi kujua kwamba amepewa uraia
wa Tanzania.

Hata hivyo, hujaeleza ni wapi na kwa nini kipindi fulani alijiita 'Mabala wa Mabalaa'
 
Helo

Kumbe Mwandishi wa kitabu Hawa the Bus Driver bwana Richard Mabala yuko live Azam UTV channel

Nimeshangaa kumbe ni mzungu ila anaongea kiswahili vizuri.Napenda kufahamu ni mbongo au mlowezi?
 
Aiseee. Nimekisoma hicho kitabu nikiwa shule ila sikifahamu kuwa mwandishi wa kitabu hicho ni mzungu. Wenye ufahamu juu yake watatujuza kwa hakika
 
Back
Top Bottom