KATIKA hali isiiyokuwa ya kawaida, Mkazi wa kijiji cha Mwisole wilayani Uyui Mkoa wa Tabora, Kabula Kayungilo (20) amejifungua mayai mawili kama kuku badala ya mtoto.
Tukio hilo ambalo liliwaduwaza wakazi wengi wa Mji wa Tabora huku wengine wakitaka mayai hayo yafanyiwe uchunguzi wa kitalaamu ili kubaini kulikoni, lilitokea jana katika Hospitali ya Misheni ya Ndalla wilayani Nzega.
Mganga mkuu wa hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Dk Reuben Nyaruga, alisema tukio hilo lilitokea jana asubuhi wakati mama huyo alipofika kwa ajili ya huduma ya kujifungua mtoto.
Dk Nyaruga alimtaja mkazi huyo kuwa ni Kabula kayungilo (20) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mwisole wilayani Uyui.
Alieleza kuwa msichana huyo alipokewa hospitalini hapo jana asubuhi akidai ni mjamzito anayejisikia uchungu wa kujifungua.
"Lakini uchunguzi wa awali uliofanywa na madaktari ulionyesha kuwa msichana huyo hakuwa na mimba ingawa alionekana kuwa na tumbo kubwa kiasi," alisema Dk Kayuga na kuongeza:
"Wakati muuguzi akiendelea kumpima ghafla msichana huyo aligumia maumivu ya kujifungua na kumfanya muuguzi amuandae kwa ajili ya kujifungua."
Alisema baada ya kuandaliwa mahala pa kujifungua, msichana huyo alijifungua mayai mawili yanayofanana na mayai ya kuku jambo ambalo lilimshangaza mwenyewe na muuguzi.
"Waliamua kuvunja yai moja ili kuona kilichokuwa ndani. Wakakuta kiini cha yai linalofanana kabisa na yai la kuku," alisema na kueleza kuwa yai lingine walimpa ndugu wa mume wa mwanamke huyo.
Kwa mujibu wa Dk Kayuga hii ni mara ya pili kwa msichana huyo kuhisi kuwa na mimba. "Mara ya kwanza mimba yake ilitoka ikiwa na miezi mitatu." alisema.
Akieleza historia ya mgonjwa huyo, Dk Nyaruga alisema katika zahanati ya kituo cha Mwisole alipokuwa akihudhuria kliniki, cheti chake kinaonyesha alihudhuria mara mbili.
"Mara ya kwanza aliwekewa alama ya mkato na mara ya pili alionekana ana mimba ya wiki kumi na sita," alisema.
Mume wa msichana huyo Bugalama Mahona alieleza kuwa mkewe huyo alianza kuhudhuria kliniki baada ya kuamini kuwa ana mimba.
"Sasa tulikubaliana kwamba aje katika hospitali hiyo kubwa ili ajifungue kwa usalama zaidi," alisema Mahona.
Akizungumzia tukio hilo msichana huyo alisema kabla ya kutaga mayai hayo alijisikia uchungu wa kujifungua.
"Nilikuwa nikitarajia kumpata mtoto wa kwanza baada ya mimba ya kwanza kutoka," alisema.