SoC03 Malezi bora ni Msingi wa jamii bora

Stories of Change - 2023 Competition

Baba Van dijk

New Member
Jun 5, 2023
1
0
Salaam watanzania wenzangu. Nimepata shauku ya kuandika juu ya swala la malezi bora kwa watoto wetu kama msingi mzuri wa jamii bora ya kesho na baadae.

MABADILIKO YANAYO WEZA KULETWA NA MAUDHUI YALIYO KATIKA ANDIKO HILI;

Ni matumaini yangu kuwa, andiko hili litakuwa chachu katika kuleta mabadiliko chanya kwa wazazi na walezi ili kuweza kuijenga jamii bora ya baadae inayo tokana na malezi bora yanayo hitajika.

Twende Sawa pamoja:

Mwenyezi Mungu ametupatia watoto kama zawadi lakini pia kama njia ya kuendeleza uzao na vizazi. Lakini katika vitabu vya kiimani au dini, Mungu ametuagiza wazazi kuwalea watoto wetu katika njia zilizo bora ili nawao waje kuwa walezi bora katika vizazi vingine.

Ndugu zangu, lilivyo shamba linavyo hitaji matunzo mazuri, mbolea na maji ya kutosha ili kustawi na kupata mavuno mazuri, hali kadhalika ndivyo ilivyo katika malezi ya mtoto au watoto.

Watoto wetu wanapaswa kupata malezi yanayo endana na maadili ya jamii zetu (Africa), pamoja na maadili ya kiimani. Mtoto apate malezi yanayo msaidia kutambua kuwa;
(a) kumsalimia mtu mkubwa ni wajibu sio hisani.
(b) lugha ya matusi ni mwiko kusikika kinywani mwake.
(c) anao wajibu wa kufanya kazi za nyumbani ata kama hajaambiwa.
(d) kuhudhuria ibada au swala katika imani anayo kuzwa nayo.

Pia wazazi wahakikishe hawawafundishi watoto wao misemo yenye ukosefu wa maadili. Wazazi wasione haya kutoa adhabu japo kidogo kwa mtoto anapokuwa amefanya kosa linalo stahili adhabu. Kwani adhabu humfanya mtoto kujua kuwa jambo ovu lina athari katika jamii.

Pia wazazi wanao wajibu wa kushirikiana katika malezi ya mtoto wao. Wazazi watenge muda wa kukaa na kuwaaasa watoto, kusikiliza changamoto za watoto na kutoa nasaha au ushauri pale penye ulazima.

Wazazi wahakikishe wanamfanya mtoto anamjua Mungu. Mtoto ajengewe mazoea ya kujua uwepo wa Mungu, aijue imani na afahamishwe kuwa Mungu ndie chanzo cha maisha ya viumbe vyote. Wazazi wahakikishe mtoto anahudhuria kwenye nyumba za ibada au swala kama inavyo agizwa katika mafundisho ya imani yao. Hofu ya Mungu ikiwa ndani ya mwanadamu yeyote mwenye utimamu wa akili, ni lazima mtu huyo atakuwa na maadili yenye kumpendeza Mungu na wanadamu.

Mzazi au Mlezi asiwe msitari wa kwanza kumtetea mtoto wake inapo tokea ameletewa mashitaka juu ya utovu wa nidhamu wa mtoto au watoto wake. Mzazi asimame katikati, aujue ukweli, ikiwa mashitaka yatakuwa na ukweli, basi mzazi ampe maonyo na karopio kali mtoto wake juu ya utovu huo.

Mzazi awe makini kufatilia michezo ya mtoto wake, ayajue makundi ya marafiki zake na kuchunguza tabia za marafiki wa mtoto kwani makundi maovu imekuwa njia nyepesi ya kuathiri maadili ya watoto na vijana wengi katika jamii zetu.

Lakini ifahamike pia, malezi bora yanategemea mahusiano bora ya wazazi. Hapa hoja yangu ni, mume na mke, wanao wajibu wa kuishi pamoja, kutatua changamoto pamoja, kumlea mtoto pamoja. Kwa kiasi fulani, watoto wetu wamekosa malezi yanayo stahiki kutokana na ndoa ya wazazi kuvunjika.

Mazingira ya elimu (Shule) yana nafasi kubwa sana kwa upande mwingine katika malezi ya mtoto au watoto. Walimu ndio watu wanao Kaa na watoto kwa muda mrefu kwa siku hadi mwaka. Nafasi ya walimu ina umuhimu mkubwa katika malezi ya mtoto. Walimu wapewe semina na mafunzo juu ya swala la maadili, ushauri na malezi. Hii itakuwa sehemu muhimu sana ya kumfanya mwalimu aweze kuwa mlezi muhimu kwa watoto zaidi ya kuwa tu mtoa maarifa kwa ajili ya kujibu mitihani. Tunaamini elimu bora ni ile iliyo ambatana na nidhamu bora kwa mwanafunzi.

Pia jamii inao wajibu mahususi sana katika malezi ya mtoto au watoto wake. Jamii yoyote iliyo bora ni matokeo ya malezi bora yaliyo fanyika Kipindi cha nyuma. Hivyo kila mwanajamii anayo nafasi ya kusaidia kumlea mtoto wa leo katika njia iliyo sahihi ili kumjenga mwanajamii bora wa baadae. Ni bahati mbaya sana kwamba, nyakati hizi za sasa zimekuwa na mkanganyiko wa kimaadili na ushirikiano hafifu miongoni mwa watu, hali ambayo imepelekea majukumu ya malezi kubaki mikononi mwa wazazi pekee. Huenda hii imechagizwa na mitindo ya maisha ya kisiasa pamoja na ongezeko la matabaka ya madaraja ya kimasiha. Lakini wajibu wa jamii ni mkubwa na muhimu katika kuwalea watoto wa leo ambao ndio wazee wa jamii ya baadae.

Bila kusahau pia, viongozi wa dini mbalimbali wanao wajibu wa kufundisha juu ya malezi bora kwa watoto. Mafundisho ya imani zetu yanapaswa kuzingatia pia malezi ya mtoto ili afanywe kuwa mtu mwenye maadili mema na manufaa kwa kizazi cha baadae.

Nihitimishe kwa kusema kuwa, Mtoto alelewavyo ndivyo akuavyo. Taifa lenye watoto walio na maadili mema, ni taifa lenye bahati nzuri.

Ahsanteni
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom