DC wa Temeke ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo ametoa siku saba kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wilayani humo kuhakikisha wanaunda vikundi vya ulinzi shirikishi ambapo amesema mitaa ambayo haina ulinzi shirikishi ndio inayoripotiwa kuwa na matukio mengi ya uhalifu.
DC Jokate ametoa agizo hilo leo Aprili 29,2022 alipokuwa akizungumza na Wenyeviti hao "Ninatoa siku 7 muhakikishe kule ambapo hakuna vikundi vya ulinzi shirikishi mnaanzisha vikundi hivyo na kule ambapo vilikuwepo ila vinalegalega mviimarishe"
"Leo tunapozungumzia kuifungua Tanzania kama afanyavyo Rais Samia, ni kwamba Watu wanaitazama Tanzania na hususan Mkoa wa Dar es Salaam kama ni eneo salama, naahidi Temeke hatutakuwa Watu wa kuibadilisha taswira hiyo, kwenye mitaa au maeneo ambayo ulinzi shirikishi unasuasua au umegubikwa na siasa wajitathimini"
Kikao hicho ambacho kimehudhuriwa na Kamanda Muliro pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ikiongozwa na OCD Temeke, wenyeviti wa serikali za mitaa pamoja na baadhi ya vikundi vya ulinzi shirikishi kilikuwa na lengo la kuweka mikakati ya jinsi ya kukabiliana na wimbi la vitendo vya uhalifu ambavyo vimeanza kujitokeza kwa siku hizi za karibuni.