Makumbusho ya Sanxingdui yarejesha ustaarabu ambao haukujulikana hapo awali

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,035
VCG211311482966.jpg


China ni nchi inayoendelea kufanya ugunduzi mkubwa wa vitu vya kale kupitia wanaakiolojia wake. Kutoka ustaarabu uliopotea, jeshi la terracotta hadi tambi za kale zaidi duniani, vyote hivi vinapatikana kwenye maeneo mbalimbali ya akiolojia hapa China.

Ikiwepo Guanghan takriban kilomita 40 kaskazini-mashariki mwa Chengdu, Mkoa wa Sichuan, Eneo la Akiolojia la Sanxingdui lina mabaki ya kale ya miaka 5,000 iliyopita ambayo yanaamiwa kuwa ni mabaki ya dola ya Shu. Hili ni jumba kubwa zaidi la makumbusho kusini-magharibi mwa China, lenye idadi kubwa ya vitu vya kale vyenye thamani, na kwa heshima kubwa linaitwa "Asili ya ustaarabu wa Mto Changjiang".

Wahenga wanasema “Usisubiri kuambiwa nenda ujionee mwenyewe”. Tukitilia maanani msemo huo, naweza kusema kwamba ilikuwa ni bahati kubwa sana kwangu kuweza kutembelea eneo hilo la Sanxingdui. Ingawa safari ilikuwa ndefu kidogo kutoka Deyang hadi Chengdu yalipo makumbusho haya, lakini baada ya kufika uchovu wote uliisha, kwani nilipata uzoefu mkubwa na kujionea mchakato mzima wa ugunduzi wa vitu vya kale, kuanzia kuchimba, kufukuliwa, kutolewa nje ya mashimo hadi kusafishwa. Mara nyingi uzoefu kama huu huwa wanaupata wenyewe wanaakiolojia tu.

Jina Sanxingdui linamaanisha 'Kalibu la Nyota Tatu' na linaangazia makalibu matatu makubwa ardhini kwenye eneo hilo, ambayo yanafikiriwa kuwa ni mabaki ya udongo na ukuta wa matofali. Zaidi ya hazina 1,000 za kitaifa, vikiwemo vinyago vya dhahabu, vyombo vya shaba, vibamba vya jade, vipande vya pembe za ndovu na mti mtakatifu, vilichimbuliwa mwaka 1986 kutoka kwenye mashimo mawili ya kafara kwenye magofu ya Sanxingdui.

Kazi hizi za sanaa za kale zilizogunduliwa na kuzishudia kwa macho yetu wakati tunatembelea jumba la makumbusho la Sanxingdui huko Sichuan, zinaonesha kuwepo kwa ustaarabu ambao haukujulikana hapo awali. Ugunduzi huu ni mfululizo wa ugunduzi mbalimbali hapa nchini China, ambao unatoa mwanga mpya unaong’arisha siku za nyuma huku watu wa sasa wakijua siku hizo zilikuwaje.

Mwaka 2019, wakati ulipofanyika uchimbaji mkubwa katika eneo la Sanxingdui, viligundulika zaidi ya vitu 500 vya sanaa vilivyotengenezwa kwa dhahabu, shaba, jade na pembe za ndovu zaidi vya miaka 3,000 iliyopita, ikiwa ni pamoja na kofia ya dhahabu ambayo inasemekana kwamba huenda ikawa imevaliwa na kuhani. Vitu hivi vinatoa ushahidi na uelewa juu ya masuala ya kijamii, kiuchumi na uzalishaji vya jamii ya Shu. Pia wataalamu wametambua kwamba eneo hilo lenye ya ardhi ya rutuba hapo zamani lilikuwa likijishughulisha na masuala ya uvuvi, uwindaji, ufugaji na kilimo, na utengenezaji wa vitambaa, na kuonesha picha ya kuwepo ustawi mkubwa kwa watu dola hiyo.

Sanxingdui iko kwenye orodha ya UNESCO ya Maeneo ya Urithi wa Dunia, pamoja na eneo la akiolojia la Jinsha na makaburi ya majeneza yenye umbo la mashua. Kwa sasa China tayari ina maeneo 55 yaliyoorodheshwa na UNESCO kuwa ni Urithi wa Dunia.

Wakati uvumbuzi huu ukiwa umetushangaza wengi tuliohudhuria kwenye makumbusho haya, katika kuangalia kwangu nimegundua kuwa vyombo vingi vya matumizi ya ndani kama vile majagi, vikombe vikubwa, vyungu n.k, ambavyo vilitumika wakati huo vilikuwa na miguu mitatu. Baada ya kuuliza kwanini viko namna hii, mwongozaji wetu alisema kwamba mbali na urembo pia vyombo hivi vilikuwa vinatumika kupikia moja kwa moja.

Matokeo ya ugunduzi wa mabaki ya kale ya Sanxingdui yanasisimua, hata hivyo yanabaki kuwa fumbo kubwa kwasababu hadi leo hakuna maandiko yaliyopatikana, na pia utamaduni huu haujatajwa katika kumbukumbu za tamaduni nyingine. Kwa mujibu wa wataalamu, uchambuzi wa vitu vilivyoonekana kwenye shaba unaonesha vyanzo ambavyo ni sawa na vile vya tamaduni nyingine kwenye sehemu za chini za Mto Changjiang. Hata hivyo, katika hatua hii, tunaweza kusema utamaduni wa kipekee ambao umefanya kupatikana kwa vitu hivi vya zamani bado unabaki kuwa fumbo na kitendawili kinachohitaji kuteguliwa.
 
Back
Top Bottom